Sunday, May 22, 2016

SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU YA 22

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI, 0715 772746
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 22
 
ILIPOISHIA
 
Nilipoisikia sauti yake nilitoka mle mvunguni nikapanda juu ya lile kabati na kutulia kimya.
 
“Nataka sigara” Yule bibi alikuwa akimwambia yule mwarabu huku akimpa pesa.
 
“Unataka sigara gani?” mwarabu akamuuliza.
 
“Nataka sigara kali mbili”
 
Pesa aliyotoa yule bibi haikuwa pesa. Kilikuwa ni kihirizi kilichogeuzwa kimazingara na kuonekana kama sarafu ya shilingi mia mbili.
 
Nikagundua kuwa kilikuwa kihirizi cha kukopera pesa. Kama mwarabu huyo angeipokea kwa kudhani ni pesa na kisha akaichanganya kwenye pesa zake, baada ya muda pesa zake zote zingeyayuka na kwenda kwa bibi huyo.
 
Wakati bibi huyo anampa mwarabu hiyo sarafu hiyo, niliwahi kuirukia nikaishika na kuiweka pale juu ya kabati. Nilipoiweka tu ikageuka kihirizi.
 
Hakuwa mwarabu tu aliyeshangaa, hata yule bibi alishangaa. Licha ya uchawi wake, hakuwa amenitambua kuwa sikuwa paka wa kawaida.
 
Nikasimama kwa miguu miwili kisha nikamuungurumia yule bibi kwa ukali.
 
Nilikuwa nikimwambia.
 
“Wewe bibi ni mchawi. Leo nitakuumbua!”
 
SASA ENDELEA
 
Niliamini kuwa alinisikia kwani nilimsikia akiguna kisha akasema.
 
“Naona leo mambo yameharibika, ngoja niondoke!”
 
Akageuka na kuondoka.
 
“Wewe bibi hebu njoo, umeacha nini hapa” Mwarabu akampigia kelele.
 
Bibi akayoyoma. Mwarabu akatoka kwenye duka kumfuata. Na mimi nikaruka chini na kutoka kwenye lile duka. Yule bibi hakuonekana tena. Mwarabu akashangaa na kurudi dukani kwake. Aliitazama ile hirizi kisha aliingia ndani. Na mimi nikamfuata.
 
Mke wake alikuwa amekaa ukumbini akifuma vitambaa.
 
“Leo nimeona mambo ya ajabu sana!” akamwambia mke wake.
 
“Mambo gani?” mwanamke huyo akamuuliza.
 
Mwarabu akamueleza kuhusu lile tukio lililotokea. Khaleed alikuwa chumbani, aliposikia yale maneno naye akaja ukumbini.
 
“Kiko wapi hicho kihirizi?” mwanamke huyo akauliza.
 
Niliposikia hivyo nilikimbilia kule dukani nikapanda juu ya kabati na kuking’ata kile kihirizi, nikaenda nacho pale ukumbuni nikakibwaga chini.
 
Kitendo kile kikazidi kuwashangaza wale watu.
 
“Huyu paka ni kama anasikia, amekwenda kuileta” mwarabu akasema na kuongeza.
 
“Hirizi yenyewe ndiyo hiyo aliyoileta”
 
“Basi huyu paka si wa kawaida na yule bibi bila shaka alikuwa mchawi” mwanamke huyo akasema.
 
“Inawezekana yule bibi ni mchawi na alitaka kunifanyia kitu ambacho si kizuri, huyu paka ndiye aliyemkimbiza. Hawa wanyama wanaona mengi” Mwarabu akamwambia mke wake.
 
Nikaing’ata ile hirizi. Khaleed aliponiona akapiga kelele.
 
“Baba unaona anataka kuila!”
 
Khaleed alitaka kunipiga teke ili niiachie ile hirizi, baba yake akamzuia.
 
“Hebu muache tuone anataka kuifanya nini?”
 
Nilipoing’ata hirizi hiyo nilikwenda nayo uani. Nilikuta jiko la mkaa likiwa na moto. Mwarabu, mke wake na Khaleed wakanifuata uani.
 
Nikaruka juu ya lile jiko kisha nikaiachia ile hirizi ikaingia kwenye moto na kuungua. Mimi mwenyewe nikaangukia upande wa pili wa jiko.
 
“Ona baba ameichoma na moto!” Khaleed akasema kwa mshangao.
 
“Huyu paka si wa kawaida. Hakuna paka wa aina hii!” Mwarabu akasema kisha akainua mikono juu kuomba Mungu akasema.
 
“Kama wewe ni paka, umepewa kipaji basi ni kazi ya Mungu. Lakini kama wewe si paka, nakuomba mwenyezi Mungu tubainishie mara 22”
                                                    
Mara baada ya yule mwarabu kuomba ile dua,  nikaona umbo langu linabadilika. Lile umbo la paka likanitoka na umbile langu la kibinaadamu likanirudia!
 
Lakini nikajikuta nipo uchi wa mnyama mbele ya mwarabu huyo na mke wake na mtoto wao!
 
Mke wa mwarabu huyo pamoja na Khaleed walipoona hivyo walishituka wakatimua mbio kurudi ndani. Baba mtu ndiye aliyebaki hapo akiwa amenikazia macho.
 
Pale uani palikuwa na kamba ya kuanika nguo na kulikuwa na taulo iliyoanikwa. Nikaichukua na kujifunga kiunoni.
 
“Wewe ni nani?” mwarabu akaniuliza kijasiri.
 
“Mimi ni binaadamu kama ulivyo wewe, wewe ndio uliyeniapiza jana usiku nikabaki kuwa na umbile la paka” nikamwambia yule mwarabu.
 
Maneno yangu yalimshangaza, akaniuliza.
 
“Mimi ndiye niliyekuapiza jana usiku ukabaki na umbile la paka?”
 
“Hukumbuki jana usiku wakati unaswali chumbani kwako alikuja paka?”
 
“Ndiyo nakumbuka”
 
“Ukasema kama wewe ni mwanga utabaki kuwa paka daima”
 
“Kumbe ulikuwa ni wewe?” mwarabu akaniuliza kwa mshangao.
 
“Nilikuwa mimi”
 
“Kumbe wewe ni mwanga”
 
“Napenda nianze kukusimulia kisa changu kilichosababisha nifike kwako nikiwa na umbile la paka” nikamwambia Yule mwarabu.
 
“Haya nisimulie”
 
Nikaanza kumsimuliza. Nilimuanzia mwanzo nilivyojuana na Chausiku tulipokuwa shule mpaka tukapeana ahadi ya kuoana.
 
Nikamueleza jinsi nilivyooa mke mwingine nilipofika Handeni baada ya kupata kazi na jinsi nilivyokutana tena na Chausiku na kumueleza kuwa nimeshoa mke mwingine.
 
Nikaendelea kumueleza jinsi mke wangu alivyouawa kwa kuchomwa kisu na mimi kulazimika kukimbia Handeni na kuja pale kijijini na kumuoa Chausiku.
 
“Niligundua kuwa Chausiku alikuwa mchawi na siku nilipomgundua alinilazimisha na mimi nijiunge katika kundi lao. Nilipokataa akaniambia kwamba atakwenda kunitolea ripoti polisi kuwa  nimemuua mke wangu wa kwanza na kukimbilia kwake.
 
“Hapo nilipatwa na mshituko pamoja na mshangao. Nilijiuliza amejuaje kuwa mke wangu aliuawa na kwamba polisi walikuwa wakinitafuta mimi wakati jambo hilo sikumueleza” nikamueleza muarabu huyo.
 
Nikamueleza jinsi nilivyolazimika  kujiunga katika  kundi hilo la wachawi ili mke wangu asiende kuniripoti polisi na mimi nikawa nachukuliwa kwenda sehemu mbalimbali ambazo wachawi hao walikuwa wanakwenda kuwachawia watu usiku.
 
Nikamdokeza kuwa yule bibi aliyekuja dukani alikuwa ndiye kiongozi wa wachawi hao.
 
“Kama ile hirizi ungeichanganya na pesa zako, pesa zako zote zingeyayuka na zingekwenda kwa yule bibi” nikamwambia.
 
Hapo nilimuona yule mwarabu akitikisa kichwa kusikitika.
 
“Sasa Jana usiku ndio tulifika kwako tukiwa katika maumbile ya paka. Wewe uliponiona ukaniapiza na kweli maapizo yako yakafanya nishindwe kujibadili na kuwa binaadamu.
 
“Mke wangu alinitesa sana. Alinitia kwenye kapu na kwenda kunitupa. Nikajitahidi kurudi nyumbani. Aliponiona tena alinifungia chumbani na kuhama nyumba. Nilitoka kwa kupanda juu nikaenda kumtafuta.
 
“Nikamkuta katika nyumba moja akiongea na rafiki yake. Alikuwa akimueleza kuwa yeye ndiye aliyemuua mke wangu wa kwanza kwa kumchoma  kisu ili mimi niende nikamuoe yeye. Jambo hilo lilinishangaza sana. Basi nikamrukia na kumtoboa jicho kisha nikakimbia na ndio nikafika hapa kwako” Nikamaliza kumuelezea yule muarabu mkasa huo.
 
Je mwarabu huyo atachukua uamuzi gani na nini kitatokea? Endelea kufuatilia mkasa huu katika blog yetu hii hapo kesho.
 
TANGU SASA ANZA KUWA MTEJA WA TANGA KUMEKUCHA  Kuna  vitu huku!!!

No comments:

Post a Comment