SIMULIZI ZA FAKI A FAKI SEHEMU YA 11
ILIPOISHIA
Ilipofika saa saba mke
wangu aliniletea chakula.
"Mbona
umekaa?" akaniuliza.
"Nimepunzika"
nikamjibu
Chausiku akaketi kando
yangu
"Umeniletea chakula
gani?" nikamuuliza huku nikikifunua
"Wali"
"Na hii ni nyama ya
nini?" niliona kipande cha nyama juu yake
"Mbona siku zote
nikikuletea chakula huniulizi, leo kwanini unaniuliza"
Aliponijibu hivyo
nikamwaambia "Leo sijisikii kula"
"Kwanini?"
"Tumbo
linaniumauma"
"Wewe muongo.Hebu
kula hicho chakula!"
"Basi utakiacha
hapahapa, nitakula baadaye"
"Kula sasa hivi na
mimi nione.Najua iliyokutisha ni hiyo nyama”
SASA ENDELEA
“Kwani ni nyama ya nini?”
nikamuuliza mke wangu.
“Ni nyama ya sungura”
"Nyama ya sungura?
umeipata wapi?"
"Bi Zaituni
alichinja sungura wake akanipa upande mmoja wa nyama"
Nikaosha mkono na
kuiangalia ile nyama.Nilipoiridhika kuwa ilikuwa ni nyama ya sungura ndipo
nilipokula kile chakula
Nilipomaliza kula mke
wangu akanifundisha mambo mengi ya kichawi.Nikagundua kwamba nilikuwa naishi na
mwanamke hatari sana.Alikuwa akijua mambo mengi ya kutisha.Ukilinganisha na
umri wake mdogo huwezi kuamini kuwa ana ujuzi mkubwa katika shughuli za
kichawi.
"Nakuambia wazi
mimi ndiyo nimeandaliwa kushika cheo cha yule bibi.Yule kikongwe akifa leo mimi
ndiyo nitakuwa gunge lenu" Chausiku akaniambia kwa kujisifu. Zilikuwa sifa
za kipumbavu lakini yeye mwenyewe hakujua.
"Na ilikuwaje mke
wangu ukaingia katika uchawi?"
"Marehemu bibi
yangu ndiye aliyeniingiza"
"Ulikuwa ni wakati
upi?"
"Wakati
nilipoimaliza shule.Wewe ulikuwa unaishi Handeni"
"Kwahiyo wakati
tunaoana tayari wewe ulikuwa mchawi?"
Mke wangu akanikubalia
kwa kichwa.Nafikiri aliona aibu kunijibu kwa mdomo
Alipoona nimenyamaza
nikionyesha kufadhaika, alinibusu kwenye shavu langu kisha akavitia vyombo
nilivyolia chakula kwenye kapu.Akaondoka
Naam.Hivyo ndivyo
nilivyolazimishwa kuingia katika uchawi.Usiku wa siku ile tuliamka tena
tukaenda makaburini.Huko tukagawanyika kwenye vikundi vitatu.Kundi moja
lilitumwa na yule bibi kwenda kuchawia kwenye maduka kule kijijini,kundi
jingine likatumwa kwenye kijiji cha Songe kwa Mwarabu mmoja kumchawia binti
yake asiolewe
Na kundi jingine ambalo
lilikuwa mimi, mke wangu na yule bibi tulikwenda porini kuchimba dawa
Huko porini tulienda
tukiwa uchi. Wenyewe walikuwa wanakuita ngome kuu.Nilioneshwa miti mbalimbali
ambayo kama mizizi yake ama majani yake yalikuwa yakitumika kwa shughuli za
kichawi
Nilionyeshwa dawa za
kufanya ukienda mahali usionekane, dawa za kujigeuza paka au mbwa, dawa ya
kuingia katika nyumba ya mtu usiku na dawa za kuchawia watu
Dawa hizo huandaliwa kwa
kuchanganywa na vitu mbalimbali vya ajabuajabu.Nyingine huandaliwa na
viungo vya binaadamu vilivyokaushwa kama vile ulimi, mkono wa mtoto
mchanga,sehemu za siri za kike na za kiume na vitu vingine.
Nilitakiwa nichimbe
mizizi ya miti.Miti mingine iliwekewa masharti kabla ya kuichimba, ni mpaka
uichanje na wewe mwenyewe ujichanje.Kisha unachukua utomvu wake unaupaka pale
ulipo jichanja.Na kisha unachukua damu yako na kuipaka pale ulipochanja ule mti.
Miti mingine unaisemea
maneno.Unaieleza wewe nani na unataka nini?.Ukisha kueleza kile unachokitaka
ndipo unauchinmba mizizi
Yalikuwa mambo ya ajabu
ambayo sijapata kuyaona.Ilikuwa kazi tuliyoifanya kwa muda mrefu.Tulipoondoka
tulikuwa tumebeba mafurushi ya mizizi,magome ya miti,vipande vya miti na majani
Tulipofika pale
makaburini ambako palikuwa ndiyo maskani yetu,yule bibi akatugawia dawa zetu
mimi na mke wangu.Nyingine akachukua yeye.
"Utakwenda
kumuonyesha mume wako jinsi ya kuzitengeza.Umesikia?" bibi alimuambia
Chausiku
"Nitamuonyesha"
"Mtakwenda zenu au
mtawangojea wenzenu?"
"Tutakwenda
zetu"
Wakati mke wangu
anamjibu tuliona kikundi cha paka wenye rangi tofauti kimetokea pale
tulipokuwa.Yule bibi akawaambia paka hao
"Haya geukeni
mniambie"
Hapohapo wale paka
wakabadilika na kuwa watu.Walikuwa ni wale wanawake wa lile kundi letu la
wachawi waliokwenda kuwachawia wafanyabiashara
"Mmeiweza
kazi?" yule bibi akawauliza
"Si kidogo,
tumeiweza sana!" mwanamke mmoja miongoni mwa wale wachawi akamjibu .
"Tumetembelea maduka matano,yote tumeyasotea"
"Kisha tukawawekea
makimba kwenye milango!" mwingine akaongeza.
"Wiki hii hawatauza
chochote"
Bibi kikongwe akacheka
"Yule Mnyiramba
mmemkumbuka?.Maana yule ndiyo kiburi mkubwa katika kijiji hiki?"
"Bi Kidawa
alimuingilia chumbani anamolala na mkewe,akawawangia wote na nywele pia
akawanyoa nusu kichwa.Kesho watashika adabu.Hawatafungua duka" alisema
mwanamke mwingine.
Bibi kikongwe alicheka
mpaka akaanguka chini.Mke wangu akamuinua
"Bibi unacheka
mpaka waanguka?"
"Nimefurahi sana
mjukuu wangu.Sasa tuwangoje wale wenzenu waliokwenda Songe kwa mwaarabu
tuwasikilize"
Nilikuwa nataka
nimwaambia mke wangu twende zetu lakini nikafanya hamu ya kutaka kujua
yaliotokea huko Songe kwa mwaarabu.Ikabidi nisubiri.
Muda si muda kundi hilo
nalo likafika lakini walikuja kama watu na siyo kama wale wenzao waliyokuja
katika maumbile ya paka.
"Kulikoni
wanangu?" bibi kikongwe akawauliza
"Tumemhemeka
sawasawa!" mwanamke mmoja akamwaambia na kuongeza "Kesho
hataamka kwa kuumwa na tutahakikisha haolewi ng’o!"
"Wacha!" bbi
kikongwe akang'aka kisha akaanza tena kucheka
Walipomuona anacheka
kila mmoja akawa anamueleza walivyokwenda kumuangia msichana huyo binti wa
mwarabu.Katika kundi hilo walikuwemo wanaume wawili, nao pia wakaeleza kivyao,
muda wote nilikuwa nikiwasikiliza na kuwashangaa.Nikajiuliza hivi mimi pia
nitakuwa ninafuatana nao kwenda kuwachawia watu? je nitaweza kuyafanya mambo
hayo ya kichawi?
No comments:
Post a Comment