Monday, February 2, 2015

YALIYONIKUTA TANGA (10)




HADITHI

YALIYONIKUTA TANGA (10)

Ilipoishia toleo lililopita

Nikajiambia yeye ndiye aliyestahili adhabu aliyoipata lakini mimi nilikuwa naonewa tu. Nikaapa kimoyomoyo kama nitasalimika sitarudia tena kushirikiana na polisi wasio waaminifu.

Kwa vile nilikuwa hoi, nikaanguka chini na kupotewa na fahamu. Nikiwa sijielewi niliota nainuliwa na mtu aliyenikuta nimeanguka.

“Mbona umelala hapa?” akaniuliza.

“Nlinguka nilikuwa nakimbia” nikamjibu.

“Oh pole sana. Ulikuwa unakimbia nini?”

Nikamueleza ule mkasa ulionitokea.

“Kwani wewe ulikuwa hujui kama yule bibi na mwanawe Maimuna ni majini?”

“Nilikuwa sijui. Kumbe majini wanaishi na binaadamu?”

“Ndio, wanaishi na binaadamu na wanafanya biashara kama binaadamu lakini hawapendi dhuluma”

SASA ENDLEA

“Lakini mimi sijawadhulumu kitu”

“Nani aliyewadhulumu?”

“Aliyewadhulumu wameshamuua”

“Si alikuwa pamoja na wewe?’

“Hapana. Yule alikuwa mkuu wangu wa kazi. Kila anachoniambia mimi nafuatisha”

“Sasa mimi nitakusaidia uweze kurudi nyumbani kwako kwa sababu mama yake Maimuna sielewani naye ingawa trunajuana sana. Kama atakasirika, wewe utakuwa umeshasalimika”

“Nitashukuru baba kama utanisaidia kwa hilo, kwa maana nimekuwa nikihangaika sana kwenye huu msitu bila kupata njia ya kutokea”

“Usiniite baba, mimi si baba yako, umenielewa?”

“Nimekuelewa. Nakushukuru sana kwa msaad wako”

“Umekosea tena. Usinishukuru kabla sijakusaidia. Ngoja nikusaidie ndipo unishukuru”

“Sawa”

“Haya, amka uende zako. Njia ile pale”

Hapo hapo nikajiona nazinduka. Nilipofumbua macho nikajiona nimelala chini ya mbuyu. Mbuyu wenyewe ulikuwa ni ule Mbuyu Kenda, mahali niliposhushwa na pikipiki wakati nakuja kwenye eneo lile.

Sasa njia nikawa nimeijua. Niliangukia mahali pengine nimezindukia mahali pengine. Kusema kweli nilishukuru kutokea mahali hapo. Nikatoa simu na kumpigia yule mwenye bodaboda. Simu yake ikawa haipatikani. Nikapiga polisi lakini kwa uoga. Nilichohofia ni kuwa simu yangu isije ikapokelewa na Maimuna.

Baada ya simu kuita kwa sekunde chache ikapokelewa.

“Kituo kikuu cha polisi hapa, unahitaji msaada gani?” Sauti iliyosikika ilikuwa ya kiume. Nikajua sasa simu ilikuwa imefika polisi.

Nikajitambulisha na kujieleza huku nikisisitiza kupata msaada wa usafiri haraka.

Polisi niliyekuwa nikizungumza naye alikuwa ni Inspekta Benenza. Nilipompa yale maelezo alishituka na kutaharuki, akaniuliza.

“Uko sehemu gani?”

Nikamtajia sehemu niliyokuwa.

“Subiri hapo hapo, polisi watafika sasa hivi. Kwa muda huu jitahidi kujilinda mwenyewe”

“Sawa afande”

Nikakata simu. Ubaridi uliokuwa ukipepea ulinidhihirishia kuwa ilikuwa ni alfajiri. Nilijifuta michanga kwenye nguo zangu kasha nikasogea kwenye kiza ili nisionekane. Macho yangu yalikuwa yakiangaza kila upande nikiwahofia Maimuna na mama yake kunifuata mahali hapo.

Kulikuwa kimya. Sauti zilizokuwa zikisikika zilikuwa za vidudu vilivyokuwa vikipigwa na baridi kwenye vichaka. Ukimya huo badala ya kunipa matumaini ulinisababishia hofu. Ulikuwa ukimya unaotisha.

Nikajiambia kama Maimuna na mama yake watatokea itabidi nikimbie kwa miguu kurudi mjini. Kutokana na hofu hiyo macho yangu yalizidi kugeuka kila upande kuhakikisha kuwa hakukuwa na chochote kinachokuja.

Nilikuwa nikihesabu dakika kwa wasiwasi. Nilikuwa nikiona polisi wenzangu walikuwa wanachelewa kufika mahali hapo. Kuchelewa kwao kungeweza kuhatarisha maisha yangu kwani mahali nilipokuwa usalama wangu ulikuwa mdogo sana.

Tangu kuzaliwa kwangu sikuwa nimewahi kufikwa na mkasa wa kutisha  kama ule. Sikuwahi kuushuhudia mwili wa mtu ninayemfahamu ukiwa hauna kichwa wala sijawahi kushuhudia kichwa cha mtu ninayemfahamu kikiwa peke yake.

Pia sijawahi kuona majini. Nilikuwa nawasikia tu na nilikuwa siamini habari zao. Kadhalika sijawahi kuona eneo likibadilika na kuwa msitu tena msitu wa kutisha kama ule niliouona…

Mwanga wa taa za gari uliotokea kwa mbali ulikatiza mawazo yangu. Nikahisi lilikuwa gari la polisi linalonifuata mimi. Mwanga huo ulisogea kwa kasi, nikaweza kuusikia muungurumo wa gari hilo. Nikajitokeza barabarani ili waweze kuniona.

Gari hilo likanipita lakini lilikuwa gari la polisi. Haraka nikatoa simu yangu na kupiga kiyuo cha polisi.

Alipokea Inspekta Beneza.

“Mimi Martin…”

Kabla sijamwambia nilichotaka kumwambia alinikatisha.

“Nimeshatuma gari…”

“Gari la polisi limenipita…”

“Limekupita mahali ulipo…hawakukuona?”

“Nafikiri hawakuniona, wamekwenda mbali zaidi”

“Ngoja niwapigie, simama kando ya barabara. Ukiliona gari hilo linakuja wapungie mkono”

“Sawa afande”

Nikakata simu.

Nilisogea kabisa kando ya barabara macho yangu yakiangalia upande ulioelekea lile gari. Gari lenyewe lilikuwa limeshafika mbali na sikuweza kuliona tena.

Ghafla nikasikia sauti za watu wanaozungumza. Nikageuza macho haraka kuelekea ule upande niliosikia sauti. Ulikuwa ni upande ule wa kuelekea kwenye nyumba ya Maimuna na mama yake.

Nikawaona watu wawili wanakuja. Nikawagundua. Walikuwa Maimuna na yule mwanaume wa kijini aliyekuwa naye. Nilishituka sana na sikuwa na pa kukimbilia. Nikajua sasa ninakufa.

“Lazima atakuwa amefika huku” Sauti ya Maimuna ikasikika.

“Kama amekuja huku tutamuona” Sauti ya kiume ikamjibu.

“Wewe ndio umekosea, yule alikuwa amejificha nyuma ya mlango”

“Tutampata tu, hana ujanja”

Je nini  kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii kesho
Usikubali kupitwa na habari na matukio yanayojiri ndani na nje ya nchi kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com



Faki A Faki

No comments:

Post a Comment