Sunday, June 11, 2017

MABAKI YA BINADAMU WA KWANZA YSPSTIKSNS

Ujenzi wa kwanza wa kisukuku cha awali zaidi cha binadamu kutoka Jebel Irhoud (Morocco) kulingana na nakala za tomografia.Uchunguzi umebainisha kuwa dhana ya kuwa asili ya binadamu wa kwanza ni kutoka Afrika ya Mashariki zaidi ya miaka laki mbili iliyopita sio kweli.
Visukuku vya binadamu watano  imepatikana Kaskazini mwa Afrika na inaonyesha binadamu wa kwanza aliishi miaka 100,000 zaidi ya vile ilivyodhaniwa.
Prof Jean-Jacques Hublin, kutoka Leipzig, Ujerumani, anasema kuwa ugunduzi huu unaweza "kuandika upya vitabu vya kiada" kuhusu kuibuka kwetu .
"Sio hadithi ya hayo kutokea kwa njia ya haraka katika 'shamba la Edeni' mahali fulani barani Afrika. Ilikuwa ni maendeleo ya taratibu. Kwa hiyo kama kulikuwa na bustani ya Edeni, ilikuwa ni kote kote Afrika.
BBC

Friday, June 9, 2017

SIMULIZI, NILIKONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 38

NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 38
 
ILIPOISHIA
 
Nikaenda nyuma ya gari na kulitoa lile shepe.
 
“Njoo hapa” akaniambia akiwa amesimama mahali fulani kando ya lile gari.
 
Nilipofika karibu yake akaniambia.
 
“Chimba mahali hapa”
 
Alinionesha pale aliposimama kisha akaondoka na kusimama kando yake.
 
Nikaanza kupachimba mahali hapo kwa kutumia lile shepe. Bahati nzuri mchanga ulikuwa laini, sikutumia nguvu nyingi. Niliendelea kuchimba  mpaka shimo likafikia urefu wa wastani wa futi mbili.
 
“Nichimbe hadi wapi?”
 
“Bado. Endelea kuchimba” Maimun akaniambia.
 
Nikaendelea kuchimba. Mwili wangu ukaanza kutoka jasho. Nikaacha kuchimba na kuvua shati.
 
“Lete nikushikie” Maimun akaniambia.
 
Nikampa lile shati na kuendelea kuchimba.
 
SASA ENDELEA
 
Niliendelea kuchimba lile shimo mpaka likanifikia usawa wa kifua. Nilikuwa nikimwaga mchanga juu ya shimo hilo. Ghafla nikaona  ninapiga kitu kama mwamba au jiwe lililokuwa chini ya ardhi.
 
“Sijui nimepiga nini hapa?” nikamuuliza Maimun kwa mshituko.
 
“Huo ni mwamba, upige tena” Maimun akaniambia.
 
Nikaupiga tena kwa shepe.
 
“Piga tena”
 
Nikaupiga kwa mara ya tatu. Ule mwamba ukapasuka.
 
“Umepasuka” nikamwambia Maimun.
 
“Hebu washa kitochi cha simu yako umulike hapo palipopasuka” Maimun akaniambia.
 
Nikajipapasa  mfukoni na kutoa simu yangu. Niliwasha kitochi nikamulika pale chini.
 
Mama yangu! Niliona  vipande vya madini yanayomeremeta vikiwa vimetawanyika!
 
“Nini hii?” nikamuuliza Maimun kwa mshituko.
 
“Kwani umeona  nini?”
 
“Sijui  ni madini haya. Huu mwaba ulikuwa na madini!”
 
“Ndiyo ni madini”
 
“Sijui  ni madini ya aina gani?”
 
“Ni Tanzanite, ni yale aliyokuwa akiuza babu yako”
 
“Niyachukue”
 
“Ndiyo yachukue”
 
Nikainama haraka na kuyachukua yale madini.
 
Vilikuwa vipande saba vya madini.
 
“Huu ni utajiri hasa! Nikajiambia kimoyomoyo kisha nikamshukuru Mungu.
 
“Mungu anipe nini tena!”
 
Yakiwa mikononi mwangu madini hayo yalikuwa yakiakisi rangi mbali mbali za dunia. Zile rangi zilikuwa kama zinazunguka. Ilikuwa ni furaha hata kuyatazama.
 
“Ni vipande vingapi?” Maimun akaniuliza.
 
“Viko saba”
 
“Haya sasa toka kwenye hili shimo”
 
“Ngoja niendelee kuupiga huu mwamba”
 
“Hapana, usirudie tena. Toka kwenye shimo” Maimun akanionya.
 
Nikayatia yale madini mifukoni mwangu kisha nikalitoa lile shepe na kuliweka juu ya shimo hilo.
 
“Lete mkono wako nikutoe” Maimun akaniambia.
 
Nikampa mkono wangu Maimun, akaushika na kunivuta. Mara moja  nikjioan niko juu ya lile shimo.
 
“Anza kulifukia haraka haraka”
 
Nikalichukua shepe hilo na kufukia lile shimo.
 
“Tutakuja lini tena kuchimba?” nikamuuliza Maimun kwa tamaa huku nikiendelea kufukia shimo hilo.
 
“Baada ya miezi sita”
 
“Ah kwanini! Mbona  mbali sana?”
 
“Ndiyo masharti yake. Haya madini yanakaliwa na majini. Huwezi kuja kienyeji tu na kuyachimba na hata ukija hutoyaona. Masharti yake ndiyo haya ninayokupa.  Kila baada ya miezi sita tunakuja kuchimba tena”
 
“Sawa”
 
Niliendelea kulifukia lile shimo mpaka nikaliweka sawa.
 
“Watu wengine hawatakuja kufukua?” nikamuuliza Maimun.
 
“Ni nani atakayethubutu?”
 
“Wanaweza kutokea watu wakaja kufukua”
 
“Hawatapata kitu chochote. Chukua shati lako tuondoke”
 
Nililichukua lile shati alilokuwa amelishika Maimun nikalivaa.
 
“Twenzetu” akaniambia.
 
Nililiweka shepe nyuma ya gari.
 
“Utaendesha wewe?” Maimun akaniambia.
 
“Sawa” nikamjibu haraka haraka na kwenda kufungua mlango wa gari wa upande wa dereva.
 
Maimun alifungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia.
 
“Washa gari tuondoke. Muda umekwenda sana”
 
Nikaliwsha gari na kuliondoa. Nilipokuja na Maimun mahali hapo nilikuwa nimefadhaika lakini wakati tunaondoka moyo wangu ulikuwa na furaha iliyopita kiasi.
 
“Hivi babu yangu ulikuwa unakuja naye hapa hapa kuchimba haya madini?”
 
“Ninajua mimi kama tulikuwa tunakuja hapa au mahali pengine”
 
“Hutaki kuniiambia”
 
“Si lazima kila kitu ukijue kwa sasa Kasim”
 
“Sawa mke wangu”
 
Nikabaki kimya mpaka tulipotokea pale mahali ambapo majambazi walitaka kulipora gari langu. Yule mtu aliyenata huku mkono wake mmoja ukipiga ngumi kwenye hewa alikuwa bado amenata vile vile na yule aliyeaguka alikuwa bado yuko chini. Lile  gari lao pia lilikuwa pale pale.
 
“Kumbe hawa watu bado wapo?”nikamuuliza Maimun.
 
“Si uwaache tu. Majambazi wanakuhusu nini?”
 
“Nilikuwa nasema tu”
 
“Sema maneno yenye maana. Achana  na watu hao”
 
“Inaonekana walikuudhi sana”
 
 
 
 
 
 
 
 
ZULIA LA FAKI
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 39
 
ILIPOISHIA
 
Maimun hakunijibu chochote na mimi nikanyamaza. Mawazo yalikuwa yakipita akilini mwangu
 
Niliwaza si muda mrefu nitakuwa mmoja  wa matajiri wakubwa hapa nchini. Nitakuwa ninazungka kwa ndege katika nchi  mbalimbali kama alivyokuwa babu yangu.
 
Huku nikiliendesha  gari kwa mbwembwe, nilijiambia fedha itakaponikubali sawasawa, nitamshawishi Maimun ninunue jumba jingine la kifahari eneo la Masaki ambalo  nilikuwa niikitamani sana kuishi.
 
Pia nilitaka ninunue gari  jingine la gharama kutoka Ulaya. Ikiwezekana magari mawili la Maimun na la  kwangu.
 
Tulipofika nyumbani Maimun aliniambia niyatoe yale madini. Nikayatoa mifukoni.
 
Aliyashika shika na kuyaangalia kisha aliniambia.
 
“Kuwa makini sana, wewe bado ni kijana mdogo. Nakuomba uwe msikivu.  Ujue kuwa ukifanya papara utakwenda na maji”
 
“Kwanini?”
 
“Si lazima kila kitu nikwambie, unapaswa kutumia akili yako. Mimi sitaki uwe mtu wa papara”
 
SASA ENDELEA
 
“Kwani umenionaje mke wangu?” nikamuuliza Maimun baada ya kutomuelewa.
 
“Nimekuona una papara. Jicho limekutoka kwenye haya madini. Unajiona tayari umeshakuwa tajiri. Nataka nikukumbushe kuwa hii mali yote ni yangu mimi. Wewe ninakupa uimiliki tu, wakati wowote utakapovunja masharti yangu nninaichukua mwenyewe”
 
“Sitavunja masharti yako, wewe acha tu niimiliki. Kila mara unapenda kunituhumu lakini mimi sina  tatizo”
 
“Sasa sikiliza. Tafuta wanunuzi wa haya madini hapa hapa nchini. Sitaki uende nje ya nchi kama alivyokuwa babu yako. Na pia huwezi kuyauza madini yote kwa pamoja. Uza moja moja”
 
“Kwanini hutaki niende nikayauze nchi za nje wakati huko nitapata bei nzuri kuliko ya hapa?” nikamuuliza.
 
“Uhitajji kupata pesa nyingi. Pesa yoyote utakayopata itakutosha kwa sababu kila baada ya miezi sita utapata madini mingine, una wasiwasi gani?”
 
“Mimi nilitaka niende nje lakini kama unataka tuyauze hapa hapa, sawa”
 
“Wewe unajua jiwe moja litakupatia kiasi gani?”
 
Pesa nyingi sana. Naweza hata kujenga jumba moja la ghorofa”
 
“Sasa kiherehere chako ni cha nini?”
 
Nikacheka kidogo kisha nikamwambia.
 
“Sina kiherehere. Sasa nitakwenda kuyauza lini haya madini?’
 
“Ni wewe tu”
 
Basi kesho  nitaanza kufanya utafiti wa wateja”
 
“Sawa”
 
Naam, hivyo ndiyo nilivyoanza kutajirika. Nilifanikiwa kuviuza vipande vyote saba. Nikapata kiasi kikubwa cha pesa. Maimun aliniambia pesa hizo nisiziweke benki, niziache pale pale nyumbani atazilinda mwenyewe.
 
Badala ya sanduku moja la pesa tulilokuwa nalo kabatini, tukawa na masanduku mawili. Kila baada ya miezi sita nilienda na Maimun kuchimba madini mengine ambayo niliyauza. Nikapata utajiri mkubwa.
 
Maimun aliniruhusu ninunue nyumba jingine Masaki. Nikanunua jumba la kifahari ambalo alikuwa akiishi mzungu mmoja. Nililinunua kwa bilioni tatu.
 
Nikaagiza magari mawili kutoka  Uingereza aina ya Benz. Moja nilitaka nimpe Maimun lakini akaniambia hataki kuwa na gari la peke yake ila tuyatumie yote mawili kwa pamoja.
 
Pia nilifungua miradi mbali mbali ya kibiashara. Nikawa mmoja wa watu maarufu katika jiji la  Dar na pia nikawa mmoja wa matijiri  wakubwa Afrika.
 
Baada ya kuishi na Maimun kwa miaka  mitatu aliniambia yale madini yamekwisha, kwa hiyo tutumie fedha tulizonazo na kwamba atakapoona inafaa atanionesha mahali pengine pa kuchimba madini mengine ya Tanzanite.
 
Siku za mwanzo mwanzo  nilizoanza kuishi na Maimun nilikuwa nikimuogopa lakini kidogo dogo nikaanza kumzoea na kumuona wa kawaida. Ilifikia mahali nilikuwa ninabishana naye kupinga maamuzi yake na kumwambia kwamba mimi ndiye mume, kwa hiyo anapaswa kunisikiliza mimi.
 
“Nimekupa  mali sasa imekulewesha”  alikuwa akiniambia baada ya kuona sitaki kumsikiliza.
 
“Sio hivyo Maimun, amri zako nyingine zinanikera”
 
“Mimi najua kinachokupa kiburi ni huu utajiri lakini ujue kwamba ninaweza kuufyeka kwa siku moja tu”
 
“Hapana, usifanye hivyo  Maimun. Nipe uhuru wa kushauriana na wewe. Kwanini ninapokushauri kitu unatishia kuchukua mali yako?”
 
“Ni kwa sababu ninataka unitii mimi”
 
“Basi yaishe. Naogopa kurudi katika umasikini”
 
Hivyo ndivyo nilivyokuwa ninaishi na Maimun. Alikuwa na wivu mwingi pamoja na kufuatilia mambo yangu kwa karibu. Wakati mwingine nilikuwa nachukia.
 
Kwa maisha ya nyumbani, Maimun alikuwa mke wa kweli aliyenionesha upendo na alinipa mamlaka ya kuimiliki nyumba  vile ninavyotaka mimi. Wakati mwingine nilimtolea ukali, Maimun akaniomba msamaha kwa kuwa nilikuwa mume wake.
 
Jamani huu ndio  mkasa wa urithi wa babu yangu. Nilikiona cha moto lakini mwishoni nikaja kupata mke wa kijini na kupata  utajiri ambao sikuutarajia.
 
Kilichokuwa kinanipa uchungu ni kuwa Maimun alipata ujauzito  wangu mara tatu lakini alikwenda kujifungulia kwao. Wale watoto alikuwa akiwaleta nyumbani usiku. Inapofika alfajiri anawarudisha kwao.
 
Nilipomuuliza ni kwanini anafanya hivyo aliniambia anataka  watoto hao wawe majini kama yeye. Hakutaka wazoeane na watu na kwamba watoto hao hawataenda shule ila  watasomea huko  huko ujinini.
 
“Watakapokuwa wakubwa watakuja kukusaidia, watakuwa kama  binaadamu na utaweza kuwatuma popote” Maimun aliniambia.
 
Mtoto wangu wa kwanza niliyemzaa na Maimun, hivi  sasa ana miaka saba. Wa pili ana miaka  minne na wa tatu bado ni mchanga. Nilikuwa kiona jinsi anavyonyonyeshwa na mama yake ifikapo  usiku anapokuja naye nyumbani pamoja na wale watoto wengine.
 
Sijui nitakapokufa Maimun atakwenda kwa nani kwani sikuwa  na mrithi. Huenda atakwenda kwa mtu mwingine atakayemchunuka.
 
Hadi hii leo niko na Maimun huko nyumbani kwangu Masaki lakini wageni ni marufuku nyumbani kwangu.
 
MWISHO

Wednesday, June 7, 2017

SIMULIZI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 37

ZULIA LA FAKI
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 37
 
ILIPOISHIA
 
Siku nilipogundua hilo nilimuuliza.
 
“Hivi  wewe Maimun hulali usiku?”
 
“Sisi majini hatulali, tunakuwa macho tu” akanijibu.
 
“Kwaninini?”
 
“Ndiyo  maumbile yetu”
 
“Kumbe usiku nalala peke  yangu?”
 
“Ukilala mimi nakulinda”
 
Kuna siku moja aliniamsha saa nane usiku akaniambia nichukue shepe kisha nitoe gari. Baada ya kulitia shepe kwenye gari nililitoa gari. Maimun akajipakia na kukaa kando yangu.
 
“Twende Kigamboni” akaniambia.
 
“Kuna  nini?” nikamuuliza.
 
“Wewe twende tu”
 
Nilikwenda kukutana na maajabu ambayo sitayasahau katika maisha yangu.
 
SASA ENDELEA
 
Tulifika Kigamboni kama saa nane na nusu hivi. Ilielekea Maimun alikuwa akilijua vizuri eneo hilo kwani aliniongoza hadi sehemu ambayo ilikuwa na pori.
 
Akaniambia niingize gari katika pori hilo. Sikumuelewa halafu pia nilipata hofu kidogo. Nikafunga breki na kumuuliza.
 
“Kwani tunakwenda wapi?”
 
“Wewe twende tu”
 
“Lakini huku unakoniambia twende hakuna njia”
 
“Mimi pia nina macho, ninaona kuwa hakuna njia. Ingiza gari hivyo hivyo”
 
“Unataka tutokee wapi?”
 
“Kassim mbona mbishi sana?”
 
“Mahali kuna pori, unaniambia niende! Njoo uendeshe wewe”
 
“Kumbe huniamini?”
 
“Ninakuamini. Tatizo nini kuwa siwezi kuendesha gari kwenye pori na pia sijui tunakwenda wapi”
 
“Kwahiyo turudi?”
 
“Tusirudi. Nimekwambia njoo uendeshe wewe”
 
“Inaelekea wewe ni muoga sana!”
 
Hapo sikumjibu. Nikanyamaza kimya kwani ukweli ni kuwa uoga pia nilikuwa nao.
 
“Shuka unipishe hapo kwenye sukani” Maimun akaniambia.
 
Nikafungua mlango na kushuka.
 
Kulikuwa na gari ambayo ilikuwa nyuma yetu ikatupita na kusimama mbele yetu.
 
Wakati ule nafungua mlango nikaona ninavamiwa na mtu mmoja miongoni mwa wanne waliotoka kwenye lile gari. Mtu huyo alinishikia bastola na kunitia kabari kwa nyuma. Mtu mwingine alifungua mlango wa upande aliokuwa Maimun akamwambia.
 
“Shuka haraka!”
 
Maimun akashuka kwenye gari.
 
“Mnataka nini?” Maimun akiwauliza.
 
Mimi nilikuwa nimeshadhibitiwa. Mkono ulionitia kabari ulikuwa ukinikaza na kunifanya nisifurukute hata kidogo. Mdomo wa bastola ulikuwa ukitekenya shavu langu la kulia.
 
Sikuweza kujua watu wale walikuwa kina nani na walikuwa wanataka nini.
 
Kulikuwa na watu wengine wawili ambao walikuwa wamefungua milango ya ile gari kama vile walikuwa wakitafuta kitu.
 
“Mnakwenda wapi?” Yule mtu aliyemtoa Maimun kwenye gari akamuuliza Maimun.
 
“Nyinyi ni majambazi sio?” Maimun akawauliza.
 
Yule mtu alitaka kumpiga Maimun kibao, bila shaka kwa vile alivyowambia ni majambazi. Maimun akatoweka ghafla mbele  yake. Kibao kikakata hewa. Maimun akaibuka tena mahali pale pale. Nikamsikia akitoa mlio kama wa fataki inayopaa juu huku na yeye akirefuka kwenda juu.
 
Wakati ule mmojawao, alikuwa ameshajipakia kwenye gari kwenye siti ya dereva. Nikahisi walitaka kutupora lile gari.
 
Lakini kitendo cha Maimun kurefuka kiliwashitua. Maimun aliendelea kurefuka akafikia kimo cha mnazi!
 
Nikawasikia wale watu wakisema kwa fadhaa. “Ha! Ha1 Ha!”
 
Yule aliyenitia kabari aliniachia akakimbilia kwenye gari lao. Yule aliyetaka kuendesha lile gari letu alitoka kwenye gari na kukimbia lakini yule aliyetaka kumpiga Maimun kibao alinata pale pale.
 
Wale waliokimbilia kwenye gari walikwama baada ya Maimun kupiga hatua moja na kutinga mbele ya gari hilo. Mtu mmoja alianguka hapo hapo. Wengine wakakimbia kwingine na kuliacha gari.
 
Baada ya tukio hilo nikauona mwili wa Maimun umerudi vile vile kama ulivyokuwa mwanzo.
 
Akaja kwenye gari letu upande wa dereva na kuniambia.
 
“Ingia garini twende”
 
Nikazunguka kwenye mlango wa upande wa pili na kujipakia. Yule mtu aliyenata alikuwa bado amesimama pale pale, mkono wake mmoja akiwa ameunyoosha mbele kama vile anampiga mtu kibao.
 
Maimun alikuwa ameshaingia kwenye gari akaliondoa na kuliingiza kwenye pori.
 
Kile kitendo cha Maimun kujirefusha, hata mimi kilinishitua kwani katika maisha yangu sijawahi kuona mtu akirefuka kwenda juu akafikia kimo cha mnazi.
 
Mpaka wakati ule nilikuwa bado nikitweta.
 
“Umewaona wapumbavu wale?” Maimun akaanza kuniambia akionekana alikuwa amekasirika.
 
“Nimewaona lakini sikujua walikuwa ni kina nani”
 
“Wale  ni majambazi, walitaka kulipora hili gari. Walitufuata kuanzia mbali sana. Nilishawaona lakini sikukwambia”
 
“Kwa hiyo walitaka watuue?”
 
“Sasa kama walitutolea bastola, unadhani walikuwa wana maana gani nyingine?”
 
“Lakini wametishika!”
 
“Walivyonuona ninakuwa mrefu sio?”
 
“Ndiyo. Hata mimi nimetishika”
 
“Wewe mume wangu pia unatishika?”
 
“Sijawahi kukuona ukiwa vile!”
 
“Acha vile naweza kujirefusha mpaka ukawa hujui  nimefikia wapi!”
 
“Sasa unafanyaje?”
 
“Ni namna yetu. Naweza pia kujigeuza mnyama kama vile punda au joka kubwa”
 
“Lakini sitapenda ufanye hivyo mbele yangu”
 
“Nikifanya mbele yako ndipo utakaponizoea”
 
“Eh! Nitaogopa sana”
 
“Utazoea tu. Utaogopa mwanzo, mwisho utakuwa huogopi tena”
 
“Sasa yule mtu aliyetaka kukupiga kibao, ataendelea kubaki pale hadi lini?”
 
“Atajua mwenyewe, achana naye”
 
Maimuna aliendesha gari huku akikata kona ndani ya msitu hadi tukatokea mahali ambapo palikuwa na mawe makubwa sana yaliyotokea ardhini.
 
Akalisimamisha gari na kuniambia tushuke.  Tukashuka. Palikuwa ni mahali panapotisha usiku huo lakini kwa vile nilikuwa na Maimun sikuwa na hofu sana. Nilijua kama kutatokea tatizo atanisaidia.
 
“Toa lile shepe nyuma ya gari” akaniambia.
 
 
 ITAENDELEA kesho hapahapa Usikose uhondo huu

Monday, June 5, 2017

SIMULIZI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 36

NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 36
 
ILIPOISHIA
 
“Nimekwambia hizo si za miradi. Hizo ni za kutumia tu. Pesa za miradi nitakupa baadaye”
“Sawa. Ngoja nichukue milioni moja”
 
“Chukua hata mbili”
 
Nikatia mkono na kuchukua burungutu moja ya zile noti za Kitanzania.
 
“Si unataka milioni mbili, chukua mawili”
 
Nikatia tena mkono na kuchukua burungutu jingine.
 
“Sasa funga hilo sanduku”
 
Nikalifunga. Maimun akanipa ufunguo wa sanduku hilo.
 
“Funguo utakaa nayo mwenyewe” akaniambia.
 
SASA ENDELEA
 
Aliponiambia hivyo, kwa bumbuwazi lililonipata kufuatia kuwa na pesa nyingi kiasi kile nikabaki nikimuangalia Maimun.
 
“Vipi mume wangu, mbona umetulia unaniangalia?”
 
“Unajua siamini macho yangu. Kwa hiyo pesa zote hizi nizitumie?”
 
 
Nilipomuuliza hivyo Maimun alitoa  kicheko laini akaniambia pesa zote zile zilikuwa zangu. Hivyo naweza kuzitumia kununua chochote nitakachotaka.
 
“Nakushukuru sana mke wangu”
 
Maimun aliachia tabasamu kabla ya kuniambia kuwa kulikuwa na jambo muhimu alinieleza.
 
“Sijui kama  unalikumbuka?”
 
“Nimesahau mke wangu ni jambo gani hilo?”
 
“Mume wangu jamani! Naona furaha yako imepita kiasi mpaka umesahau jambo muhimu nililokueleza. Kweli umesahau au unataka tu nikueleze tena?”
 
“Siyo hivyo mke wangu, ningekumbuka ningekwambia. Naomba unikumbushe maana umeniacha njia panda mwenzio”
 
SASA ENDELEA
 
“Haya njoo hapa kitandani nikueleze tena” Maimun akaniambia. Kidogo nilipatwa na wasiwasi. Nikamfuata.
 
“Mbona hujafunga kabati?” Maimun akaniuliza na kuongeza.
 
“Funga kabati kwanza ndio uje”
 
Nikarudi kunako kabati. Nikalifunga kisha nikaenda pale kitandani ambako  Maimun alikuwa ameketi.
 
Maimun akauzungusha mkono wake mmoja kwenye shingo yangu, mkono mwingine ukawa unapapasa kifua changu.
 
“Kassim una manyoya marefu kifuani!” akaniambia halafu akawa anacheka kama mtoto
 
Aliendelea kunipapapasa huku akiendelea kusema peke yake.
 
“Utadhani jini…!”
 
Aliposema hivyo aliangua kicheko kabisa.
 
“Hivi majini wanakuwa  na manyoya marefu?”  nikamuuliza.
 
“Hunioni mimi?” akaniambia huku akinionesha mikono yake ambayo ilikuwa na malaika marefu.
 
Akaendelea kunionesha miguu yake.
 
Ingawa alinionesha miguu na mikono lakini kifuani kwake kulikuwa na manyoya zaidi. Niliyaona usiku uliopita.
 
“Nilidhani ni wewe tu” nikamwambia.
 
“Hapana, hivi ndivyo tulivyo. Tena mimi ni mafupi lakini majini  wenzangu wana manyoya marefu sana”
 
“Kwa hiyo unapenda malaika marefu?”
 
“Sana”
 
Maimun aliposema neno ‘sana’ aliurudisha mkono wake kwenye kifua changu.
 
Mbona hujaniambia hilo jambo muhimu ulilotaka kunieleza”
 
“Ni kukukumbusha tu, nilishakwambia jana kwamba sitaki siri yangu uitoe nje. Hizi pesa  ninazokupa  ziwe siri yako na bado nitakupa  nyingi zaidi. Sitaki nikuone unamueleza mtu kwamba mke wako ni jini na anakupa  pesa. Umenielewa?”
 
“Nimekuelewa”
 
“Siku nikikusikia ukimwambia mtu habari zangu ujue umenivunjia mwiko wangu. Sawa”
 
“Sawa mke wangu. Sitamueleza mtu.  Kwanza nimueleze mtu ili iweje?”
 
“Mimi nazijua tabia za binaadamu. Wengine wanapenda sifa sana. Na sifa haifai”
 
“Ni kweli lakini mimi sina tabia hiyo”
 
“Nataka nikukumbushe kitu kiingine kwamba usiwe  na mahusiano na mwanamke yeyote na kama ulikuwa naye umuache”
 
Hapo nikanyamaza kidogo. Nikamfikiria msichana wangu mmoja ambaye ndiye niliyekuwa nimepanga kuoana naye.
 
“Mbona umenyamaza?” Maimun akaniuliza.
 
“Sikufichi. Kuna msichana mmoja ambaye nilikuwa na uhusiano naye na tulikuwa tumepanga kuoana…”
 
Nilikuwa sijamaliza sentensi yangu,  nikauona uso wa Maimun ukiwa mwekundu mpaka niliogopa.
 
“Unasemaje?” akaniuliza huku akiwa amekunja  uso.
 
“Nilikuwa nataka kukueleza kwamba huyo msichana itabidi  niachane naye…”
 
Maimun akabaki kunitazama. Hata hivyo kwa vile nilikuwa nimeshamzoea nikamshika kiuno chake na kumvuta upande wangu. Wakati namvuta alikuwa laini kama si yeye aliyekuwa amekasirika.
 
“Unakasirika nini” nikapata ujasiri wa kumuuliza nikiwa nimemkumbatia.
 
“Sitaki shirika. Siku nikikufuma naye ujue ninamuua” akaniambia kwa sauti ya kudeka kama ya mtoto mdogo. Hasira zilikuwa zimeshamtoka.
 
“Hutonifuma naye ila itabidi nimueleze kuwa sitaoana  naye tena”
 
“Kwa hilo  ninakuruhusu”
 
“Yaani Maimun unafikiri mimi ni mjinga sana, nikupate wewe mrembo ambaye unanipa utajiri halafu nitafute mwanamke mwingine wa kunifilisi!”
 
Maneno hayo yakamfurahisha Maimun ambaye bado nilikuwa nimemkumbatia.
 
“Si kukupa utajiri tu, pia nakupa mapenzi adhimu” akaniambia kwa kunilegezea sauti.
 
“Ni kweli. Sasa baada ya hayo yote nitafute nini tena kwa mwanamke mwingine?”
 
Sikujua Maimun alipandwa na mori gani, akanipindua kitandani kisha akanikalia juu.
 
“Hutatoka humu chumbani leo. Nakwambia tutashinda humu humu nikuoneshe mahaba ya kijini” akaniambia.
 
Ni kweli siku ile siikutooka nje. Kumbe babu yangu alikuwa akifaidi! Majini wanajua mapenzi ya kweli. Kuoana na Maimun kuliniingiza katika enzi mpya katika maisha yangu, enzi ya mapenzi adhimu.
 
Mapenzi yetu hayakuwa chumbani tu, yalikuwa mahali popote, kwenye chakula, kwenye kuoga na hata kwenye mazungumzo.
 
Kitu ambacho niliokiona kilikuwa kero ni wivu wa mwanamke huyo.  Alikuwa na wivu wa kupindukia. Siku akiamua nisitoke nyumbani,  sitoki. Nitashinda naye chumbani mchana kutwa.
 
Siku ambayo ninapomuudhi anakasirika mchana kutwa. Anakuwa hataki kusema na mimi lakini siku akifurahi atakuenzi mpaka basi.
 
Saa moja asubuhi Maimun anakuwa ameshanitayarishia kifungua kinywa. Saa sita mchana ameshatayarisha chakula cha mchana.  Chakula cha  usiku kinakuwa tayari saa mbili.
 
Vyakula ambavyo Maimun alikuwa akivipenda ni uji uliochanganywa na nyama ya mbuzi, anauita ‘shurba’ Pia hupenda  chai ya maziwa, chapatti, mkate wa mchele, pilau ya kuku, biriani na wali kwa maziwa ya mgando.
 
 
Vitu ambavyo alipenda kuvinunua kila siku ni aina  za manukato. Kwenye kabati letu kulikuwa na chupa karibu ishirini za manukato tofauti tofauti.
 
Alikuwa akipenda kuoga. Mchana mmoja alioga karibu mara sita na akiingia bafuni huchukua muda mrefu kutoka. Ngozi yake ilikuwa safi na laini kama ngozi ya mtoto mchanga.
 
Kuna kitu kimoja nilikuja kukigundua kwamba Maimun alikuwa halali usingizi. Ninapolala naye usiku anafanya geresha tu.  Ninapopitiwa na usingizi mwenzangu anabaki macho akiwa na kazi ya kuniamgalia tu. Wakati mwingine hushuka kitandani na kwenda kukaa sebuleni usiku kucha.
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose uhondo huu.