Uchambuzi huu kutoka magazetini unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita kwa masomo tofauti. Kituo pia kinatoa kozi ya Kiingereza na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Sakata la uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow limemng’arisha Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR- Mageuzi), David Kafulila
baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufichua
ufisadi huo uliohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya
Tanzania (BoT).
Katika sakata hilo, mawaziri wawili
walipoteza nyadhifa zao pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya
Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuwahusisha na sakata
hilo.
Maofisa wengine kadhaa wa Serikali wamesimashwa au kufunguliwa mashtaka kutokana na kuhusika kwao kwenye ufisadi huo.
Sakata hilo lililoteka kwa kiasi kikubwa
mkutano wa Bunge wa 16 na 17 kabla ya kufika bungeni, liliibuliwa na
Gazeti la The Citizen, linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi
Communications Ltd na Kafulila kuwasilisha hoja ndani ya Bunge ili
kujadiliwa.
Tuzo aliyopewa Kafulila jana na Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu unaounganisha asasi za kiraia
zinazotetea haki za binadamu (THIRD-Coalition), ni moja kati ya tuzo tatu zilizotolewa kwa Watanzania walioonyesha ujasiri katika kutetea haki za binadamu nchini.
Kwa mujibu wa THIRD-Coalition, vigezo
vilivyotumika kuwapata washindi hao vilizingatia mazingira ya kazi na
hali hatarishi aliyokutana nayo mshindi wa tuzo hiyo, ikiwamo taarifa
zilizokusanywa kupitia ripoti za matukio ya ukiukwaji wa haki za
binadamu kwa mwaka jana.
MWANANCHI
Vikundi vya uhalifu nchini vyenye muundo ‘Panya Road’ vinazidi kuwapa hofu wananchi kutokana na vitendo vyao vya kutishia amani, utafiti wa Taasisi ya kiraia ya Twaweza umebainisha.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa
jana, yalibainisha kuwa watu wanane kati ya 10 84% wanaamini kuna
uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na vijana wahalifu.
Utafiti huo unaoitwa ‘Je, tuko Salama?’
ulieleza kuwa wananchi watatu kati ya 10 wameshakumbana na wizi ndani
ya kipindi cha mwaka jana, sawa na nusu ya Watanzania wote.
Takwimu za utafiti huo zilikusanywa kwa kuwahoji watu 1,401 kutoka Bara kati ya Februari na Machi mwaka huu.
Katika utafiti huo, wananchi sita kati
ya 10 60%, walisema wamewahi kusikia kuhusu ‘Panya Road’ wakati wananchi
tisa kati ya 10 87% walidai hakuna kikundi kama hicho katika maeneo
yao.
Matokeo hayo yanabainisha zaidi kuwa wananchi bado wanaamini kuwa mfumo wa sheria haufanyi kazi ipasavyo.
“Zaidi
ya nusu ya wananchi (asilimia 53) wanaamini kuwa raia wa kawaida
ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria akitenda kosa, lakini kuadhibiwa kwa
watu wenye kipato cha juu ni vigumu.
“Asilimia
14 wanaamini kuwa watu wenye kipato cha juu wanaweza kuadhibiwa iwapo
watavunja sheria na wengine (asilimia 21) wanaona hilo pia linawezekana
kwa watumishi wa umma,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Ilibainisha kuwa idadi hiyo imeshuka ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2013.
Katika kipindi hicho, asilimia 39 ya wananchi walidhani kuwa watumishi wa umma watakumbana na mkono wa sheria wakitenda kosa.
Ilieleza kuwa pamoja na hayo yote,
wananchi sita kati ya 10 (asilimia 60), wanaamini Jeshi la Polisi
linawahudumia zaidi watu wenye fedha kuliko wa kipato cha chini.
Utafiti huo wa maoni ya wananchi juu ya
usalama na haki ni sehemu ya mfululizo wa tafiti zitokanazo na mradi wa
Sauti za Wananchi.
MWANANCHI
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya
leo atawasilisha mwelekeo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2015/16 inayotarajiwa kuwa na ongezeko la kati ya asilimia 15 na 16,
akidokeza kuwa “imewakumbuka wafanyakazi na huduma za jamii” na wafanyakazi.
Serikali pia imesema fedha nyingi kwenye
bajeti ya mwaka huu hazitaelekezwa kwenye Uchaguzi Mkuu unaotakiwa
kikatiba kufanyika wiki ya mwisho ya Oktoba, ikisema kuwa fedha hizo
zilishatengwa kwenye bajeti inayoisha mwaka huu.
Mwaka 2014/15, Serikali ilipanga kutumia
asilimia 27 ya bajeti yake ya Sh18.2 trilioni kwa ajili ya malipo ya
mishahara ya wafanyakazi, ikiwa ni ongezeko la asilimia moja ya kiwango
kilichotumika mwaka wa fedha uliopita.
Bajeti ya mwaka huu wa fedha ni Sh19.8
trilioni na hivyo ongezeko hilo la asilimia 16 kwa kiwango cha juu,
yaani asilimia 16, litamaanisha bajeti ya Sh23.03 trilioni.
“Vipaumbele tumeelekeza kwenye huduma za jamii na pia tumewakumbuka wafanyakazi,” , Saada Mkuya, lakini hakutaka kutoa ufafanuzi zaidi wa viwango vya ongezeko hilo kwa wafanyakazi na huduma za jamii.
Mkuya alisema Serikali imekusudia
kupunguza utegemezi wa wafadhili kwenye bajeti kwa kuongeza makusanyo ya
kodi kutoka vyanzo mbalimbali nchini.
“Serikali
lazima ijitegemee hatuwezi kusimamisha huduma za jamii, barabara na
mambo mengine… fedha kwa ajili ya uchaguzi na kwa ajili ya Serikali mpya
zipo,” Mkuya.
Kwa mujibu wa bajeti ya 2014/15, mapato
mengi ya Serikali yalitegemea makusanyo ya kodi, ambayo yalikuwa
asilimia 61 na misaada na mikopo ya kibiashara ya nje, misaada mikopo
nafuu ya miradi ya maendeleo na misaada na mikopo ya kibajeti ambayo kwa
pamoja ilikuwa asilimia 28 ya bajeti.
Taarifa iliyotolewa juzi na Idara ya
Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ya Ofisi ya Bunge
inasema kuwa leo Mkuya atatoa mwelekeo huo kwa Kamati za Bunge za sekta
mbalimbali.
Mwelekeo wa bajeti unatolewa kwa mujibu wa kanuni za Kudumu za Bunge Ibara ya 97 toleo namba 2013.
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amezindua meli mbili kubwa za kisasa za kivita na kuzikabidhi kwa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji.
Uzinduzi wa meli hizo zenye mizinga
mikubwa miwili na ya kawaida sita kila moja, na uwezo wa kupiga
makombora umbali wa kilometa saba angani na kilometa tisa chini,
ulifanywa jana, makao makuu ya kamandi hiyo yaliyopo Kigamboni jijini
Dar es Salaam.
Rais Kikwete, alisema meli hizo zina
ukubwa wa takribani meta 60 hivyo kuwezesha usalama wa uhakika katika
ukanda wa bahari wa Tanzania dhidi ya maharamia.
Alisema uzinduzi wa meli hizo unaifanya
Tanzania kuandika historia mpya ya kuwa na meli za kivita na zenye
ukubwa wa jinsi hiyo kwa mara ya kwanza tangu kupatikana kwa uhuru,
hivyo kurahisisha usalama wa ukanda wa bahari wa Tanzania ambao kwa
sehemu kubwa ulikuwa unahujumiwa na maharamia wakiwamo wa kutoka nchini
Somalia.
Meli hizo zilizopewa majina ya melivita P77 Mwitongo
kuwakilisha eneo alilozaliwa kiongozi wa kwanza wa Tanzania, hayati
Julius Nyerere na melivita P78 Msoga, eneo alilozaliwa Rais Kikwete.
Alisema awali kamandi hiyo ilikuwa
inakabiliwa na changamoto ya kuwa na meli za kivita zenye uwezo wa
kwenda masafa marefu kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi ndani ya
ukanda wa bahari ya Tanzania kutokana na meli zilizokuwapo kukosa uwezo
huo kwani zote zilikuwa chini ya urefu wa mita 60 ambao ndiyo
unaotakiwa.
“Meli
hizi zinafanya tuandike historia mpya ya kuwa na meli kubwa na za kisasa
kwa mara ya kwanza nchini…..rasilimali zetu nyingi zikiwamo samaki
zimeibwa sana ndani ya ukanda wa bahari yetu kutokana na meli zetu
kukosa uwezo wa kukabiliana na vitendo vya uharamia dhidi ya maharamia
na wezi wa samaki wetu……lakini kwa hizi, zinatuhakikishia usalama kwa
arasilimali zetu,” Rais Kikwete.
Meli hizo ambazo zimepatikana kwa
ushirikiano kati ya Serikali ya China zina uwezo wa kusafiri siku saba
umbali mrefu bila kuongeza mafuta.
Pia zina uwezo wa kupiga makombora kwa umbali wa kilometa saba kwenda juu na chini kilometa tisa.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi,
alisema, meli hizo zitakuwa tegemeo kubwa katika kulinda eneo la maji
ya Tanzania na rasilimali zake ikiwamo gesi asilia kwani zina uwezo wa
kasi kubwa katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu vya uharamia.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usama nchini, Jenerali Davis Mwamunyange,
alisema, lengo la kuwa na meli za jinsi hiyo ni katika jitihada za
kuhakikisha jeshi la nchi linakuwa na silaha za kisasa za kivita na
kutoa mafunzo.
NIPASHE
Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia , ameitaka serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT),
kuchukua hatua haraka na madhubuti kunusuru kuporomoka kwa thamani ya
Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani ambayo imeporomoka kwa
asilimia 21.
Mbatia alisema sababu zilizochangia
kuporomoka kwa Shilingi ni Bajeti tegemezi kwa wafadhili, mauzo kidogo
kutoka ndani kwenda nje ya nchi, manunuzi makubwa kutoka nje kuja ndani
na siasa zisizokuwa na hofu ya Mungu.
“Ndani
ya mwezi mmoja Shilingi yetu imeporomoka kwa zaidi ya asilimia 20 hadi
21 kutoka Sh. 1,650 kwa Dola moja ya Kimarekani hadi Sh. 2,010 kwa
takwimu za juzi, poromoko hili ni tishio kwa uchumi. Sayansi anuai
inatuonyesha kwamba nguvu ya mporomoko wa kiasi hiki inaweza kutikisa
vibaya mfumo wa uchumi kama hatua za kifedha hazitachukuliwa haraka
iwezekanavyo,”
Mbatia alisema bajeti ya Taifa kwa kiasi
kikubwa, zaidi ya asilimia 30 inategemea fedha za wafadhili wa miradi
mbalimbali ambao wanapoamua kushikilia fedha zao, poromoko la Shilingi
hutokea na inapokuwa kinyume wanashikilia fedha yao.
Alisema ni lazima BoT itoe matumaini kwa Watanzania kuhusu hali ya uchumi kabla hali haijawa mbaya zaidi.
“Uchumi
ni kushirikiana katika kutumia rasilimali za dunia ili kuishi katika
hali ya utu tuliokirimiwa na Mungu. Tunao wajibu wa kushiriki kikamilifu
katika uchumi wa dunia kwa sababu rasilimali tulizonazo juu ya ardhi na
ndani ya ardhi, ushirikiano wa kibiashara ni sehemu ya maisha,” Mbatia.
Alisema ni lazima Tanzania ijitambulishe kwa Shilingi yake kwa kuhakikisha inalindwa isiporomoke dhidi ya Dola ya Marekani.
Mbatia alisema uwezo wa kuongeza mapato
ya Tanzania kutoka mauzo ya nje ni mkubwa kwa kupitia sekta za uvuvi,
utalii na usafirishaji wa anga na kwamba zinaweza kutumika ili kuongeza
fedha kutoka nje na kukabili poromoko hilo.
“Kanuni
kuu ya maisha ni mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe, naomba
tujiulize kwanini tunatumia Dola katika shughuli zetu za kibiashara
ndani ya nchi? Hii inaitwa ‘dollarization’, athari zake ni kubwa kwa
uchumi na wananchi. Ni lazima tuwe na sheria ya kuzuia ‘dollarization’,
na huu ndiyo muda mwafaka kwa usalama wa nchi yetu,” alisema.
Alisema kwa hali ilivyo nchini kwa sasa,
Mtanzania anayepokea Sh. milioni moja, thamani yake ni Sh. 800,000,
huku posho za viongozi wanaposafiri nje ya nchi kwa kutumia ndege kwa
daraja la kwanza na pili kwa siku ni Dola 504 ambayo awali ingekuwa Sh.
600,000, lakini kwa sasa ni milioni moja kwa siku.
Alisema atapeleka hoja bungeni ya
kuitaka serikali kuchukua hatua ikiwamo kuacha kuagiza samani na bidhaa
nyingine ambazo zinaweza kupatikana nchini kutoka nje ya nchi.
Mbatia alisema hali inazidi kuwa mbaya
nchini pale serikali inapokwenda kukopa kwenye taasisi binafsi za fedha
na watu binafsi pia kufanya hivyo na kuzifanya taasisi hizo kuitunishia
misuli serikali.
“Tuendako na hali ikiachwa kuwa hivi,
nchi inaweza isitawalike, wafanyabiashara wakubwa wanaacha kuwekeza
nchini na kuzalisha bidhaa za kuuza nje, bali wananunua nje na kuuza
ndani kwa wingi,” alisema.
Saada Salum Mkuya alisema kiasi cha Dola
kilichopo kwenye mzunguko siyo cha kudhuru uchumi na kwamba athari
zinazojitokeza kwa Shilingi haiko Tanzania pekee bali imezikumba nchi
nyingi ikiwamo Uganda na nyingine zinazotumia Euro na paundi.
Alisema kuporomoka kwa Shilingi
kunasababishwa na kuimarika kwa uchumi wa Marekani na kudorora kwa
biashara ya utalii ambayo ndiyo inayoingiza fedha nyingi za kigeni.
Mkuya alitaja sababu nyingine kuwa ni
tishio la ugaidi na kuagiza bidhaa zaidi kutoka nje kuliko kuuza nje na
wafanyabiashara wakubwa kuamini kuwa na Dola nyingi ndiyo faida kubwa.
NIPASHE
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani
hapa, kimempa muda wa siku mbili Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Leonard Paul, kuwaachia watu 20 waliokamatwa kwa tuhuma za kumjeruhi
askari polisi Koplo Ramadhani, vinginevyo wataitisha maandamano.
Akizungumza na waandishi wa habari wmjini hapa jana, Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Morogoro, James Mkude,
alisema kitendo cha polisi kuvamia eneo la Mindu na kukamata watu ambao
walikuwa katika maeneo hayo bila kuchunguza kama walihusika ama
hawajahusika katika tukio hilo hakikubaliki.
Alisema Chadema haitetei uhalifu wa aina
yoyote ile, lakini Jeshi la Polisi lilipaswa kuwatuma makachero wake
katika eneo hilo kwenda kufanya uchunguzi kubaini waliohusika na tukio
hilo na siyo kukamata kila mtu waliyemkuta na kuwaweka ndani pasipo
kuwapa dhamana au kuwafikisha mahakamani.
Alisema endapo waliokamatwa hawataachiwa
au kufikishwa mahakamani, Chadema itafanya maandamano makubwa ikiwamo
kushirikisha wenye bodaboda ambao askari hao wamekuwa wakiwaonea na
kwenda katika makao makuu ya polisi mkoa kushinikiza kuachiwa kwa
watuhumiwa hao.
Wiki iliyopita askari huyo anayeendesha
pikipiki ya polisi maarufu ‘Polisi wa Tigo” akiwa kazini alijeruhiwa na
watu wasiojulikana baada ya kupigwa na kitu butu kichwani wakati akitaka
kumkamata kijana wa bodaboda aliyekuwa akimkimbia.
Kijana huyo wa podaboda wakati akijaribu
kukimbia aligongana na gari lililokuwa karibu na polisi huyo alipofika
alipigwa na kitu kichwani na kisha watu hao kuchukua pikipiki ya
bodaboda kwa lengo la kuificha.
MTANZANIA
Kikao cha viongozi wa vyama vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kimeshindwa kuendelea baada ya
baadhi ya wajumbe kushindwa kuafikiana kuhusu hoja iliyowasilishwa na
Chama cha NCCR-Mageuzi, ya kutaka kujitoa kwenye umoja huo, imefahamika.
Viongozi hao walikutana jijini Dar es
Salaam jana katika Ofisi Kuu ya Chama cha Wananchi (CUF), ambapo pamoja
na mambo mengine walikuwa wakijadili hatima ya kuachiana majimbo
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Katika kikao hicho ambacho kilitarajiwa
kuanza saa 4 asubuhi kama ilivyokuwa imepangwa na badala yake kilianza
saa 6 mchana, ajenda kuu zilikuwa ni kujadili namna ya kuachiana majimbo
ambayo bado mwafaka haujapatikana pamoja na utaratibu wa kumpata
mgombea urais kupitia Ukawa.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya
kikao hicho kilichokuwa chini ya Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, ambaye pia
ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kilishindwa kutoa
mwelekeo wa majimbo 18 yenye mvutano huku kila chama kikitaka kugombea
kivyake.
Hata hivyo hoja hiyo iliibua mvutano
mkali baina ya wajumbe wa kikao hicho ambapo kwa upande wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ujumbe wake uliongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe, Katibu Mkuu Dk. Willibrod Slaa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho Tundu Lissu.
Kwa upande wa CUF, ujumbe wake uliongozwa na Prof. Lipumba, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya na Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Shaweji Mketo.
NCCR-Mageuzi kiliongozwa na Mwenyekiti wake James Mbatia ambaye baada ya kuwasilishwa hoja ya chama chake alishindwa kuendelea na kikao na kulazimika kutoka nje ya ukumbi wa mikutano.
“Mwanzo
tulianza kujadili suala la uandikishaji wapigakura kwa mfumo wa BVR na
changamoto zake zilizojitokeza pamoja na hatima ya uwezekanao wa kuwapo
kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu.Pia tulijadili kwa kina mwendelezo
wa ugawaji wa majimbo yaliyobaki, lakini hata hivyo tuliacha ajenda hiyo
kutokana na kuibuka kwa hoja nzito kwa kila upande,”
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho
zinapasha kuwa ilipotimu saa 7 mchana, aliingia Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, Mbatia, ambaye alishiriki katika hatua za awali za
majadiliano hayo, lakini ilipofika saa 9:20 aliondoka kabla kuwasilishwa
hoja ya chama chake kutaka kujitoa Ukawa.
Hata hivyo wajumbe walishindwa kuendelea
na kikao hicho kutokana na NCCR-Mageuzi kutokuwa na mjumbe ambaye
angeweza kueleza kwa undani sababu za kutaka kuchukua uamuzi wa kujitoa.
“Hoja iliyokuwa katika ajenda ni ya
NCCR-Mageuzi waliyowasilisha ya kutaka kujitoa Ukawa na dai lao kuu ni
kutotendewa haki kwa baadhi ya mambo, hasa katika Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa uliopita.
“Na hili jambo si geni kwani mnapokuwa
kwenye jumuiya yoyote inawezekana ikatokea hali ya kutoelewana kwa
baadhi ya wajumbe kwa kuona kuna sehemu kuna mmoja anaona hajatendewa
haki.
“Na jambo ambalo lilitakiwa ni
kuzungumza na kulimaliza ili watu wasonge mbele, na NCCR-Mageuzi
walileta kama malalamiko… siwezi kulizungumzia vizuri kwa sababu
halijazungumziwa kwa undani kwenye kikao,” kilisema chanzo chetu.
Mtoa habari wetu alisema kikao hicho
kilitarajiwa kumalizika jana usiku, lakini kutokana na hoja ya
NCCR-Mageuzi, ilimlazimu Mwenyekiti wa kikao hicho Profesa Lipumba
kukiahirisha saa 11 jioni hadi leo ambapo kitaendelea.
Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kinachoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi.
Hivi sasa joto la kuwatangaza wagombea
urais ndani ya vyama vinavyounda Ukawa pamoja na Chama Cha Mapinduzi
(CCM) linazidi kupanda huku kila upande ukimvizia mwenzake katika
kutangaza mgombea nafasi hiyo.
MTANZANIA
Wafanyakazi milioni 2.3 duniani wanafariki dunia kila mwaka kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi Duniani.
Alisema takwimu hizo ambazo ni kwa
mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kwamba kila sekunde
15 mfanyakazi mmoja anafariki kutokana na ajali au magonjwa duniani
kote.
“Aidha zaidi ya wafanyakazi milioni 160
wanapata magonjwa yanayohusishwa na kazi, takwimu ambazo zinatuonyesha
kuwa kila baada ya dakika 15 wafanyakazi 153 wanapata magonjwa duniani
kote,” alisema.
Dk. Mahanga alisema ajali na magonjwa
yanayotokea sehemu za kazi kutokana na kutokuboresha mazingira
husababisha gharama kubwa kwa ajili ya matibabu, malipo ya fidia,
uharibifu wa mali mbalimbali na kupotea kwa muda wa uzalishaji.
“Suala la kutoa elimu ya kujikinga na
ajali na magonjwa yatokanayo na mazingira mabaya ya kazi ni jambo la
msingi kwa kuwa jambo linalosababisha ajali kwa kiwango kikubwa
linatokana na makosa ya kibinadamu,” alisema.
Aidha alisema mojawapo ya magonjwa
yatokanayo na kazi ni maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na
magonjwa yasiyoambukizwa.
“Suala la janga la Ukimwi ni sehemu ya
usalama na afya mahali pa kazi kwa sababu nguvu kazi inayotegemewa na
nchi ndiyo iliyoko kwenye hatari ya kuambukizwa VVU,” alisema.
MTANZANIA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeshindwa kupitisha hesabu za Mkoa wa Rukwa baada ya kubaini kuwapo ufisadi katika baadhi ya matumizi za fedha za Serikali.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Amina Mwidau, alisema ufisadi huo umebainika katika hesabu za mwaka 2012/13.
Mwidau alisema Sh 44,394,927 zimetumika kumlipa mzabuni Julius Akilimali kwa ajili ya matengenezo ya gari lenye namba za usajili STK 5508 bila ya kuonyesha vielelezo vya matumizi ya fedha hizo.
Alisema malipo hayo yametumika ndani ya mwaka mmoja, jambo ambalo limewafanya wajumbe wa kamati hiyo kuwa na shaka.
“Tumeshindwa kupitisha hesabu za Mkoa wa Rukwa baada kubaini kuwapo upungufu wa hesabu zao, hatukubaliani na hali hii,” Mwidau.
Alisema licha ya kufanyika kwa malipo
hayo, kamati hiyo imebaini magari kumi ya Serikali yaliyotolewa kwa
shughuli mbalimbali ndani ya mkoa huo, matatu yameuzwa bila ya kuonyesha
viambatanisho.
Mwidau alisema mkoa huo pia umetumia Sh
milioni 20, kwa ajili ya kuchapisha vitabu wakati wa maadhimisho ya
sherehe za Uhuru mwaka 2012 bila ya kuambatanisha vielelezo vya matumizi
ikiwamo risiti.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati
imewapa wiki tatu kutafuta nyaraka zote zilizotajwa kwenye kikao hicho
na kuziwasilisha Mei 15, mwaka huu mkoani Dodoma ili wajumbe wa kamati
waweze kuzipitia.
Hata hivyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa
Rukwa, Smythies Pangisa alikiri kuwapo udhaifu kwa baadhi ya watendaji,
jambo ambalo limesababisha baadhi ya vyaraka kutoonekana.
“Ni kweli kuna tatizo kwa baadhi ya
watendaji wetu ambao wameshindwa kuweka kumbukumbu sahihi za matumizi ya
Serikali, suala hili nitalishughulikia kabla ya kuwasilisha taarifa hii
mjini Dodoma,” alisema Pangisa.
Alisema kutokana na hali hiyo, watendaji
ambao watabainika kwenda kinyume watachukuliwa hatua za kinidhamu ili
iwe fundisho kwa wengine.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete leo
anaongoza waombolezaji, wakiwemo viongozi mbalimbali wa nchi za Kusini
mwa Afrika, katika maziko ya Brigedia Jenerali mstaafu, Hashim Mbita yatakayofanyika jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wa nje wameanza kuwasili
nchini tangu jana, ambapo watashiriki katika maziko yanayofanyika katika
makaburi ya Kisutu.
Akizungumza juzi msibani hapo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
alisema wameshapokea uthibitisho wa ushiriki wa Waziri wa Mambo ya Nje
na wakuu wa majeshi wa Namibia, maofisa wa juu wa Jeshi la Zimbabwe na
viongozi wengine.
“Nadhani
atakayeongoza ni Mheshimiwa Rais na ndiyo sababu ya haya mazishi
kufanyika siku ya Jumatano kwa sababu kesho (jana) amebanwa na kazi
nyingi na ndiyo sababu ya kuomba,” Membe.
Aidha, alisema, wageni wengine ni
wajumbe wa Kamati Kuu ya chama tawala cha Msumbiji cha Frelimo na
wajumbe wa nchi za Zambia, Afrika Kusini na Umoja wa Afrika (AU).
Akimzungumzia Mbita, Membe alisema
atakumbukwa kama mkombozi wa nchi nyingi za Afrika hasa za Kusini, hali
iliyomjengea umaarufu kwa kuwa katika miaka ya 1990 nchi zote za Afrika
zilikuwa huru, isipokuwa Afrika Magharibi.
Alisema jambo la faraja ni kwamba
Brigedia Mbita ameacha matoleo nane ya vitabu vinavyozungumzia masuala
ya ukombozi wa nchi za Afrika, ambavyo vitaendelea kuweka historia yake
kwa vizazi vijavyo.
“Ni
mtu mwenye heshima kubwa sana, na ndiyo sababu yeye kutunukiwa tuzo ya
Monomotapa ya Msumbiji ambayo ni kubwa sana, hapa Tanzania alipata yeye
na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.
Alisema, wizara yake itaanza kuchapisha
makala za Brigedia Mbita ili jamii na vizazi vijavyo viweze kumfahamu
shujaa huyo. Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo,
Zitto Kabwe alisema kila Mtanzania anapaswa kumtambua Brigedia Mbita,
kutokana na mchango wake katika ukombozi wa nchi nyingi.
“Ni
mtu ambaye Mungu amemwezesha kutimiza mambo magumu ambayo wengine
hawawezi kuyatimiza, ametuachia funzo kubwa sana juu ya kuwa wazalendo
na nchi zetu,” Zitto.
Zitto alishauri Barabara ya Kilwa iitwe
jina la Mbita, ikiwa ni hatua ya kuendelea kumuenzi kwa kuwa inaelekea
nchi ambazo alishiriki ukombozi wake.
Brigedia Mbita alifariki Jumapili katika
Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, alikokuwa amelazwa kwa matibabu bada ya
kuugua kwa muda mrefu.
Mwanasiasa huyu mkongwe aliyeacha mke na
watoto, mwili wake unaagwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kabla
ya maziko kufanyika makaburi ya Kisutu.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment