Simulizi za faki a faki 0713 340572
NILIVYOGEUZWA PAKA
(19)
ILIPOISHIA
Baada ya kucheza kwa karibu dakika
tano, tulianza kujipenyeza ndani ya duka hilo.Alianza bibi, akafuatia bibi
Chaurembo, halafu mimi na Chausiku. Bibi na bi Chaurembo pamoja na mke wangu
walilisotea duka hilo na kujaza kinyesi kila mahali.Wakati wakifanya hivyo
walikuwa wakitoa sauti za kunuizia kuharibu biashara katikia duka hilo
“Tunalisotea duka hili liingie
nuksi, mwarabu asipate biashara.Asije mtu yeyote kununua kitu hapa. Duka hili
life kabisa na mwenyewe afilisike arudi kwao……..”
Ndiyo maneno waliyokuwa wakisema
bibi na bi Chaurembo kwa sauti zao za kipaka bila kujali kama kelele zao
zilikuwa zinasikiwa.
Tulipotoka hapo dukani
tulijipenyeza ukumbini. Huku nako bibi na bi Chaurembo walieneza kinyesi
“Sasa twendeni zetu.Kesho tukija
tutawaingilia vyumbani tuwawangie mpaka wahame” bibi akatuambia
Tukarudi kwenye duka kisha
tukatoka na kurudi kiwanjani
Tulipofika kiwanjani bibi
akajigeuza mtu na kuanza kucheka.Chausiku naye akageuka mtu, nikafuatia mimi
kisha bi Chaurembo
Vilikuwa vicheko vitupu.Mimi tu
ndio sikuwa nikicheka.Sikuona la kunifurahisha. Bibi na bi Charembo wakawa
wanajisifia kuwa watamuonyesha yule mwarabu
Kumbe wachawi baada ya kufanya
uovu hufurahia kwa vicheko kama watu waliofanya jambo la maana lenye kuleta
tija
Wachawi wenzetu walipofika, kila
kikundi kikawa kinahadithia juu ya kazi waliyokwenda kuifanya.Baadaye bibi
akawapa pongezi kisha akaamrisha tucheze ngoma.Tukacheza ngoma yetu ya
kichawi.
SASA ENDELEA
Usiku wa siku ya pili yake tulipokutana
tena kiwanjani kundi letu likaenda tena nyumbani kwa yule mwaarabu.Safari hii
hatukuishia dukani tu, tuliingia hadi vyumbani. Tulisumbua watu kwelikweli
kwa sauti zetu za kutisha
Katika chumba kimoja ambacho
tuliingia mimi na Chausiku tulikuta mzee mmoja mwaarabu akiswali
Chausiku alitoka haraka mle
chumbani. Mimi nikawa namuangalia yule mzee akiomba dua. Alipogeuza uso
akaniona kando ya mlango
Nikamsikia akiniapiza kwa
kusema “ Kama wewe ni mwanga utabaki kuwa paka daima inshaallah!”
Nilivyomsikia akisema hivyo
nilikimbia na kutoka nje. Niliwakuta wenzangu walikuwa wameshatoka. Tukarudi
kiwanjani
Wenzangu wakajigeuza binaadamu
lakini mimi nilishindwa. Kila nilivyojaribu kunuia niwe binaadamu sikuweza
kubadilika. Nikabaki kuwafuatafuata wenzangu ili wanisaidie. Lakini kila
niliyemfuata aliniuliza “Yaani unashindwa kujigeuza binaadamu?”
Nikatikisa kichwa changu kuonesha
kuwa nilikuwa nashindwa kuurudisha mwili wangu wa kibinaadamu
“Wacha ujinga wewe, mbona juzi na
jana uliweza kujigeuza!” bibi akanifokea
“Leo ninashindwa. Kila ninavyonuia
naona sibadiliki” nilijibu kwa kutoa mlio mrefu wa kipaka ulioonesha jinsi
nilivyofadhaika
“Labda tatizo limetokea kule
tulikotoka” Chausiku akamuambia bibi
“ Kama tatizo ni kule tulikotoka sote
tungeshindwa” bibi akamjibu.
Chausiku akanitazama
“Hebu jigeuze mume wangu tuondoke,
muda unakwenda” akaniambia
Kwa mara nyingine nilijaribu
kunuia kuwa binaadamu lakini umbo langu la kipaka halikubadilika. Nikatikisa
kichwa changu. Ilikuwa ni kuonesha fadhaa na pia kuonesha kuwa nimekwama
“Bibi huwezi kumsaidia huyu mume
wangu?” Chausiku alimuambia bibi
Bibi akanitabania maneno na
kunichezea ngoma kisha akavunja kijiti juu ya kichwa changu
“Jigeuze uwe binaadamu!”
akaniambia kwa sauti kali
Nikajaribu tena. Nikashindwa
Nikaona wachawi wakianza kuondoka
mmoja mmoja
Mwisho bibi naye akatuambia
“Jamani nimeshindwa.Naenda zangu” akasema na kuondoka. Akatuacha mimi
na mke wangu Chausiku
“Sasa tutakwendaje nyumbni namna
hiyo? Wenzetu wameshatukimbia” Chausiku akaniambia
Sikuwa hata na la kumjibu.
Nikamuona mke wangu akiondoka kwa hasira, nikamfuata nyuma nyuma.
Alikuwa akienda kwa haraka haraka
huku akigomba peke yake njia nzima. Aliwalaumu wenzake kwa kutotupa msaada na
kutuacha pale kiwanjani
Pia alinilaumu mimi kwa kile
alichodai nimejiingiza katika uchawi nusunusu, ndiyo sababu nafikwa na
matatizo
“Sasa mimi nitamfanyaje paka
huyu?” nilimsikia akijiuliza peke yake wakati tunatembea
Tulipofika nyumbani alipofungua
mlango tu nikaingia.Nilihofia kuwa angeweza kuingia yeye kisha akanifungia
mlango ili nisiingie. Vilevile alipofungua mlango wa chumbani niliwahi
kuingia
Akaketi kwenye kiti. Mimi nilibaki
chini nikimuangalia
“Sasa mimi nitakufanyaje?. Humu
ndani utakaa mpaka lini,watu si watakuona?” Chausiku akaniuliza
Nilikuwa nikiunguruma unguruma
nikimwambia kuwa kama kuna dawa anayoifahamu anifanyie ili niweze kuwa
binaadamu
Chausiku alibetua mabega yake
“Mimi sina dawa yoyote. Bibi
mwenyewe ameshindwa, nitaweza mimi?”
“Najuta kujiingiza katika kundi
lenu!” nikasema kwa kuunguruma
“Utajuta sana . Ule unafiki wako
wa kukubali kitu lakini moyoni mwako hukitaki ndio uliokuletea matatizo”
“Sasa nitabaki hivi mpaka lini?”
“Sijui”
Mke wangu siku ile kitanda
alikiona cha moto. Alilala kwenye kiti akiwa amejiinamia hadi asubuhi. Mimi
nilikesha miguuni kwake
Asubuhi kulivyokucha Chausiku
alitoka akanifungia mlango kwa nje. Sikujui alikwenda wapi. Nikahisi labda
alikwenda kwa wenzake kunitafutia dawa ya kunirudisha kwenye umbo langu la
kibinaadamu
Jambo moja ambalo lilikuwa ndani
ya akili yangu ni kuwa katika ile nyumba tuliyokwenda kufanya uchawi usiku,
yule mzee aliyekuwa anaswali aliniapiza kwa kuniambia “ kama wewe ni mwanga
utabaki kuwa paka daima inshaallah!”. Na hivyo ndivyo ilivyotokea.
Sasa sikujua “inshaallah” ile
ingekuwa mpaka lini.
Chausiku alirudi tena baadaye,
akaufungua mlango na kuingia ndani.Alikuwa ameshika kapu.Alivyoingia tu
alinibeba na kunitia kwenye lile kapu. Akatoka na kapu yake
Mimi nilidhani alikuwa amepata
mtaalamu ambaye angeweza kunirudisha katika umbo langu la kibinaadamu na
hivyo alikuwa ananipeleka. Safari ilikuwa ndefu kweli
Ingawa nilikuwa ndani ya kapu
lakini nilihisi akipanda kwenye mawe makubwa na kisha kushuka chini.Baadaye
alilimimina lile kapu na kunimwaga
Nilipotupa macho niliona nilikuwa
katika eneo la majabali karibu na ziwa. Ulikuwa ni mwendo mrefu kutoka
kijijini kwetu.
Aliponimwaga hapo Chausiku
alipanda juu ya jiwe kubwa, akaendelea na safari yake. Hapo nilihisi kuwa mke
wangu alikuja kunitupa ili nisubiri kufa kwani hapakuwa mahali pa kuishi
Nilihisi wazo la kunileta hapo
alilipewa huko kwa bibi yake alikokwenda asubuhi. Bila shaka aliambiwa
sitaweza kurejea katika umbo langu la kibinaadamu na ufumbuzi ni kwenda
kunitupa
Nilipogundua kuwa mke wangu
alikuja kunitupa nikamfuata.Nilijaribu kulipanda lile jiwe lakini nilishindwa
kwani kucha zangu zilikuwa zinateleza
Nikatumia njia nyingine. Nilishuka
chini kabisa ya genge hilo la mawe. Nikazunguuka hadi upande ule alioelekea
Chausiku lakini sikumuona tena. Bila shaka alikuwa ameshaondoka
Nikaamua kurudi nyumbani mwenyewe
kwani njia nilikuwa naijua
Nilitembea taratibu huku
nikipishana na watu walionidhani kuwa ni paka. Hawakuwa wakinipatiliza na
mimi sikuwapatiliza. Nikaendelea na safari yangu.
Masikini kijna wa watu amegeuka
paka moja kwa moja! Je nini kitatokea? Haya ndio mambo ya blog yetu hii. Hebu
tutembelee tena hapo kesho kama kweli unamhurumia kijana huyu.
ITAENDELEA
|
No comments:
Post a Comment