HADITHI
SIMULIZI A FAKI A FAKI 0713 340572 0655 340572
MWANAMKE 2
ILIPOISHIA
Hapo hapo taa zikazimwa na
filamu ya Dosti ikaanza. Ile filamu ilikuwa ikizungumzia marafiki wawili, mmoja
kipofu na mwingine mlemavu wa miguu. Ilikuwa filamu nzuri na ya kusikitisha sana. Ilikuwa
na nyimbo nne. Nyimbo tatu ziliimbwa na muimbaji maarufu wa India Mohamed Rafiy
ambaye kwa sasa ni marehemu na moja iliimbwa na Usha Mangesh ambaye ni dada wa
Lata Mangesh.
Sinema ilipomalizika
tuliinuka kwenye viti na kutoka. Kwa vile kulikuwa na watu wengi, nilipotoka
sikumuona tena yule msichana, nikaenda kuchukua pikipiki yangu nikaiwasha na
kuondoka.
Kutoka Majestic Cinema
nilishika barabara ya Eckenford hadi bustani ya Uhuru ambapo nilikata kushoto
na kushika barabara ya Pangani. Wakati nalivuka eneo la Tangamano niliona mtu
akinipungia mkono mbele yangu. Alikuwa mwanamke na nilihisi alikuwa anataka
kuniomba lifti.
Kusema kweli muda ule wa
usiku nilikuwa sipakii mtu nisiyemfahamu hata kama
ni mwanamke. Kwa hiyo nilitaka kumpita lakini pikipiki ikazimika moto ghalfa.
Mwanamke huyo akaona nilisimama kwa ajili yake, akanifuata.
Alipofika karibu yangu
nikaona alikuwa ni yule msichana niliyekuwa naye sinema. Nikajiuliza alifikaje
pale wakati nilimuacha kule Majestic?
SASA ENDELEA
Nilipomuona nikatabasamu.
“Ni wewe kumbe?” nikamuuliza.
“Ni mimi, naomba unisaidie
lifti”
“Unaishi wapi?” nikamuuliza.
Kabla hajanijibu alikuwa
ameshakaa nyuma yangu.
“Unaishi wapi?” nikamuuliza
tena.
“Mikanjuni” akanijibu.
Nikaguna lakini bila kutoa
sauti. Eneo alilolitaja, wakati huo lilikuwa kama pori la miti ya mikanju. Viwanja vilikuwa
vikipimwa sasa na kama kulikuwa na nyumba
zilikuwa chache na za kienyeji. Kwenda huko usiku ule ilikuwa ni hatari.
Lakini msichana alikuwa
ameshakaa nyuma yangu akijisogeza upande wangu ili akae vizuri.
Nikajikuta nikipiga kiki ya
pikipiki ili kuiwasha kwani pikipiki ilikuwa imezima moto. Pikipiki ikawaka,
nikatia gea ya kwanza ya kuondokea na kuondoka.
Msichana aliupitisha mkono
wake kwenye tumbo langu ili kujizua. Mkono huo uliniletea changamoto na hisia
toauti kwenye akili yangu.
“Kama
unakaa Mikanjuni kwanini unakwenda sinema za usiku?” nikamuuliza.
“Nimeshazoea” akanijibu.
Kidogo aliliminya tumbo langu, pengine ni kwa bahati mbaya, nikashituka.
“Mbona unashituka?”
akaniuliza.
“Nilikuwa najiweka sawa”
“Mh!” Msichana akaguna.
Sikujua ni kwanini aliguna.
“Ulitegemea ungerudi nyumbani kwa usafiri gani usiku huu?”
nikamuuliza.
“Ninaomba lifti tu kwa watu”
“Ukikosa lifti unakwenda kwa
miguu?”
“Naweza kukodi teksi lakini
sijawahi kukosa lifti hata siku moja”
Baada ya hapo tukabaki kimya.
Nilikwenda hadi Duga kisha nikakata kushoto na kushika barabara ya
kuelekea Mikanjuni. Hapo ndipo nilipoanza kupita kwenye eneo la vichaka na miti
ya mikanju.
Tulipoingia katika eneo la
Mikanjuni nikamuuliza.
“Unaishi sehemu gani?”
“Twende tu, nitakuonesha”
akaniambia.
“Una maana hatujafika bado?”
“Bado”
Nikaendelea kwenda mbele.
Laiti angekuwa mwanaume mwenzangu, ningemshusha hapo hapo nikarudi kwa hofu ya kutaka kunipora pikipiki.
Sasa tulikuwa tunaingia
kwenye pori
kamili. Kulikuwa na nyumba moja moja tena zikiwa mbali mbali na hazina taa za umeme . Sehemu nyingi
vilikuwa ni viwanja vitupu.
“Simama hapa hapa” Msichana
akaniambia tulipokuwa tunaupita mti wa muwembe.
Nikasimamisha pikipki.
Msichana akashuka.
“Asante
sana kaka”
akaniambia.
“Unaishi wapi?” nikamuuliza
kwa sababu sikuona nyumba karibu.
“Naishi mtaa wa pili”
akaniambia. Mtaa huo pia sikuuona lakini nilimkubalia ili niwahi kurudi.
“Uende salama, mimi nakwenda
zangu” nikamwambia huku nikiigeuza pikipiki.
Nikamuona msichana akichapuka
kuelekea mtaa huo aliosema. Nikatia gea kwa nguvu na kuingia gea ya pili na kuondoka.
Wakati narudi nilimsikitikia sana msichana yule, alikuwa anaishi pembeni sana na katika mazingira
ambayo hayakulingana naye.
Nilipotokea kwenye barabara
ya Duga nilikata kulia nikarudi nyumbani kwangu.
Nilifungua mlango nikaingiza
pikipiki yangu ukumbini kisha nikaingia chumbani kwangu. Nilivua nguo
nikajifunga taulo na kwenda bafuni.
Nilijimwagia maji ya baridi
ili kuuosha mwili wangu ulikuwa umetota kwa jasho. Nilipotosheka nilirudi
chumbani kwangu na kujiandaa kulala.
Asubuhi kulipokucha nilitoka
kwenda kazini kwangu. Baada ya kama wiki moja
hivi nilikutana tena na yule msichana. Nilikuwa nimekwenda katika duka moja la
vitabu kununua kitabu cha “Mashimo saba ya Mfalme Suleyman”
Mara nyingi niwapo nyumbani
hupenda kujisomea vitabu vya hadithi. Katika orodha yangu ya vitabu kitabu
hicho hakikuwemo hivyo nikataka nikinunue ili niwe nacho.
Kabla sijaingia kwenye duka hilo nilikiona kitabu
hicho kwenye safu ya vitabu vilivyokuwa kwenye kioo. Nilipoingia humo dukani
nilimwambia muuzaji kuwa nataka kitabu cha Mashimo Saba ya Malme Suleiman.
“Vimekwisha” akaniambia.
“Kipo kimoja, nimekiona
kwenye kioo” nikamwambia.
“Umekiona?” akaniuliza.
“Ndiyo nimekiona”
“Njoja nitazame”
Muuzaji huyo alizunguka nyuma
ya kioo akakiona kitabu hicho.
“Ni kweli kipo, kilibaki
kimoja tu” akaniambia huku akikifuta vumbi na kunipa.
“Bei gani?”
Akanitajia bei yake nikatoa
pesa na kumlipa.
Wakati ninatoka nje ya duka
nikakutana na msichana aliyekuwa akiingia dukani humo. Akanishitua
aliponiambia.
“Kaka habari ya tangu siku
ile?”
Nikaangaza macho yangu
kumtazama. Nikamkumbuka. Alikuwa ni yule msichana niliyekutana naye sinema siku
ile.
“Oh nzuri! Hujambo?” nilijibu
salamu yake.
“Sijambo. Leo tumekutana
tena”
“Imekuwa kama bahati.
Nilikuwa natoka kununua kitabu”
“Mimi pia nimekuja kununua
kitabu. Nilikuwa nahitaji kitabu cha “Mashimo Saba ya Malme Suleiman”
“Vimeisha. Kilikuwa kimebaki
kimoja tu nilichonunua mimi” nikamwambia.
“Kumbe wewe pia ulikuja
kununua kitabu hicho hicho?”
“Nilikuja kununua kitabu
hicho”
Nikakitoa kile kitabu na
kumuonesha.
Akakishika na kukitazama.
“Una umuhimu nacho sana kwa leo na kesho?”
akaniuliza.
“Ni kwa ajili ya kujisomea
tu”
“Basi naomba uniazime kwa
siku mbili tu halafu nitakurudishia”
Sikuwa na sababu yoyote ya
kukataa. Nilihisi yule msichana alikuwa akikihitaji zaidi.
“Nitakuazima, sasa sijui
nitakipata vipi?”
No comments:
Post a Comment