SASA ENDELEA
Nilimsikia Chausiku
akimueleza mwenzake jinsi nilivyomuacha yeye na kwenda kuoa mke mwingine huko
Handeni wakati nilipopata kazi ya ulinzi.
Chausiku akaendelea kueleza
jinsi alivyofanya hila ya kupajua tunapoishi na kulikuwa na siku alikuja
asubuhi na kusubiri nje kunako nyumba ya tatu.
Aliponiona ninatoka kwenda
kazini, alingoja nifike mbali kisha akaingia katika nyumba niliyokuwa ninaishi.
Kwa vile chumba changu alikuwa anakijua, aliingia na kumkuta mke wangu
akitandika kitanda.
Alichofanya hapo ni kutoa
kisu alichokuwa amekitia kwenye mfuko akamchoma mke wangu kifuani na kumuua
kisha akatoka na kutokomea zake.
Nilikumbuka kwamba siku ile
nilisahau kitu nikarudi nyumbani na kumkuta mke wangu amechomwa kisu kifuani
bila kumjua aliyefanya kitendo hicho.
Tatizo lile likanikuta mimi.
Mimi ndiye niliyeshitumiwa kuwa nimemuua mke wangu jambo ambalo lilinifanya
nitoroke Handeni na kukimbilia Songe kujificha.
Pale ndipo nilipogundua kuwa
Chausiku ndiye aliyemuua mke wangu na kunisababishia mimi matatizo.
Kumbe alikuwa msichana katili
kuliko nilivyomfikiria.
Akaendelea kumueleza rafiki
yake kuwa alilolitaka alilipata kwani nilikimbia Handeni nikarudi kijijini kwao
na kumuoa yeye. Wakati akieleza hivyo alijiona alikuwa hodari na aliyekuwa
amechukua uamuzi wa maana sana.
Hapo ndipo nilipojua kuwa
Chausiku alikuwa akikijua kitendo hicho na ndio sababu nilipokataa kujiunga na
kundi lao la uchawi aliniambia angekwenda kuniripoti polisi kuwa nilimuua mke
wangu huko Handeni.
Msichana huyu ameniharibia
maisha yangu kupita maelezo. Amenifanya naishi kwa kujificha ficha huku
nikitafutwa na polisi kwa kosa alilolifanya yeye. Isitoshe amenilazimisha
nijiunge katika kundi lao la uchawi mpaka akasababisha nilaaniwe na kugeuka
paka.
Nilikuwa nimesogea karibu na
mlango wa uani nikiwachungulia. Niliwaona wameketi kwenye mswala wakila ugali.
“Mpumbavu yule, ameniacha
nyumbani na njaa, yeye amekuja huku anakula ugali” nikajiambia kimoyomoyo.
Kwa hasira zilizonipanda,
nilimrukia kutoka pale mlangoni nikamtia kucha katika jicho lake la upande wa
kushoto na kulitoboa!
Sikutosheka na hapo, alikuwa
ameshika kipande cha nyama nikamnyang’anya na kukibana kwenye meno yangu. Baada
ya kufanya unyama huo nilitoka mbio kwa kutumia mlango wa uani.
Nilikimbia huku nikimuacha
Chausiku akipiga kelele. Sikusimama mpaka nilipofika mbali. Niliingia kwenye
kichochoro kimoja nikala ile nyama. Nilipomaliza nikaendelea na safari yangu.
“Na yeye nimemkomesha
nimemtoboa jicho. Usichana wake sasa umekwisha!” nilijiambia kimoyomoyo wakati
ninakwenda.
Sikujua nilikuwa ninakwenda
wapi, nilikuwa ninajiendea tu kokote kule nitakakoelekea. Sikuwa na mpango
wowote kwani tayari nimeshakuwa paka na nilihisi nitaendelea kuwa paka hadi
kifo changu. Nilizaliwa binaadamu nitakufa kama paka, nilijiwazia kwa uchungu.
Wakati natembea huku
nikiangaza huku na huku kutafuta penye chakula, ghafla nikajikuta nimetokea
katika ile nyumba ya mwarabu tuliyokwenda kuichawia usiku uliopita mpaka
nikaapizwa na kubaki kuwa paka.
Niliona panya akitoka katika
duka la yule mwarabu, nikaenda mbio na kumrukia.
Wakati namrukia yule panya,
mlango wa ile nyumba ulifunguliwa akatoka kijana mmoja ambaye baadaye
niligundua alikuwa anaitwa Khaleed, akasimama na kunitazma.
Nikamsikia akimuita baba
yake.
“Baba njoo uone paka
amekamata panya anamla”
Yule mwarabu ambaye alikuwa
ndiye baba yake alitoka mle dukani akaja kunitazama. Alikuwa ndiye yule
aliyeniapiza usiku.
“Ametokea wapi huyu panya?”
akauliza.
“Nadhani ametokea huko
dukani” Khaleed akamjibu.
“Na huyu paka alikuwa wapi?”
“Sijui, nilimuona tu
akimrukia”
Wakati wakizungumza hivyo
mimi nilikuwa nikiendelea kumla yule panya.
“Humu ndani kuna panya wengi
sana, ningepata paka kama huyu akakaa humu dukani angenisaidia sana”
“Mchukue huyu huyu umuweke
dukani, atawala panya wote”
“Sijui kama atakubali”
Yule mwarabu alirudi kwenye
mlango wa duka lake akanifanyia ishara ya kuniita.
Nilikuwa nimeshamla yule
panya, nikamtazama yule mwarabu. Alikuwa akiendelea kuniita. Nikamfuata na
kuingia mle dukani mwake.
Niliingia kwenye mvungu wa
kabati, Dakika ile ile nikaona panya mwingine akikatiza mbele yangu, nikamrukia
na kuburuzika naye hadi karibu na miguu ya yule mwarabu.
Nikamshika na kumla. Nilimuona yule mwarabu akitabasamu
huku akijisemea peke yake.
“Huyu paka hodari sana”
Nilipomaliza kumla yule panya
niliingia tena mvunguni mwa lile kabati, nikatulia kimya.
Ghafla nikasikia sauti ya
yule bibi kigagula, kiongozi wa kundi la kina Chausiku.
Alikuwa amefika pale dukani
akijidai anataka kununua sigara.
Nilipoisikia sauti yake
nilitoka mle mvunguni nikapanda juu ya lile kabati na kutulia kimya.
“Nataka sigara” Yule bibi
alikuwa akimwambia yule mwarabu huku akimpa pesa.
“Unataka sigara gani?”
mwarabu akamuuliza.
“Nataka sigara kali mbili”
Pesa aliyotoa yule bibi
haikuwa pesa. Kilikuwa ni kihirizi kilichogeuzwa kimazingara na kuonekana kama
sarafu ya shilingi mia mbili.
Nikagundua kuwa kilikuwa
kihirizi cha kukopera pesa. Kama mwarabu huyo angeipokea kwa kudhani ni pesa na
kisha akaichanganya kwenye pesa zake, baada ya muda peza zake zote zingeyayuka
na kwenda kwa bibi huyo.
Wakati bibi huyo anampa
mwarabu huyo sarafu hiyo, niliwahi kuirukia nikaishika na kuiweka pale juu ya
kabati. Nilipoiweka tu ikageuka kihirizi.
Hakuwa mwarabu tu
aliyeshangaa, hata yule bibi alishangaa. Licha ya uchawi wake, hakuwa
amenitambua kuwa sikuwa paka wa kawaida.
Nikasimama kwa miguu miwili
kisha nikamuungurumia yule bibi kwa ukali.
Nilikuwa nikimwambia.
“Wewe bibi ni mchawi. Leo nitakuumbua!”
JE NINI KITATOKEA? TUKUTANE TENA
HAPO KESHO.
|
Friday, May 20, 2016
SITOSAHAU NILIVYOGUZWA PAKA SEHEMU YA 21
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment