SIMULIZI A FAKI A FAKI 0713
MWANAMKE 6
ILIPOISHIA
“Mzee samahani, naomba msaada
wako” nikamwambia.
“Msaada gani?”
“Mimi sijui nilivyofika hapa,
ninaomba unioneshe njia ya kutoka nje”
“Unasema hujui ulivyofika
hapa?”
“Sijui, nimejiona tu
nikitokea katika nyumba hii”
“Kwani unatoka wapi?”
“Ninatoka katika nyumba ya
msichana mmoja ambaye nilimuazima kitabu changu, wakati ule natoka nikaona nimetokea kwenye pango. Baadaye tena
naona nimetokea kwenye nyumba hii”
“Wakati unatoka ulimuaga
mwenyeji wako?”
“Sikumuaga”
“Kwanini hukumuaga?”
Hapo nikanyamaza kimya,
sikuwa na jibu. Nilishindwa kumueleza niliyoyaona kwa sababu yule mzee naye sikujua
alikuwa ni nani.
Pakapita kimya cha sekunde
kadhaa. Yule mzee alikuwa akinitazama akisubiri jibu langu na mimi nilikuwa
nikimtazama uso wangu ukiwa
umenywea ukionesha
sikuwa na jibu.
“Ulifanya kosa kutomuaga
mwenyeji wako na ndio sababu unahangaika. Siku nyingine usirudie kosa kama hilo” Yule mzee
akaniambia.
SASA ENDELEA
Akanyamaza kimya kisha
akanimabia.
“Mlango huu hapa, nenda zako”
Alinionesha mlango uliokuwa
ubavuni kwake.
“Asante
sana,
nashukuru” nikamwambia huku nikivuta hatua kuelekea kwenye mlango huo.
Mzee alikuwa akinitazama.
Niliufungua ule mlango
nikatazama nje na kutoka. Nilipotoka nikajiona niko nje ya nyumba ya Zena! Jambo
hilo lilinipa
mshangao lakini nilishukuru nikaanza kutoka mbio nikiwa pekupeku. Sikukumbuka
tena ile pikipiki yangu.
Nilikimbia kwa miguu nikiwa
peke yangu usiku ule katika njia iliyokuwa na vichaka vinavyotisha. Vivuli vya miti
iliyokuwa ikitikiswa na upepo vilizidi kunitisha lakini sikuwa na la
kufanya, nilikuwa nimeshajitolea.
Baada ya nusu saa nikawa nimefika
kwenye barabara ya lami nikakata kushoto na kuendelea kukimbia. Nilipokuwa
ninakikaribia kituo cha polisi cha Mabawa nikaanza kuchoka. Nguvu zilikuwa
zimeniishia kabisa.
Nilisimama huku nikitweta.
Nikatazama nyuma. Kulikuwa kimya. Kile kituo cha polisi kilinipa matumaini
nikaanza kutembea taratibu. Nilikipita kituo
hicho nikaendelea kutembea hadi nikafika nyumbani kwangu.
Nilifungua mlango nikaingia
nyumbani kwangu. Mwili wote ulikuwa unaniuma. Shati langu lilikuwa limeloa kwa
jasho. Nilivua nguo nikaenda kuoga. Niliporudi chumbani kwangu nikasikia
dirisha langu linagongwa.
Nilikuwa nimeshazima taa na kupanda kitandani.
Nikatega masikio yangu kusikiliza. Dirisha liliendelea kugongwa.
“Amour! Amour!” Sauti ya
kiume ikawa inaita jina langu.
Nilijaribu kuifikiria ilikuwa
sauti ya nani lakini sikuweza kutambua ilikuwa sauti ya nani miongoni mwa watu
niliokuwa nawafahamu. Nikaamua kunyamaza kimya.
Sauti ile ikaendela.
“Amour fungua mlango
nimekuletea viatu vyako na funguo za pikipiki yako”
Nilishituka niliposikia
maneno yale nikajua mtu aliyekuwa akiniita alitoka kule kwa Zena ambako
niliacha pikipiki yangu na viatu vyangu.
Nikajiambia kwa vyovyote vile
atakuwa si mtu bali ni jini. Hofu
yangu ilianzaa tena upya. Moyo ukaanza
kunienda mbio.
Dirisha liliendelea kugongwa
na ile sauti ikaendelea kuniambia nifungue mlango nichukue viatu vyangu pamoja
na funguo za pikipiki yangu niliyoiacha kwa Zena.
Sikujibu chochote,
nikaendelea kubaki kimya.
Baada ya muda kidogo ile
sauti ikapotea, kukawa kimya. Nikasubiri kuona kama
kutatokea kitu chochote, sikuona kitu. Nikaendelea kuwa macho huku hofu ikiwa imenitawala
hadi nikapitiwa na usingizi.
Nilichelewa sana kuamka asubuhi. Nilishukuru kuwa ilikuwa
ni jumapili siku ambayo ni ya mapumziko, vinginevyo ningechelewa kufika kazini.
Mara tu niliposhuka kitandani
nilitazama saa. Ilikuwa saa mbili na robo.
Nikatoka nje nikiwa nimejifunga taulo. Wakati nafungua mlango wa mbele nikaona
viatu vyangu nilivyoviacha kwa yule msichana, vimewekwa mbele ya mlango wangu
pamoja na funguo za pikipiki yangu. Nikashituka.
Wakati huo mpangaji mwenzangu
wa upande wa pili alikuwa anatoa pikipiki yake. Nikamuita.
“Alphonce!”
Alphonce akanifuata na
kunisalimia.
“Kuna tatizo limenitokea”
nikamwambia.
“Tatizo gani?” akaniuliza.
“Unaviona hivi viatu?”
“Ninaviona”
“Sasa njoo ndani nikueleze
mkasa ulionitokea jana usiku”
Alphone akiwa amepatwa na
mshangao aliigesha pikipiki yake karibu na mlango wangu akaingia ndani.
Nilimkaribisha sebuleni kwangu. Vile viatu na funguo za pikipiki yangu nilikuwa
nimeviondoa pale mlangoni.
“Haya nieleze kuna nini?”
Alphonce akaniuliza.
Nikamueleza ule mkasa
ulionitokea usiku uliopita uliosababisha nirudi nyumbani kwangu usiku nikiwa
pekupeku.
“Wakati nimerudi niko
chumbani kwangu, nikasikia sauti ya mtu kwenye dirisha akiniambia ameniletea
viatu vyngu na funguo za pikipiki. Kwa kweli sikumjibu. Nilinyamaza kimya”
Wakati ninamueleza Alphonce
alikuwa ameshangaa
kweli kweli.
“Halafu ikawaje?” akaniuliza.
“Baada ya kunyamaza kimya ile
sauti sikuisikia tena, sasa hii leo asubuhi nafungua mlango nakuta viatu vyangu
na funguo za pikipiki yangu vimewekwa mbele ya mlango wangu”
“Una maana yule mwanamke
alikuwa ni jini?”
“Alikuwa jini”
“Na huyo aliyekuletea hivyo
viatu na funguo ni nani?”
“Sijui, lakini watakuwa ni
wamoja”
“Unajua mimi huwa nazisikia
habari za majini lakini siamini kama kuna
viumbe hao. Unaonaje kama tutakwenda mimi na wewe kwenye hiyo nyumba?’
“Mimi nilikuwa nimepanga
kwenda polisi kwa sababu ya pikipiki yangu”
“Twende huko Mikanjuni
kwanza, kama pikipiki yako hutaipata ndio
utakwenda polisi kwa ajili ya kupata msaada zaidi”
“Sawa. Subiri nivae tutoke”
“Nitakusubiri”
Nikanyanyuka na kuingia
chumbani kwangu. Baada ya nusu saa nikatoka nikiwa nimeshavaa.
“Twende” nikamwambia Alphonce.
Tukatoka. Alphonce alinipakia
kwenye pikipiki yake tukaelekea Mikanjuni. Nilimuelekeza mahali ilikokuwa ile
nyumba ya yule msichana, tukaenda hadi mahali hapo lakini jambo la ajabu
lililotokea ni kuwa ile nyumba hatukuiona. Badala yake tuliona eneo lote
lilikuwa makaburi matupu ya watu wa zamani.
Nikapatwa na mshangao. Wakati
naangalia angalia nikaiona pikipiki yangu ikiwa kando ya mti. Mti huo ndio ule uliokuwa uani
mwa nyumba ya Zena. Kando
yake palikuwa na kisima ambacho yule msichana na mwenzake walikuwa wakioga.
Wakati ule kile kisima
hakukuwepo tena, badala yake tuliona dimbwinl maji ya mvua.
“Pikipiki yangu ile pale!”
nikamwambia Alphonce ambaye naye alikuwa ameshangaa.
“Sasa mbona iko kwenye
makaburi na hapana nyumba?” akaniuliza.
“Na mimi ndio nashangaa. Ile
pikipiki niliiweka uani mwa hiyo nyumba niliyokwambia. Ule mti unaouona ulikuwa
uani na lile dimbwi la maji kilikuwa ni kisima”
“Hebu twende pale karibu”
JE WAKIFIKA HAPO KARIBU
WATAONA NINI? HUU NI MKASA WA KUSISIMUA SANA
AMBAO WEWE MSOMAJI WA BLOGY HII HUTAKIWI KUUKOSA. SASA ANZA KAWAIDA YA
KUTEMBELEA BLOG HII KILA SIKU BILA KUKOSA NA MWAMBIE NA MWENZAKO USIFAIDI PEKE
YAKO. Kila mnapokuwa wengi ndio mimi hufurahi.
No comments:
Post a Comment