SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
MWANAMKE 4
Ilipoishia
Nilikuwa nikilitupia macho
lile jumba, nikataka kumuuliza alikuwa amepangisha chumba au alikuwa akiishi
kwao. lakini nilishindwa kumuuliza ili asione ninayachunguza maisha yake.
“Nimepaona” nikamjibu.
“Karibu ndani” akaniambia.
“Asante”
“Karibu” Msichana
akanisisitizia.
“Hapa panatosha” nikamwambia
nikiwa nimekaa kwenye pikipiki yangu.
“Unataka uishie nje, si
vizuri. Tuingie ndani. Ninaishi peke yangu tu usiogope”
“Unaishi peke yako humu
ndani?” nikamuuliza.
“Nimejenga mwenyewe kutokana
na biashara zangu na ninaishi mwenyewe. Msichana aliniambia huku akifungua
geti.
“Karibu”
Kwa jinsi alivyokuwa
akinibembeleza ilibidi nishuke kwenye pikipiki. Niliposhuka tu msichana
aliishika pikipiki yangu akaikokokota na kuiingiza ndani, nikawa namfuata
nyuma.
Tulipoingia ndani msichana
aliiegesha pikipiki kando ya mti mkubwa uliokuwa umeota katika ua wa jumba hilo. Aliiacha pikipiki
akaenda kufunga geti.
“Karibu” akaniambia huku
akitangulia kwenda kwenye mlango wa kuingilia kwenye jumba hilo. Nikamfuata.
SASA ENDELEA
Alifungua mlango
akanikaribisha tena, tukaingia ndani. Tulitokea kwenye sebule pana iliyokuwa na
makochi ya chini chini ambayo hutumiwa zaidi na watu wenye asili ya kiarabu. Ilikuwa sebule iliyonakishiwa na
kupendeza.
“Karibu ukae” akaniambia.
Nikaa kaa kwenye kochi mojawapo.
“Nikuletee kinywaji gani, cha
moto au cha baridi” akaniuliza.
“Hapana, sihitaji kinywaji
chochote” nikamwambia.
Msichana akanitazama na
kukunja uso kisha akaondoka hapo sebuleni. Nikajua kuwa amekwenda kunichukulia
kitabu changu ili niondoke.
Baadaye kidogo akarudi.
Alikuwa ameshika chano kilichokuwa na kijibiika kidogo na vikombe viwili vya
kahawa. Chano hicho pia kilikuwa na kisahani kilichokuwa na tende.
Akakiweka chini mbele yangu.
Yeye mwenyewe alikuwa
amevua
baibui na kubaki na dera la mikono mirefu lililoziba kabisa miguu yake.
Dera hilo lilikuwa limedariziwa nyuzi zilizokuwa zikimemeta kama hariri.
Pia alikuwa ameiondoa hijabu
na badala yake alijitanda mtandio mwepesi uliokuwa unaonya. Uso wake uliweza
kuonekana vizuri. Nywele zake ndefu za maboga kama
za kiarabu zilikuwa zimefikia kwenye mabega yake.
“Karibu” akaniambia na
kuongeza.
“Kunywa kahawa kidogo. Kahawa
inachangamsha”
Sikupenda kuikataa ile
takirima ingawa nilimwambia sikuhitaji kinywaji chochote.
Msichana akaketi chini karibu
yangu akachukua kile kibirika na kunimiminia kahawa kisha akajimiminia na yeye.
Alichukua kikombe hicho
akaionja kahawa kisha akakirudisha chini na kuokota tende moja na kuitia
midomoni.
Na mimi niliokota tende
kwanza, nikaitia midomoni kisha nikainua kikombe cha kahawa kusukumizia.
“Wewe una asili ya kiarabu?”
nikamuuliza.
“Nimechanganya uarabu na
uswahili”
‘Muarabu ni baba yako au mama
yako?”
“Baba yangu ni muarabu wa
Ajemi, mama yangu ndio amechanganya. Zamani tulikuwa tunaishi Zanzibar”
“Sasa wazazi wako wako wapi?”
nikamuuliza baada ya kutoa kokwa ya tende mdomoni.
“Iweke hapo kwenye sinia”
aliniambia akinionesha kile chano.
Nikaiweka ile kokwa kwenye
chano hicho kisha nikaokota tende nyingine.
“Baba yangu yuko Zanzibar na mama yangu
yuko Ajemi” akaniambia.
“Kwa hiyo wewe unaishi hapa
peke yako?” nikamuuliza.
“Ninaishi peke yangu”
Msichana akanikubalia kwa haraka.
“Uliniambia hii nyumba
uliijenga mwenyewe kwa biashara zako, unashughulika na biashara gani?”
“Ninauza madini”
“Madini gani?”
“Madini ya kila aina”
“Unayapata wapi?”
“Baba yangu ananiletea kutoka
Zanzibar”
“Yeye anayapata wapi?”
Msichana akabetua mabega
yake.
“Sijui anayapata wapi”
“Ninavyojua mimi Zanzibar hakuna madini”
“Hayatoki Zanzibar, anayapata
kutoka nje ya Zanzibar
lakini sio Afrika ila mahali penyewe sipafahamu na hajawahi kuniambia”
“Ndiyo yamekuwezesha kujenga
nyumba hii?”
“Ndiyo”
“Hongera sana. Sasa kwanini unaishi peke yako?”
“Sijapata mwenzangu wa kuishi
naye”
Kahawa aliyonitilia kwenye
kikombe nikaimaliza. Akataka kuniwekea nyingine, nikamwambia.
“Imetosha, asante sana”
“Ngoja nikakuchukulie kitabu
chako” akaniambia huku akiinuka. Macho yangu yalimsindikiza hadi alipotoka
mlangoni.
Kusema kweli baada ya
msichana huyo kuondoka sikujua tena kilichotokea kwani usingizi ulinipitia hapo
hapo bila kutarajia. Nikalala fofofo.
Nilipokuja kuzinduka
nilijikuta nimekaa peke yangu mahali pale pale nilipokuwa. Kile chano cha
kahawa na tende kilikuwa kimeondolewa. Kwa kutaka kujua ilikuwa ni saa ngapi
nilitazama saa yangu ya mkononi, nikaona ilikuwa saa tisa kasorobo ya usiku.
Nikashituka sana kuona nilikuwa nimelala nyumbani kwa
msichana huyo hadi muda huo. Nikataka kuinuka ili nimuite mwenyeji wangu ambaye
sikujua alikuwa wapi.
Kabla ya kuinuka nikaisikia
sauti yake ikitoke nje ya dirisha la kile chumba. Kisha nilisikia sauti nyingine ya kiume
ikijibishana naye. Sauti ile ya kiume ikanishitua kwa sababu yule mwanamke
aliniambia alikuwa akiishi peke yake mle ndani.
Nikapenua pazia nakuchungulia
uani. Nikaiona pikipiki yangu niliyokuwa nimeiegesha kando ya mti. Mbele ya pikipiki niliona kitu
kama kisima cha maji. Wakati tunaingia mle
ndani kisima hicho sikukiona.
Maji yaliyokuwa kwenye kisima
hicho yalikuwa mekundu kama damu na yalikuwa
yakitoa harufu ya damu ya binaadamu mpaka nikahisi yalikuwa ni damu kweli.
Ndani ya kile kisima kulikuwa
na watu wawili waliokuwa wakioga na ndio waliokuwa wakizungumza. Mmoja akatoka
na kusimama kando
ya kisima hicho. Mara moja nikatambua kuwa ni yule mwenyeji wangu lakini safari
hii alikuwa na umbile la kutisha sana.
Kwanza nywele zake zilikuwa nyingi na ndefu zilizoteremka na
kumfikia kiunoni. Zilikuwa nywele nyeupe kama
mvi za bi kikongwe. Yeye mwenyewe ngozi yake ilibadilika na kuwa nyeupe kama ya mzungu. Macho yake yalikuwa ya kijivu na mboni
zake zilikuwa nyembamba na zilizosimama kama
mboni za paka.
Bado alikuwa ameota manyoya
marefu mwili mzima. Nikagundua kwenye miguu yake hakuwa na vitanga vya miguu
kama walivyo binaadamu wote bali alikuwa na kwato nyeusi kama
za farasi au punda. Hakuwa amevaa chochote. Alikuwa uchi wa mnyama!
Mwenzake naye akatoka kwenye
kisima. Yeye alikuwa mwanaume lakini alikuwa na umbile kama
la yule msichana. Miguu yake pia ilikuwa na kwato.
Walikuwa wakizungumza kwa
lugha ambayo sikuielewa. Kwa kweli nilishituka sana. Nikapata hofu
na uoga mpaka mwili wangu ukawa
unatetemeka.
Nikahisii kwamba yule
msichana aliyenikarisha mle ndani hakuwa binaadamu bali alikuwa jini na pale
alikuwa akizungumza na jini mwenzake.
Nikatengeza mawazo kwamba
huenda msichana yule aliniingiza katika nyumba ile kwa hila ili wanidhuru kwani
ile damu iliyokuwa kwenye kile kisima ilikuwa ni ya binaadamu kama
mimi. Na bila shaka waliingizwa mle ndani na kuuawa kikatili.
Hapo ndipo
nilipochanganyikiwa nikajua kwamba dakika zangu za kuishi zilikuwa zimekaribia
kwisha.
HAYO NDIO MAMBO YA BlOG YA tangakumekucha. SASA KUMEKUCHA KWELI. Sijui
jamaa atafanya nini? Kesho si mbali. Tuombe Mungu atuweke hai tukutane tena hapa
hapa.
No comments:
Post a Comment