HADITHI
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
SITASAHAUNILIVYOGEUZWA PAKA
14
ILIPOISHIA
Katika
nyumba nyingi za waswahili swichi ya taa ya ukumbini hukaa katikati ya ukumbi.
Nikasikia hatua za mtu akitembea hapo ukumbini. Nilihisi mtu huyo ndiye huyo
aliyeambiwa awashe taa ya ukumbini.
Nilijua
kuwa taa ikiwaka nitaonekana pale mlangoni na kipigo nitakacho kipata kitakuwa
cha kunimaliza kabisa. Hofu ya kuuawa kikatili ikanifanya niusukume tena ule
mlango, sasa kwa nguvu zaidi. Ulipogoma tena nikajaribu kuuvuta kwa ndani.
Mlango ukafunguka.
Kumbe
mlango huo ulikuwa ukifunguka kwa ndani lakini kwa kiwewe kilichonipata nikawa
niliusukumia kwa nje.
Mlango
huo ulipofunguka nilichomoka kama nta uliotoka kwenye upinde. Nilikwenda mbio
nikiwa uchi. Nikapita kwenye vichochoro na hatimaye kwenye mapori mpaka
nikatokea kwenye ule uwanja wetu tunapokutania.
Wachawi
wenzetu wote walikuwa wamejikusanya wakijadiliana. Wakashituka waliponiona
ninakuja mbio.
"Kulikoni...kulikoni...mbona
unakuja mbio, tena uko peke yako? Wenzako wako wapi?" bibi akaniuliza
akiwa amepatwa na mshituko.
"Huko
tulikokwenda si kuzuri. Wenzangu wamenasa chumbani kwa mwalimu, hawawezi
kutoka. Niliyeweza kutoka ni mimi peke yangu, tena nilipitia kwenye mlango”
Wachawi
wote wakashikwa na mshangao.
"Hebu
tueleze vizuri, imekuwaje?" bibi akaniuliza.
Nikawaeleza
yote yaliyotokea tangu tulivyokwenda mpaka nilivyotoka kwa kuponea tundu ya
sindano.
"Nina
hakika hivi sasa, Bi Kisindano na Bi Tausi wameshakamatwa mle chumbani. Sasa
sijui nini kitatokea!"
"Ni
wapumbavu, kwani wao walishindwa kujua kwamba nyumba yenyewe haiingiliki?"
bibi akasema kwa kufoka kisha akaongeza.
"Kwanza
unapokwenda kwenye nyumba ya mtu unaipima, unapoona haingiliki unaiacha. Sasa
wao wameingia ndani kisha wanashindwa kutoka. Shauri zao!"
"Wakati
wanakuambia tumenasa, wewe ulikuwa unajionaje?"
"Mimi
nilijiona niko sawasawa tu"
"Ni
kwa sababu wewe bado hujaiva sawasawa, ni kama mwanafunzi. Pia mle ndani
hukuwachawia wale watu, ulikuwa unaangalia tu”
"Ni
kweli, mimi nilikuwa nawaangalia tu"
"Sasa
tuondokeni, kila mtu aende kwake. Asubuhi tutapata habari zao"
Tukachangukana.
Mimi na mke wangu tukaenda kuvaa nguo zetu tukaondoka.
Karibu
njia nzima nilikuwa namueleza mke wangu kisa hicho. Hofu ilikuwa bado
imenitawala.Tulipofika nyumbani tulilala hadi asubuhi.
Asubuhi
ndipo tulipopata habari kuwa kuna wanawake wawili walikutwa usiku chumbani mwa
mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya pale kijijini wakiwa uchi. Walipoulizwa wao
ni kina nani hawakuwa na jibu. Wakatolewa nje wakapigwa mpaka wakauawa.
Mimi
na mke wangu tulipozisikia habari hizo tukajua walikuwa ni Bi Kisindano na Bi
Tausi.
"Kumbe
wameuawa masikini!" nikajiwazia kimoyomoyo.
Mke
wangu alipopata habari hizo akatoka kwenda kuwambia wenzake. Baadaye alirudi na
kuniambia.
"Bibi
alikuwa anazo habari"
"Habari
zipi?" nikamuuliza
"Kuwa
Bi Kisindano na Bi Tausi wameuawa"
"Sasa
amejua kuwa hii kazi si nzuri?"
"Amesema
wameuliwa kwa upumbavu wao"
Nikatikisa
kichwa changu kusikitika.
"Hakuwaonea
huruma wenzake?”
"Si
bora wewe umesalimika"
"Je
kama ningeuawa na mimi?"
"Wewe
ni mume wangu, ungeuawa ningesikitika na ningelia lakini sio yule bibi"
Nikashusha
punzi.
"Mke
wangu kwanini tusiachane na huu uchawi?"
"Unasemaje?"
"Huoni
hii ni kazi ya kifo?"
"Fuata
miko unayopewa.Bila shaka wale wamevunja miko"
"Kwa
maana hiyo unataka tuendelee tu?"
"Hatuwezi
kuacha. Ukiacha wenzako watakuua!"
"Tutaondoka
hapa kijijini"
"Hakuna.
Hatuwezi kuacha wala hatuwezi kuondoka. Acha maneno hayo. Wale wanawake
wamekutia hofu, kwani wanakuhusu nini visirani wale?"
"Wale
ni wenzenu, unawaita visirani?"
"Na
wewe pia ni wenzako, si mlikwenda pamoja?"
Nilipomuona
mke wangu anaanza kuhamaki nikaamua kuachana naye, yasije yakaja mengine kwani
nilijua angeweza kuniletea vitisho vya kwenda kuniripoti polisi kuwa nimemuua
mke wangu wa kwanza.
Kwa
kweli tukio la kunasa, kukamatwa na hatimaye kuuawa kwa wanawake hao lilikuwa
limenitia hofu sana. Kwanza mimi sikujua kama mchawi anaweza kunasa mahali. Na
pia sikujua kuwa mchawi anaweza kuuawa kama mwizi.
Kwa
hiyo nilijua tukio kama hilo iko siku linaweza kunitokea mimi au mke wangu.Tunaweza
kwenda sehemu tukanasa na kukamatwa kisha tukapigwa na kuuawa.
Lakini
sikuwa na la kufanya. Nisingeweza kujitoa peke yangu. Ilibidi nimshawishi mke
wangu. Lakini mke mwenyewe kila ninavyomueleza alikuwa hanielewi.
Jingine
nililojifunza kwa wachawi hao ni kuwa hawahurumiani wala hawana
ushirikiano.Ushirikiano wao ni kwenye uchawi tu. Kwa upande wangu niliona
nisingeweza kuendelea kuishi na watu kama hao.
Sasa
nifanye nini? nikajiuliza.
Kama
mke wangu angekubali kutoka kusingekuwa na tatizo.Tatizo ni kujitoa mimi peke
yangu. Hilo lisingewezekana. Kwa hiyo kwa ajili ya kulinda usalama wangu
niliona niendelee kuwa katika kundi hilo huku nikitafuta namna ya kuwakimbia.
Ilipofika
usiku nilimuuliza Chausiku kama mkutano wetu utakuwepo kule uwanjani.
"Kwanini
usiwepo!" akanijibu kwa sauti ya kuhamaki.
Endelea
kufuatilia hapo kesho
|
Friday, May 13, 2016
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU YA 14
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment