Tuesday, February 6, 2018

UNA SIKU CHACHE ZA KUISHI SEHEMU YA 44

HADITHI

UNA SIKU CHACHE ZA KUISHI 44

ILIPOISHIA

Zainush alikuwa akitabasamu.

“Usimpe kero mama” Omar akamwambia Zainush.

“Namkera kwa ajili yako. Hutaki kunisikiliza mimi. Unamsikiliza mchumba wako aliyeko Ujerumani” Zainush akamwambia.

“Umar una mchumba Ujerumani?” Sauti ya Ummi Mariam ikasikika kutoka upande wa pili wa pazia.

“Nilikuwa naye lakini nimeamua kuachana naye”

“Afadhali uachane naye. Zainush atakusumbua na anaweza kumdhuru”

“Sitamuoa tena. Kwanza baba yake ndiye huyo rais wetu anayetaka kuniua”

“Mwache kabisa. Wewe kuwa na Zainush. Utakubali kumuoa Zainush?”

Omar hakujibu.

“Jibu sasa. Utakubali kunioa?” Zainush akamuuliza.


SASA ENDELEA


“Nitakubali” Omar akajibu.

“Mwache aseme kwa hiyari yake, usimlazimishe” Ummi Mariam akasema.

“Amesema amekubali”

“Eti Omar unakubali kwa hiyari yako?”

“Nimekubali” Omar akasema.

“Sawa. Sasa mtapanga wenyewe siku ya kuoana”

“Kwani ni lazima tuoane huku huku?” Omar akauliza.

“Ni hiyari yenu. Mtakavyoamua wenyewe”

“Basi tutapanga na Zainush”

“Sawa”

“Lakini unavyoona, ninaweza kuja kuwa rais?”

“Utakuwa lakini kwa sharti moja”

“Sharti gani?”

“Sharti hilo ni kwamba wakati wote ukuwa kwenye harakati zako uwe sambamba na Zainush” Ummi Mariam alimwambia Omar.

“Nakubaliana na hilo” Omar alimwambia huku akimkubalia kwa kichwa.

“Zainush ni mjanja na anaweza kujigeuza sura za watu mbalimbali. Naamini kwamba atakusaidia sana”

“Mara nyingi anapenda kujigeuza kama mimi na kwa kweli amenisaidia sana”

“Na ataendelea kukusaidia. Yeye anapenda sana uwe rais na yeye awe mke wako”

“Ameshaniambia hivyo”

“Halafu waangalie sana watu walio karibu yako. Baadhi yao ni watu waliopachikwa kukuhujumu wewe na kuhujumu chama chako”

“Mimi sitaweza kuwajua wote lakini nikiwa na Zainush nitaweza kuwajua”

“Usimtegemee  Zainush kwa kila kitu. Zainush ni kiumbe kama wewe. Kuna mambo mengine uwe makini nayo wewe mwenyewe. Umenielewa?”

“Nimekuelewa. Umesema sawa”

“Vile vile mtegemee Mungu”

“Ni kweli”

Pakapita kimya cha sekunde kadhaa kabla ya sauti ya Ummy Mariam kusikika tena.

“Sasa utarudi lini nyumbani kwako?”

Omar akamtazama Zainush.

“Eti Zainush utanirudisha lini?”

“Tutakwenda kupanga sasa hivi, inawezekana ikawa kesho au keshokutwa” Zainush akasema.

“Kwanini unamchelewesha?” Ummi Mariam akamuuliza.

“Ni kwa sababu ya usalama wake. Omar bado anatafutwa”

“Sawa lakini usimuweke sana huku, ukiona hali imekuwa shwari mrudishe haraka”

“Sawa maa”

“Umar urudi salama kwenu” Ummy Mariam alimuaga.

“Asante mama na wewe ukae salama”

“Mimi naitwa Ummy Mariam, mama yake Zainush”

“Nimefurahi kukufahamu”

“Na mimi pia nimefurahi kukufahamu. Ishaallah tutaonana tena”

“Panapo majaliwa”

“Haya Zainush, nendeni. Usiku mwingi, mwenzako anataka kulala” Ummy Mariam alimwambia Zainush.

“Mama naye! Kwani amekwambia ana usingizi?”

“Kwani mpaka aniambie, yeye ni binaadamu usiku analala, si jini kama wewe”

“Omar nyanyuka twende zetu” Zainush akamwambia Omar.

Omar akanyanyuka.

Wakatoka. Wakati wanarudi Zainush akamwambia Omar.

“Vipi unajisikia njaa?’

“Hapana, sihitaji kula saa hizi”

“Au unataka ugali uliouzoea kwenu?”

“Hapana, lile bokoboko nililokula bado nalisikia tumboni”

“Sasa unaonaje tukatembee kidogo?”

“Tukatembee usiku huu?’

“Huku kwetu harakati zinaendelea usiku na mchana”

“Tutakwenda kutembea wapi?”

“Twende gulioni. Nataka nikanunue asali”

“Ni mbali sana”

“Si mbali sana”

“Twende”

 Wakaenda. Kwa vile walikuwa wakitembea huku wakizungumza walikwenda mwendo mrefu bila Omar kujua. Omar aliona barabara za ujinini. Walipishana na punda waliobebeshwa mizigo. Zainush alimwambia Omar punda hao walikuwa wakitoka kwenye gulio.

Pia walipishana na watu mbalimbali weusi na weupe waliokuwa wamevaa mashuka kama waarabu na wengine wako na madevu hadi chini.

Kitu ambacho kilimshangaza Omar ni kuwa kila waliyepishana naye alikuwa na ndevu ndefu zilizokaribia kufika chini.

Zainusha alimtambulisha Omar kuwa hao walikuwa majini wakiwa kwenye harakati zao. Lakini majini hao hawakuwa wakizungumza. Kila mmoja alikuwa akiendelea na hamsini zake kimya kimya.

Hatimaye walifika hapo kwenye gulio. Ulikuwa uwanja ulioonekana kama jangwa. Kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa majini uliokuwa umeshamiri kelele.

Majini walikuwa wakinadi bidhaa zao na wengine wakiuza na kununua. Palikuwa na mitindo tofauti ya biashara, kuanzia ule wa kuuza kwa mnada, kuuza kwa kupatana bei na kuuza kwa kubadilishana vitu, toa mali upewe mali.

Zainush alimwambia Omar pesa zilizokuwa zinatumika ni za falme za  kiarabu, pesa ya India, Ujerumani na China.

“Kwanini zinatumika pesa hizo tu?” Omar akamuuliza.

“Kwa sababu majini hupenda kutembelea katika nchi hizo kununua vitu”

“Una maana bidhaa na vitu ninavyoviona hapa vimetoka katika nchi ulizotaja?”

“Baadhi yake si vyote, vingine vimetoka hapa hapa”

Kulikuwa na vyombo vya kaure na vilivyofinyangwa kwa udongo kama vile sahani, mabakuli, vyungu na mitungi.

Pia kulikuwa na ngozi za wanyama zilizokaushwa, mabusati, miswala, mazulia na vitu vingine ambavyo Omar hakufahamu matumizi yake.

Baada ya kuzunguka pande zote wakiwa wamefuatana pamoja, walitokea kwenye mnada wa asali na uyoga. Zainush akanunua kibuyu cha asali kwa real ya Oman yenye thamani ya shilingi elfu moja.


Wakati wanaondoka Omar alimuona mnunuzi akinunua ndama wa mbuzi kwa kutoa kuku wanne.

Kitu ambacho kilimchusha Omar ni harufu za majini hao ambazo Omar hakuwa amezizoea. Kama vile Zainush aliyaelewa mawazo ya Omar akamuuliza.

“Unasikia harufu tofauti?”

Omar akacheka kidogo.

“Kwanini umeniuliza hivyo?”

“Nimejua kuwa ni lazima utakuwa unasikia harufu ambayo hukuizoea”

“Ni kweli”

“Na wenzako pia wanakusikia wewe una harufu tofauti na wao. Wanakugundua wewe ni binaadamu kwa harufu yako ingawa wewe mwenyewe hujisikii”

“Una maana wameshanigundua kuwa si mwenzao?”

“Wameshakugundua lakini wanakuona uko na mwenyeji wako”

“Unilinde wasije wakanidhuru”

“Hakuna kitu kama hicho”

“Naona umetoa real, umeipata wapi?” Omar akayabadili yale mazungumzo.

“Umeishangaa ile? Mbona nina pesa nyingi za nchi za kiarabu”

“Unazipata wapi?”

“Kote huko ninafika. Wakati mwingine nikiishiwa ninaiba”

“Unaiba? Unaibaje?”

“Ninaiba benki usiku. Ninaingia bila kuonekana na kutoka na pesa”

“Kumbe unafanya hivyo?”

“Lakini mama yangu hajui na sipendi ajue. Unataka kuonja kidogo?”

Zainush alikuwa akiramba ile asali.

“Hebu nipe”

Zainush akampa Omar kile kibuyu cha asali. Omar naye akaionja.

“Tamu kweli”

Hapo hapo kibuyu kikaporwa juu kwa juu. Aliyekipora alikimbia nacho.

Je ni nani aliyekipora kibuyu hicho na nini kitatokea? Usikose toleo lijalo

1 comment: