Monday, December 25, 2017

HADITHI, MWANAUME WA KIJINI SEHEMU YA 2

SITASAHAU NILIVYOKUMBANA NA MWANAUME WA KIJINI 2

ILIPOISHIA

Nilipomtajia namba yangu aliiandika kwenye simu yake kisha akanipigia hapo hapo.

Simu yangu ilipoita aliniambia.

“Namba  yangu ndiyo hiyo, ahsante sana”

Hakurudi tena kwenye meza yake akatoka. Kwa vile mtu aliyefanya niamue kuondoka alishatangulia kutoka nikaona niendelee kukaa kidogo.

Lakini sikutimiza hata nusu saa nikainuka na kutoka. Nilirudi nyumbani kwa teksi. Nikafikia kuoga na kujilaza kitandani.
Wakati usingizi unataka kunichukua, simu yangu ikaita. Nilipoichukua na kutazama kwenye sikrini ya simu niliona namba ya yule mzungu. Nikaipokea simu yake.

“Hello!” nikasema kwenye simu.

SASA ENDELEA

“Hello! Mambo vipi?” Sauti ya yule mzungu ikasikika kwenye simu. Nilifurahi alivyoniuliza “Mambo vipi?” Niliona alikuwa mzungu aliyebobea katika lugha ya Kiswahili.

“Poa” Na mimi nikamjibu kwa kutumia lugha ile ile ya mitaani.

“Uko poa kabisa?” akaniuliza.

“Mimi niko poa, sijui wewe?”

“Mimi pia niko poa. Umesharudi nyumbani?”

Mara moja nikagundua kuwa mzungu huyo alikuwa anataka kurefusha mazungumzo.

“Nimesharudi. Hapa niko kitandani” nikamjibu.

“Samahani sana. Mimi naitwa Mr Smith, sijui mwenzangu unaitwa nani?”

“Naitwa Enjo”

“Okey. Jina lako zuri sana. Unaishi wapi?”

“Naishi Sinza”

“Unafanya kazi?”

“Hapana. Kwa sasa niko nyumbani tu”

“Okey. Mimi ni Muingreza. Ninapenda kuja Afrika Mashariki mara kwa mara kutembea. Huwa ninafikia hoteli tu”

“Ndio…ndio”

“Nimefurahi kukufahamu Enjo na ninapenda uwe rafiki yangu”

“Kuna aina nyingi za urafiki, wewe umependelea urafiki wa aina gani?”

“Urafiki wowote tu lakini tutazungumza zaidi tutakapokutana. Enjo una mchumba?”

“Sina mchumba”

“Vizuri. Unadhani tunaweza kukutana wapi kwa ajili ya mazungumzo zaidi”

“Sema wewe”

“Mimi si mwenyeji sana hapa Dar”

“Umefikia katika hoteli gani?”

“Hoteli ya Lux hapa Masaki. Niko chumba namba 35. Unaweza kufika.

Mzungu kanitajia hadi namba  ya chumba chake akidhani ningeweza kwenda kwake.

“Kwanini tusikutane mahali pengine?” nikamwambia.

“Tunaweza. Sasa sema wewe ni mahali gani”

“Ngoja, kesho nitakupigia kukufahamisha”

“Kesho saa ngapi”

Nikafikiri kidogo kisha nikamjibu.

“Kesho mchana”

“Ningefurahi zaidi kama utanitajia saa ili nisubiri simu yako”

“Tuweke saa tano”

“Sawa. Nipige mimi au utanipigia wewe?”

“Nitakupigia mimi”

“Sawa. Nitasubiri simu yako saa tano”

“Nashukuru. Usiku mwema”

“Usiku mwema na kwako”

Nikatangulia mimi kukata simu kisha nikaiweka kwenye kimeza cha mchagoni. Baadaye niliona niizime kabisa kwani sikupenda nikatishwe usingizi wangu kwa milio ya simu.

Usingizi haukuchelewa kunipitia, nikalala. Wakati niko usingizini nikaota niko kwenye ufukwe wa bahari mimi na yule mzungu tukikimbizana huku tukirushiana michanga. Sote wawili tulikuwa tumevaa mavazi hafifu ya kuogelea.

Mimi nilivaa chupi na sidiria yake na mzungu alivaa chupi peke yake. Lakini rangi ya chupi yake na yangu zilikuwa zikifanana.

Baada ya kufukuzana na kuangushana kwa dakika kadhaa tuliingia kwenye maji na kuanza kuogelea kwa pamoja. Tuliogelea hadi tukafika maji mengi.

Mimi nilikuwa nyuma, yule mzungu alikuwa mbele yangu. Ghafla tukajikuta tuko katikati ya bahari. Ule ufukwe wa bahari hatukuuona tena.


Itaendelea kesho hapahapa kuwa nami

No comments:

Post a Comment