Saturday, September 30, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA ( 1 )

HADITHI

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 1

Ulikuwa ni wakati wa chakula cha usiku. Waziri Mkuu Dastan Lazaro na familia yake ya watoto watatu Vero, Monica na Sofia pamoja mke wake Vicky walikuwa katika chumba cha kulia chakula nyumbani kwa Waziri Mkuu, Msasani jijini Dar.

Walikuwa wanakula chakula.

Upande mmoja wa meza aliketi Waziri Mkuu mwenyewe na mke wake Vicky. Upande mwingine walikuwa wamekaa mabinti zao Vero, Monica na Sofia.

Akiwa mtoto wa kwanza wa mheshimiwa Dastan Lazaro, Veronica alikuwa mrefu na mweupe kama alivyokuwa baba yake. Lakini urefu wake haukuchusha kwa vile alikuwa na maungo yaliyojaa na yaliyoumbika vizuri.

Alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha mlimani akichukua masomo ya sheria. Alikuwa mchangamfu na aliyependa sana mzaha.

Monica ndiye aliyefuatia kwa kuzaliwa. Yeye alimshabihi mama yake kwa sura na kwa umbo. Alikuwa mfupi wa rangi ya maji ya kunde. Uso wake mpana na wa duara ulionekana kama unaotabasamu wakati wote.

Alikuwa akisoma kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wanafunzi wenye vipaji maalum. Licha ya kushabihiana sana na mama yake, alikuwa kipenzi mkubwa wa baba yake.

Sofia ndiye aliyekuwa kitinda mimba wao na aliyeonekana kuwa mzuri zaidi. Alikuwa na urefu wa wastani. Hakuwa mnene wala mwembamba. Alikuwa na umbo la katikati.

Akiwa mwanafunzi wa kidato cha nne, alikuwa na tabia ya kiburi na hasira za haraka haraka lakini ndiye aliyekuwa akisikilizwa zaidi na wazazi wake.

Alikuwa akipenda sana kikolezo cha pilipili. Alipoona chupa ya pilipili haikuwekwa mezani, aliondoka kwenye kiti na kuelekea jikoni.

Mke wa Waziri Mkuu akamtazama mume wake.

“Unajua mwanao anakwenda wapi?” akamuuliza.

Dastan Lazaro akabeua mabega yake.

“Sijui”

“Amekwenda kuchukua pilipili jikoni. Mwanao anapenda sana pilipili”

“Pilipili si nzuri sana. Unatakiwa umkataze asipendelee sana pilipili”

“Nimeshamkataza mara nyingi lakini hasikii. Si unamjua Sofia alivyo mbishi!”

“Subiri arudi”

“Yaani anaweza kuacha chakula ukimwambia aache pilipili”

“Pilipili ya nini msichana mdogo!”

Zikapita karibu dakika kumi kabla ya Sofia kutokea.

“Mbona haji?” Dastan Lazaro akauliza.

“Labda amesikia tulivyosema amechukia” Vicky akasema.

“Monica hebu kamtazame Sofia, anafanya nini jikoni” Lazaro akamwambia Monica.

Monica akanyanyuka na kuelekea jikoni. Alipoingia kwenye chumba cha jiko alitoa sauti ya kimako iliyosikika. Alitoa sauti hiyo mara tu alipomuona Pili, mpishi wa nyumbani kwao amelala chini huku akiwa na michirizi ya damu iliyoganda kwenye shingo yake.

Nguo aliyokuwa amevaa ilikuwa imechanwa kwenye bega. Kiatu kimoja cha Pili kilikuwa karibu yake.

“Baba!” Monica akaita kwa sauti ya kugutusha.

“Kitu gani?” Lazaro akauliza kwa taharuki.

“Njoo baba!”

Hakuondoka Lazaro peke yake, waliondoka wote. Walikwenda jikoni na kumuona mpishi aliyekuwa amelala chini.

“Nini?” Lazaro akauliza.

“Nimemkuta mpishi ameanguka, sijui ana nini?”

Lazaro akainama na kumtazama, akaiona ile michirizi ya damu kwenye shingo yake.

“Pili! Pili!” akajaribu kumuita.

Pili alikuwa kimya huku macho yake yakiwa wazi lakini yalikuwa hayaangalii chochote hali iliyoonesha kutokuwa na dalili yoyote ya uhai.

Ilimchukua dakika moja tu Dastan Lazaro kugundua kuwa Pili alikuwa amekufa!.

Akainuka.

“Kuna kila dalili zinazoonesha kuwa huyu msichana ameshakufa” akasema.

“Sasa amepatwa na nini?” Vicky akauliza kwa hofu.

“Hatujui lakini kwenye shingo yake kuna michirizi ya damu na kwenye bega lake nguo yake imechanwa”

“Kwani Sofia yuko wapi?”

“Sijui, sikumkuta huku jikoni. Kuna kiatu chake kimoja tu hapa” Monica akajibu.

“Au amekwenda juu” aliuliza Lazaro.

Nyumba ya Waziri Mkuu ilikuwa ina ghorofa moja. Vyumba vya mabinti hao vilikuwa juu.

Waziri mkuu akatoka jikoni haraka akapanda ngazi kuelekea ghorofani. Alikuta kiatu kingine cha Sofia kikiwa kwenye ngazi kitu ambacho kilimpa imani kuwa Sofia alikuwa ghorofani.

Alipomaliza kupanda ngazi alitembea kwenye korido kuelekea kwenye chumba cha Sofia.

Alipofika kwenye chumba hicho alifungua mlango na kuchungulia ndani. Alimkuta Sofia akiwa amelala kwenye kitanda.

‘Sofia!” akamuita.

Alipoona Sofia hakuitika aliingia na kusogea kando ya kitanda.

“Sofia!” akamuita tena.

Sofia alikuwa amelala kimya kifudifudi, uso wake ukiwa ameeelekeza kwenye mlango. Macho yake yalikuwa yamefumba kama aliyekuwa kwenye usingizi lakini midomo yake ilikuwa wazi ikivuja damu.

Kwenye kiganja cha mkono wake wa kulia alikuwa amefumbata kitu. Waziri Mkuu alipokiangalia aligundua kilikuwa kipande cha kitambara kilichochanwa begani mwa nguo aliyokuwa amevaa Pili.

Wakati Lazaro akimtazama binti yake, mke wake na na mabinti zao wengine wakaingia mle chumbani.

“Nini tena?” Mke wa Waziri Mkuu akauliza kwa mshangao.

Hali ile waliyomkuta nayo Sofia ilikuwa imewashitua wote.

“Sijui!” Dastan Lazaro alisema akionekana kuduwaa. Akaongeza.

“Mdomoni kwake kunatoka damu na anaonekana amelala usingizi”

Vicky alisogea kwenye kitanda na kumuamsha.

“Sofia! Sofia!”

Sofia akazinduka na kufumbua macho. Akawatazama kwa zamu baba yake, mama yake na ndugu zake.

Macho yake yalikuwa mekundu kama aliyekuwa amelala mchana kutwa.

“Una nini?” Mama yake akamuuliza.

Sofia akajitazama kama aliyekuwa akijishangaa. Alikunjua kile kiganja chake alichokuwa amekifumba. Akakitazama kwa mshangao kile kipande cha nguo alichokuwa amekishika kabla ya kukiachia.

Akajiinua na kuketi kitandani. Kama vile alihisi ladha ya damu midomoni aliupitisha mkono wake kujifuta midomo kisha akaitazama damu aliyoipangusa mkononi.

“Sofia una nini?” Mama yake alimuuliza tena.

Sofia akainua uso na kumtazama mama yake.

“Mbona nina damu midomoni?” akauliza kwa mshangao.

Waziri Mkuu na mke wake wakatazamana.

“Hujui ni kwanini una damu midomoni?” Lazaro akamuuliza.

“Sijui, naona damu tu iko midomoni mwangu!”

Sofia aliendelea kuifuta ile damu na kuitazama.

“Na hicho kipande cha kitambaa ulichokuwa umeshika ni cha nini?”

Sofia alikitazama kile kipande cha kitambaa kabla ya kuuliza.

“Hiki?’

“Ndiyo, hicho”

“Sijui”

“Unajisikia kuumwa?” Lazaro akaendelea kumuuliza.

“Nasikia kichwa kinagonga kwa mbali”

“Hukuuma mtu?”

Sofia akatikisa kichwa.

“Sijauma mtu”

“Wewe si ulikuwa umekwenda jikoni baada ya kuondoka kwenye chakula?”

Sofia alifikiri kisha akajibu.

“Ndiyo nilikwenda jikoni kuchukua pilipili”

“Ulimkuta Pili?”

“Ndiyo nilimkuta”

“Halafu nini kilitokea?’

Sofia alivuta kumbukumbu kisha akatikisa kichwa.

Je nini kilitokea? Usikose kuendelea na riwaya hii hapo kesho.
Ungana nami hapahapa na ndio KUMEKUCHA UPYA