Friday, May 6, 2016

HADITHI SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA SEHEMU YA 11

HADITHI na Faki A Faki 0655 340572
Hadithi hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle ni kituo kilicho bora cha Elimu wanaorisiti masomo na kujiendeleza, Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
HADITHI
Tuliporudi nyumbani ilikuwa inakaribia kuwa alfajiri. Tukafikizia kulala. Asiubuhi kama kawaida yangu nikaenda shamba. Ilipofika saa nne mke wangu akaja shamba na kapu lenye yale madawa ya kichawi. Akawasha moto wa kuni na kuanza kuyataarisha huku akinionesha kila kitu kinavyofanywa
 
Kutoka muda huo sikuendelea tena na kazi za shamba. Mke wangu alikuwa akinifundisha vitendo vya kichawi kutokana na zile dawa.
 
Alinifundisha jinsi ya kujiandaa kwenda kumchawia mtu. Kulikuwa kuna dawa zake za kujiandalia. Pia alinifundisha jinsi ya kumchawia mtu nikiwa nje ya nyumba yake, jinsi ya kuingia ndani ya nyumba yake na jinsi ya kutoka.
 
Alinifundisha pia jinsi ya kujibadili kuwa mnyama kama paka na kwenda katika shughuli za kuwangia watu.
 
Mke wangu akanikabidhi dawa zangu. Aina mbili ya dawa aliniwekea katika pembe na aina nyingine ya dawa hizo aliniwekea kwenye chupa.
 
Siku ile tulirudi sote kutoka shamba.Tulirudi mapema tukiwa na kapu letu lililokuwa na dawa zetu za kichawi.
 
Tulipofika nyumbani nilikwenda kuoga.Yeye akaingia jikoni na kuanza kupika. Nilipomaliza kuoga nilivaa kisha nikatoka. Nilikuwa nimepanga kumtembelea yule bibi kikongwe.
 
Nilipofika nyumbani kwake ndiyo alikuwa anarudi kutoka shuleni alikokuwa anauza mbaazi zake  za kichawi ambazo ni mavi ya mbuzi. Alikuwa amebeba sufuria lake kichwani.
 
Nikakumbuka maneno aliyonieleza mke wangu kuwa mbaazi za bibi huyo ni mavi ya mbuzi wake anayoyageuza kuwa mbaazi kwa uchawi wake.
 
“Shikamoo bibi” nikamuamkia
 
“Oh! Marahaba. Hujambo”
 
“Sijambo.Ndiyo unarudi?”
 
“Ndiyo narudi mjukuu wangu”
 
Bibi huyo akalitua sufuria lake barazani mwa nyumba yake.
 
“Mbaazi zangu leo zimebaki nyingi. Nasikitikia nazi zangu. Sijui leo amenipitia mdudu gani!”
 
“Kwani zimebaki nyingi bibi?” nikamuuliza
 
“Nyingi”
 
Alifunua sufuria akanionesha. Kama siyo kuambiwa na Chausiku nisingeweza kujua kuwa ni mavi ya mbuzi na kingekula . Zilikuwa kama mbaazi za kawaida tu, tena zilikolea nazi na kuvutia. Sufuria ilikuwa imejaa mpaka juu. Zilizouzika zilikuwa kidogo sana.  
 
“Hakukuwa na biashara kabisa.Wengi wamerudi na vitu vyao”
 
“Unaweza kuziuza hapa hapa nyumbani” nikamwaambia
 
“Saa hizi hakuna biashara tena”
 
Alilibeba lile sufuria akaliingiza ndani ya nyumba yake.
 
“Karibu ndani” akaniambia
 
Nikaingia mle ndani ya kijumba chake kilichokuwa na vyumba viwili.
 
“Kaa hapo” akanionesha kiti cha marimba kilichokuwa pale ukumbini.
 
“Nasubiri usiku nikazimwage jalalani”
 
“Kwanini unakwenda kuzimwaga?” nikamuuliza nikijifanya sijui kuwa ni mavi ya mbuzi.
 
“Sasa nizifanye nini?” akaniuliza kwa hasira kidogo kisha akaniambia  “Wewe acha maswali yako”
 
Nilijua kuwa alikuwa amekasirika lakini nilishangaa nilivyomuona akicheka peke yake
 
“Wee mjukuu wangu usiulizeulize maswali. Wewe bado mchanga, hujajua mambo. Mke wako amekuandalia zile dawa zako?”
 
“Tayari”
“Leo usiku tutatoka na wewe twende hukooo…..”
 
“Twende wapi?”
 
“Utakujua. Subiri huo usiku”
 
“Sawa”
 
“Sasa leo umekuja kunitembelea, unasemaje?”
 
“Nimekutembelea tu”
 
Yule bibi akacheka tena kisha akaketi chini kwenye mchanga. Alionekana kama afukani kidogo.
 
“Usivunje miko. Ukivunja miko utaona!” akaniambia huku akininyooshea kidole cha kunionya.
 
“Miko ipi bibi?” nikamuuliza.
 
“Ebo! Unauliza tena!”
 
Akainuka na kuingia chumbani. Nikaisikia sauti yake akiniambia. 
 
“Umeshasahau niliyokuambia juzi?”
 
“Uliniambia nisitoe siri na nitii amri unazoniambia”
 
“Haya njoo humu ndani”
 
Nikainuka pale nilipokuwa nimekaa nikamfuata mle chumbani. Kijichumba chenyewe kilikuwa kiza na kilikuwa kimejaa makorokoro. Nikahisi hata nyoka wanaweza kukaa mle ndani bila yule bibi kujua.
 
Kwanza nilisimama kando ya mlango nikaangalia bila kuona vizuri mpaka macho yangu yalipozuea kiza.
 
Niliona kitanda cha kamba kikiwa pembeni mwa chumba.Yule bibi alikuwa amesimama kando ya kitanda hicho. Akaniambia. 
 
“Funga huo mlango”
 
Nikaufunga. Nikamuona akivua nguo na kubaki mtupu kisha akajilaza kichalichali pale kitandani na kuniambia. 
 
“Sasa vua na wewe uje hapa!”
 
Nilishituka na kumuuliza. 
 
“Nije nifanye nini?”
 
“Nitakumbia hapa hapa”
 
“Hapana bibi, siji hapo”
 
“Si nilikumbia usivunje amri yangu”
 
“Bibi acha utani. Mimi natoka”
 
Nikageuka na kufungua mlango.
 
“Usitoke, njoo wewe!”
 
Sikumjibu kitu. Nilitoka.
 
“Bibi naenda zangu” nikamwambia nikiwa ukumbini.
 
Nilimsikia akiangua kicheko pake yake
 
“Wewe muoga sana. Hebu ningoje usiende”
 
“Kuna sehemu ninakwenda nitachelewa bibi”
 
Nikatoka nje na kuondoka. Kabla sijafika mbali nikasikia sauti yake nyuma yangu.
 
“Nisalimie mke wako!”
 
Nikamtazama. Alikuwa ametoa kichwa kwenye mlango.
 
“Haya bibi nitakusalimia” nikamjibu huku nikiendelea kwenda.
 
Njiani nikawa najiuliza, yule bibi alikuwa anataka nini? jibu lilikuwa wazi kuwa alitaka nifanye naye ngono. Nikajiuliza je huo nao ulikuwa ni uchawi au ni akili yake mwenyewe. Hapo sikupata jibu. Hata hivyo nilishawahi kusikia kuna watu waliobaka vikongwe au maiti kwa imani za kishirikina.
 
Hata kama ilikuwa ni lazima nifanye naye kitendo hicho kama sharti mojawapo la uchawi, nisingekubaliana naye. Mzee yule wa kazi gani.
 
Nilipofika nyumbani nilimkuta mke wangu ameshapika chakula. Ulikuwa ni ugali kwa mboga ya bamia na perege wa kuchoma.
 
Yeye alikuwa ameshakula sehemu yake. Na mimi nilikula sehemu yangu. Nilipomaliza kula aliondoa vyombo kisha akaja kukaa na mimi.
 
“Ulikuwa umekwenda wapi?” akaniuliza
 
“Nilikwenda kwa bibi”
 
“Kufanya nini?”
 
“Nilikwenda kumtembelea tu”
 
“Mmezungumza nini?”
 
“Bibi leo amenionesha jambo la ajabu sana. Aliniita chumbani akavua nguo kisha akalala kitandani na kuniita. Sasa sikuelewa alikuwa na maana gani”
 
Nilitegemea Chausiku angeshituka ama kushangaa lakini nilimuona akiangua kicheko.
 
“Alivyokuita ulikwenda?” akaniuliza.
 
“Sikwenda, nilikataa nikatoka na kwenda zangu”
 
Chausiku akaendelea kucheka
 
“Ungeenda tu” akaniambia
 
“Halafu...?”
 
“Ungefanya hivyo anavyotaka”
 
“Kwani pia ni uchawi?”
 
“Ungemuuliza yeye”
 
“Wewe pia unajua, usingecheka”
 
“Nacheka tu kwa sababu najua yule bibi ana vituko”
 
Nikatikisa kichwa changu na kusikitika.
 
“Hata kama ni kwa masharti ya kiuchawi, yule bibi siwezi kufanya naye kitendo kama hicho”
 
“Kwanini?”
 
“Yule ni mzee sana. Ina maana wale wanaume walioko kwenye kundi lenu pia walifanya naye hivyo?”
 
“Siwezi kujua”
 
Nikanyamaza kimya. Pakapita ukimya wa karibu nusu dakika kabla ya kumwambia Chausiku. 
 
“Leo usiku sitatoka”
 
Chausiku akagutuka na kuniuliza kwa haraka. 
 
 “Kwanini hutatoka?”
Itaendelea kesho
Usikose kufuatilia kesho kujua yule alikuwa kikongwe au Chausiku ama ni vitimbi vya kichawi hapo kesho hapahapa tangakumekuchablog 
 

No comments:

Post a Comment