Thursday, August 4, 2016

HADITHI, MWANAMKE SEHEMU YA 51

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572

MWANAMKE 52

ILIPOISHIA

“Bila mimi mwenyewe kwenda kujaribiwa?”

“Hiyo kazi niachie mimi. Hata paspoti utapata bila kwenda wewe mwenyewe”

“Lakini hiyo paspoti itakuwa ya nchi gani?”

“Wewe ulitaka ya nchi gani?”

“Ya Tanzania”

“Utaipata bila shaka yoyote. Hapa kuna mabingwa wa kugushi. Nipe wiki moja tu. Utawekewa na mihuri ya tarehe uliyoingilia hapa Somalia”

Aliponiambia hivyo nilitabasamu.

“Inaonekana wewe hushindwi na kitu hapa Somalia” nikamwambia.

“Serikali yenyewe nimeiweka mikononi mwangu. Kuna maafisa wa polisi ambao wanakuja kuchukua mishahara kwangu kila mwezi kwa ajili ya kulinda miradi yangu. Wewe umeona mwenyewe juzi meno ya tembo tulivyoyaingiza na kuyapakia kwenye meli. Usifikiri kuwa polisi hawajui, wanajua. Baadhi ya mawaziri pia ni marafiki zangu. Likitokea tatizo niwapigia simu”

“Ninakuamini. Mambo yako ni makubwa!”

Nilipomsifu Abdi alicheka akanipa mkono. Alionekana kuwa ni mpenda sifa.

Tuliondoka hapo Hoteli tukaenda studio kupiga picha za papo kwa papo. Alichukua picha zangu kadhaa za usawa wa paspoti.

Wakati ananirudisha hotelini, nilimwambia kuwa nilikuwa ninahitaji saa.

“Saa tu, twende dukani tukanunue” akaniambia.

SASA ENDELEA

Abdi akageuza gari. Tulikwenda katika duka moja la kuuza saa akaniambia nichague saa niliyokuwa nahitaji. Nikachagua saa moja. Abdi akailipia.

“Unahitaji nini tena?” akaniuliza.

“Nilikuwa nahitaji saa tu”

“Basi twenzetu”

Tukaondoka. Alisimama tena kwenye duka moja akashuka na kuniambia nimsubiri. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa ameshika gomba lililokuwa limefungwa vichnga vya mirungi.

Akaliweka kwenye siti kisha akawasha gari tukaondoka. Alinirudisha hoteli akaniacha hapo na kuondoka.

Sikumuona tena hadi siku ya pili yake. Alikuja hotelini saa nne akaniambia nichukue vitu vyangu.

“Kule nyumba iko tayari”

“Sawa. Ngoja nitie nguo zangu kwenye begi, sina vitu vingi hapa”

Nilitia vitu vyangu kwenye begi nikalishika begin a kumwambia Abdi.

“Twenzetu”

Tukatoka. Tukiwa nje ya hoteli tulijipakia kwenye gari tukaondoka.

Tulikwenda katika ile nyumba ambayo Abdi alikuwa ameitayarisha kwa ajili yangu.

Tulipoingia ndani nilikuta ilikuwa imebadilika. Kulikuwa kumewekwa fanicha mpya. Nilikagua sebule, vyumba, hadi jiko. Kote kulikuwa kunaridhisha sana.

Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu ndio nilianza kuishi katika nyumba yenye hadhi kama ile. Kama ingekuwa Tanga ningeonekana mtu wa kuheshimika sana. Lakini historia inaonsha mara nyingi mtu hupata utukufu mbali na kwao. Ndiyo ilivyokuwa kwangu mimi.

“Umeangalia kila kitu, labda kuna kitu kilichopungua” Abdi akaniuliza baada kuipitia nyumba nzima.

“Naona kila kitu kipo”

“Mimi nafikiri bado kitu kimoja tu?” Abdi akaniambia.

“Kitu gani?” nikamuuliza.

“Nyumba inahitaji kupambwa”

“Ipambwe kivipi?”

Abdi akacheka kidogo.

“Hivi hujaelewa kama nyumba hupambwa kwa kuwa na mke mzuri”

“Na mimi nikacheka.

“Ni kweli, sasa huyo mke yuko wapi?”

“Ndiyo nataka tukae chini tulizungumzie suala hilo”

“Sawa”

“Sema mwenyewe unataka mke wa kibarawa, wa kigunya au wa kisomali?”

“Wote uliowataja wanafaa”

“Nikutafutie mke wa kisomali aliyechanganya na ubarawa, mweupe kama karatasi”

Abdi aliponiambia hivyo tukacheka.

“Abdi bwana! Mweupe kama karatasi?”

“Huyo akiwa chumbani uhitaji kuwasha taa, nuru yake inatosha kabisa kuangaza chumba!”

“Atapatikana kweli?”

“Mbele ya fedha hakuna kisichopatikana”

“Sawa. Mimi namsubiri”

“Nipe muda kidogo nikuchagulie mke anayefaa. Najua kuwa wewe unahitaji mke mweupe”

“Umenijuaje”

Abdi akacheka kisha hakunijibu chochote, akagonga mkono wangu na kuelekea kwenye mlango. Alikuwa kama aliyetaka  kutoka kisha akageuka na kunitazama.

“Suala lako ninalishughulikia, usijali. Nilikuahidi kukupatia gari, ungependa gari hii ninayotumia au nikupatie gari jingine”

“Wewe ndio utajua”

“Basi ngoja nikupatie leseni hapo kesho, nitakupa gari zuri”

“Sawa”

Nilipomjibu hivyo Abdi aligeka akafungua mlango na kutoka bila kuniambia chochote. Nilimchungulia kwenye dirisha nikaona akipanda gari lake na kuondoka.

Alikuwa kama aliyekwishamaliza kazi.

Niliingia katika chumba changu nikafungua kabati na kulikagua ndani. Lilikuwa tupu na safi. Nikaanza kupanga nguo zangu chache..

Nilipomaliza nilitoka nikaenda kukaa sebuleni kujipumzisha Siku ile nilishinda pale nyumbani. Saa saba mchana Abdi alikuja akanipa shilingi laki moja za kisomali kwa ajili ya matumizi yangu.

Akaniambia kwamba leseni yangu inashugulikiwa. Alinichukua kule hotelini kwake tukala chakula pamoja kisha akanirudisha nyumbani.

Saa mbili usiku alikuja tena tukaenda kula.

Siku ile nililala peke yangu katika ile nyumba. Asubuhi kulipokucha Abdi alinifuata kwa ajili ya kunipeleka kule hoteli kuanza kazi.

Tulipofika alinitambulisha kwa wafanyakazi kama meneja mpya. kuanzia siku ile. Abdi pamoja na mtu ambaye aliwekwa awe  msaidizi wangu walinitembeza katika hoteli nzima kabla ya kunikabdidhi ofisi pamoja na nyaraka zote zinanazihusu shughuli za hoteli.

Kutoka siku ile nikaanza kazi ya umeneja katika hoteli ya AL ASAD. Siku iliyofuata Abdi alinipatia leseni ya kuendesha na akanikabidhi moja ya magari yake.

TUKUTANE TENA HAPO KESHO

No comments:

Post a Comment