Mkusanyiko wa Stori 9 kubwa kutoka kwenye kurasa za MAGAZETI, leo February 18, 2015
MWANANCHI
Wakati Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
imeziagiza kampuni za simu kutoa maelezo kuhusu mabadiliko ya gharama
za vifurushi vya muda wa maongezi, Vodacom Tanzania imeeleza kuwa
mabadiliko hayo yanatokana na ongezeko la kodi na hivyo kulazimika “kubadili mazingira ya kibiashara ili kuepuka hasara”.
Kampuni nyingine kubwa ya mawasiliano,
imeahidi kutoa ufafanuzi wa suala hilo kesho wakati Airtel imesema
haijafanya mabadiliko yoyote kwenye gharama za vifurushi vyake.
Kumekuwapo na mijadala mingi katika
mitandao ya kijamii kupinga bei mpya za vifurushi hivyo ambazo
zimeelezwa kuwa ni megabati nane kwa vifurushi vyote vya saa 24, na
megabati 60 kwa vifurushi vya wiki.
Bei hizo zinaelezwa kuwa zimeanza
kutumika kwa wateja wanaotumia mitandao mbalimbali ya simu ambayo
inachuana sokoni, huku baadhi ya wateja wa kampuni ambazo hazifanya
mabadiliko ya gharama hizo wakiwashiwishi wenzao kuhama ili kutokuwa
hewani kutokana na kukosa vifurushi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Prof. John Nkoma
alisema kuwa tayari mazungumzo kati ya mamlaka yake na kampuni hizo za
mawasiliano yameshafanyika na kilichobaki ni wao kutoa maelezo ya hatua
walizoichukua.
“Matumizi
ya intaneti yameongezeka nchini na wananchi wengi wamekuwa hawajui
namna ya kutofautisha vifurushi vya muda wa maongezi na vile vya
intaneti. Lakini nimezungumza na kampuni zote na tumefikia mwafaka.
Ndani ya wiki hii watatoa tamko lao pamoja na msimamo wa bei za
vifurushi,”:-Nkoma.
MWANANCHI
Mama wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi
ambaye alitekwa juzi na watu wasiofahamika mkoani Geita, amefanyiwa
upasuaji wa kichwa na jopo la madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando mjini Mwanza.
Mama huyo aliyefahamika kwa jina la Ester Jonas
(30), alilazimika kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushambuliwa kwa
kukatwa mapanga na watu hao ambao walimteka mtoto wake juzi akiwa
amembeba mgongoni nyumbani kwake.
Mkuu wa Kitengo cha dharura cha Hospitali ya Bugando, Dk Darick David alisema mama huyo alifikishwa hapo jana akiwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi.
“Namkumbuka mwanangu Yohana Bahati,”
hayo ni maneno aliyoyasema mama mzazi wa mtoto huyo akiwa hospitalini
hapa kwenye chumba namba 903 cha uangalizi maalumu (ICU).
“Kama
mnavyomuona hali yake siyo nzuri, hata kuzungumza hawezi, alikatwa panga
kichwani jeraha kubwa liko puani, tumelazimika kumfanyia upasuaji wa
kichwa ili kusafisha damu iliyokuwa imeganda ndani,” alisema Dk David na
kuongeza: “Bado anatatizo kubwa na madaktari bingwa wanaendelea
kumchunguza.”
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, ProF. Alfred Mteta alisema: “Inasikitisha
kuona binadamu unamfanyia unyama binadamu mwenzako, kamwe vitendo hivi
haviwezi kukubalika tumempokea mgonjwa huyu na madaktari wanaendelea
kumpatia matibabu ili kuokoa maisha yake.”
MWANANCHI
Matukio ya ujambazi na mauaji ya kutumia silaha, yameanza kuibuka kwa kasi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hali hiyo imekuwa ikihojiwa na wananchi
na wapenda amani na zaidi ni kuhusu intelijensia ya polisi kushindwa
kugundua mipango ya uhalifu.
Wachunguzi wa mambo wanasema kuwa
kushamiri kwa matukio hayo kunaleta hofu katika jamii huku jamii yenyewe
ikilaumiwa kwa kukaa kimya kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha
sheria na hutumia isivyo halali.
Hali hiyo imetokea mjini Magu, mkoani
Mwanza kwa watu wanaodhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto
usiku wa kuamkia jana walifunga Mtaa wa Kisesa Kata ya Kisesa, Wilaya ya
Magu mkoani Mwanza na kumuua mfanyabiashara Nestory Andrew umbali wa
mita 50 kilipo Kituo cha Polisi.
Tukio hilo lilitokea saa 8:00 usiku,
majambazi hayo yalifunga Barabara ya Mwanza-Musoma kwa muda na
kusababisha taharuki kwa wakazi wa Kisesa huku milio ya bunduki
ikitawala anga.
Wakizungumza na Mwananchi eneo la tukio
jana, mashuhuda walisema walianza kusikia milio mizito ya vitu kama bomu
na kwamba baada ya muda wakaona watu wakivamia duka la mfanyabiashara
huyo na kupiga risasi hewani.
Mmoja ya mashuhuda hao, Daud Mwalimu alisema “Mimi
ni fundi baiskeli hapa stendi jana (juzi) muda kama wa saa mbili usiku
nilisikia sauti ya vishindo kama bomu, lakini baada ya muda nikasikia
sauti za bunduki hewani,”
NIPASHE
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge,
‘amefunguka’ kuhusu kashfa inayomkabili ya kupata mgawo wa Sh. bilioni
1.6 kutoka kwenye fedha zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta
Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), akisema hastahili kuitwa
mwizi, bali anapaswa kuitwa ‘nyoka wa makengeza’.
Amesema anapaswa kuitwa ‘nyoka wa
makengeza’ kwa kuwa yeye ni mjanja wa kutafuta fedha kwa ajili ya
wananchi wa jimbo lake, ambao wanapaswa kupuuza madai ya wizi
yanayoelekezwa kwake, badala yake wamwamini zaidi.
Chenge, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG) mstaafu, alisema hayo wakati akihutubia wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mahaha kata ya
Bunamala, Wilaya Bariadi mkoani Simiyu juzi.
Alisema kwa muda mrefu amekuwa kimya, lakini ameshangazwa na kitendo cha kuandamwa kuhusiana na kashfa ya akaunti hiyo.
“Wanasema
Chenge na Escrow…Pale nimeenda kutafuta kwa ajili ya wananchi wa jimbo
langu wala sikwenda kubomoa duka. Bali tunatumia akili kutafuta pesa kwa
ajili yenu,” :- Chenge.
NIPASHE
Siku moja baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, kutangaza kumsimamisha kazi kwa muda usiojulikana Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Madeni Kipande,
Mkurugenzi huyo ameibuka na kueleza kuwa ameshangazwa na uamuzi huo kwa
kuwa hakuwahi kuitwa kabla na Bodi ya Wakurugenzi wa TPA kuelezwa
tuhuma hizo kama taratibu na sheria zinavyoelekeza.
Sitta alisema alimsimamisha kazi Kipande
kutokana na tuhuma za kukiuka taratibu za zabuni pamoja na mahusiano
mabaya na wateja wa mamlaka hiyo.
Kipande alisema tuhuma zilizotolewa
kwake siyo za kweli na wala hakuna taratibu zozote za zabuni
zilizokiukwa kama ilivyoelezwa na Sitta.
“Sijaitwa
na Bodi kuulizwa kabla kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwangu isipokuwa
Waziri alikuja jana (juzi) na kusema anataka kikao cha Bodi kuzungumza
na wajumbe,” alisema.
Kwa mujibu wa taratibu, Mkurugenzi wa
TPA ndiye Katibu wa Bodi, hivyo vikao vyote vya Bodi vinapaswa
kuitishwa na yeye kujadili mambo yote yanayohusu TPA.
Kipande alisema kwa kuwa Waziri Sitta
ameunda kamati kuchunguza tuhuma zilizoelekezwa kwake, ana imani kuwa
kamati hiyo itatenda haki ili ukweli wa mambo aliyotuhumiwa ujulikane.
“Tumekutana
katika kikao cha dharura cha Bodi ya Bandari kutokana na kuzingatia
malalamiko ya sehemu mbalimbali kwamba taratibu za zabuni TPA hazikukaa
sawa, zinaendeshwa katika namna ambayo hazileti imani, nampongeza Dk. Harrison Mwakyembe, alianza vizuri kushughulikia suala hili, lakini bado tatizo halijaisha,” :- Sitta.
NIPASHE
Zaidi ya wanafunzi 3, 000 wa shule nne
za msingi za Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa
Mbeya, wameandamana na kufunga barabara Kuu ya Tunduma – Sumbawanga na
ya Tanzania – Zambia na kusababisha shughuli za kiuchumi kusimama kwa
zaidi ya saa tano katika mji wa Tunduma.
Katika tukio hilo, wanafunzi hao walimgomea Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abiudi Saideya, alipowaomba watawanyike.
Wanafunzi hao kutoka Shule za Msingi
Tunduma, Mlimani, Umoja na Mwaka, waliandamana jana kuanzia saa 12:30
alfajiri na kuendelea kukaa barabarani hadi saa 5:40 asubuhi
wakiishinikiza serikali kuweka matuta eneo la Mwaka lilikopo barabara
kuu ya Tunduma – Sumbawanga jirani na wanakosoma ili kuepusha ajali
kuendelea kutokea.
Hatua ya wanafunzi kuandamana ilitokana
na ajali ya lori lililokuwa likitokea Sumbawanga kwenda Tunduma
kuwagonga watatu na kusababisha wawili kufa na mwingine kujeruhiwa
vibaya.
Mmoja alikufa papo hapo na mwingine wakati akipatiwa matibabu Kituo cha Afya cha mjini Tunduma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi,
alisema mwanafunzi Emmanuel Sichone, alifariki dunia papo hapo baada ya
kugongwa na lori hilo na Betiel Mbwambwa, alifariki dunia wakati
akipatiwa matibabu kwenye kituo hicho.
Kamanda Msangi alisema mwanafunzi, Jackson Sichone amejeruhiwa vibaya na anaendelea kupatiwa matibabu kituoni hapo.
MTANZANIA
Muuza mishikaki mmoja katika kituo cha daladala cha Temeke mwisho jijini Dar es Salaam maarufu kwa jina la Said Mishikaki, amekamatwa na kupigwa na wananchi kwa tuhuma za kuuza mishikaki ya nyama ya paka.
Said alikamatwa jana asubuhi baada ya
taarifa kusambaa katika eneo hilo zikimtuhumu kwamba amekuwa na kawaida
kuuza mishikaki ya nyama ya paka badala ya ng’ombe, mbuzi na wanyama
wengine wanaoliwa.
Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la
tukio zinasema kuwa, baada ya taarifa hizo kuenea, wananchi walilazimika
kumtafuta muuza mishikaki huyo ili wamchukulie hatua.
Baada ya kumsaka kwa dakika kadhaa,
hatimaye walifanikiwa kumkamata na kumkuta akiwa na paka mmoja aliyekuwa
amemchinja na kumuweka kwenye ndoo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao
walipomuona paka huyo akiwa amechinjwa, walichachamaa na kuanza
kumshushia kipigo muuza mishikaki huyo na kumuumiza sehemu mbalimbali za
mwili wake.
“Nilikwenda
eneo la tukio na kukuta kielelezo cha mfuko wa nyama hiyo. Niliona
nyama na utumbo mkubwa unaoonekana kama ni wa mnyama anayekula majani
mfano wa ng’ombe.
“Inawezekana
kuna matatizo katika biashara, huenda kweli ile ilikuwa nyama ya paka,
lakini hatuna uhakika, hivyo tumechukua vipande vya nyama kwa ajili ya
kuvipeleka kwa mtaalamu wa mifugo kwa uchunguzi zaidi ili kubaini aina
hiyo ya nyama”Alisema kamanda Kihenya.
HABARILEO
Wakati serikali ikianza kutafuta
suluhisho la kudumu la matatizo wafanyabiashara ndogo, mama lishe kuhusu
upatikanaji wa maeneo, imebainika kuwapo mchezo ‘mchafu’ wa
wafanyabiashara wakubwa kutumia mgongo wa wamachinga, kusambaza na kuuza
bidhaa zao maeneo yasiyoruhusiwa.
Katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es
Salaam, imebainika yako maghala 12 ya bidhaa za chakula eneo la Ubungo,
ambako wafanyabiashara ndogo wamekuwa wakigawiwa bidhaa kuziuza maeneo
yasiyoruhusiwa na kisha jioni hupeleka hesabu kwa matajiri kwa ujira
mdogo.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Mhowera
alisema wamebaini tatizo hilo na wanapaswa kulizingatia wakati wa
kutekeleza mpango wa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), wa kusaidia wamachinga kufanya biashara zao kwa amani kwenye maeneo yanayoruhusiwa.
Aidha, katika kutekeleza azma hiyo ya
Tamisemi, Manipsaa ya Ilala imeainisha maeneo kadhaa, ikiwemo Viwanja
vya Jangwani ambako itajengwa miundombinu kama vile vyoo, taa na
kuwekewa ulinzi, litumike kwa ajili ya soko la kila siku.
Hatua hizo za halmashauri za jijini Dar es Salaam, ni utekelezaji kwa vitendo mpango aliosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika mkutano wa 18 wa Bunge ulioahirishwa hivi karibuni.
Pinda alisema kimeundwa kikosi cha
kiofisi kitakachohusisha wajasiriamali hao kwa lengo la kukubaliana
kuhusu maeneo na muda muafaka wa kuendesha shughuli zao.
HABARILEO
MADEREVA wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA)
wamelalamikia shirika hilo kuwapunguza kazini hivi karibuni bila
kufuata utaratibu unaofaa, ikiwa ni pamoja na mchanganuo wa malipo yao.
Wakizungumza na gazeti hili jana,
madereva hao walilalamikia shirika hilo kuvunja mkataba waliowekeana na
kampuni hiyo ambao ni wa miaka miwili na kuamua kutafuta sababu za
kuwasimamisha kazi.
Baadhi ya madereva walikuwepo katika
ofisi za UDA zilizoko Kamata, Ilala walisema wameshangazwa na shirika
hilo kuwatafutia sababu wafanyakazi za kuwafukuza kazi na kupuuza haki
zao.
“Awali
tulikuwa tukifanya kazi kwa utaratibu wa dereva wawili kwa gari moja
ambapo leo ukiwa kazini kesho yake unapumzika na mwenzako anaingia
kazini, lakini ghafla tulibadilishiwa utaratibu mwezi huu ikawa kila
gari dereva ni mmoja tu ambaye anatakiwa kufanya kazi siku tano
mfululizo,”:-Simon Kamwela.
Alisema hata hivyo walipewa fomu ambazo
ni za hiari za kusaini ambayo zimeshajazwa zilizokuwa zinawataka
kukubali mfumo huo wa kuendesha gari siku tano mfululizo katika wiki na
pia kukiri kupeleka mapato ya kampuni kama dereva alivyopangiwa kila
siku.
Madereva hao wanadai kuwa baada ya
kufukuzwa kazi barua wamepewa kuanzia Februari 10 mwaka huu na wengine
wanaendelea kupewa mpaka sasa wakati barua zinaeleza kuwa wamepunguzwa
kazi toka Februari 9 mwaka huu.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia , niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment