Tuesday, May 24, 2016

MWANAMKE SEHEMU YA 1

Kutana tena na Faki A faki katika hadithi hii kali ya kusisimua.
 
 
Hadithi
 
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572, 0713 340572
 
MWANAMKE (1)
 
Sitausahau mwaka elfu moja mia tisa na sabini na nane. Nina sababu tatu za kutousahau mwaka huo. Sababu ya kwanza ni kuwa kulitokea vita vya Kagera. Majeshi ya Iddi Amin aliyekuwa Rais wa Uganda yalivamia nchi yetu na kusababisha maafa makubwa.
 
Kaka yangu wa kwanza alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa mstari wa mbele waliokwenda kuikomboa nchi yetu na aliuawa katika vita hivyo.
 
Sababu ya pili ya kutousahau mwaka huo ni kuwa ndio mwaka nilioanza kufanya kazi. Niliajiriwa na kampuni ya STC iliyokuwa na maduka ya ushirika nchi nzima. Na mwaka huo pia ndio nilitimiza umri wa miaka ishirini.
 
Lakini sababu ya tatu na iliyokuwa kubwa zaidi ya kutousahau mwaka huo ni kuwa nilikutana na tukio ambalo lilibadili maisha yangu.
 
Je lilikuwa tukio gani?
 
SASA ENDELEA
 
Ilikuwa februari 18 mwaka 1978. Nilikuwa mmoja wa wafanyakazi wa STC tuliokopeshwa pilipiki. Furaha yangu ikanituma kwenda kuangalia sinema. Wakati huo hakukuwa na video wala televisheni. Kulikuwa na majumba ya sinema. Kwa pale Tanga nilikokuwa naishi kulikuwa na majumba matatu ya sinema.
 
Kulikuwa na Majestic Sinema, Novelty Sinema na Regal Sinema. Majestic Sinema ndiyo iliyokuwa kubwa na maarufu zaidi na ilikuwa katikati ya jiji.
 
Mimi nilikuwa mpenzi sana wa filamu za kihindi. Filamu za kihindi zilikuwa zikioneshwa siku ya jumapili tu, yaani mara moja kwa wiki na zinakuwa zinajaza watu kuanzia wahindi wenyewe hadi waswahili.
 
Tikiti huanza kukatwa tangu asubuhi. Ukienda jioni hupati kitu. Nakumbuka filamu iliyokuwa inaoneshwa siku hiyo iliitwa Dost, ilikuwa filamu ambayo nilishapata sifa zake, hivyo kutokana na furaha ya  kupata pikipiki nikaona niende nikaione.
 
Pikipiki tulikabidhiwa siku ya jumamosi, siku ya jumapili ndio niliamua kwenda kuitazama filamu hiyo ya Dost.
 
Nilikwenda na pikipiki yangu hadi Majestic Cinema. Nikaiegesha katika eneo la kuegesha na kwenda kupanga foleni. Nilikuta foleni ndefu ya watu waliokuwa wanakata tikiti.
 
Nilifika hapo saa nne asubuhi. Mpaka nafika kwenye kidirisha cha kukata tikiti ilikuwa saa tano kasorobo. Mbele yangu kulikuwa na watu watatu. Wakimalizika wao kukata tikiti ndio inafika zamu yangu. Akaja msichana mmoja ambaye alikuwa amevaa baibui na hijabu akaniomba nimkatie tikiti.
 
Ilikuwa ni kawaida mtu kukufata ukiwa kwenye foleni na kukuomba umkatie tikiti. Hivyo sikushngaa msichana huyo ambaye sikumfahamu aliponiomba nimkatie tikiti.
 
Alikuwa anataka kunipa pesa nikakataa kuchukua pesa yake.
 
“Nitakukatia kwa pesa yangu kisha utanipa” nikamwambia.
 
“Asante kaka yangu”
 
Alikuwa na sauti nzuri ya kusisimua.
 
Wakati amebaki mtu mmoja mbele yangu, kundi la vijana wakihuni likavamia pale kwenye kidirisha na kuharibu foleni, ikawa vurugu. Mmoja wa vijana hao alinibana na kunikatia vifungo vya shati langu. Nikajaribu kutumia nguvu mpaka nikafanikiwa kukifikia kidirisha, nikakata tikiti mbili za usiku.
 
Nikazitia mfukoni tikiti hizo kisha nikaanza kumtafuta yule kijana aliyeniumiza. Nikamuona akiuza tikiti yake kwa bei ya juu kwa mhindi mmoja. Nikamkwida ukosi na kumtikisa.
 
“Wewe mshenzi umenifanya nini pale?” nikamuuliza.
 
“Hebu niache fala wewe…” akaniambia huku akiukutua mkono wangu.
 
Nikamtandika ngumi moja tu iliyomtupa chini. Damu ikawa inamtoka mdomoni.
 
Yule msichana aliyeniomba nimkatie tikiti akanifuata haraka.
 
“Usipigane” akaniambia huku akinishika bega.
 
“Angalia jinsi alivyokata vifungo vyangu”
 
Nikamuonesha yule msichana papi za shati langu ambalo lilichomoka vifungo vitatu.
 
“Basi muache”
 
Yule kijana alinyanyuka na kukimbia.
 
Nilitoa zile tikiti mbili, nikampa tikiti moja yule msichana.
 
“Asante kaka yangu, ngoja nikupe pesa zako” akaniambia.
 
Nikaona nimuachie tu.
 
“Basi usinipe pesa, nimekukatia kwa pesa zangu”
 
“Kwnini unakataa pesa?” akaniuliza.
 
“Nimekukatia mimi kama zawadi yako”
 
“Asante kaka yangu”
 
“Haya, kwaheri” nikamuaga.
 
“Basi tutaonana jioni” akakiambia kichogo changu. Nilikuwa nimeelekea kwenye mlango nikitoka.
 
Nikiwa nje ya jumba hilo nilichukua pikipiki yangu nikaondoka kurudi nyumbani.
 
Nilikuwa ninaishi eneo la Mabawa kwenye nyumba ya kupanga. Nyumba yenyewe ilikuwa na sehmu mbili. Sehemu moja nilipangisha mimi na sehemu nyingine alipangisha kujana mmoja wa kichaga aliyekuwa akifanya biashara ya duka la nguo barabara ya kumi na tatu.
 
Nilipofika nyumbani niliingiza ndani pikipiki yangu nikakaa sebuleni kwangu na kutafakari.
 
Nilikuwa sijaoa, sikuwa na mke wala mtoto. Ndiyo nilikuwa naanza maisha. Wakati huo mzazi wangu aliyebaki alikuwa mmoja, ni mama yangu. Baba yangu alikuwa ameshafariki dunia miaka miwili iliyopita.
 
Mama yangu alikuwa akiishi barabara ya tisa kwenye nyumba yetu tuliyozaliwa. Kaka yangu wa pili alikuwa akiishi eneo la Chuda na kaka yangu mwingine aliyefuata alikuwa akiishi eneo la Kwaminchi.
 
Usiku ulipowadia nilitoa pikipiki yangu nikaenda kwenye mkahawa mmoja kula chakula kisha nikaongoza njia kuelekea Majestic.
 
Nilifika Majestic saa mbili na nusu. Sinema ilikuwa inaanza saa tatu hadi saa sita usiku. Baada ya kuegesha pikipiki yangu niliingia kwenye ukumbi huo nikatafuta siti yenye namba yangu nikakaa. Mpaka imebaki dakika moja kuanza trela, siti ya upande wangu wa kulia ilikuwa tupu. Nilishuku ilikuwa siti ya yule msichana niliyemkatia tikiti kwani siti hizo zilikuwa zikifuatana na namba zilizomo kwenye tikiti.
 
Ghafla taa zikazimwa na trela ikaanza. Hapo ndipo nilipomuona msichana akiingia na kuja kukaa kwenye kile kiti kilichokuwa kitupu. Alikuwa ni yule msichana niliyemkatia tikiti. Sikujua alijuaje kuwa kiti chake kilikuwa pale. Nikawaza kwamba pengine aliwahi kuingia mapema akakiona kiti chake kisha akatoka.
 
“Tumekutana tena” akaniambia huku akitabasamu.
 
“Nilikuwa najiuliza huyu msichana yuko wapi”
 
“Nilichelewa kidogo, unajua ninaishi mbali”
 
Sikumuuliza anaishi wapi, akili yangu ilikuwa kwenye ile trela iliyokuwa ikioneshwa.
 
Sote tukawa kimya. Tuliangalia trela hadi ikaisha. Msichana alitoka, mimi sikutoka. Baada ya muda kidogo alirudi akaketi kwenye kiti chake. Mkononi alikuwa ameshika chupa mbili za soda na pakiti mbili za karanga.
 
“Chukua soda” akaniambia huku akinipa ile chupa moja.
 
Nikaipokea.
 
“Chukua na karanga”
 
Akanipa na pakiti moja ya karanga.
 
“Asante’
 
Hapo hapo taa zikazimwa na filamu ya Dosti ikaanza. Ile filamu ilikuwa ikizungumzia marafiki wawili, mmoja kipofu na mwingine mlemavu wa miguu. Ilikuwa filamu nzuri na ya kusikitisha sana. Ilikuwa na nyimbo nne. Nyimbo tatu ziliimbwa na muimbaji maarufu wa India Mohamed Rafiy ambaye kwa sasa ni marehemu na moja iliimbwa na Usha Mangesh ambaye ni dada wa Lata Mangesh.
 
Sinema ilipomalizika tuliinuka kwenye viti na kutoka. Kwa vile kulikuwa na watu wengi, nilipotoka sikumuona tena yule msichana, nikaenda kuchukua pikipiki yangu nikaiwasha na kuondoka.
 
Kutoka Majestic Cinema nilishika barabara ya Eckenford hadi bustani ya Uhuru ambapo nilikata kushoto na kushika barabara ya Pangani. Wakati nalivuka eneo la Tangamano niliona mtu akinipungia mkono mbele yangu. Alikuwa mwanamke na nilihisi likuwa anataka kuniomba lifti.
 
Kusema kweli muda ule wa usiku nilikuwa sipakii mtu nisiyemfahamu hata kama ni mwanamke. Kwa hiyo nilitaka kumpita lakini pikipiki ikazimika moto ghalfa. Mwanamke huyo akaona nilisimama kwa ajili yake, akanifuata.
 
Alipofika karibu yangu nikaona alikuwa ni yule msichana niliyekuwa naye sinema. Nikajiuliza alifikaje pale wakati nilimuacha kule Majestic?
 
 
MAMBO YAMEANZA. JE NINI KITATOKEA? USIKOSE KUENDELEA NA MKASA HUU WA KUSISIMUA MWANZO HADI MWISHO.

No comments:

Post a Comment