SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
NILIVYOGEUZWA PAKA (18)
IPOISHIA
"Shikamoo bi Chaurembo"
nikamuamkia na Chausiku naye akamuamkia
"Marahaba.Mmekuja kumuamkia
bibi yenu?"
"Hayakuhusu bibi.Sema
ulilonalo" bibi akamkatiza.
"Mh! ngoja nikae kwanza niseme
niliyonayo niondoke, maana leo bibi yenu kawa mkali. Sijui mmemletea
pesa!"
Bi Chaurembo aliketi kwenye kiti
kilichokuwa pale ukumbini
"Nimekuja kukueleza wewe gunge
kwa maana tukiona jambo ni lazima kwanza tuje tukueleze wewe.Una habari kwamba
kuna duka jipya la mwaarabu limefunguliwa jana kijijini kwetu?"
"Sina habari.Liko wapi hilo
duka?" bibi akamuuliza na kuwa na shauku ya kujua
"Liko jirani na ile shule. Nasikia
yule mwaarabu alikuwa akikaa Songe. Huko pia ana duka lakini duka amemuachia
mwanawe.Yeye amekuja kuingilia mji wetu bila taarifa.Nimepita leo nimeona duka
limejaa khanga tele na kaniki."
"Usiniambie dadaa!" bibi
akang'aka
"Utakwenda kuliona
mwenyewe.Nataka leo katika pita pita zako uende ujifanye unauliza kitu"
"Utanipeleka wewe.Ukiondioka
hapa twende mguu kwa mguu ukanioneshe hilo duka"
"Twende sasa hivi"
"Subiri wageni wangu waondoke
twende"
" Kwanza sisi hatukai bibi,
tunakwenda zetu.Nataka nikawahi kupika.Ikifika saa sita tu mume wangu anataka
kula" mke wangu akamwaambia bibi
"Ehee!" bibi akatoa
kicheko cha kajeli "Si mume wako peke yako dada, ni mume wetu
sote.Kama ikifika saa sita anataka kula, mimi nitampikia saa tano"
"Sasa nikuachie niende
zangu"
"Kila mtu na zamu yake
bibi.Zamu yangu nitakuja kuipanga mwenyewe.Atakula huku atalala huku lakini leo
nendeni zenu.Tukutane huo usiku.Nataka niende nikaliangalie hilo duka la mwarabu"
SASA ENDELEA.
Mimi na Chausiku tukaondoka
"Yule bibi yako anachekesha
sana.Ananitaka mimi ataniweza?" nikamwaambia Chausiku wakati tunaenda
"Si anakutania tu, kwani
anakutaka kweli"
"Siku moja alinivulia nguo
kabisa"
"Sasa ndiyo ungemjaribu uone
kama anakuweza"
"Anatafuta mauti
bure.........."
"Wazee wa zamani wale wamekula
miti mingi.Siku moja aliniambia ana umri wa miaka mia moja.Ameshakata karne
nzima na bado anaonekana ana nguvu"
"Ni mzee kweli lakini
anaonekana katika usichana wake alikuwa hashikiki"
Chausiku akacheka halafu akanyamaza
kimya
"Huko kwa mwarabu wanakokwenda
kunawahusu nini?" nikamuuliza Chausiku
Chausiku akanitupia jicho kali kama
vile hakufurahishwa na swali hilo
"Wenyewe wanajua"
akanijibu kwa sauti ya chini halafu akayabadili yale
mazungumzo,akaniambia "Umeona leo umeweza kugeuka paka?"
"Ni kweli,nyinyi mnadawa kali
sana "
"Bado kuna mambo mengi
atakufundisha"
"Sasa nitaweza kujigeuza paka
kila siku au ni leo tu?"
"Utaweza kujigeuza kila siku
isipokuwa ufuate masharti.Wewe ni mbishi sana "
"Masharti gani?"
"Wewe hutaki kula nyama za watu
mpaka ulazimishwe.Inatakiwa kwa mwezi ule hata mara moja na usiku utoke kama
wenzako"
“Na ile dawa uliyonirambisha
ilikuwa ni ya nini?”
“Ndiyo iliyokupa uwezo wa kujigeuza
na ile unatakiwa uirambe kila wiki”
“Na nisiporamba kila wiki sitaweza
kugeuka paka?”
“Hutaweza. Ni lazima urambe kila
wiki”
Nikanyamaza.Nilichokuwa nikiwaza ni
kuwa sikuwa na ulazima wa kuendelea kuramba dawa nisizo zielewa kwani sikupenda
kuendelea na ile tabia ya kujigeuza paka
Nilitaka kujaribu tu na nimeona
matokeo yake, imetosha. Lakini sikutaka kumwambia Chausiku mawazo yangu kwa
sababu nilijua angechukia
Tulipofika nyumbani aliingia jikoni
akapika chakula. Chakula kilipokuwa tayari tulikula kisha tukapunzika chumbani
Saa nane usiku Chausiku akaniamsha
usingizini.Nilipoamka aliniambia “Jiandae tutoke”
Usingizi ulikuwa
umenikolea.Nilitamani nikatae lakini sikuweza.Nikajilazimisha kunyanyuka
kitandani na kujiandaa kwa safari ya kwenda kiwanjani.
Tulipotoka nje akaniambia
“Sasa jigeuze paka twende”
“Wewe je?”
“Mimi pia nitajigeuza”
Nikatia nia ya kujigeuza paka na
hapo hapo nikageuka paka.Chausiku aliponiona nimekuwa paka na yeye akajigeuza
paka. Tukaenda zetu
Kabla hatujafika kiwanjani
tulikutana na mlevi aliyekuwa anakuja upande wetu.Alikuwa akitembea huku
akiyumba
Alipofika karibu yetu alisimama na
kutuambia
“Nyinyi ndiyo wanga wenyewe.Bibi na
bwana mnakwenda kuwanga!” akatuambia kama vile alikuwa anatujua
Hakuishia hapo, aliinama na kuokota
jiwe ili atupige.Nikawaza kwamba kama jiwe lile litampata mmoja wetu kichwani
ungekuwa ndio mwisho wake.Umezaliwa kama binaadamu lakini unakufa kama
paka!
Mlevi akaliinua juu lile jiwe.
Chausiku aliyekuwa mbele yangu alinyanyuka kama ngedere. Akasimama kwa miguu
miwili. Mkono mmoja akamnyooshea yule mtu na kumuambia.
“Wewe koma!”
Mlevi alipomuona paka amesimama kwa
miguu miwili na akimsemesha kama binaadamu, alilitupa jiwe na kutimua
mbio.Tulivyomuona mara ya kwanza alikuwa anayumba lakini sasa baada ya kupata
hofu aliweza kukimbia sawasawa huku akipiga kelele “Jamani
nakufaa….jamani nakufaa……!”
“Twende zetu” Chausiku akaniambia
Tukaendelea na safari
Tulipofika kiwanjani tulikuta
wenzetu wamekwisha fika.Tulikuwa sisi wawili tu tuliokuwa na miili ya
paka.Wenzetu wote walikuwa na miili ya kibinaadamu
Jinsi walivyokuwa wanawahi kufika
pale kiwanjani, nilihisi kulikuwa na wengine hawalali majumbani kwao kwa
kusubiri saa nane waje pale kiweanjani
“Nilikuwa nawasubiri nyinyi” bibi
akatuambia
“Kulikoni bibi?” Chausiku
akamuuliza.Tulikuwa bado katika maumbo yaleyale ya paka
“Nataka mimi na nyinyi na bi
Chaurembo twende katika lile duka la mwaarabu tukammwagie kimavi. Hatutaki
aweke duka lake hapa kijijini kwetu”
“Twendeni” Chausiku akamuambia
Bibi akawageukia wale wachawi
wengine tuliowakuta
“Sasa mgawanyike katika
vikundi viwili, mwende katika kazi nilizowatuma” akawaambia
Wachawi hao wakajigawa katika
vikundi viwili.Kila kikundi kikashika njia yake.
Kilibaki kikundi chetu cha watu
wanne.Bibi akamuambia bi Chauermbo na wao wajigeuze paka kama sisi twende huko
kwa mwaarabu
Hapo hapo na wao wakageuka paka.
Bibi akatuongoza njia,tukamfuata
Kama mtu yeyote angetokea usiku huo
na kutuona tulivyojipanga mstari lazima angeshuku kuwa tulikuwa wanga na
angetukimbia
Tulipofika kwenye hiyo nyumba
iliyokuwa na duka tulikuta taa ikiwaka nje.Hapo nilijifunza kitu tofauti tukiwa
na miili ya kipaka. Tulianza kucheza huku bibi na bi Chaurembo wakitoa sauti za
kipaka zinazotisha
Baada ya kucheza kwa karibu dakika
tano, tulianza kujipenyeza ndani ya duka hilo.Alianza bibi, akafuatia bibi
Chaurembo, halafu mimi na Chausiku. Bibi na bi Chaurembo pamoja na mke wangu
walilisotea duka hilo na kujaza kinyesi kila mahali.Wakati wakifanya hivyo
walikuwa wakitoa sauti za kunuizia kuharibu biashara katikia duka hilo
“Tunalisotea duka hili liingie
nuksi, mwarabu asipate biashara.Asije mtu yeyote kununua kitu hapa.Duka hili
life kabisa na mwenyewe afilisike arudi kwao……..”
Ndiyo maneno waliyokuwa wakisema
bibi na bi Chaurembo kwa sauti zao za kipaka bila kujali kama kelele zao
zilikuwa zinasikiwa.
Tulipotoka hapo dukani tulijipenyeza
ukumbini. Huku nako bibi na bi Chaurembo walieneza kinyesi
“Sasa twendeni zetu.Kesho tukija
tutawaingilia vyumbani tuwawangie mpaka wahame” bibi akatuambia
Tukarudi kwenye duka kisha tukatoka
na kurudi kiwanjani
Tulipofika kiwanjani bibi akajigeuza
mtu na kuanza kucheka.Chausiku naye akageuka mtu, nikafuatia mimi kisha bi
Chaurembo
Vilikuwa vicheko vitupu.Mimi tu ndio
sikuwa nikicheka.Sikuona la kunifurahisha. Bibi na bi Charembo wakawa
wanajisifia kuwa watamuonyesha yule mwarabu
Kumbe wachawi baada ya kufanya uovu
hufurahia kwa vicheko kama watu waliofanya jambo la maana lenye kuleta tija.
Wachawi wenzetu walipofika, kila
kikundi kikawa kinahadithia juu ya kazi waliyokwenda kuifanya.Baadaye bibi
akawapa pongezi kisha akaamrisha tucheze ngoma.Tukacheza ngoma yetu ya kichawi.
No comments:
Post a Comment