Uchambuzi huu wa m,agazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga kilichopo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
NIPASHE
Zaidi ya abiria 1,000 wa treni ya abiria
waliokuwa wakielekea Dar es Salaam, jana walikwama kuendelea na safari
yao kutokana na reli kusombwa na mafuriko katika stesheni ya Kidete na
Mzaganza.
Abiria hao walikwama mjini Dodoma wakitokea Mikoa ya Kigoma, Mwanza na Tabora wakielekea Dar es Salaam na Morogoro.
Kufuatia hali hiyo, uongozi wa Kampuni
ya Reli Tanzania (TRL), ulilazimika kukodi mabasi 17 kwa ajili ya
kuwasafirisha abiria hao kwenda Dar es Salaam.
Mkuu wa usafirishaji abiria na mizigo
Dodoma, Haruna Mwano, alithibitisha kukwama kwa abiria hao huku akisema
uongozi wa TRL umeshafanya utaratibu ili abiria hao waendelee na safari.
“Ni kweli abiria takriban 1,090
wameshindwa kusafiri ni wa kutoka Mikoa ya Kigoma, Mwanza na Tabora
kuelekea Morogoro na Dar es Salaam na wamekwama katika stesheni ya
Dodoma kutokana na reli kusombwa na mafuriko,” alisema Mwano.
Alifafanua kuwa abiria hao walianza
safari juzi jioni na wamerudishiwa fedha ya chakula ili wajikimu wawapo
njiani kuelekea Dar es Salaam.
Alisema wametumia mabasi 17 kusafirisha abiria hao na bado hajajua huduma zitarejea lini katika hali yake ya kawaida.
Wakati huo huo, uongozi wa TRL,
umetangaza kusitisha kwa muda kuanzia Januari mosi, mwaka huu kutoa
huduma zake za usafiri baada ya eneo la reli kati ya Kilosa mkoani
Morogoro na Gulwe mkoani Dodoma kutokana na tuta la reli kukumbwa na
mafuriko.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Mhandisi Elias Mshana, taarifa za
kiufundi eneo lililoathiriwa na mafuriko ni kubwa, hivyo wahandisi na
mafundi wa TRL wako eneo la mafuriko kutathmini ukubwa wa kazi yenyewe.
Aidha, ilisema uongozi utatoa taarifa kamili kuhusu lini huduma za TRL kwenda bara zitaanza tena.
HABARILEO
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) inakusudia kuwafikisha wakuu wa shule zake 15 kwenye vyombo vya
sheria kutokana na madai ya ubadhirifu wa fedha.
Akizungumza jana jijini Dar es SaIaam,
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alisema zaidi ya shule 26
walizozifanyia ukaguzi, 15 zimekutwa zikiwa na upungufu na kubwa ikiwa
ni pamoja na ubadhirifu wa fedha.
“Katika ukaguzi tulioufanya,
tumebaini tatizo kubwa kwenye matumizi, watu wamegeuza shule kuwa
kichaka cha kutafuna fedha, sasa hawa tutawafikisha kwenye vyombo vya
sheria,” alisema Bulembo.
Alitoa mfano wa walimu wa shule za
Tegeta, Tabata na Mwembe Tongwa ambao wameshafikishwa mahakamani
kutokana na ubadhirifu. Aidha, Bulembo alisema taasisi yake imejizatiti
katika kuhakikisha inabaki katika soko la elimu kwa kuimarisha na kutoa
elimu bora katika shule wanazomiliki.
“ Kwa sasa Serikali imejipanga
kuboresha shule zake, hivyo kutakuwa na ushindani wa kupata wanafunzi,
ili tubakie kwenye soko ni lazima tuimarishe shule zetu,”
alisema. Bulembo alisema pia taasisi yake imejikita katika kuanzisha
vyuo mbalimbali vya elimu ya juu kwa fani mbalimbali ikiwamo kozi ya
ualimu.
Akizungumzia ada elekezi, Bulembo
alisema anaamini serikali itakuja na ada elekezi ambayo inaendana na
wakati uliopo kwani kuendesha shule kuna gharama nyingi ambazo mzazi
anachangia kupitia ada.
Serikali pamoja na kufuta ada kwa shule
inazozimiliki kuanzia shule za msingi hadi kidato cha nne, inakusudia
kuja na ada elekezi kwa shule binafsi lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo
wananchi.
HABARILEO
Wadau wa masuala ya siasa nchini
wameeleza kuridhishwa na uteuzi wa idadi kubwa ya makatibu wakuu huku
wakisisitiza kwamba Rais John Magufuli apewe muda pamoja na Baraza lake
la Mawaziri wafanye kazi hatimaye wapimwe kwa ufanisi wao na si kwa
ukubwa au udogo wa baraza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na
gazeti hili, watu wa kada tofauti wakiwemo wasomi na wanasiasa wamesema
kitendo cha Magufuli kuteua watendaji wengi ni cha kupongezwa kwani
amelenga kuleta ufanisi.
Kauli hizo za kuunga mkono uteuzi wa
makatibu wakuu 27 walioapishwa Januari mosi mwaka huu kuongoza wizara
19, zimekuja huku kukiwa na baadhi ya watu wanaokosoa kwa kudai Rais
Magufuli hakupunguza ukubwa wa serikali bali ameongeza kutokana na kuwa
na makatibu wakuu wengi.
Aliyekuwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne, Dk Makongoro Mahanga alikaririwa
na baadhi ya vyombo vya habari akikosoa uteuzi huo, akidai Rais
Magufuli ameunda serikali yenye wizara 27 tofauti na wizara 19
alizotangaza huku akisisitiza kuwa baraza lake la mawaziri ni kubwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni
Sefue akizungumza na waandishi wetu, alieleza kushangazwa na mwanasiasa
huyo (ambaye sasa yuko upinzani) kutoelewa kwamba makatibu wakuu si
sehemu ya Baraza la Mawaziri. “Sidhani kama kuna haja ya kumjibu.
Mtu aliyekuwa Naibu Waziri kwa muda
mrefu sana, inashangaza hajui kuwa makatibu wakuu si sehemu ya Baraza la
Mawaziri. Hivyo idadi yao si kipimo cha ukubwa au udogo wa baraza la
mawaziri,” alisema.
Alisema, “hata wewe ukijumlisha
idadi ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu waliokuwepo serikali
iliyopita na waliopo sasa utaona kuwa jumla yao ni wachache sasa kuliko
kabla.” Kwa mujibu wa Balozi Sefue, jumla ya makatibu wakuu wa Serikali iliyopita walikuwa 54.
Rais apongezwe Mhadhiri wa Chuo Kikuu
cha Mzumbe na aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph
Kuzilwa, alisema kitendo cha Rais Magufuli kuteua watendaji wengi ni cha
kupongezwa kwani amelenga kuleta ufanisi.
“Hii nchi ni kubwa na ina vitu vingi vya
kusimamiwa hivyo kuteua idadi kubwa ya watendaji kwa maana ya makatibu
wakuu ni sahihi kwani wao ndio wasimamizi wakuu wa sekta mbalimbali
zilizo chini ya wizara husika,” alisema Profesa Kuzilwa.
Profesa Kuzilwa alisema suala si ukubwa
wa baraza au serikali, bali Rais amelenga kuwa na serikali ambayo
itakuwa na ufanisi mkubwa na kuleta matokeo sahihi ya utendaji. Alisema
kuwa na makatibu wakuu ambao wengi wao ni wataalamu watamsaidia zaidi
rais kusimamia kazi za serikali kikamilifu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Kitivo cha Siasa na Utawala, Dk Benson Bana alisema katika fani
ya utawala, haiwezekani kutumia hoja ya idadi ya makatibu wakuu kupima
ukubwa au udogo wa serikali.
Dk Bala alisema pia aliyetoa hoja ya
kukosoa, ambaye ni naibu waziri wa zamani, hawezi kutoa hoja iliyo
katika mizani kwa kuwa ni majeruhi wa kisiasa aliyekuwa serikalini na
sasa yuko kwenye upinzani.
Alisema muundo wa serikali huwa
unabadilika mara kwa mara na jambo la msingi ni kuwa na watu bora wa
kusaidia serikali katika kutatua matatizo ya wananchi. Acheni fitina
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema,
aliwataka Watanzania wampe Rais Magufuli muda wa kuwatumikia kwa kuunda
serikali ambayo anadhani itakuwa na tija kwa taifa.
“Naomba Watanzania tumpe Rais John
Magufuli miezi sita, tuache fitina na majungu na kuanza kukosoa kosoa
vitu,” alisema Mrema. Mrema alisema kuwa nchi imepata Rais mzuri na
makini kwani anaongoza nchi vizuri na matokeo tumeanza kuyaona kwa
kipindi kifupi kwa kudhibiti ufisadi na wizi katika maeneo mbalimbali.
Alisema Rais aachwe aunde serikali
ambayo anadhani itamsaidia katika kuwaletea wananchi maendeleo na
kupambana na ufisadi uliokithiri nchini, vitendo vya rushwa na hata
majambazi. “Makatibu wakuu ndiyo wasimamizi wa sekali kwa ujumla,”
alisema.
Mrema alisema awali walikuwa
wakilalamikia ukubwa wa Baraza la Mawaziri kutokana na kukosa fedha za
kulipa lakini hivi sasa matokeo yanaonesha ni mazuri kwa udhibiti wa
mianya ya rushwa.
Kwa upande wake, Rais wa East Africa
Bureau, Paul Mashauri, alishauri Watanzania kuwa na imani na rais na
uteuzi anaoufanya kwa kuwa unalenga katika ufanisi. “Bila kujali ni
baraza la namna gani, rais ameliunda lakini kubwa ambalo tunatakiwa
kuliangalia ni ufanisi utakao tokana na baraza hilo pamoja na watendaji
wake,” alisema Mashauri.
Awali, Dk Makongoro ambaye alihama CCM
baada ya kushindwa kwenye kura za maoni, na kuingia Chadema, alikaririwa
na vyombo vya habari akidai kwamba si kweli kwamba Rais Magufuli
amepunguza ukubwa wa serikali bali ameongeza.
“Sina hakika kama wasaidizi wa rais
wamemshauri na kumweleza kwamba wizara si ofisi ya waziri bali wizara ni
ofisi ya Katibu Mkuu (mtendaji mkuu, afisa masuhuli). Mtendaji mkuu
ndiye mwenye dhamana.
Ndiyo maana hata katika ngazi ya kata,
ofisi ile inaitwa Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kata siyo ofisi ya Diwani,”
Mahanga alinukuliwa. Alidai kwamba, ukubwa wa serikali hautegemei sana
wingi wa mawaziri bali wingi wa makatibu wakuu huku akisema ahadi ya
Rais Magufuli kwenye kampeni kwamba ataunda serikali ndogo hakuitimiza.
HABARILEO
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi imeteua shule sita za sekondari nchini kuingia katika mpango
maalumu wa wanafunzi wake kufundishwa somo la lugha ya Kichina kuanzia
mwaka huu.
Kutokana na uamuzi huo, walimu 12 kutoka
China wamekamilisha utaratibu wa mpango kazi wa namna ya ufundishaji wa
somo hilo kwa shule zilizoteuliwa mara zitakapofunguliwa rasmi mwezi
huu.
Ofisa Elimu Mkuu wa Wizara ya Elimu,
Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Salum Salum, alitaja shule zilizoingizwa
kwenye mpango huo katika awamu ya kwanza ni Benjamin Mkapa na Chang’ombe
(Dar es Salaam), Msalato na Dodoma (Dodoma), Morogoro na Kilakala za
mkoani Morogoro.
Salum alitoa taarifa hiyo juzi wakati
akifungua mafunzo ya kazi na mipango mikakati iliyoandaliwa na Taasisi
ya China inayojihusisha na lugha ya Kichina kwa walimu wake walioteuliwa
kufundisha somo la lugha ya kichina katika shule hizo.
Alisema kabla ya kufunguliwa kwa shule,
viongozi wa China wamekutana kwa siku mbili mjini Morogoro kufanya
mafunzo ya kazi ya kujiandaa kuingia darasani baada ya shule
kufunguliwa.
“Mafunzo kazini ni ya kujiandaa na
kupeana mikakati na nini kifanyike kabla ya shule kufunguliwa ili
kuingia madarasani kufundisha wanafunzi wa kitanzania lugha ya kichina,”
alisema Ofisa Elimu Mkuu.
Alisema wanafunzi watatahiniwa somo hilo
la lugha ya kichina katika mitihani yao na watakapohitimu watahesabiwa
alama za ufaulu sawa na yalivyo masomo mengine yanayofundishwa katika
shule za sekondari kama ilivyo kwa Kifaransa na Kijerumani.
Alisema wizara inaona ni njia nzuri kwa
vijana wa Kitanzania kuwa na lugha ya mawasiliano katika kuwasaidia
kujifunza zaidi na kutumia fursa zitakazopatikana China ikiwemo
kujiendeleza na elimu ya juu zaidi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya China ya lugha
ya kichina, Ambar Zheng, kutoka katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
alisema walimu 12 wa China wameshapatiwa mafunzo ya namna ya kufundisha
somo hilo kwenye shule husika.
Alisema kila shule ya sekondari
iliyoteuliwa katika mikoa hiyo ya Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro,
zitapangiwa walimu wawili kila moja kwa ajili ya kufundisha somo hilo
kuanzia mwaka wa masomo unaoanza mwezi huu.
Alipongeza ushirikiano mzuri uliooneshwa
kati ya Serikali ya Tanzania na China na wizara husika kuwezesha
kuanzishwa kwa somo hilo katika baadhi ya shule za sekondari nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Waislamu cha Morogoro, Profesa Hamza Njozi
alipongeza Serikali ya China kwa kuendeleza ushirikiano katika nyanja
mbalimbali, ikiwemo elimu ya vyuo vikuu.
HABARILEO
Watanzania wamehadharishwa kuendeleza
siasa za majukwaani badala yake, wametakiwa kumwacha Rais John Magufuli
afanye kazi yake na wamuunge mkono katika kuwabana wakwepa kodi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo alitoa angalizo hilo jana wakati
akizungumzia madai ya kuwapo kwa uonevu, vitisho na kuongezewa kodi kwa
wafanyabiashara walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani.
Madai hayo yalitolewa na aliyekuwa
mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa. “Wakati wa siasa
za majukwaani umeisha. Rais amepatikana aachwe afanye kazi, na ili
afanya kazi yake vizuri ni lazima akusanye kodi na tusianze kudhoofisha
kasi na utendaji wake kwa maneno kama haya,” alisema Bulembo.
Lowassa anadaiwa kusema hayo wakati wa
ibada maalumu ya kukaribisha mwaka mpya iliyofanyika katika Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Monduli alipopewa
nafasi ya kutoa neno la shukrani na kutoa salamu za mwaka mpya.
Alikaririwa akidai kuwa serikali imekuwa
ikiwaandama wafanyabiashara na wananchi waliokuwa wakiunga mkono
upinzani katika uchaguzi mkuu uliopita na kuwaambia wafuasi wake kwamba
kazi ya kutafuta mabadiliko ndiyo kwanza imeanza.
Katika mkutano na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Bulembo alimtaka mwanasiasa huyo kujitokeza
hadharani na kutaja kwa majina, wafanyabiashara wanaodai kuongezewa kodi
kutokana na kuwa wafadhili wa Chadema.
Alisema haitoshi kwa Lowassa kutoa
malalamiko hayo kiujumla bila kubainisha watu hao kwani kwa kufanya
hivyo, kutachangia mgongano kati ya Serikali na wafanyabiashara. Bulembo
alisema kauli ya Lowassa pia imelenga kudhoofisa kasi na jitihada za
Rais John Magufuli za kukusanya kodi na kudhibiti mianya ya ukwepaji
kodi iliyokuwapo.
“Suala la kulipa kodi ni la wote
wanaotakiwa kulipa kodi, bila kujali kama mtu huyo alisaidia au
kufadhili CCM, CUF (Chama cha Wananchi) au Chadema. Kama unatakiwa
kulipa kodi wewe lipa tu na suala la kukwepa kodi katika uongozi wa
awamu ya tano halipo,” alisema.
Alisema wakati Rais Magufuli anaingia
madarakani, Sh bilioni 850 zilikuwa zikikusanywa kwa mwezi na kwa muda
mfupi wa kuwapo madarakani zaidi ya Sh trilioni moja zimekusanywa.
Alisisitiza kuwa juhudi hizo ni lazima ziungwe mkono na Watanzania
wanaopenda maendeleo ya nchi.
“Tunamtaka ajitokeze na kuwataja kwa
majina watu wanaoonewa na kuongezewa kodi kubwa eti kwa sababu ni
wafadhili wa Chadema, kauli kama hizi sio nzuri, zinalenga kuibua
mgongano kati ya serikali na wafanyabiashara ambao ndio walipakodi,”
alisema Bulembo.
Wakati Jumuiya ya Wazazi kupitia kwa
Bulembo ikielezwa kukerwa na wanaoendeleza siasa za majukwaani, kutoka
mkoani Arusha, inaripotiwa kuwa viongozi wa kimila wa kabila la Kimasai
maarufu kwa jina la Laigwanani wa wilayani Monduli, wamemtaka Lowassa
kumuunga mkono Rais Magufuli katika vita ya kupambana na ufisadi nchini.
Walisema hayo mjini Monduli mwishoni mwa
wiki kwa waandishi wa habari baada ya mkutano wao uliolenga kuzungumzia
masuala mbalimbali yakiwamo ya kimila. Akizungumza na waandishi wa
habari kwa niaba ya viongozi hao wapatao 50 waliotajwa kutoka kwenye
kata zote za Wilaya ya Monduli, Lota Sanare alisema viongozi hao wa
kimila wamemtaka Lowassa aliyekuwa mbunge wao, kuunga mkono mkakati wa
Magufuli wa ‘kutumbua majipu’ .
“Kama yeye Lowassa hawezi au
hataki kumuunga mkono Rais Magufuli katika kutumbua majipu ya wakwepa
kodi, wazembe, wabadhirifu wa mali ya umma na mafisadi, basi akae kimya
amwache mwenzake (Rais Magufuli) awatumikie Watanzania kama alivyoahidi
wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na si kulalamika ,”alisema Sanare.
Sanare alisema, “anachofanya Rais
Magufuli na serikali ni kuwashughulikia wafanyabiashara wanaokwepa kodi,
wawe CCM au Ukawa (umoja wa vyama vinne), sasa anapotokea mwanasiasa
anapinga vita hiyo maana yake anaunga mkono ukwepaji kodi na huyo ni
fisadi na adui mkubwa wa Watanzania.”
Alisema kodi na ushuru wa serikali ndiyo
nguzo ya maendeleo ya nchi. Alisisitiza wanaokwepa kulipa kodi
washughulikiwe bila kujali ni akina nani. “Lazima washughulikiwe hata
awe nani, kwa mujibu wa sheria na sisi tunaunga mkono hatua zote
zinazochukuliwa na serikali na tuko tayari kusaidiana nayo kuyatumbua
yale majipu yaliyojificha huku kwetu,” alisisitiza Sanare.
Kauli ya viongozi hao wa kimila imekuja
siku chache baada ya Lowassa kunukuliwa hivi karibuni akilalamika
kanisani Monduli kwamba serikali inawaandama wafanyabiashara waliokuwa
wakiunga mkono Ukawa.
MWANANCHI
Hali ya taharuki imeanza kuwakumba
wateja wa taasisi za fedha nchini, hasa benki kutokana na kuibuka kwa
matukio ya wateja kuporwa wanapotoka kuchukua fedha.
Katika siku za karibuni kumekuwapo na
matukio ya watu mbalimbali kuporwa fedha na watu wenye silaha, ikiwa ni
muda mfupi baada ya kutoka benki, hali ambayo inajenga wasiwasi juu ya
sehemu ambazo majambazi hao hupata taarifa za watu wanaokwenda benki
kuchukua fedha.
Wateja wa benki mbalimbali wanatupia
lawama uongozi wa benki kwa kufumbia macho matumizi ya simu za mikononi
ndani ya benki, huku ikihisiwa baadhi yao ndio ambao hutoa siri kwa
majambazi.
Hofu miongoni mwa wateja ilizidi zaidi
baada ya majambazi kumuua kwa risasi meneja wa operesheni wa Zantel,
Gabriel Kamukala muda mfupi baada ya kuchukua Sh10 milioni benki.
Kamukala aliuawa Desemba 28 saa 4:00
asubuhi jijini Dar es Salaam na kumekuwapo na matukio ya aina hiyo
katika miji mingine mikubwa kama Arusha, Mwanza na Moshi.
Jana kulikuwapo na ujumbe unaosambazwa
katika mitandao ya kijamii, ukiwaonya wateja kutothubutu kuchukua fedha
kupitia matawi ya benki zilizopo eneo moja jijini Dar es Salaam.
“Benki zote za (jina limehifadhiwa) zina
majambazi. Wanakupiga picha na wahudumu wanawaeleza umebeba kiasi gani.
Usipende kutoa pesa utakimbizwa na pikipiki,” unasema ujumbe huo.
Mkurugenzi wa kampuni ya Destination
Travel ya mjini Moshi, Rogatus Lucas alisema uporaji wa fedha kwa wateja
wanaotoka benki usipodhibitiwa, unaweza kuhamia mikoa mingine. Lucas
alitaka sheria iwe ni msumeno, kama hairuhusiwi kutumia simu ukiwa ndani
ya benki, basi agizo hilo litekelezwe na si kwa wateja tu hata watunza
fedha ili kudhibiti kuvuja kwa siri.
“Tujiulize ni nani wanaotoa siri hizi?
Kama baadhi ni wafanyakazi wa benki, basi wasiruhusiwe kutumia simu na
kama ni wateja wazizime kabla ya kuingia benki,” alisisitiza Lucas.
Mkurugenzi wa benki ya CRDB mkoani Kilimanjaro, Francis Mollel alitupia
lawama wateja kuwa wanapuuza matangazo hayo. “Hata pale kwangu (tawi la
Moshi) kuna matangazo, lakini utakuta bado mteja anaongea na simu.
Unawaambia tunazuia hii kwa faida yako,
lakini hawakuelewi,” alisema Mollel. Mollel aliishauri Serikali kutunga
sheria kali ya kuzuia matumizi ya simu ndani ya benki na pia mtu yeyote
anayechukua kiwango kikubwa cha fedha iwe lazima kuomba ulinzi wa
polisi.
Kwa mujibu wa Mollel, ujio wa huduma ya
utoaji na uwekaji fedha benki kwa njia ya simu, Simbanking, unaweza
kudhibiti uporaji wa fedha, akisema bado matumizi yake yako chini na
kusisitiza kuwa huduma hiyo ni salama zaidi kwa miamala ya fedha.
Mfanyabiashara wa jijini Arusha, Nurdin
Mahmood, alisema kumekuwa na wateja feki ndani ya benki wanaokaa kwa
muda mrefu bila kuhitaji huduma yoyote. “Benki zinatakiwa ziwe makini
sana na kufuatilia mienendo ya watu wa aina hii,” alisema.
Mmiliki wa kampuni ya mabasi ya
Capricorn, George Mberesero alisema kuna ulegevu katika usimamizi wa
kanuni za benki kutokana na baadhi ya wateja kuingia na silaha kwa kuwa
hakuna ukaguzi. “Kuwepo na utaratibu wa polisi au walinzi kusimama
mlangoni kuhakikisha mteja amezima simu yake au amekabidhi bastola yake,
lakini siku hizi imekuwa ni holela. Watu wanaingia na silaha,” alisema.
MWANANCHI
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amesema
ameshangazwa na kauli ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk
Makongoro Mahanga kuwa wingi wa makatibu wakuu unakinzana na dhana ya
kupunguza ukubwa wa Serikali alioahidi Rais John Magufuli.
Akizungumza na Mwananchi juzi, mbunge
huyo wa zamani wa jimbo la Segerea (CCM), mbali na kupongeza kazi
inayofanywa na Rais, alisema kuteua makatibu wakuu 27 ni sawa na kuwa na
wizara 27 badala ya 15 kama inavyoelezwa.
Dk Mahanga alisema huko si kupunguza
ukubwa wa Serikali bali ni kuongeza ukubwa wake na kwamba wizara ni
ofisi ya katibu mkuu na si ofisi ya waziri.
Lakini, Balozi Sefue alipotafutwa na
gazeti hili kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya Dk Mahanga, alisema kauli ya
kiongozi huyo imemshangaza. “Kwa mtu aliyekuwa naibu waziri kwa muda
mrefu sana, inashangaza hajui kuwa makatibu wakuu si sehemu ya Baraza la
Mawaziri,” alisema Sefue.
“Idadi yao si kipimo cha ukubwa au udogo wa Baraza la Mawaziri,” alisema Balozi Sefue.
Sefue aliongeza kuwa idadi ya makatibu
wakuu na naibu wao waliokuwapo kwenye Serikali iliyopita na waliopo sasa
ni tofauti, kwa kuwa wamepungua. “Jumla ya makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu wa Serikali iliyopita ilikuwa 54. Hivi sasa wako 49 tu,” alisema Sefue.
Ikumbukwe kuwa baada ya kupunguzwa kwa
Baraza la Mawaziri kutoka mawaziri 55 wa baraza lililopita hadi mawaziri
34 wa baraza la sasa, hata nafasi za makatibu wa wizara zimepungua pia.
Rais alisema makatibu ambao
hawajateuliwa, watapangiwa kazi nyingine. Kauli ya Dk Mahanga, ambayo
pia aliituma kwenye ukurasa wake wa facebook, iliibua mjadala kwenye
mitandao ya kijamii baada ya wananchi kugawanyika, baadhi wakimuunga
mkono na wengine wakimkosoa.
MWANANCHI
CCM imesema kauli ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuwa
wafadhili wa Chadema wananyanyaswa, ina lengo la kuichonganisha
Serikali na walipa kodi na kumtaka ataje waliofanyiwa vitendo hivyo.
Juzi, Lowassa alikaririwa na vyombo vya
habari kutoka Monduli akisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
maelekezo ya Serikali imekuwa ikiwatoza kodi kubwa wafanyabiashara kwa
sababu waliifadhili Chadema kwenye kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana.
Lowassa aliwahi kutoa kauli kama hiyo
jijini Mwanza akiwa kwenye msiba wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema wa
mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo aliyeuawa kwa kushambuliwa kwa mapanga.
Pia wakati wa harambee ya Chadema
iliyofanywa Septemba 22 mwaka jana, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman
Mbowe alisema kulikuwa na matajiri watano wenye uwezo kiuchumi ambao
walikuwa tayari kukisaidia kwenye shughuli zake za kampeni, lakini
hawataki kutajwa majina yao kwa hofu ya kufuatiliwa na vyombo vya dola.
Jana, akizungumza na waandishi wa habari
jijini, Abdallah Bulembo, ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya
CCM, alisema kauli ya Lowassa haina ukweli wowote na kwamba ina lengo la
kuigombanisha Serikali na walipakodi ambao wanahitajika sana kipindi
hiki.
“Kama kweli Lowassa anawafahamu
wafanyabiashara au kampuni ambazo zinatozwa kodi kubwa kwa sababu
walikuwa wamekifadhili chama hicho, basi ni vizuri awataje ili
wajulikane na waseme wao wenyewe,” alisema Bulembo ambaye wakati wa
kampeni alikuwa bega kwa bega na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli.
Akijibu suala hilo, Lowassa alisema kuna
wafanyabiashara wengi waliokuwa wakikifadhili chama ambao wanalalamika
kutozwa kodi kubwa.
“Kuna watu wengi wanalia kutozwa kodi
kubwa,” alisema Lowassa ambaye aligombea urais kwa tiketi ya Chadema
baada ya kuihama CCM Julai mwaka jana. “Suala hapa si kuwataja majina,
mkihitaji majina yao fanyeni research (utafiti) mtawapata. Lakini
mfahamu kwamba kuna tatizo hilo.”
Alisema ana uhakika vyombo vya habari
vitawapata watu hao na kwa kuwa ni wengi watatoa malalamiko yao.
Akifafanua zaidi, Bulembo alisema kauli ya Lowassa inadhoofisha nguvu ya
Rais Magufuli ambaye ameongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh850
alipoingia madarakani hadi Sh1.3 trilioni kwa mwezi.
“Tunawahitaji walipakodi wengi wakati
huu kwani tunahitaji kupata fedha zaidi ili kutekeleza ahadi
tulizowaahidi wananchi. Kauli ya Lowassa inatugombanisha na walipakodi,”
alisema.
Alisema anachofahamu ni kwamba kodi
inatozwa bila kumpendelea mfadhili wa CCM au kumwonea mfadhili wa
Chadema. “Masuala ya vyama ya siasa yameshapita, sasa hivi ni kujenga
nchi na kodi inatozwa bila kuangalia vyama vya siasa,” alisema Bulembo.
Alimwomba Lowassa kumsaidia Magufuli
katika kazi ya kutafuta mapato ili kuwaletea wananchi maisha mazuri
“Namwomba Lowassa tujenge nchi yetu, huu si wakati wa kufanya siasa,
asubiri mwaka 2020 kama atagombea tena urais tutakutana kwenye
majukwaa,” alisema.
Alisema kuendelea kupigana vijembe kipindi hiki ni kurudisha nyuma maendeleo ambayo yanahitaji zaidi walipakodi.
“Kodi zina vipimo vyake kama kuna watu
wameonewa ukweli utajulikana,” alisema Bulembo ambaye pia ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya CCM. Alisema Serikali ya CCM itaendelea kutenda haki kwa
wananchi wake ili kukiwezesha chama hicho kushinda uchaguzi kwa kishindo
mwaka 2020.
Alipoulizwa kuhusu madai hayo,
mkurugenzi wa idara ya elimu na huduma kwa walipakodi wa TRA, Richard
Kayombo alisema mamlaka hiyo haijapata malalamiko yoyote.
Alisema mamlaka hiyo inafanya kazi kwa
kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na haifanyi kazi kwa kufuata
maagizo ya vyama vya siasa. “Sisi hatuko kwenye siasa tunafanya kazi
zetu kwa kuongozwa na sheria na kanuni. Hatumwonei mtu wala kupendelea,”
alisema.
Kauli kama ya Lowassa ilitolewa pia na
mkuu wa idara ya habari ya Chadema, Tumaini Makene aliyesema hoja ni
kueleza kuwapo kwa tatizo ambalo halitaishia kwenye ubaguzi wa
kiitikadi. “Ukianza kubagua watu kivyama, huwezi kuishia hapo. Utaanza
kuwabagua kikabila, kikanda na hata kidini.
Hii ni kinyume na ahadi ya Rais Magufuli
kuwa atakuwa Rais wa watu wote,” alisema Makene. Makene alitoa mfano wa
kukataliwa kwa misaada ya vifaatiba katika zahanati za Serikali mkoani
Kagera uliotolewa na mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare.
Mara baada ya kuingia Ikulu, Rais
Magufuli alikutana na watumishi wa Hazina na kuwaelekeza kukusanya kodi
bila ya kuangalia sura, huku Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifanya ziara
za mara kwa mara bandarini ambako ameibua kashfa za ukwepaji kodi na
upitishaji makontena kifisadi.
MWANANCHI
Sakata la bomoabomoa kwa wakazi wa mabondeni limechukua sura mpya baada ya mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia kufungua kesi katika Mahakama ya Ardhi kupinga ubomoaji wa nyumba bila kutoa njia mbadala za makazi.
Kazi ya ubomoaji wa nyumba zilizojengwa
mabondeni, maeneo ya wazi, kwenye kingo za mito na fukweni, ilisitishwa
kwa muda hadi Januari 5, ukiwa ni mpango wa kuwapa muda wakazi kuhamisha
vifaa vyao na kubomoa wenyewe nyumba zao, lakini sasa itakutana na
kikwazo kipya.
Jana, mbunge huyo wa Kinondoni
aliwaambia wanahabari kuwa shauri hilo linatarajiwa kusikilizwa leo na
kitengo hicho cha ardhi cha Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuanzia
saa 4:00 asubuhi, na itasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu, Kitengo cha
Ardhi, Panterine Kente.
Alisema anachopinga ni kitendo cha
Serikali kuwavunjia nyumba wakazi hao badala ya kuwahamishia eneo lenye
usalama. “Serikali ingekuwa inawahamisha mimi sina tatizo kabisa.
Lakini unawavunjia makazi yao halafu
haujui wataishi wapi na kuwaacha wanalala juu ya kifusi. Serikali
ilitakiwa iwahamishie kwenye viwanja vilivyopimwa,” alisema Mtulia.
Mtulia alisema kesi hiyo iliyosajiliwa
Desemba 28, 2015 itasimamiwa na wakili Abubakar Salim na kuwataka wakazi
wa Kinondoni kujitokeza kuifuatilia.
Mratibu wa wenyeviti wa mitaa 18
inayoguswa na bomoabomoa hiyo, Godwin Cathberth alisema Serikali
ingesitisha kuvunja nyumba hizo ili wakae chini na kuzungumza.
Alisema viongozi wa mitaa hawakupata taarifa rasmi za kuhamishwa kama ambavyo Serikali hufanya mawasiliano yake.
“Wanasema sisi tuhame ghafla tu wakati
Serikali imejenga miundombinu ya gharama kubwa, kama kituo cha mabasi
yaendayo kasi na moja ya majengo ya hospitali ya (Taasisi ya Mifupa ya
Muhimbili) Moi.
Inapenda watumishi wake au wagonjwa wafe na mafuriko?” alisema Cathberth.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira, January Makamba alisema hadi jana walikuwa
hawajapokea zuio lolote la mahakama, hivyo operesheni hiyo itaendelea.
kama ilivyotangazwa awali.
Alisema shauri kama hilo lilishapelekwa
mahakamani miaka ya nyuma na mahakama ikaamua wahame na tayari kwa wiki
kadhaa zilizopita watu wengi wameondoka wenyewe kama inavyotakiwa.
Alisema katika utekelezaji wa sheria ya
usimamizi wa mazingira, mipango miji na misitu, Serikali haitamuonea mtu
na uhakiki ulishafanywa kabla ya uamuzi wa kuwaondoa.
“Watu wote wanaoishi katika
maeneo yasiyostahili wana taarifa ya muda mrefu kuwa wanatakiwa kuhama,
si tu kwa sababu ya kukidhi sheria, bali kwa ajili ya kuokoa maisha yao
pale mvua zinaponyesha,” alisema.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment