HADITHI
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI
MWANAMKE 3
ILIPOISHIA
Nikaangaza macho yangu
kumtazama. Nikamkumbuka. Alikuwa ni yule msichana niliyekutana naye sinema siku
ile.
“Oh nzuri! Hujambo?” nilijibu
salamu yake.
“Sijambo. Leo tumekutana
tena”
“Imekuwa kama bahati.
Nilikuwa natoka kununua kitabu”
“Mimi pia nimekuja kununua
kitabu. Nilikuwa nahitaji kitabu cha “Mashimo Saba ya Malme Suleiman”
“Vimeisha. Kilikuwa kimebaki
kimoja tu nilichonunua mimi” nikamwambia.
“Kumbe wewe pia ulikuja
kununua kitabu hicho hicho?”
“Nilikuja kununua kitabu
hicho”
Nikakitoa kile kitabu na
kumuonesha.
Akakishika na kukitazama.
“Una umuhimu nacho sana kwa leo na kesho?”
akaniuliza.
“Ni kwa ajili ya kujisomea
tu”
“Basi naomba uniazime kwa
siku mbili tu halafu nitakurudishia”
Sikuwa na sababu yoyote ya
kukataa. Nilihisi yule msichana alikuwa akikihitaji zaidi.
“Nitakuazima, sasa sijui
nitakipata vipi?”
SASA ENDELEA
“Keshokutwa nitakuwa majestic
Cinema, utakuja?” akaniuliza.
“Ninaweza kuja kwa ajili yako
tu”
“Basi njoo usiku saa mbili na
nusu hivi utanikuta nakusubiri pale nje”
“Kutakuwa na picha gani?”
“Picha nzuri ya James Bond”
“Inaitwaje?”
“Dk No”
“Inarudia. Nakumbuka Dk No ndio picha ya kwanza ya James Bond,
ilitoka kwa mara ya kwanza mwaka 1961”
“Sijui. Mimi sikuwahi kuiona
lakini ni ya Seen Conary mwenyewe?”
“Mimi pia sikuwahi kuiona ila
niliisikia tu. Mbabe wake ni Seen Conary mwenyewe”
“Nimekuuliza hivyo kwa sababu
kuna mtu mwingine anakuja kwenye picha za James Bond anaitwa Roger Moor”
“Ile ni ya Seen Conary si
Roger Moor”
“Huyo ndiye ninayemtaka mimi”
“Basi mimi nitafika hapo
Majestic Cinema keshokutwa”
“Asante
kaka, ngoja niingie humu dukani nione kama
nitapata vitabu vingine vya hadithi”
‘Sawa”
Msichana akaingia mle dukani
na mimi nikapanda pikipiki yangu na kuondoka.
SASA ENDELEA
Yule msichana alikuwa
ameniambia nikutane naye kesho kutwa saa mbili usiku nje ya Majestic
Cinema.
Ilipofika siku hiyo niliondoka nyumbani kwangu saa mbili usiku kuelekea
Majestic Cinema kufuatia kitabu changu. Nilipofika ilikuwa saa mbili na
nusu kama tulivyoahidiana na msichana huyo ambaye sikuwahi
hata kumuuliza jina lake.
Nikamkuta amesimama mbele ya
mlango wa jumba hilo
akiwa na mavazi yake yale yale, baibui jeusi la kiiran na hijabu.
“Niko hapa nakusubiri”
akaniambia.
“Nimeshakuona”
“Vipi hali yako?”
“Mimi sijambo, sijui wewe”
“Mimi mzima tu, karibu”
“Asante”
Msichana alikuwa ameshika
tikiti mbili mkononi. Akanipa tikiti moja.
“Nimekukatia tikiti uingie”
“Mbona mimi sikupanga
kuangalia sinema” nikamwambia huku nikipokea ile tikiti.
“Hukupanga? Si nilikwambia
juzi…”
“Wewe ndio ulisema utakuja
sinema, mimi nilikuwa nije kuchukua kile kitabu tu”
“Kwa vile nimeshakukatia,
ingia tu tuangalie pamoja”
Wakati akiniambia hivyo watu
walikuwa wanatoka ndani ya jumba hilo.
Onesho la jioni lilikuwa limekwisha.
Tulisimama kwa pembeni
kuwapisha watu hao, walipomalizika na sisi tukaingia. Tulitafuta siti zetu,
tulipozipata tukaketi. Saa tatu kamili trela ikaanza. Baada ya trela kwisha
msichana alitoka. Baadaye alirudi akiwa na chupa mbili za soda na pakiti mbili
za njugu.
“Chukua’
Akanipa chupa moja ya soda na
pakiti moja ya njugu.
“Asante”
Onesho la sinema likaanza.
Tukaitazama filamu ya Dk No mwanzo hadi mwisho. Mara kwa mara msichana huyo
alikuwa akimshangilia James Bond kutokana na ujanja wake wa kipelelezi. Filamu
ilipomalizika tukatoka.
“Si utanipeleka nyumbani?”
msichana akaniuliza tulipokuwa nje ya jumba hilo.
“Kitabu kiko wapi?”
nikamuuliza.
“Nilikisahau nyumbani,
nitakwenda kukupa huko huko”
Nikaguna kimoyomoyo kwa vile
ahadi yetu haikuwa hivyo. Nikaitoa pikipiki yangu na kuiwasha.
“Panda twende” nikamwambia.
Msichana ambaye alionesha
alikuwa mzoevu wa kupanda pikipiki alikaa nyuma yangu akauzungusha mkono wake
kwenye tumbo langu. Nikatia gea na kuiondoa pikipiki.
“Unaitwa nani?” Msichana huyo
akaniuliza.
“Naitwa Amour na wewe unaitwa
nani?”
“Naitwa Zena, unaishi wapi?”
“Ninaishi Mabawa”
“Unafanya kazi wapi?”
“Nafanya kazi shirika la STC”
“Nimefurahi sana kukufahamu Amour”
“Na mimi pia nimefurahi
kukufahamu”
Tukaendelea kuzungumza hili
na lile mpaka tukafika Mikanjuni. Safari hii alinifikisha hadi katika nyumba
aliyokuwa anaishi. Lilikuwa jumba zuri la kifahari. Ingawa eneo hilo lilikuwa giza, jumba hilo lilikuwa linawaka taa
ya umeme.
“Mimi naishi hapa” Msichana
akaniambia huku akishuka kwenye pikipiki.
Nilikuwa nikilitupia macho
lile jumba, nikataka kumuuliza alikuwa amepangisha chumba au alikuwa akiishi
kwao. lakini nilishindwa kumuuliza ili asione ninayachunguza maisha yake.
“Nimepaona” nikamjibu.
“Karibu ndani” akaniambia.
“Asante”
“Karibu” Msichana
akanisisitizia.
“Hapa panatosha” nikamwambia
nikiwa nimekaa kwenye pikipiki yangu.
“Unataka uishie nje, si
vizuri. Tuingie ndani. Ninaishi peke yangu tu usiogope”
“Unaishi peke yako humu
ndani?” nikamuuliza.
“Nimejenga mwenyewe kutokana
na biashara zangu na ninaishi mwenyewe. Msichana aliniambia huku akifungua
geti.
“Karibu”
Kwa jinsi alivyokuwa
akinibembeleza ilibidi nishuke kwenye pikipiki. Niliposhuka tu msihana
aliishika pikipiki yangu akaikokokota na kuiingiza ndani, nikawa namfuata
nyuma.
Tulipoingia ndani msichana
aliiegesha pikipiki kando ya mti mkubwa uliokuwa umeota katika ua wa jumba hilo. Aliiacha pikipiki
akaenda kufunga geti.
“Karibu” akaniambia huku
akitangulia kwenda kwenye mlango wa kuingilia kwenye jumba hilo. Nikamfuata.
JAMAA AMESHAINGIA NDANI YA
NYUMBA YA MWANAMKE HUYO AMBAYE HAMJUI. Je Nini kitatokea?
No comments:
Post a Comment