SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572
MWANAMKE 54
ILIPOISHIA
Shamsa akacheka kidogo.
“Hapana. Babu yangu mzaa mama
ndiyo alikuwa mzigua lakini mimi mwenyewe ni msomali, upande mwingine ni
mbarawa”
“Mmezaliwa wangapi katika
familia yenu?”
“Tulizaliwa wawili tu, mimi
na dada yangu ambaye alishafariki zamani. Kwa hiyo nimebaki mimi peke yangu”
“Wazazi wako wapo?”
“Pia walishafariki. Kwa sasa
hivi mtu pekee ambaye niko karibu naye ni Abdi”
“Oh Pole sana”
“Asante. Abdi ameniambia kama nitafunga ndoa na wewe, yeye ndiye atakayenisimamia
kwa sababu sina ndugu”
“Nimekuelewa. Pole sana”
“Asante. Abdi ameniambia wewe ni
ndugu yake, ni kweli?”
“Ni kweli”
Hapo nilisema uongo kumuunga
mkono mwenyeji wangu. Abdi hakuwa ndugu yangu. Kwa vile alishamwambia msichana huyo kuwa mimi ni ndugu yake,
nikaona nikubali. Pengine Abdi alimwambia hivyo ili msichana huyo aweze kunikubali
kirahisi.
“Kwa hiyo umeamua kuja kuishi
hapa Somalia?”
Shamsa akaniuliza.
“Ni ushauri wa Abdi,
amenitaka nibaki huku”
“Ameniambia amekupa ile
hoteli yake ya Al Asad?”
“Amenipa kwa maana ya
kuiongoza”
“Lakini wewe si ndiye meneja
wake?”
“Ndiyo”
“Sasa turudi katika
mazungumzo yetu, unatarajia utanioa lini?”
“Hilo ni suala ambalo nitalipanga na Abdi. Kwa
upande wangu ningependa tuoane haraka iwezekanavyo”
“Sawa”
SASA ENDELEA
Usiku wa siku ile Abdi
alikuja nyumbani kwangu akaniuliza.
“Mmezungumzaje na Shamsa?”
“Tumekubaliana”
“Umemuonaje yule binti, si
anakufaa?”
“Anafaa”
“Sasa ungependa umuoe lini?”
“Mimi nakusikiliza wewe”
“Wazazi wake walishafariki na
hana ndugu. Nimemwambia kuwa ndoa yake nitaisimamia mimi”
“Sasa panga siku”
“Nisingependa ichukue muda
mrefu, unaonaje kama tutasubiri kwa wiki mbili
hivi?”
“Si mbaya”
“Si najua kuna matayarisho
ingawa nisingependa iwe ndoa ya sherehe kubwa”
“Sawa”
Siku iliyofuata Abdi alimzuia
Shamsa kuja kazini kwa ajili ya maandalizi ya ndoa yetu. Abdi ndiye
aliyeshughulikia kila kitu. Kutoka siku ile nilikutana na Shamsa mara mbili tu.
Baada ya hapo sikukutana naye
tena hadi siku ya ndoa yetu. Ndoa ilifanyika usiku. Niliozeshwa mke msikitini
saa mbili usiku. Baada ya ndoa, mimi, Abdi na wasindikizaji wetu tulikwenda
nyumbani kwa shamsa. Nikampa mke wangu mkono.
Usiku huo huo nikamchukua mke
wangu nyumbani kwangu. Hakukuwa na sherehe kubwa. Abdi aliniambia sherehe kubwa
itazusha umbeya.
Baada ya kuoana na Shamsa
ndipo nilipoanza kusahau kwetu. Msichana alinionesha mapenzi ya kisomali ambayo
nilikuwa siyajui. Aliniheshimu, alionesha upendo wa dhati na alijivunia kuolewa
na mimi.
Siku zikapita. Biashara ya
hoteli ilikuwa inakwenda vizuri. Abdi aliniruhusu kuchukua kiasi chochote cha
pesa ninachotaka kila mwezi ila niweke katika hesabu.
Aliniambia kuwa kila mwaka
tutakuwa tunagawana mapato.
Kwa vile nilishadhamiria
kuendelea kuishi Somalia
nilikubaliana naye.
Sikuona kitu cha kunirudisha
nyumbani. Nilikuwa na nyumba nzuri ya kuishi. Nilikuwa na gari zuri la kutembelea
nilikuwa na kazi nzuri iliyokuwa ikinipatia kipato cha kutosha, isitoshe
nilikuwa na mke mzuri wa kunituliza. Sikuona sababu yoyote ya kutaka kurudi Tanzania.
Siku moja baada ya chakula
cha usiku, Shamsa aliniambia.
“Unajua huyu ndugu yako Abdi
ana siri kubwa sana”
“Siri ya nini?”
“Unajua alitaka kukuozesha
wewe mke lakini yeye hana mke?”
“Hivi hana mke, siku zote
ananiambia mke wake yuko kwao. Kumbe ananidanganya”
“Hana mke”
“Aliachana naye au hajaoa”
“Ni afadhali angeachana naye”
“Kumbe…!”
“Kulikuwa na tetesi kuwa
alimuua!”
“Ha! Unaniambia ukweli?
Kwanini amuue mke wake? Alimkosea nini?”
“Ni afadhali angemkosea
lakini hakumkosea kitu chochote”
“Alimuua bure bure tu?”
“Alimuua kutokana na imani
zake za kishirikina”
Nikanyamaza kimya na
kumtazama Shamsa ili aendelee kunieleza.
“Huyu ni mtu tajiri lakini
anataka utajiri zaidi…”
“Una maana kwamba alimuua mke
wake ili apate utajiri kwa njia za kishirikina?”
“Ina fanana na hivyo lakini
yeye aliambiwa na mganga wake kuwa katika familia yao kuna jini la utajiri. Mganga alimwambia hivyo baada ya
kuona ile pete anayovaa, alimwambia ile ni pete ya jini ambaye ukiwa naye
unakuwa tajiri wa kupindukia”
Hapo ndipo nilipoanza
kuzinduka.
Shamsa akaendelea kunieleza
kuwa alivyoelezwa na Abdi mwenyewe kuwa asili yake ni mzigua. Baba yake alitoka
Tanga, Tanzania. Alikuwa mvuvi wa samaki.
Siku moja boti aliyokuwa anavulia samaki na wenzake ilipata hitilafu wakiwa
baharini.
Walikokotwa na maji hadi
katika pwani ya Somalia.
Wenzake wane walifariki dunia lakini yeye alipona. Baada ya kuokolewa na wavuvi
wa Somalia alihifadhiwa
kwenye nyumba ya mvuvi mmojawapo na akalowea huko huko Somalia.
Shughuli zake zikawa ni zile
zile za uvuvi. Akaoa mke wa kisomali akamzaa Abdi na mdogo wake ambaye anaitwa
Yusufu.
Abdi hakupata elimu yoyote
lakini ni mjanja, ana akili ya kuzaliwa. Tangu akiwa mtoto alionekana kuwa na
kipaji.
Alipokuwa mkubwa alijiingiza
katika biashra za magendo ya pembe za ndovu zilizompa utajiri mpaka akaweza
kununua hoteli anazomiliki pamoja na kuanzisha miradi mengine.
Baba yake Abdi alikufa wakati
Abdi akiwa mkubwa. Huyo baba yake ndiye aliyekuwa na ile pete aliyokuwa anavaa
Abdi. Abdi aliichukua siku baba yake alipokufa akaivaa yeye bila kujua maana
yake.
Kwa vile Abdi ni mpenda ushirikina alikuwa mganga wake mzee mmoja
mrefu ambaye alimwambia kuwa ile pete ni ya jini mwanamke ambaye alikuwa mke wa
babu yake aliyekufa zamani huko Tanga.
Abdi akaambiwa kwamba kama atampata jini huyo na atamuoa na yeye atakuwa
tajiri. Hapo ndipo Abdi alipopata kichaa. Akaanza kufanya makafara ya kumvuta
huyo jini lakini ilishindikana.
Akaambiwa na mganga, kwa vile
yeye ameshaoa mke, huyo jini hawezi kumpata kwani jini huyo haendi kwa mtu
mwenye mke wake. Asubiri kama mke wake atakufa ndio huyo jini anaweza kumpata.
Abdi akaona hakuwa na sababu
ya kumtaliki mke wake akamtilia sumu kwenye chakula ili afe. Baada ya kumuua
mke wake akarudi tena kwa yule mganga. Akafanyiwa makafara lakini huyo jini
hakutokea.
Safari hii akaambiwa kwamba
huyo jini tayari ana mtu mwingine na mtu huyo ni ndugu yake aliyeko Tanga,
yaani mwana wa baba yake mdogo.
Akaambiwa ndugu yake huyo
anaitwa Umari au Amiri au Amour na nyota yake ni Nge.
MAMBO YANAFICHUKA
SASA. TUKUTANE
KESHO KWA TAARIFA ZAIDI
No comments:
Post a Comment