Friday, September 2, 2016

KAMANDA MPYA WA POLISI TANGA ATEMA CHECHE

Tangakumekuchablog
Tanga, KAMANDA mpya wa Polisi Tanga, Benedict Wakulyamba, ametangaza vita na wapitishaji wa madawa ya kulevya na wasafirishaji wa mali za magendo mpakani na njia ya baharini.
Pia ametoa salamu kwa waendesha vyombo vya moto wakiwemo wafanyabiashara wa pikipiki maarufu kama bodaboda kuzingatia sheria za barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu kwa mwendeshaji na abiria.
Akizungumza katika mkutano wake wa kujitambulisha kwa waandishi wa habari ofisini kwake jana, Wakulyamba alisema anataka kukomesha upitishaji wa madawa ya kulevya katika mpaka wa Horohoro na njia za panya pamoja na baharini.
Alisema kuna taarifa za baadhi ya wafanyabiashara  wenye pesa wamekuwa wakiwatumia vijana kupitisha madawa ya kulevya kutoka nje hivyo kusema kuwa ulinzi utaimarishwa pamoja na kufuatilia vyendo za watu wanaohisiwa kujihusisha na biashara ya unga.
“Tuko na taarifa za watu ambao wanajishughulisha na biashara ya unga na upitishaji wa mali za magendo mpakani na habarini, hili tunataka kulikomesha mara moja” alisema Wakulyamba na kuongeza
“Kwanza tutaanza na watu ambao wamekuwa wakiwatumia vijana kupitisha unga kwa njia ya mpakani na njia za panya ambazo tunawajua, hii tunataka kusafisha njia ambazo tunazijua” alisema
Akizungumzia usalama wa barabarani, kamanda Wakulyamba alisema bodaboda yoyote ambaye atapakiza abiria bila kuvaa kofia ngumu wote watashitakiwa kwa kupelekwa mahakamani.
Alisema kila mfanyabiashara wa bodaboda lazima kuwa na kofia mbili ya dereva na abiria wake  na kutoa tahadhani kwa abiria kujiepusha kupanda  pikipiki ambayo haitakuwa na kofia ya abiria.
Alisema ili kulikomesha hilo ametoa agizo kwa askari wa usalama barabani kufanya ukaguzi katika vituo vya maegesho ya bodaboda na ukaguzi wa vyombo vyengine vya moto barabarani.
“Natoa agizo kwa madereva wa bodaboda kuwa na kofia ngumu ya abiria na atakae kaidi agizo hili hatua za kisheria ikiwemo kupelekwa mahakani zitafuat” alisema Wakulyamba  na kuongeza
“Abiria usipande bodaboda ambayo haina kofia ya abiria na anaekaidi kosa litakuwa la wote wawili dereva na abiria na moja kwa moja mahakamani” alisema
Aliwataka waendesha vyombo vya moto barabarani kuzingatia sheria na kuacha kutumia vilevi na kusema kuwa ugaguzi kwa wanaotumia vilevi kwa kutumia kifaa maalumu utafanywa.
                                       Mwisho

No comments:

Post a Comment