Magazeti yanaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wale ambao wanajiendeleza kielimu. Kituo kimesajiliwa na NECTA. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 7727246
Siku 17 baada ya madereva wa mabasi mchini kugoma na kutikisa nchi, Chama cha Wamiliki wa Mabasi yaendayo mikoani (TABOA) kimetangaza mgomo mwingine nchi nzima.
Mgomo wa Aprili 9, mwaka huu uliodumu
kuanzia alfajiri hadi saa 7:00 mchana ulitikisa nchi na kuwaathiri
abiria wengi waliokuwa wanasafiri kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.
Jana Taboa walitangaza kusitisha utoaji
huduma kuanzia kesho ikiwa ni hatua ya kupinga nauli mpya za mabasi
zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).
Kufuatia hali hiyo, Taboa kimewataka
mawakala kutokatisha tiketi kuanzia leo kwa abiria hadi hapo Sumatra
itakapotoa taarifa za kuruhusu nauli ya zamani ziendelee kutumika.
Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, alitoa taarifa hiyo jana wakati akitoa majumuisho ya mkutano mkuu wa dharura uliojumuisha wadau wa usafirishaji.
Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu tatu
ambazo ni ajali za barabarani, nauli mpya zilizotangazwa na Sumatra,
madaraja ya mabasi, mgomo wa madereva na vituo vya kubadilishia madereva
wanaokwenda umbali mrefu.
“Kesho
hakuna gari ambalo litatoka kituo cha mabasi Ubungo kwenda mkoani na
kama tutapigwa mabomu tupigwe, ila msimamo wetu uko pale pale wa kutotoa
magari hadi Sumatra watakapotoa tamko la kutaka nauli za awali
ziendelee kutumika,” alisema.
Kuhusu ajali, alisema kutokana na
kukithiri kwa ajali za mabasi, wanakubaliana na utaratibu uliowekwa na
serikali wa madereva kubadilishana wanaokwenda masafa marefu katika
vituo ambavyo vitatengwa ili kupunguza ajali hizo.
MWANANCHI
Kiganja cha mtoto Baraka Cosmas mwenye ulemavu wa ngozi kilichokatwa Machi 8 kwenye kijiji cha Kipeta Sumbawanga kimepatikana mwishoni mwa wiki Wilayani Mbozi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi alisema kiganja hicho kilipatikana kutoka kwa mkazi wa kijiji cha Malonje Sajenti Kalinga ambaye anafanya kazi ya Useremala.
Alisema awali walimkamata mganga mganga
wa kupiga ramli ambaye ndiye aliyehusika kukata kiganja hicho na baada
ya kumbana Mganga huyo alimtaja Kalinga ndiye aliyemtuma kuleta kiganja
hicho cha albino.
“Tulimbana mtuhumiwa akatuambia aliyemtuma ni Kalinga kwa dau la milioni 100″ Msangi.
“Polisi walifika kwa mtuhumiwa Kalinga na walipomuhoji kwa kina alikitoa kiganja hicho na kuwakabidhi”
Hadi juzi watu sita walishikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo wakiwemo waliokamatwa mwaka jana na wengine mwaka huu.
MWANANCHI
Helkopta ya Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, imeleta kizaazaa, baada ya Kada wa CCM, Buni Ramolle
ambaye aliikodi kwa ajili ya mikutano yake ya kutangaza nia ya kugombea
ubunge katika jimbo hilo, kudai kuwa ni mbovu na ilitaka kumuua.
Kada huyo akaenda mbali na kueleza kuwa kutokana na hitilafu hiyo, ameitaka kampuni ya General Aviation Services (T) Ltd, iliyomkodishia
helkopta hiyo, kumrejeshea fedha zake zote alizoilipa kwa ajili ya
kuitumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
Oktoba mwaka huu.
Hata hivyo, Ndesamburo ambaye ni mmiliki
wa helkopta hiyo kupitia kampuni yake ya Keys Aviation, alikanusha
madai hayo akisema kuwa hayana msingi.
“Anasema helikopta ni mbovu wakati ilimpeleka na kumrudisha? Alihoji Ndesamburo na kusisitiza kuwa “tutawaomba wakaguzi wa ndege waifanyie ukaguzi na ripoti hiyo ndio tutaitumia kumshitaki nayo.”
Kuhusu madai ya Ramolle kuwa amerejeshewa fedha zake alizolipa, Ndesamburo alihoji “Tunamrudishia fedha gani wakati hakulipa? Kuwa na Proforma Invoice ndio kulipia?”
Awali taarifa zilieleza kuwa Ramolle
alitoa tuhuma hizo, baada ya viongozi wa CCM, kumbana wakimtaka aeleze
kwa nini ameamua kutumia helkopta ya Ndesamburo ambaye ni mpinzani wake
kisiasa.
Lakini tayari Ndesamburo mwenyewe
ameshajitokeza hadharani na kudai kuwa helkopta hiyo ni mali yake na
kwamba ameingia mkataba wa kuikodisha kwa kampuni ya General Aviation
Services (T) Ltd.
Kwa mujibu wa Ramolle, kinachofanyika
sasa ni mbinu za kumchafua ndani ya chama ili asiaminike na aenguliwe
kama alivyoenguliwa mwaka 2010.
Ramolle alisema kutokana na Ndesamburo
kudai helkopta hiyo ni yake, tayari kampuni ya General Aviation Services
wamemrudishia fedha zake alizokuwa amekodishia na ameishtaki kampuni
hiyo kwa Meneja wa TRA mkoa wa Kilimanjaro kutokana na kutompa risiti ya
malipo aliyoyafanya.
MWANANCHI
Mwanasiasa na mkongwe aliyewahi kuwa waziri katika Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, Njelu Kasaka amekishauri chama chake cha CCM
kuwaruhusu wanachama wanaotaka kuwania urais kujitangaza ili kutoa muda
wa kutosha kwa wananchi kuwachambua na hatimaye kumpata kiongozi bora
mwenye uwezo wa kuongoza nchi.
Chama hicho tawala, kimewapiga ‘kufuli’ makada wake sita, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kwa madai ya kufanya kampeni mapema.
Lakini ushauri huo wa Kasaka, aliyewahi pia kuwa mkuu wa mkoa, umetulipiwa mbali na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ambaye amesisitiza kwamba hawawezi kufuata maoni hayo, bali wataendelea na utaratibu wa vikao katika kumpata mgombea wake.
Nape alisema: ‘‘Chama kina utaratibu wa vikao na ndiyo utakaofuatwa. Maoni ya Njelu Kasaka ni haki yake.” Alipoulizwa ni lini vikao vya uteuzi vitaanza, alijibu kwa mkato “bado.”
Akizungumza kwa simu jana, Kasaka
alisema hivi sasa hatua ya kujitangaza imecheleweshwa na kwamba
kinachotakiwa ni ifikapo Julai mwaka huu, mgombea urais awe
ameshapatikana baada ya wananchi kumpima uwezo wake.
“Hatuwezi
kuambiwa na mtu mwingine uwezo wa mgombea urais, bali tunataka kusikia
kutoka kwake kwani atatakiwa kututhibitishia yeye mwenyewe na wananchi
wakamsikiliza na kumpima kuona kama anakidhi kuendesha nchi na
kukabiliana na matatizo tuliyonayo,” alisema.
Kasaka alisema hatua ya wagombea
kuchelewa kujitangaza italeta athari itakayokigharimu chama chake na
nchi kwa ujumla huku akisema ni vigumu kumpata kiongozi bora atakayekuwa
ameteuliwa na viongozi pekee.
Alisema kuwa CCM itamtoa mgombea
anayekubalika, aliyefuata maadili, taratibu na kanuni za chama katika
utekelezaji wa majukumu yake.
MWANANCHI
Koplo Laura Mushi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ni miongoni mwa Watanzania 42 waliotunukiwa nishani na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu juzi Dar es Salaam.
Laura alitunukiwa Nishani ya Ushupavu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika hafla hiyo Rais Kikwete alitunuku Nishani ya Kumbukumbu ya
miaka 50 ya Muungano Daraja la Pili, la Tatu na la Nne, Nishani ya
Muungano Daraja la Pili na Nishani ya Ushupavu.
Kabla ya kupokea nishani hiyo, ilielezwa kwamba usiku wa Machi 14
mwaka huu, Koplo Laura , akiwa kwenye kituo chake cha ulinzi, alivamiwa
na kundi la majambazi waliomkaba kwa kamba na kumburuza kwa lengo la
kutaka kumuua na kupora bunduki aliyokuwa nayo ikiwa na risasi 30.
Ilielezwa kwamba wakati majambazi hao wakimburuza kutoka katika lindo
lake, Koplo Laura alijitahidi na kufanikiwa kudhibiti kamba hiyo
isimnyime pumzi kwa kuwa walikwisha mfunga shingoni, huku akipambana
kuzuia asinyang’anywe bunduki aliyokuwa nayo na kufanikiwa.
Alifanikiwa kuidhibiti kamba hiyo na kisha kuifikia chemba ya risasi ya bunduki na kuweza kufyatua risasi nne huku akiburuzwa.
Hali hiyo iliwafanya majambazi hao kumwachia na kukimbia, hivyo kuokoa maisha yake na silaha aliyokuwa nayo.
“Kitendo hicho kimeonyesha ushupavu, uzalendo na heshima ya hali ya
juu kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wanawake wote nchini,” alisema
mshereheshaji wa shughuli hiyo.
Akizungumza baada kupokea tuzo hiyo, Koplo Laura alisema: “Sikutarajia
kupata nishani hii, imenitia moyo, nguvu na morali zaidi wa kufanya
kazi kuilinda nchi yangu, pia kuonyesha kwamba inawezekana kila palipo
na juhudi. Ninamshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kutambua mchango wangu.”
Katika hafla hiyo, watu wengine wa kada mbalimbali wakiwamo
wanasiasa, watumishi wa umma pia wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama
wastaafu na majaji wastaafu walitunukiwa nishani.
Kupitia nishani hizo, Rais Kikwete pia amemkumbuka marehemu Brigedia Jenerali Moses Nnauye aliyekuwa Katibu wa Oganaizesheni wa CCM na mwasisi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), aliyetunukiwa Nishani ya Kumbukumbu ya Muungano Daraja la Tatu.
HABARILEO
Serikali imetenga Sh bilioni tisa kwa
ajili ya posho ya kujikimu na nauli kwa ajili ya walimu 31,056 na
mafundi sanifu maabara 10,625, ambao ajira zao zimetangazwa jana huku
wakitakiwa kuanza kazi Mei Mosi mwaka huu.
Aidha, watumishi hao wapya,
wamehadharishwa juu ya ucheleweshaji, wakiambiwa kwamba, atakayeripoti
mwisho wa mwezi wa Mei, hatapokewa isipokuwa, kama ana matatizo
yanayotambulika.
Wakati kawaida walimu wapya hupangiwa
halmashauri ambazo ndizo zenye jukumu la kuwapangia vituo vya kazi, kwa
upande wa walimu wa sekondari wa masomo ya Sayansi na Hisabati ambao
idadi yao ni 2,700, wamepangwa moja kwa moja kwenye shule ambazo hazina
walimu.
Hayo yalibainishwa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Jumanne Sagini
alipokuwa akielezea kile alichosema ni sababu za kiufundi za kushindwa
kutangaza majina ya ajira mpya za walimu Aprili 24, mwaka huu kama
ilivyokuwa imetangazwa awali.
Katika kuhakikisha kunakuwa na uwiano
sawa wa walimu na wanafunzi, halmashauri zilizojitosheleza au zenye
idadi ya kuridhisha ya watumishi hao, hususani za mjini, hazikupangiwa
kabisa walimu.
Posho Alisema fedha hizo ambazo ni posho
ya kujikimu kwa siku saba na fedha za nauli zinatakiwa kulipwa na
halmashauri ambao ni mwajiri. Zinatakiwa kulipwa ndani ya siku saba bila
kuzidi siku 14 tangu kuripoti kwa mtumishi katika kituo cha kazi.
“Mwenye
jukumu la kutuma fedha kwenye halmashauri ni Wizara ya Fedha. Lakini
tumeziambia halmashauri zihakikishe zinalipa walimu ndani ya siku 14
tangu kuripoti na tuna uhakika kwamba halmashauri zina fedha,” alisema.
Alisema upo mfumo katika Tamisemi, ambao
unaangalia fedha zilizoko katika halmashauri jambo alilosisitiza kwamba
wanao uhakika kwamba zipo kuwezesha malipo hayo.
HABARILEO
Ikulu imesema Rais Jakaya Kikwete
atasaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, kwa kuwa
umepitia taratibu zote. Pia, Ikulu imesisitiza kuwa sheria hiyo ni nzuri
na itadhibiti matumizi mabaya ya mtandao.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alitoa taarifa hiyo jana, alipozungumza na waandishi wa habari, Ikulu
jijini Dar es Salaam. Rweyemamu alisema sheria ya Makosa ya Mtandao
itasainiwa na rais muda wowote.
“Hii
ni sheria nzuri, kwanza inadhibiti matumizi mabaya ya mitandao, wote
watakaohusishwa ama kutuma au kutumiwa vitu au picha mbaya sheria
itawabana wote, na kama umetumiwa bila idhini yako, toa taarifa polisi,
ili uwe kwenye upande salama,” Rweyemamu.
Alisema madai ya wadau kwamba inanyima uhuru wa kupata taarifa, hayako sahihi kwa kuwa hiyo si sheria ya habari.
Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao
ulipitishwa katika mkutano wa 19 wa Bunge, uliofanyika Dodoma hivi
karibuni. Katika mjadala, wabunge wengi walikemea vitendo vilivyokithiri
vya uhalifu wa mtandao nchini, na kutaka sheria hiyo itakaposainiwa,
itumike ipasavyo kudhibiti.
Wabunge wengi walisema viongozi, watu
maarufu na jamii kwa ujumla, wamekuwa waathirika wakubwa wa matumizi
hayo mabaya ya mtandao, kutokana na kutukanwa, kutishiwa kuuawa,
kuzushiwa uongo na hata wakati mwingine kutapeliwa.
Hata hivyo, baada ya kupitishwa muswada
huo, kumekuwapo na kauli za ukosoaji kutoka kwa watu binafsi na makundi
mbalimbali, wakitaka rais asisaini hadi baadhi ya vifungu virekebishwe.
Miongoni mwa mambo yaliyokosolewa ni
pamoja na sheria kubana pia mtu anayetumiwa vitu au picha mbaya . Wakati
huo huo, Rweyemamu akizungumzia Muswada wa Sheria ya Takwimu kuhusu
maombi ya wadau ya kutaka ziangaliwe pande zote mbili wakati wa kutiwa
hatiani, kutokana na kutoa au kuandika takwimu zisizo sahihi. Alisema
maombi hayo yatazingatiwa.
MTANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda,
amekana kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa
Singida, Mgana Msindai na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Mkoa wa Dar
es Salaam, John Guninita.
Amedai kwamba alichozungumza kiliungwa mkono na viongozi wa juu wa chama hicho akiwamo John Malecela na Waziri Mkuu mstaafu Cleopa Msuya.
“Si kweli kwamba maneno niliyotoa yalikuwa yanawakashifu walalamikaji na kuwaathiri hadi kuwasababishia madhara,” alidai.
Makonda anadai kwamba walalamikaji
walitakiwa kufuata katiba, kanuni na taratibu zilizowekwa ndani ya chama
kwa kuwasilisha malalamiko hayo ndani ya chama badala ya kukimbilia
mahakamani.
Mdaiwa huyo mwishoni aliiomba mahakama kuyatupa madai yaliyopo dhidi yake kwa gharama.
Mahakama iliwapa nafasi walalamikaji
kuwasilisha hoja za nyongeza kama zipo Mei 5, mwaka huu na kesi hiyo
itatajwa Mei 11, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Msindai na
Guninita wanaiomba mahakama hiyo imwamuru Makonda awaombe msamaha na
kuwalipa kila mmoja Sh milioni 100.
Msindai na Guninita wanaotetewa na
Wakili Benjamini Mwakagamba, wanaiomba mahakama pamoja na mambo mengine
itoe zuio la kudumu kwa Makonda asizungumze tena maneno ya kashfa wala
kuyasambaza kama alivyofanya awali.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment