Atakeyehusisha watoto na dawa za kulevya jela miaka 30
Dar es Salaam.
SERIKALI imesema kuwa mtu yeyote
atakayekamatwa kwa kosa la husisha au kushawishi mtoto kujiingiza katika
matumizi au biashara ya dawa za kulevya atahukumiwa kifungo cha miaka
isiyopungua 30.
Hayo yamesema na Mkuu wa Kitengo
cha Elimu, Habari na Takwimu wa Tume ya kuratibu na kudhibiti wa Dawa za
Kulevya, Amani Msami kupitia Taarifa ya tume hiyo kwa vyombo vya
habari.
Msami alisema adhabu hiyo ni kwa
mujibu wa Sheria ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Na.5 ya
mwaka 2015 tofauti na Sheria ya Kuzuian Biashara Haramu ya Dawa za
Kulevya Na. 9 ya mwaka 1995 iliyokuwa na mapungufu.
Alisema mbali na adhabu hiyo,
sheria hiyo mpya imeweka adhabu ya kifungo cha maisha na faini ya
shilingi Milioni 200 kwa kumiliki mitambo ya kutengeneza dawa za
kulevya.
Msami aliongeza kuwa Sheria hiyo
pia imeweka adhabu kali ya kifungo cha maisha pamoja na faini
isiyopungua Shilingi Bilioni moja kwa watu wanaofadhili biashara ya Dawa
za Kulevya.
“Aidha, sheria hii imeweka adhabu
kali ya kifungo cha maisha pamoja na faini isiyopungua Shilingi Bilioni
moja kwa watu wanaofadhili biashara ya Dawa za Kulevya ambao mara
nyingi ni watu wenye uwezo,”alisema Msami.
Mkuu huyo wa Kitengo, alisema
Serikali kupitia vyombo vya Dola iliwabaini, kuwakamata na kuwachukulia
hatua za kisheria baadhi ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa dawa za
kulevya.
Aliwataja baadhi ya watuhumiwa
wakubwa wa dawa hizo waliokamatwa na kuchukuliwa hatua kuwa ni Ali
Khatibu haji (maarufu kwa jina la Shkuba, Mohammed Mwarami (maarufu kwa
jina la Chonji na Mwanaidi Mfundo (maarufu kwa jina la Mama Leila).
Msami alisisitiza wito wa
Serikali kwa wananchi kutoa ushirikiano wa dhati kwa ajili ya kutoa
taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa ya kulevya ili
waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment