SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 7
ILIPOISHIA
Nikanyanyuka na kuingia
chumbani kwangu. Baada ya nusu saa nikatoka nikiwa nimeshavaa.
“Twende” nikamwambia
Alphonce.
Tukatoka. Alphonce alinipakia
kwenye pikipiki yake tukaelekea Mikanjuni. Nilimuelekeza mahali ilikokuwa ile
nyumba ya yule msichana, tukaenda hadi mahali hapo lakini jambo la ajabu
lililotokea ni kuwa ile nyumba hatukuiona. Badala yake tuliona eneo lote
lilikuwa makaburi matupu ya watu wa zamani.
Nikapatwa na mshangao. Wakati
naangalia angalia nikaiona pikipiki yangu ikiwa kando ya mti. Mti huo ndio ule uliokuwa uani
mwa nyumba ya Zena. Kando
yake palikuwa na kisima ambacho yule msichana na mwenzake walikuwa wakioga.
Wakati ule kile kisima
hakukuwepo tena, badala yake tuliona dimbwinl maji ya mvua.
“Pikipiki yangu ile pale!”
nikamwambia Alphonce ambaye naye alikuwa ameshangaa.
“Sasa mbona iko kwenye
makaburi na hapana nyumba?” akaniuliza.
“Na mimi ndio nashangaa. Ile
pikipiki niliiweka uani mwa hiyo nyumba niliyokwambia. Ule mti unaouona ulikuwa
uani na lile dimbwi la maji kilikuwa ni kisima”
“Hebu twende pale karibu”
SASA ENDELEA
Tukaenda hadi pale ilipokuwa
pikipiki yangu. Karibu yake palikuwa na kaburi la zamani. Lilikuwa limejengewa
kiukuta kilichoandikwa jina la Zena binti Ashraf.
Tarehe aliyokufa pia
iliandikwa pamoja na tarehe aliyozikwa. Alikufa tarehe kumi mwezi wa kwanza
mwaka 1920.
“Yule msichana aliniambia
anaitwa Zena na hili kaburi lina jina la Zena, sasa hata sielewi” nikasema.
Nikamsikia Alphonce akitoa
mguno. Hakusema chochote. Nikaiangalia pikipiki yangu.
“Ichukue tuondoke, huku Tanga
kuna mambo ya ajabu sana”
Nikatia ufunguo na kuikokota
hadi kwenye barabara ya vumbi. Nilipoiwasha ikawaka.
“Twenzetu” Alphonce
akaniambia huku akipanda pikipiki yake.
Nikapanda pikipiki yangu,
tukaondoka.Tukiwa njiani tunarudi tulikuwa tunazungumza.
“Jana ulikunywa pombe?”
Alphonce akaniuliza.
“Mimi situmii ulevi wa aina
yoyote”
“Sasa ilikuwaje, wewe
umeniambia uliingia katika nyumba lakini pale ni makaburini?”
“Yaani pamebadilika. Ilikuwa ni nyumba. Yale makaburi hayakuwepo, ndio nayaona
sasa”
“Ni miujiza mikubwa lakini
shukuru Mungu umenusurika na pikipiki yako umeipata”
“Aisee nashukuru sana. Na yule mwanamke
nikimuona nitamkimbia mbali sana.
Sitataka anikaribie, anaweza kutoa roho yangu”
“Mimi sasa naamini kweli
majini wapo na wanajigeuza binaadamu”
Tulipofika Mabawa mimi
nilielekea nyumbani kwangu, Alphonce akaenda kwenye shughuli zake.
Siku ile nilishinda nikiwa na
mawazo ya yule msichana. Kwa kweli alikuwa amenitia hofu
sana. Sikutaka
nikutane naye tena. Ili kujiondoa wasi wasi
niliwaeleza mkasa ule watu mbali mbali niliokuwa nawafahamu akiwemo kaka yangu.
Wote walinipa matumaini wakaniambia hakutakuwa na madhara yoyote
yatakayonitokea.
Baada ya wiki mbili
nilikuwa
narudi nyumbani kwangu kutoka kazini. Nilikuwa naendesha pikipiki yangu
taratibu. Tukio lile la wiki mbili zilizopita nilikuwa nimeshaanza
kulisahau.
Wakati nikiwa katika barabara
ya Pangani nikikaribia kwenye mzunguko wa barabara nne uliokuwa eneo la mabanda
ya papa nikamuona msichana amesimama kando ya barabara
akinipungia mkono. Nilipomtupia macho mara moja nikatambua alikuwa ni Zena!
Moyo ulinishituka sana.
Hapo hapo nikaongeza mwendo.
Nilitakiwa nisimame
kwenye mzunguko huo wa barabara nne uliokuwa mbele yangu. Lakini sikusimama.
Gari lililokuwa linakuja kutoka upande wangu wa kushoto ambalo nilitakiwa
nilipishe lilinikwepa na kwenda kugonga nguzo ya umeme na kisha kuingia kwenye mfereji wa maji ya mvua.
“Nguzo hiyo iling’oka, waya
za umeme zikatikisika na kutoa cheche za moto. Mimi nikaendelea kwenda mbio na
kushika barabara ya Pangani kabla ya kuingia katika eneo nililokuwa ninaishi.
Nilipofika nyumbani
niliingiza pikipiki yangu ndani nikakaa sebuleni na kuanza kuwaza. Nilijua kuwa
nilikuwa nimesababisha
ajali kutokana na kuvunja sheria za barabarani baada ya kumuona yule msichana.
Kwa vile nilikuwa na hakika
kwamba namba za usajili
za pikipiki yangu zilionekana, nilijiambia sitaitimia tena pikipiki yangu hadi
lile tukio litakaposahalika.
Zikapita tena wiki mbili.
Nilikuwa siitumii tena ile pikipiki yangu kwa kuogopa kukamatwa na polisi. Siku
hiyo nilikuwa niko kazini nikawaona polisi wawili wa usalama barabarani wakiingia.
Mfanyakazi wa kwanza waliyekutana naye niikuwa mimi.
Wakanisalimia na kuniambia
walikuwa wanamtaka Amour.
Amour nilikuwa ni mimi.
Nikasita kuwajibu. Badala
yake nikawauliza.
“Amour nani?”
“Hatujui anaitwa Amour nani,
kwani hapa kuna Amour wangapi?”
“Kuna Amour mmoja tu”
“Yuko wapi?”
“Ni mimi”
“Sasa mbona hutuambii,
unatuuliza maswali. Pikipiki yako iko
wapi?”
“Mmejuaje kama
nina pikipiki”
“Tumeelekezwa. Tafadhali
tuambie”
“Iko nyumbani”
“Ina namba hizi?”
Polisi huyo alinionesha
kikaratasi kilichokuwa kimeandikwa namba za usajili za pikipiki yangu.
“Ndiyo” nikamkubalia polisi
huyo baada ya kukiangalia kile kikaratasi.
“Tunakuhitaji wewe na hiyo
pikipiki yako”
“Mimi nina nini na pikipiki
yangu ina nini?” nikawauliza.
“Uliwahi kufanya makosa ya
barabarani wiki mbili zilizopita”
“Sijawahi kufanya kosa lolote
labda mmeifananisha pikipiki yangu”
“Tutajua huko kituo cha
polisi. Kwa sasa tutaondoka na wewe twende nyumbani kwako tuichukue hiyo
pikipiki, twende nayo kituo cha polisi”
Sikuwa na la kupinga.
Nikakakamatwa. Polisi hao ambao walikuja na gari lao walinipakia kwenye gari hilo, nikaenda nao
nyumbani kwangu.
Niliwatolea pikipiki yangu,
walipoiona tu wakasema ndiyo waliyokuwa wanaitafuta kwa karibi wiki mbili.
Nikafikishwa kituo cha
polisi. Huko ndiko nilikoelezwa kuwa tarehe fulani siku fulani nilisababisha
ajali eneo la Mabanda ya Papa baada ya kuendesha pikipiki kwa uzembe na kuvunja
sheria za barabarani.
Nikaelezwa kuwa kutokana na
uzembe wangu wa kutosimama mahali ambapo nilipaswa kusimama ili nipishe gari
lililokuwa linatoka kuliani kwangu, nilisababisha gari hilo aina ya Toyota Landa
Cruiser linikwepe na kugonga nguzo ya umeme na kutumbukia kwenye mfereji.
Ingawa nilijitahidi kukana
kosa hilo
nilifikishwa mahakamani baada ya kulala ndani kwa siku moja. Katika mahakama ya
Chumbageni nikashitakiwa kwa makosa matatu.
Kosa la kwanza lilikuwa
kuendesha kwa uzembe, kosa la pili kusababisha ajali na kosa la tatu kuharibu mali
na kulitia hasara shirika la Umeme iliyokadiriwa kufikia shilingi milioni kumi
na mbili.
Niliyakana mashitaka yote na
kumuomba hakimu anipe dhamana. Ndugu zangu walikuwa wamejitokeza kutaka
kuniwekea dhamana.
HAYA JAMANI MNAYAONA MAMBO
HAYO! NI MAKUBWA. SIJUI KAMA JAMAA ATAPEWA DHAMANA.
MH! HEBU TUNGOJE HAPO KESHO
TUONE NINI KITATOKEA. NI KATIKA BLOG YAKO HII HII YA TANGA KUMEKUCHA. KUMEKUCHA
KWELI!
No comments:
Post a Comment