HADITHI Inaletwa na kituo Bora Cha Bora Cha Candle Education Centre Tanga, Kituo Bora cha Elimu Tanga, simu 0715 772746
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572, 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 18
ILIPOISHIA
Nikataka kumjibu lakini sauti yangu haikutoa maneno kama
ilivyokuwa yeye.Iliishia kuunguruma tu.
Lakini alinielewa nilichotaka kumuambia.Nilitaka
kumuambia
"Nimefurahi kujiona nimekuwa paka"
Akaniambia "Hutaweza kusema kama mimi lakini
nimekusikia.Unaonaje?"
"Nasikia furaha sana" nikaunguruma.Ingawa maneno
hayakutoka lakini alinielewa akanijibu.
"Hata mimi nasikia furaha sana.Kutoka hii leo ukitaka
kuwa paka utakuwa tu. Lakini usitokeze nje isipokuwa kwa usiku tu"
"Sawa" nikamjibu.Hata hivyo sauti yangu ilikuwa
ya kuunguruma tu.Sikuweza kusema
"Nitaweza kusema lini?" nikauliza kwa kuunguruma
"Bado kwanza,mpaka tukukate kilimi"
Tukasikia mlango wa mbele ukibishwa hodi.Sote tukashituka
na kutega masikio.
SASA ENDELEA
"Hodi mpaka ndani" sauti ya mwanamke ikasikika
tena
"Nani wewee?" bibi akimuuliza kwa sauti ile ile
ya kipaka
"Ni mimi bi Chaurembo"
Bi Chaurembo alikuwa mmoja wa wachawi wa kundi la yule
bibi.Hapo hapo bibi akabadilika na kurudi katika umbile lake lile lile la kibinaadamu
"Karibu ndani bi Chaurembo" akasema huku akivaa
kaniki yake.Akafungua mlango na kutoka
Mke wangu naye akabadilika na kuwa mtu
Na mimi nikanuia kuwa mtu.Hapo hapo nikajiona nimebadilika
na kuwa mtu.Sikuweza kuamini, nikawa najiangailia angalia huku nikijiuliza ni
uchawi gani wa aina ile.
Chausiku alikuwa akivaa nguo zake na mimi
nikavaa.Alipomaliza kuvaa alitoka ukumbini na mimi nikatoka.
Bi Chaurembo alikuwa amesimama na bibi yetu pale ukumbini.
Alipotuona tunatoka akashangaa
"Eh! mlikuwa mnafanya nini wenzangu?"
"Sema kilichokuleta babu, mbona umbea umekuzidi!"
bibi akamwaambia akiwa amemshikia kiuno kama aliyetaka kupigana naye.
Bi Chaurembo akacheka
"Makubwa!" akasema huku akiniangalia
"Shikamoo bi Chaurembo" nikamuamkia na Chausiku
naye akamuamkia
"Marahaba.Mmekuja kumuamkia bibi yenu?"
"Hayakuhusu bibi.Sema ulilonalo" bibi
akamkatiza.
"Mh! ngoja nikae kwanza niseme niliyonayo
niondoke,maana leo bibi yenu kawa mkali.Sijui mmemletea pesa!"
Bi Chaurembo aliketi kwenye kiti kilichokuwa pale ukumbini
"Nimekuja kukueleza wewe gunge kwa maana tukiona
jambo ni lazima kwanza tuje tukueleze wewe.Una habari kwamba kuna duka jipya
la mwaarabu limefunguliwa jana kijijini kwetu?"
"Sina habari. Liko wapi hilo duka?" bibi
akamuuliza
"Liko jirani na ile shule. Nasikia yule mwaarabu
alikuwa akikaa Songe.Huko pia ana duka lakini duka amemuachia mwanawe.Yeye
amekuja kuingilia mji wetu bila taarifa.Nimepita leo nimeona duka limejaa
khanga tele na kaniki."
"Usiniambie dadaa!" bibi akang'aka
"Utakwenda kuliona mwenyewe.Nataka leo katika pita
pita zako uende ujifanye unauliza kitu"
"Utanipeleka wewe.Ukiondoka hapa twende mguu kwa
mguu ukanioneshe hilo duka"
"Twende sasa hivi"
"Subiri wageni wangu waondoke twende"
"Kwanza sisi hatukai bibi, tunakwenda zetu.Nataka
nikawahi kupika.Ikifika saa sita tu mume wangu anataka kula" mke wangu
akamwaambia bibi
"Ehee!" bibi akatoa kicheko cha kajeli
"Si mume wako peke yako dada, ni mume wetu sote. Kama ikifika saa sita
anataka kula, mimi nitampikia saa tano"
"Sasa nikuachie niende zangu"
"Kila mtu na zamu yake bibi.Zamu yangu nitakuja
kuipanga mwenyewe.Atakula huku atalala huku lakini leo nendeni zenu.Tukutane
huo usiku.Nataka niende nikaliangalie hilo duka la mwarabu"
Mimi na Chausiku tukaondoka
"Yule bibi yako anachekesha sana.Ananitaka mimi
ataniweza?" nikamwaambia Chausiku wakati tunaenda
"Si anakutania tu, kwani anakutaka kweli"
"Siku moja alinivulia nguo kabisa"
"Sasa ndiyo ungemjaribu uone kama anakuweza"
"Anatafuta mauti bure.........."
"Wazee wa zamani wale wamekula miti mingi.Siku moja
aliniambia ana umri wa miaka mia moja.Ameshakata karne nzima na bado
anaonekana ana nguvu"
"Ni mzee kweli lakini anaonekana katika usichana wake
alikuwa hashikiki"
Chausiku akacheka halafu akanyamaza kimya
"Huko kwa mwarabu wanakokwenda kunawahusu nini?"
nikamuuliza Chausiku
Chausiku akanitupia jicho kali kama vile hakufurahishwa na
swali hilo
"Wenyewe wanajua" akanijibu kwa sauti ya chini
halafu akayabadili yale mazungumzo,akaniambia "Umeona leo umeweza
kugeuka paka?"
"Ni kweli, nyinyi mnadawa kali sana"
"Bado kuna mambo mengi atakufundisha"
"Sasa nitaweza kujigeuza paka kila siku au ni leo
tu?"
"Utaweza kujigeuza kila siku isipokuwa ufuate
masharti.Wewe ni mbishi sana"
"Masharti gani?"
"Wewe hutaki kula nyama za watu mpaka
ulazimishwe.Inatakiwa kwa mwezi ule hata mara moja na usiku utoke kama
wenzako"
Wakati ninazungumza na Chausiku sikujua kuwa arobaini
yangu ilikuwa ikikaribia kwa haraka.
Je nini kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii hapo
kesho hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment