Monday, December 25, 2017

HADITHI, MWANAUME WA KIJINI SEHEMU YA 2

SITASAHAU NILIVYOKUMBANA NA MWANAUME WA KIJINI 2

ILIPOISHIA

Nilipomtajia namba yangu aliiandika kwenye simu yake kisha akanipigia hapo hapo.

Simu yangu ilipoita aliniambia.

“Namba  yangu ndiyo hiyo, ahsante sana”

Hakurudi tena kwenye meza yake akatoka. Kwa vile mtu aliyefanya niamue kuondoka alishatangulia kutoka nikaona niendelee kukaa kidogo.

Lakini sikutimiza hata nusu saa nikainuka na kutoka. Nilirudi nyumbani kwa teksi. Nikafikia kuoga na kujilaza kitandani.
Wakati usingizi unataka kunichukua, simu yangu ikaita. Nilipoichukua na kutazama kwenye sikrini ya simu niliona namba ya yule mzungu. Nikaipokea simu yake.

“Hello!” nikasema kwenye simu.

SASA ENDELEA

“Hello! Mambo vipi?” Sauti ya yule mzungu ikasikika kwenye simu. Nilifurahi alivyoniuliza “Mambo vipi?” Niliona alikuwa mzungu aliyebobea katika lugha ya Kiswahili.

“Poa” Na mimi nikamjibu kwa kutumia lugha ile ile ya mitaani.

“Uko poa kabisa?” akaniuliza.

“Mimi niko poa, sijui wewe?”

“Mimi pia niko poa. Umesharudi nyumbani?”

Mara moja nikagundua kuwa mzungu huyo alikuwa anataka kurefusha mazungumzo.

“Nimesharudi. Hapa niko kitandani” nikamjibu.

“Samahani sana. Mimi naitwa Mr Smith, sijui mwenzangu unaitwa nani?”

“Naitwa Enjo”

“Okey. Jina lako zuri sana. Unaishi wapi?”

“Naishi Sinza”

“Unafanya kazi?”

“Hapana. Kwa sasa niko nyumbani tu”

“Okey. Mimi ni Muingreza. Ninapenda kuja Afrika Mashariki mara kwa mara kutembea. Huwa ninafikia hoteli tu”

“Ndio…ndio”

“Nimefurahi kukufahamu Enjo na ninapenda uwe rafiki yangu”

“Kuna aina nyingi za urafiki, wewe umependelea urafiki wa aina gani?”

“Urafiki wowote tu lakini tutazungumza zaidi tutakapokutana. Enjo una mchumba?”

“Sina mchumba”

“Vizuri. Unadhani tunaweza kukutana wapi kwa ajili ya mazungumzo zaidi”

“Sema wewe”

“Mimi si mwenyeji sana hapa Dar”

“Umefikia katika hoteli gani?”

“Hoteli ya Lux hapa Masaki. Niko chumba namba 35. Unaweza kufika.

Mzungu kanitajia hadi namba  ya chumba chake akidhani ningeweza kwenda kwake.

“Kwanini tusikutane mahali pengine?” nikamwambia.

“Tunaweza. Sasa sema wewe ni mahali gani”

“Ngoja, kesho nitakupigia kukufahamisha”

“Kesho saa ngapi”

Nikafikiri kidogo kisha nikamjibu.

“Kesho mchana”

“Ningefurahi zaidi kama utanitajia saa ili nisubiri simu yako”

“Tuweke saa tano”

“Sawa. Nipige mimi au utanipigia wewe?”

“Nitakupigia mimi”

“Sawa. Nitasubiri simu yako saa tano”

“Nashukuru. Usiku mwema”

“Usiku mwema na kwako”

Nikatangulia mimi kukata simu kisha nikaiweka kwenye kimeza cha mchagoni. Baadaye niliona niizime kabisa kwani sikupenda nikatishwe usingizi wangu kwa milio ya simu.

Usingizi haukuchelewa kunipitia, nikalala. Wakati niko usingizini nikaota niko kwenye ufukwe wa bahari mimi na yule mzungu tukikimbizana huku tukirushiana michanga. Sote wawili tulikuwa tumevaa mavazi hafifu ya kuogelea.

Mimi nilivaa chupi na sidiria yake na mzungu alivaa chupi peke yake. Lakini rangi ya chupi yake na yangu zilikuwa zikifanana.

Baada ya kufukuzana na kuangushana kwa dakika kadhaa tuliingia kwenye maji na kuanza kuogelea kwa pamoja. Tuliogelea hadi tukafika maji mengi.

Mimi nilikuwa nyuma, yule mzungu alikuwa mbele yangu. Ghafla tukajikuta tuko katikati ya bahari. Ule ufukwe wa bahari hatukuuona tena.


Itaendelea kesho hapahapa kuwa nami

Saturday, December 23, 2017

SITASAHAU NILIVYOKUTANA NA MWANAMKE WA KIJINI (1 )

SITASAHAU NILIVYOKUMBANA NA MWANAUME WA KIJINI

Nilichozoea kusikia ni kwamba kuna majini wanawake wanaojigeuza binaadamu na kuwatongoza wanaume.

Wengi wa majini hao hutaka kuishi na  binaadamu kama mke na mume jambo ambalo baadhi ya watu linawavutia kutokana na tamaa ya kupata utajiri.

Lakini nimekuja gundua kuwa hawapo majini wanawake pekee,  bali pia wapo majini wanaume ambao huwatongoza wanawake wa kibinaadamu na kutaka waishi nao kama mume na mke.

Hilo ndilo lililonitokea mimi na kuniingiza katika mkasa uliyoyatatanisha maisha yangu. Nilifikia mahali sasa nilitamani kufa.

Jina langu naitwa Enjo, ukipenda Engle. Ni mtoto wa tatu katika familia ya mzee Sabastian Chacha. Wa kwanza alikuwa mwanaume. Jina lake ni Raymond au Ray kama marafiki zake walivyozoea kumuita.

Yeye anafanya kazi Uingreza. Ameshaoa na ana watoto wawili. Wa pili alikuwa mwanamke kama mimi, anaitwa Miriam. Anaishi Dar ninapoishi mimi, naye pia ameshaolewa na ana mtoto mmoja.

Kwa wanaomkumbuka mzee Sabastian Chacha aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Handeni kisha akawa mbunge wa jimbo la Kibaha iliko nyumba yetu.

Mzee Chacha alifariki dunia miaka michache iliyopita kwa ajali ya gari. Miaka miwili baadaye mama yetu naye alifariki ghafla katika hospitali ya Muhimbili kutokana na shinikizo la damu.

Baada ya masomo yangu ya chuo kikuu nilipata kazi wizara ya afya. Haikutimia hata miaka miwili nilifukuzwa kazi kutokana na sababu ambayo haikuelezwa wazi.

Lakini nilijua kuwa nilitofautiana na bosi wangu aliyekuwa akinitaka kimapenzi nikamkataa. Yeye ndiye aliyenisingizia madai ya kuwa mzembe hadi nikafukuzwa kazi.

Kulikuwa na mwanaume Mzanzibari ambaye nilikuwa na matarajio naye sana kwamba angekuja kunioa. Yeye alikuwa akisoma huko Uingreza. Kwa vile alikuwa na ndugu zake huko ambao walikuwa wakijiweza, alikuwa akinitumia pesa mara kwa mara.

Wakati ule nafanya kazi nilipangisha nyumba huko Sinza. Hiyo nyumba tulichangia watu wawili. Upande mmoja alipangisha mtu mmoja aliyekuwa na familia yake na upande mwingine nilipangisha mimi lakini tulikuwa tunatumia mlango mmoja.

Siku moja nilikuwa nimealikwa katika hafla moja iliyokuwa ikifanyika katika hoteli moja kule Masaki.

Watu tulikuwa tumekaa kwenye viti tukipata vinywaji. Katika meza ya pembeni kwangu aliketi mzungu mmoja aliyekuwa akinitazama sana.

Mzungu huyo alikuwa amevaa suti iliyokuwa imempendeza sana na alikuwa amejifunga kikuba cha rangi nyekundu shingoni. Jinsi alivyokuwa amezichonga vyema ndevu zake alionekana kama muungwana na mtu aliyejistahi sana.

Alikuwa akinywa kinywaji chake taratibu huku jicho lake likiwa  upande wangu.

Sikuweza kujua ni kwanini alikuwa akinitazama sana. Kwanza nilidhania pengin e alikuwa amenifananisha na  mtu aliyekuwa anamfahamu au aliniona mahali fulani na alikuwa akijaribu kunikumbuka.

Lakini nilipomuangalia ili niweze kumuelewa vyema alikuwa akikwepesha macho yake na kutazama upande mwingine. Na ninapogeuza uso wangu anaanza tena kunitazama bila kujua kuwa nilikuwa nikimtazama kwa pemebeni mwa macho yangu.

Kusema kweli alinikosesha raha. “Kama amenipenda angeniambia tu kuliko kunitazama vile” nikajiambia kimoyo moyo nikiwa nimekasirika.

Kwa vile muda ulikuwa umepita sana niliona bora niondoke nirudi nyumbani. Lakini kama aliyekuwa amesoma mawazo yangu aliinuka haraka akanifuata nilipokuwa nemeketi na kuniambia.

“Samahani dada, kuna kitu nataka kukuomba” akanimabia kwa kiswahili fasaha.
Nikahisi alikuwa mzungu mwenyeji kwani alikuwa akiifahamu vyema lugha yetu.

“Bila samahani, niombe tu” nikamjibu.

“Lakini natanguliza samahani, sijui kama utaridhika”

“Niambie tu, ni kitu gani?”

“Naomba namba yako”

Nilielewa kuwa alikusudia namba yangu ya simu kwa sababu hiyo ni tabia ya wanaume wengi, lakini nikamuuliza.

“Namba yangu ya….?”

“Nilikuwa na maana namba yako ya simu”

“Kama ni hilo tu hakuna tatizo” nikamwambia.

Nikampa namba yangu. Nilimpa ili anipigie na kunieleza kile alichokuwa nacho moyoni mwake.


itaendelea kesho usikose