Simulizi za faki a faki 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 23
ILIPOISHIA
Nikamdokeza kuwa yule bibi
aliyekuja dukani alikuwa ndiye kiongozi wa wachawi hao.
“Kama ile hirizi
ungeichanganya na pesa zako, pesa zako zote zingeyayuka na zingekwenda kwa yule
bibi” nikamwambia.
Hapo nilimuona yule mwarabu
akitikisa kichwa kusikitika.
“Sasa Jana usiku ndio
tulifika kwako tukiwa katika maumbile ya paka. Wewe uliponiona ukaniapiza na
kweli maapizo yako yakafanya nishindwe kujibadili na kuwa binaadamu.
“Mke wangu alinitesa sana.
Alinitia kwenye kapu na kwenda kunitupa. Nikajitahidi kurudi nyumbani.
Aliponiona tena alinifungia chumbani na kuhama nyumba. Nilitoka kwa kupanda juu
nikaenda kumtafuta.
“Nikamkuta katika nyumba moja
akiongea na rafiki yake. Alikuwa akimueleza kuwa yeye ndiye aliyemuua mke wangu
wa kwanza kwa kumchoma kisu ili mimi
niende nikamuoe yeye. Jambo hilo lilinishangaza sana. Basi nikamrukia na
kumtoboa jicho kisha nikakimbia na ndio nikafika hapa kwako” Nikamaliza
kumuelezea yule muarabu mkasa huo.
SASA ENDELEA
Mke wake na mwanawe waliokuwa
wamekimbia walikuwa wamesogea karibu na kunisikiliza.
Mwarabu baada ya kukisikia
kisa changu alitaharuki sana akaniambia.
“Huyo mke wako ni mtu mbaya
sana. Sasa umesharudi katika umbile lako la kibinaadamu utamchukulia hatua
gani?”
“Nataka niende polisi Handeni
nikatoe ripoti kuwa yeye ndiye aliyemuua mke wangu”
“Kwa vile hiki kisa
kimenigusa sana, mimi niko tayari kukupatia nguo na kukusindikiza hadi Handeni
uende ukamripoti mke wako”
Dakika chache baadaye mimi na
mwarabu huyo tukawa kwenye basi linalokwenda Handeni. Alikuwa amenipa shati na
suruali.
Tulipofika Handeni tulikwenda
kituo cha polisi.
Polisi walipotuuliza tuna
shida gani, niliwaeleza kuhusu lile tukio la mauaji ya mke wangu wa kwanza ambalo lilitokea
karibu miaka miwili iliyopita.
Kwa vile niliwatajia jina la
marehemu, tarehe, mwezi na mwaka aliouawa, mara moja walilipata faili lake.
Baada ya kulisoma faili hilo polisi hao waliniambia.
“Mtuhumiwa ni mume wake na
tunaendelea kumtafuta”
“Mume wake nilikuwa mimi.
Marehemu aliuawa na msichana anayeitwa Chausiku” nikawambia.
“Wewe ndiye uliyekuwa mume
wake?” Polisi mmoja akaniuliza kwa kutaharuki.
Kabla sijamjibu akaniambia
“Wewe ndiye tuliyekuwa tunakutafuta!”
Mwarabu kusikia hivyo
aliingilia kati akawaeleza polisi jinsi tukio
hilo lilivyotokea.
“Tuna sampuli za alama za
vidole tulizozipata kwenye kisu kilichotumika katika mauaji. Tutachukua alama
zako sasa hivi” Polisi wakaniambia.
“Sawa chukueni tu”
“Hukugusa kile kisu?” Polisi
mmoja akaniuliza.
“Hapana, sikukigusa”
Alama zangu za vidole
zilichukuliwa na kwenda kulinganishwa na alama zilizokuwa zimehifadhiwa. Baada
ya muda jibu lilikuja kwamba alama zangu sizo zilizokuwemo katika kisu
kilichotumika kumuua marehemu.
Hapo hapo polisi sita wakiwemo polisi wawili
wamawake na mimi pamoja na Mwarabu tulipakiwa katika gari la polisi tukaenda
kijijini kumkamata Chausiku.
Lakini Chausiku hakupatikana
kijijini. Tuliambiwa kuwa alikuwa amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Handeni
baada ya jicho lake moja kutobolewa na paka.
Paka mwenyewe nilikuwa mimi!
Tukarudi tena Handeni hadi katika hospitali ya wilaya.
Tulimkuta Chausiku amelazwa wodini, jicho lake moja likiwa limefungwa bendeji.
Aliponiona na polisi alishangaa.
Polisi walichukua alama zake
za vidole na kumuweka chini ya ulinzi wao.
Siku ile tulilala katika
nyumba ya wageni Handeni. Asubuhi tulipokwenda kituo cha polisi tuliambiwa kuwa
alama za vidole za Chausiku ndizo zilizokutwa katika kisu kilichomuua marehemu.
Hivyo polisi walikuwa wanasubiri aruhusiwe kutoka hospitali wamfikishe
mahakamani.
MWISHO
No comments:
Post a Comment