HADITHI
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA (20)
ILIPOISHIA
Asubuhi kulipokucha Chausiku alitoka
akanifungia mlango kwa nje. Sikujui alikwenda wapi. Nikahisi labda alikwenda
kwa wenzake kunitafutia dawa ya kunirudisha kwenye umbo langu la kibinaadamu
Jambo moja ambalo lilikuwa ndani ya
akili yangu ni kuwa katika ile nyumba tuliyokwenda kufanya uchawi usiku, yule
mzee aliyekuwa anaswali aliniapiza kwa kuniambia “ kama wewe ni mwanga utabaki
kuwa paka daima inshaallah!”. Na hivyo ndivyo ilivyotokea
Chausiku alirudi tena baadaye,
akaufungua mlango na kuingia ndani.Alikuwa ameshika kapu.Alivyoingia tu
alinibeba na kunitia kwenye lile kapu. Akatoka na kapu yake
Mimi nilidhani alikuwa amepata
mtaalamu ambaye angeweza kunirudisha katika umbo langu la kibinaadamu na hive
alikuwa ananipeleka. Safari ilikuwa ndefu kweli
Ingawa nilikuwa ndani ya kapu lakini
nilihisi akipanda kwenye mawe makubwa na kisha kushuka chini.Baadaye
alilimimina lile kapu na kunimwaga
Nilipotupa macho niliona nilikuwa
katika eneo la majabali karibu na ziwa. Ulikuwa ni mwendo mrefu kutoka kijijini
kwetu.
Aliponimwaga hapo Chausiku alipanda
juu ya jiwe kubwa, akaendelea na safari yake. Hapo nilihisi kuwa mke wangu
alikuja kunitupa ili nisubiri kufa kwani hapakuwa mahali pa kuishi
Nilihisi wazo la kunileta hapo
alilipewa huko kwa bibi yake alikokwenda asubuhi. Bila shaka aliambiwa sitaweza
kurejea katika umbo langu la kibinaadamu na ufumbuzi ni kwenda kunitupa
Nilipogundua kuwa mke wangu alikuja
kunitupa nikamfuata.Nilijaribu kulipanda lile jiwe lakini nilishindwa kwani
kucha zangu zilikuwa zinateleza
Nikatumia njia nyingine. Nilishuka
chini kabisa ya genge hilo la mawe. Nikazunguka hadi upande ule alioelekea
Chausiku lakini sikumuona tena. Bila shaka alikuwa ameshaondoka
Nikaamua kurudi nyumbani mwenyewe
kwani njia nilikuwa naijua
Nilitembea taratibu huku nikipishana
na watu walionidhani kuwa ni paka. Hawakuwa wakinipatiliza na mimi sikuwapatiliza.
Nikaendelea na safari yangu
SASA ENDELEA
Wakati nakaribia kufika kule
kijijini kwetu nilimuona paka dume mbele yangu. Aliponiona alijivimbisha na
kuinua mkia wake kisha akaanza kuunguruma
Mimi sikumjali. Nilitaka kumpita na
kuendelea na safari yangu lakini paka huyo alinirukia ghafla akanipindua chini
na kuanza kunishambulia kwa kucha zake
Nilikurupushana naye kwa dakika
kadhaa. Tukawa tunapigana. Alinilaza chini karibu mara tatu na kuuharibu uso
wangu kwa kuuparura makucha. Mimi nilimlaza chini mara moja. Sikuwa na uzoevu
wa kupigana kipaka. Hivyo alinizidi nguvu.
Kwa bahati njema alitokea kijana
mmoja akaturushia jiwe likampata yule paka mwenzangu, akaniacha na kutimua
mbio. Na mimi nikatimua mbio. Sikusimama mpaka nilipofika mbali, nikatazama
nyuma. Sikumuona tena yule paka wala yule kijana. Ndipo nikaendelea na safari
yangu taratibu.
Mpaka ninafika nyumbani kwetu
nilikuwa nimechoka kutokana na kutembea mwendo mrefu.Nilikuta mlango wa mbele
uko wazi nikaingia. Ukumbini sikuona mtu. Nikaenda kwenye mlango wa chumba
chetu. Mlango huo ulikuwa umefungwa na sikuweza kuufungua.
Nikaunguruma mara mbili kumuita
Chausiku. Mara niliona mlango unafunguliwa. Chausiku akachungulia, aliponiona
akaguna.
“Yaani umerudi?” akauliza akiwa
amekunja uso. Lakini mimi tayari nilishajipenyeza ndani.
“Sasa nitakuachia wewe hiki chumba.
Mimi mwenyewe nitakwenda kutafuta mahali pengine pa kuishi” akaendelea
kuniambia kwa hasira.
Nikawa namzunguka kwenye miguu kama
ishara ya kumrai asinikasirikie kwani yote yasingetokea kama si wao.
“Safari yote ile niliyokwenda
kukutupa pia umerudi!” Chausiku alikuwa bado akinisimanga. Nikahisi moyo wake
ulikuwa umeshabadilika. Hakuwa mwenzangu tena.
Hapo ndipo nilipogundua wachawi si
watu kabisa. Ni sawa na wanyama! Jana na juzi tulikuwa wamoja na akanishikilia
nishirikiane na kundi lao. Lakini leo hana haja na mimi tena.
Chausiku akatoka mle chumbani na
kunifungia mlango kwa nje. Nikaa humo chumbani mchana kutwa. Upande mmoja wa
akili yangu nilihisi kwamba huenda Chausiku hatarudi tena. Ndiyo
ameshanikimbia! Kama ni kurudi labda aje kuangalia kama nimeshakufa kwa njaa!
Alishaniambia kuwa atahama
kunikimbia mimi. Pengine ndio ameshahama. Haikuwa kawaida yake kuondoka mchana
kutwa..
Ile dhana kwamba nitafungiwa humo
chumbani hadi nife ilinifanya nipande ukuta. Nyumba yenyewe haikuwa na dari.
Nilipokuwa juu nilitembea kwenye kuta hadi upande wa nje, nikaruka chini
Pale barazani palikuwa na watoto
wakicheza, waliponiona walinifukuza kwa kwa mawe.
“Jipaka shume hilo …..jipaka shume
hilo ….!” Walikuwa wanasema huku wakinitimua
Jiwe moja lilinipiga kwenye kiuno.
Nilisikia uchungu mkali lakini nilijikaza nikaendelea kukimbia.
Wale watoto waliponiona nimefika
mbali waliniacha wakarudi.
Nilipowaona wanarudi nikawa natembea
taratibu. Njaa ilikuwa inaniuma na mwili pia ulikuwa unauma. Sikujua nitakula
nini na nitakula wapi.
Wakati natembea nilitokea kwenye
jalala. Nikamuona mwanamke mmoja akimwaga maji ya vumba la samaki. Harufu ya
vumba hilo ilipita kwenye pua yangu. Nikakimbilia kwenye jalala hilo kwa tamaa
ya kupata matumbo ya samaki.
Kumbe kulikuwa na paka wenzangu
wakisubiri kwa pembeni. Yale maji yalipomwagwa tu paka wote waliruka na
kuibukia kwenye jalala. Kulikuwa na matumbo ya samaki na mashavu. Tukawa
tunagombeana. Kuna paka mmoja alinitia ukucha karibu na jicho. Nusura alitoboe
jicho langu. Tulikuwa tunagombea kipande cha shavu. Shavu hilo nililipata mimi
nikakimbia nalo. Nilikwenda kulila mbali sana . Nilipolimaliza nilitaka nirudi
tena lakini niliona nisingeweza kupata kitu kwani paka niliowaacha walikuwa
wengi
Nikaendelea na safari yangu taratibu
hadi nikafika nyumbani kwa yule bibi kigagula wa wachawi. Hisia zangu ni kuwa
Chausiku ningemkuta kwa bibi huyo’ Lakini nilipoiingia ndani sikukuta mtu
yeyote. Nikasimama mbele ya mlango wa chumba cha bibi huyo na kuunguruma.
Lakini sikuona dalili yoyote ya kuwemo mtu humo chumbani.
Nikatoka na kujiuliza niende wapi
ambako nitaweza kumpata rafiki mkubwa wa Chausiku. Walikuwa marafiki kwa sababu
wote wawili walikuwa bado wasichana. Pia Chausiku aliwahi kuniambia yeye ndiye
aliyemshawishi rafiki yake huyo awe mchawi kutokana na urafiki wao.
Nikaona niende nyumbani kwa mwanamke
huyo. Hakuwa akiishi mbali sana na ilipokuwa nyumba ya yule bibi. Nilitembea
huku nikijihadhari kwa hofu ya kushambuliwa na paka wenzangu au kupigwa mawe na
watoto
Tangu nilivyoanza kuzurura asubuhi
nimejifunza kwamba katika wanyama wanaoishi katika mazingira ya binaadamu, paka
wanapata taabu sana . Ni mnyama pekee ambaye akionekana mahali watoto hujisikia
kumpiga mawe bila sababu yoyote
Ndiyo sababu wakati wa mchana
kunakuwa na paka wachache wanaoonekana mitaani kuliko wakati wa usiku. Wakati
huo wa mchana huutumia kujificha na kujitokeza wakati wa usiku watu wanapokuwa
wamelala.
Nikajiuliza endapo nitabaki kuwa
paka maisha yangu, nitaweza kuishi katika mazingira ya aina ile, au nitauawa
haraka?
Inanipasa nijute. Kama si huyu
mwanamke ambaye sasa ananikimbia, mambo haya yasingenitokea, nikajiambia kwa
uchungu.
Nilipofika nyumbani kwa kwa yule
msichana nilikuta mlango wa mbele uko wazi, nikaingia. Tangu naingia nilianza kuzisikia
sauti za Chausiku na rafiki yake huyo zikitokea uani.
Walikuwa wakizungumza kitu ambacho
sikukitegemea na kwakweli kilinishitua sana .
JE WALIKUWA WANAZUNGUMZA NINI?
ENDELEA KUFUATILIA HAPO KESHO.
|
Thursday, May 19, 2016
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment