Sunday, September 4, 2016

WAZIRI, UMMY MWALIMU AWAFUNDA MADIWANI HALMASHAURI ZA MKOA WA TANGA



Tangakumekuchablog
Tanga,WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, amewataka Madiwani wanawake kusimamia mapato na matumizi katika halmashauri zao ili pesa hizo ziweze kujenga vituo vya Afya maeneo yao.
Akifungua kongamano la Madiwani wanawake kutoka halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Pangani, Mkinga na Tanga  mjini  juzi lililoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserkali linaloshughulikia maendeleo ya wanawake Tanga (TAWODE) kwa ufadhili wa Hans Seidel Foundation,  alisema kama Madiwani hao watasimamia  mapato na matumizi kero ya upatikanaji huduma za matibabu itakwisha.
Alisema wanawake wajawazito na wazee wamekuwa wakipata shida ya kufuata matibabu masafa marefu na baadhi ya nyakati wamekuwa wakijifungulia njiani hivyo ili kuondosha kero hiyo inawapasa kufuatilia matumizi katika halmashauri zao.
“Madiwani simamieni mapato na matumzi katika halmashauri zenu ili kuzuia mianya ya ubadhirifu wa pesa za wananchi na kuweza kujenga zahanati ambazo zitakuwa msaada kwa wanawake wajawazito na wazee  pamoja na watoto” alisema Ummy na kuongeza
“Kuna baadhi ya halmashauri kila mwaka hupokea hati chafu na hii ni kutokana na ubadhirifu wa pesa za wananchi na kuwa chanzo cha kudorora huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu” alisema
Alisema Serikali inataka kuondosha kero ya ufuataji wa matibabu masafa marefu kwa kila kata na  kujenga zahanati ambayo wanawake wajawazito wataweza kujifungua na kuondosha kero ya kufuata masafa marefu.
Kwa upande wake Diwani kata ya Maramba, Hadija Mohammed (CCM) alisema mafunzo hayo yamewaongezea uelewa wa kutetea haki za wanawake ndani ya Mabaraza na nje ya chombo hicho.
Alisema wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi za wanawake wajawazito na wazee hivyo kwa elimu hiyo itasaidia katika kuhakikisha jamii hiyo inapata haki zao.
‘Tunawashukuru Hans Seidel Foundation na Tawode kwa kutupatia elimu ya kuibua changamoto katika mabaraza yetu ya madiwani, hii italeta chachu na mabadiliko  katika kata zetu” alisema Hadija
Aliyataka mashirika na Asasi za Kiraia kuiga mfano wa Tawode kutoa  elimu kwa madiwani ikiwa na lengo la kufuatilia miradi iendeshwayo katika halmashauri pamoja na kutetea haki za wanawake.
                                            Mwisho

  Madiwani wa halmashauri za Wilaya ya Kilindi, Pangani, Mkinga na Tanga mjini wakiwa katika kongamano la Madiwani wanawake lililoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na mambo ya wanawake (TAWODE) kwa ufadhili wa Hans Seidel Foundation kuzungumzia ufuatiliaji wa haki za wanawake na miradi ya maendeleo katika halmashauri zao mkutano uliofanyika ukumbi wa YDPC.

 Waziri Ummy Mwalimu akifunga kongamano ukumbi wa YDPC Tanga jana

 Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, akizungumza na waandishi wa habari Tanga mara baada ya kufunga kongamano la Madiwani wanawake liliitishwa na Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na maendeleo ya wanawake kwa ufadhili wa Hans Seidel Foundation mkutano uliofanyika ukumbi wa YDPC.










No comments:

Post a Comment