SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 5 na Faki A Faki 0655 340572
ILIPOISHIA
Ndani ya kile kisima kulikuwa
na watu wawili waliokuwa wakioga na ndio waliokuwa wakizungumza. Mmoja akatoka
na kusimama kando
ya kisima hicho. Mara moja nikatambua kuwa ni yule mwenyeji wangu lakini safari
hii alikuwa na umbile la kutisha sana.
Kwanza nywele zake zilikuwa nyingi na ndefu zilizoteremka na
kumfikia kiunoni. Zilikuwa nywele nyeupe kama
mvi za bi kikongwe. Yeye mwenyewe ngozi yake ilibadilika na kuwa nyeupe kama ya mzungu. Machoyake yalikuwa ya kijivu na mboni
zake zilikuwa nyembamba na zilizosimama kama
mboni za paka.
Bado alikuwa ameota manyoya
marefu mwili mzima. Nikagundua kwenye miguu yake hakuwa na vitanga vya miguu
kama walivyo binaadamu wote bali alikuwa na kwato nyeusi kama
za farasi au punda. Hakuwa amevaa chochote. Alikuwa uchi wa mnyama!
Mwenzake naye akatoka kwenye
kisima. Yeye alikuwa mwanaume lakini alikuwa na umbile kama
la yule msichana. Miguu yake pia ilikuwa na kwato.
Walikuwa wakizungumza kwa
lugha ambayo sikuielewa. Kwa kweli nilishituka sana. Nikapata hofu
na uoga mpaka mwili wangu ukawa
unatetemeka.
Nikahisii kwamba yule
msichana aliyenikarisha mle ndani hakuwa binaadamu bali alikuwa jini na pale
alikuwa akizungumza na jini mwenzake.
Nikatengeza mawazo kwamba
huenda msichana yule aliniingiza katika nyumba ile kwa hila ili wanidhuru kwani
ile damu iliyokuwa kwenye kile kisima ilikuwa ni ya binaadamu kama
mimi. Na bila shaka waliingizwa mle ndani na kuuawa kikatili.
Hapo ndipo
nilipochanganyikiwa nikajua kwamba dakika zangu za kuishi zilikuwa zimekaribia
kwisha.
SASA ENDELEA
“Nitatokaje humu ndani?”
nikajiuliza.
Nililirudisha lile pazia.
Nikaenda kwenye mlango na kutoka ukumbini. Ukumbi ulikuwa
kiza. Sikuweza kuona kitu. Sikuelekea upande wa uani tulikoingilia, nikalekea
mlango wa mbele. Nilitaka nitoka kwa kutumia mlango huo bila Zena na mwenzake
kujua. Pikipiki yangu nilikuwa nimeshaisamehe.
Kwa muda ule pikipiki haikuwa
na umuhimu kwangu, kilichokuwa muhimu illikuwa ni kujisalimisha roho yangu.
Nilijiambia kama nitafanikiwa kutoka mle ndani na kukimbia nitakuwa nimeweza
kujisalimisha kuuawa.
Nikawa natembea haraka haraka
ili niwahi kutoka kabla sijagunduliwa. Kwa sababu ukumbi
ulikuwa kiza nikakumba kitu kama meza
iliyokuwa imewekwa ukumbini.
Niliikumba kwa nguvu hadi ikatoa mlio wa kuburuzika.
Hapo hapo nikasikia sauti ya
Zena ikiuliza.
“Amour unanitafuta?”
Sikujibu kitu, nikaikwepa ile
meza na kundelea kwenda mbele sasa kwa haraka zaidi.
“Amour unaondoka?” Sauti ya
Zena ikasikika tena.
Sikujibu. Nikaendelea kwenda.
Sasa nilikuwa nahema kwa hofu.
Mdomo nilikuwa nimeuacha wazi huku mikono yangu ikiwa mbele ili niweze kuugusa
mlango nitakapoufikia.
“Amour usiondoke, nisubiri”
Sauti ya Zena ilizidi
kunichanganya. Ndani ya moyo wangu nikawa naomba Mungu anisalimishe.
“Yarabi nisitiri…Yarabi
nisitiri…”
Mara moja nikaufikia
mlango.
Nikawa naupapasa haraka haraka mpaka nikaushika ufunguo uliokuwa
umeachwa kwenye kitasa, nikaufungua kisha nikauvuta mlango. Mlango
haukufunguka.
Nikagundua kuwa kulikuwa na
vifungulio vingine vilivyokuwa chini ya na juu ya mlango. Nikapeleka mkono
wangu juu na kupapasa. Nikapata kifungulio kimojawapo nikakivuta chini.
“Amour umeona nini?” Sauti ya
Zena sasa ikasikika kutokea mlango wa uani.
Bila shaka alikuwa
akinichungulia kupitia mlango huo. Sikutaka hata kugeuka nyuma kumtazama.
Nikainama chini ili nifungue kifungulio kingine kilichokuwa chini.
“Amour usiondoke!” Zena
aliendelea kuniambia.
Aliposikia nafungua kile
kifungulio cha mlango cha chini akaniambia.
“Hebu nisubiri”
Sasa nikazisikia hatua zake
akinifuata kwa mwendo wa haraka. Kwa vile miguu yake ilikuwa na kwato, kwato
hizo zilisikika kama za farasi wa kwenye
sinema, “Kwa…kwa…kwa…”
Mwili ukanisisimka.
Nikajiambia sasa nakufa.
Nikauvuta mlango. Licha ya
kufungua vifungulio vya juu na chini. Mlango haukufunguka.
Kwato za Zena zilikuwa
zimeshanikaribia. Akili yangu iliunda picha nikikabwa na mwanamke huyo wa
kijini na kunifyonza damu yangu kupitia kenye tundu za pua yangu…
Mkono wa Zena wenye kucha
ndefu ukanishika
kwenye bega. Nikaukutua…
“We Amour nini…?” akaniambia
kwa hamaki
baada ya kuukutua mkono wake.
Niliuvuta tena ule mlango kwa
nguvu. Safari hii ukafunguka.
Zena alikuwa ameshanishika
shati kwa nyuma. Nikapiga hatua kutoka nje. Zena akaliachia shati.
“We Amour…utaona!”
akaniambia.
Nilikuwa nimeshavuka kizingiti cha mlango.
“Hutakwenda popote” Sauti ya
Zena iliyokuwa na hasira ikasikika nyuma yangu.
Wakati napiga hatua kutoka
nje niliona nimetokea nje ya ile nyumba lakini Zena aliponiambia “Hutakwenda
popote” nikaona nimetokea kwenye eneo jingine ambalo sikulielewa. Lile jumba la
Zena sikuliona tena. Nikajiona kama nimo ndani
ya pango la kutisha lenye njia nyembamba ya kupita.
Vile nilivyokuwa nakimbia
niliendelea kukimbia ndani ya hilo
pango nikiifuata ile njia nyembamba. Kwenye kuta za mawe za lile pango kulikuwa
kumewekwa mishumaa iliyokuwa inawaka.
Kadiri nilivyokimbia
nilikutana na njia zingine zilizonichanganya. Sikuweza kujua nishike njia ipi. Kadhalika kulikuwa na
mashimo yaliyokuwa yakifuka moshi. Wakati nakimbia niligundua nilikuwa
nikizunguka tu ndani ya pango hilo kwani nilikuwa nikitokea mahali pale pale
nilipoanzia kukimbia.
Nikajaribu kushika njia
nyingine ambayo nilihisi ingeweza kunitoa ndani ya pango hilo,
nikajikuta nimetokea kwenye mlango kama mlango
wa nyumba. Nikaufungua ule mlango na kuchungulia ndani. Nikaona kumesakafiwa na
kulikuwa na kuta kama za nyumba. Kuta hizo
zilikuwa zimepakwa rangi ya samawati.
Nikaingia ndani na kukutana
na hewa safi
yenye harufu ya mawaridi. Sasa nilikuwa kwenye ukumbi mpana ambao haukuwa na kitu
chochote. Nilitembea kwenye ukumbi
huo uliokuwa kimya huku nikiwa nimejaa hofu.
Sikujua nilikuwa nimetokea
katika nyumba gani na inayoshi nani. Mazingira yaliyonifikisha hapo yalinifanya
nipate hofu.
Nilikuta mlango uliokuwa wazi, nikaingia katika huo mlango. Nilimkuta mzee
mmoja aliyevaa shuka nyeupe akiwa ameketi kwenye mswala.
Alikuwa amejifunga kilemba
kirefu kama muarabu. Mwenyewe pia alionekana kama muarabu. Alikuwa na ndevu ndefu na sharafa.
Wakati naingia katika hicho
chumba alichokuwemo, mzee huyo alikuwa
ameinama akisoma kitabu. Kitabu chenyewe kilikuwa ni kile nilichomuazima Zena.
Nikasimama mbele yake na
kumtazama. Mzee alikuwa akiendelea kufungua karasa.
Nikamuamkia.
“Shikamoo mzee”
Mzee akainua kichwa na
kunitazama. Macho yake yalikuwa madogo ya kijivu.
“Marahaba” akaniitikia. Sauti
yake ilikuwa na lafidhi ya kiarabu.
“Mzee samahani, naomba msaada
wako” nikamwambia.
“Msaada gani?”
“Mimi sijui nilivyofika hapa,
ninaomba unioneshe njia ya kutoka nje”
“Unasema hujui ulivyofika
hapa?”
“Sijui, nimejiona tu
nikitokea katika nyumba hii”
“Kwani unatoka wapi?”
“Ninatoka katika nyumba ya
msichana mmoja ambaye nilimuazima kitabu changu, wakati ule natoka nikaona nimetokea kwenye pango. Baadaye tena
naona nimetokea kwenye nyumba hii”
“Wakati unatoka ulimuaga
mwenyeji wako?”
“Sikumuaga”
“Kwanini hukumuaga?”
Hapo nikanyamaza kimya,
sikuwa na jibu. Nilishindwa kumueleza niliyoyaona kwa sababu yule mzee naye
sikujua alikuwa ni nani.
Pakapita kimya cha sekunde
kadhaa. Yule mzee alikuwa akinitazama akisubiri jibu langu na mimi nilikuwa
nikimtazama uso wangu ukiwa
umenywea ukionesha
sikuwa na jibu.
“Ulifanya kosa kutomuaga
mwenyeji wako na ndio sababu unahangaika. Siku nyingine usirudie kosa kama hilo” Yule mzee
akaniambia.
Akanyamaza kimya kisha akanimabia.
JAMAA HAJIELEWI YUKO WAPI. JE
HUYO MZEE NI NANI NA ATAMWAMBIA NINI JAMAA HUYO? WEWE UNAFIKIRI KITU GANI
KITAMTOKEA JAMAA HUYO?
HUWEZI KUJUA MPAKA UTEMBELEE
TENA BLOG HII HAPO KESHO.
No comments:
Post a Comment