Thursday, April 2, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOANDIKWA MAGAZETI YA LEO APRIL 02 TZ

Uchambuzi huu unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kwa kufaulisha wanafunzi wanaorisiti kidato cha pili hadi sita. Kituo kimesajiliwa na NECTA. Kipo Tanga mkabala na CRDB Bank simu 0715 772746

egMWANANCHI
Treni ya kisasa (Delux), kwenda Bara yenye mabehewa 22 ilianza safari yake ya saa 30 kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma ikiwa ni tofauti ya saa sita ikilinganishwa na safari ya treni ya zamani.
Kutokana na tofauti hiyo, abiria walioanza safari kwa furaha na matumaini jana saa tano asubuhi wanatarajiwa kufika Kigoma leo saa 11 jioni badala ya saa tano usiku.
Hata hivyo, abiria hao watalazimika kuingiza mikono yao zaidi mifukoni, kutokana na kiwango kipya cha nauli kuwa Sh79,400 badala ya Sh75,700 za awali kwa daraja la kwanza.
Huku nauli za daraja la pili ikishuka kutoka Sh55,400 hadi Sh,47,600 zile za daraja la tatu zimepanda kutoka Sh27,700 hadi Sh35,700.
Kwa mtazamo wa haraka, mabehewa hayo yanavutia yakilinganishwa na yale ya awali yaliyokuwa yamekithiri kwa uchakavu, yaliyokuwa yamejaa mende na yenye milango na madirisha mabovu.
Mabehewa hayo yana viti vya kutosha, huduma ya intaneti, swichi za umeme za kuchajia simu na kuunganisha kompyuta na safari zake zimeongezeka kutoka mbili hadi tatu kwa wiki.
Akizungumza muda mfupi kabla uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Mhandisi Kipallo Kisamfu alisema wamelazimika kupandisha viwango vya nauli kutokana na gharama zitakazokuwa zinatumika katika uendeshaji wa treni hiyo.
Licha ya kuongeza kidogo kiwango cha nauli, dhamira yetu ni kuwapatia abiria huduma safi na ya raha… kila msafiri atasafiri akiwa ameketi kwenye kiti chake. Hakuna abiria atakayesafiri akiwa amesimama,” alisema na kuongeza:
“Treni inayozinduliwa leo inatumia mabehewa mapya 22 yaliyonunuliwa kutoka Korea Kusini na kichwa cha treni kiliundwa upya kwenye karakana ya TRL iliyopo Morogoro mabehewa mapya yamegharimu Serikali Sh28.6 bilioni.”
Kuhusu vituo vya ambavyo treni hiyo alisema itasimama kwenye vituo vikubwa ambavyo vingi ni vile vya miji, wilaya na mikoa.
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Dk Shabaan Mwinjaka aliwataka abiria kuwa walinzi wa treni hiyo ili kuhakikisha usafiri huo unadumu.
“Kumekuwa na tabia ya watu kujiamulia kuharibu mali za umma, ninawaomba abiria mtakaopanda treni hii muwe walinzi wa wenzenu kwa sababu baadhi ya abiria wamekuwa na tabia ya kuchora kwenye viti,”  Dk Mwinjaka.
Mmoja wa abiria, Saida Roman alisema Serikali inahitaji kupewa pongezi kwa hatua hiyo kwani hivi sasa abiria wanaotumia usafiri wa treni kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma watasafiri kwa raha tofauti na ilivyokuwa zamani.
MWANANCHI
Wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) jana walianzisha tafrani bungeni na kusababisha kikao cha Bunge kuvunjika saa 5.18 asubuhi baada ya kusimama na kupaza sauti wakishinikiza Serikali itoe kauli juu ya hatima ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura na upigaji wa Kura ya Maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Huku wakiwa wamesimama walikuwa wanapiga kelele wakisema, ‘hatutaki kuburuzwa’, ‘tumechoka kupelekeshwa’, Watanzania wapo njia panda’ na ‘tunataka majibu,’ ‘Bunge lisitumiwe kuilinda Serikali’, ‘Waziri Mkuu yupo bungeni kwa nini asitoe kauli’ na maneno mengine mengi bila mpangilio.
Wabunge hao wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chadema na CUF, kwa umoja wao walimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa majibu hayo muda huohuo, kabla ya jioni kutoa hutuba na kuahirisha mkutano huo wa 19 wa Bunge.
Baadaye jana usiku katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge hadi Mei 12, utakapoanza Mkutano wa 20, Waziri Mkuu Pinda alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itatoa taarifa siku za hivi karibuni kuhusu upigaji wa kura ya maoni.
“Ni dhahiri muda uliobaki kuanzia sasa ni mfupi lakini Tume ndiyo itakayotujulisha ratiba kamili,” alisema.
Kelele hizo zilitokana na hoja za wabunge wawili, Suleiman Jafo wa Kisarawe na yule wa Ubungo, John Mnyika waliotaka Bunge lisitishe shughuli zake zote lijadili suala hilo kwa kuwa ni muhimu na Taifa halielewi hatima yake, wakati Bunge lilikuwa linaahirishwa jana.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alikataa suala hilo kujadiliwa, akisema ni hoja iliyowasilishwa katika mkutano uliopita, akataka Bunge liendelee na shughuli zake, lakini wabunge wa upinzani walikataa kukaa na wakaendelea kupaza sauti.
Hata alipobadili kauli akasema, “nimesema kauli itatolewa, wabunge hao walisisitiza itolewe papohapo. Hata alipowataka waondoke ndani ya ukumbi huo, wabunge hao ambao ni wachache ukilinganisha na wale wa CCM, walikataa, wakisema; “hatutoki hadi kauli itolewe.”
Kelele za wabunge hao zilimfanya Spika Makinda kutoa kauli kali, “Njooni mwendeshe (kikao) nyinyi basi. Njooni hapa mkae tena wote.”
Baada ya kuona kelele hizo zimedumu kwa dakika tatu, Spika Makinda alilazimika kusitisha shughuli za Bunge hadi baadaye (jioni), bila kutaja muda ambao Bunge lingerejea na kuwaacha wabunge wakiwa wamesimama katika makundi ndani ya ukumbi wakijadili tukio hilo.
Jafo ndiye aliyeanza kuomba mwongozo wa Spika akitaka chombo hicho cha kutunga sheria kisitishe kujadili jambo lolote lile, badala yake kijadili mustakabali wa Katiba Mpya, akitaka Serikali iwasilishe muswada wa sheria kwenye mkutano wa 20 wa Bunge (wa Bajeti) ili Katiba ya Mpito ipitishwe.
MWANANCHI
Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani ameshauri Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iahirishwe na badala yake Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iendelee kuboresha Daftari la Wapigakura.
Pia, alisema Serikali iachane na mfumo wa uandikishaji wananchi wa Biometrick Voters Registration (BVR) kwa kuwa ilikurupuka bila ya kufanya maandalizi ya kutosha na fedha na vifaa havitoshi kuendeshea mpango huo.
Jaji Bomani alisema jana kuwa mujibu wa Tangazo la Rais, Kura ya Maoni itapigwa Aprili 30 mwaka huu, lakini walioandikishwa hawazidi milioni moja.
Alisema Serikali ikilazimisha upigaji kura, itasababisha mgogoro mkubwa na manung’uniko mengi nchini.
“Hadi hii leo, uandikishaji wapigakura bado unasuasua, zaidi ya watu milioni 20 wataweza kweli kuandikishwa katika wiki nne zilizobaki?
“Itakuwa ni muujiza kufanya hivyo na ni Mkoa wa Njombe tu ambao wanaendelea kuandikishwa,” Jaji Bomani.
Alisema Tume ya Jaji Joseph Warioba ya kukusanya maoni, ilifanya kazi kwa umakini na kukamilisha Desemba 2013 na kuitishwa Bunge Maalumu la Katiba liangalie ripoti ya Rasimu Iliyopendekezwa.
Alisema Bunge lilifanya kazi yake, lakini ilikuwa siyo nzuri, hivyo kusababisha baadhi ya wajumbe kutoka nje ya ukumbi kwa kutofautiana.
Pia, alisema baadhi ya mambo mazuri yaliyomo kwenye Katiba Inayopendekezwa yafanyiwe mabadiliko ili yatumike kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
NIPASHE
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma Mjini, Roda Ngimilanga, imemrudishia dhamana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini, Johnson Minja.
Hatua ya kumfutia dhamana mfanyabiashara huyo ilizua mjadala mkali bungeni juzi, baada ya wabunge wengi kuilalamikia na kuituhumu serikali kwamba inahusika kuishawishi mahakama kuchukua hatua hiyo.
Wabunge hao walitaka Minja arudishiwe dhamana yake ili kuwezesha kufanyika kwa majadiliano kati ya serikali na wafanyabiashara ambao walikuwa wamegoma na kufunga maduka katika sehemu mbalimbali za nchi kushinikiza kiongozi wao arejeshewe dhamana yake.
Mahakama hiyo ilimfutia dhamana kiongozi huyo wa wafanyabiashara na kuamuru awekwe rumande kwa muda wa wiki moja kwa tuhuma za kuvunja kanuni za dhamana aliyopewa na mahakama hiyo Januari 28, mwaka huu.
Jana baada ya kusikiliza hoja zilizowasilishwa mahakamani hapo na  pande za utetezi na Jamhuri, Hakimu Ngimilanga alieleza kuwa Mahakama haioni sababu yoyote ya kuendelea kumshikilia Minja gerezani, kwani madai yaliyowasilishwa na Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Rose Shio, hayana mashiko ya kisheria ya kumuondolea dhamana Minja.
Aidha, alisema kuwa kwa mujibu wa jalada la kesi hiyo, hakuna kifungu chochote cha dhamana ambacho mtuhumiwa amekivunja na kwamba kwa mujibu wa masharti ya dhamana husika, hakuna kifungu chochote kinachomkataza Minja kufanya mkutano na wanachama wake.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia jalada la kesi, ninatamka kuwa Minja ataendelea kuwa huru kwa masharti ya dhamana yake ya Shilingi milioni nne na wadhamini wawili,Hakimu Ngimilanga.
Kadhalika, alisema kuwa masharti mengi yanayodaiwa kuwa chanzo cha kufutwa kwa dhamana ya mtuhumiwa katika kesi iliyosomwa mahakamani hapo wiki moja iliyopita, hayakuandikwa katika jalada la kesi hiyo.
Shio aliitaka Mahakama kuendelea kumshikilia mshtakiwa kwa tuhuma kwamba hali ya amani nchini bado siyo shwari kutokana na migomo ya wafanyabiashara inayoendelea maeneo mengi nchini.
Pia Shio alidai kuwa wafanyabiashara wengi bado wanaigomea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutumia mashine maalum ya kufanyia malipo  (EFD).
Kwa upande wake, Wakili wa Minja, Godfrey Wasonga, aliieleza Mahakama kuwa kwa mujibu wa ibara (13 (6) b na 15 (1) za Katiba ya nchi, mteja wake hakustahili kufutiwa dhamana na kuwa  jukumu la kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanafungua maduka siyo la mteja wake, bali la Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, mwanasheria huyo aliiambia Mahakama kuwa kama kweli mteja wake alikuwa na makosa ambayo yalisababisha kufutiwa dhamana, Polisi walitakiwa kumkamata wakati ule ule walipobaini akiwa katika mwendelezo wa kufanya makosa hayo.
Hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo kwa ajili ya kutajwa hadi Aprili 9, mwaka huu huku  Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi.
Kabla ya kuanza kwa kesi, idadi kubwa ya wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini walikusanyika kwenye eneo la Mahakama, wakisubiri kuletwa kwa Mwenyekiti wao huku polisi waliovaa sare na makachero wakiwa wamelizunguka eneo hilo kuimarisha ulinzi. Kabla mahakama hiyo haijamrejeshea dhamana mshtakiwa huyo, maduka katika maeneo kadhaa nchini yalikuwa yamefungwa.
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, aliwataka wafanyabiashara kufungua maduka yao wakati serikali ikiendelea kushughulikia tatizo hilo.
NIPASHE
Mchungaji Christopher Mtikila, ameiondoa mahakamani kesi ya kupinga serikali kupeleka bungeni Muswada wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, baada ya jopo la majaji kumshauri kufanya hivyo kutokana na taarifa za kuondolewa bungeni.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Watendaji wakuu wa serikali akiwamo Warizi Mkuu, Mizengo Pinda.
Hatua hiyo ilifikiwa jana mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Mwenyekiti, Richard Mziray, akisaidiana na Jaji Lawrence Kaduri na Said Kihio katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Kaduri alihoji kama kuna haja ya kuendelea na kesi hiyo mahakamani wakati Ikulu imesema serikali haina mpango wa kuanzisha Mahakama hiyo na Bunge limeshauondoa muswaada huo.
Alisema kusikiliza kesi inayozungumzia muswada huo uliondolewa bungeni haina maana na hata maamuzi yake yatakuwa hayana mashiko kisheria.
“Watanzania hatujaelimishwa nini kinaanzishwa na kitakuwa na majukumu gani hali ambayo imetuacha tumechanganyikiwa … kuna mgawanyiko mkubwa mara maaskofu wanasema hili mara wabunge na wananchi pia wanasema mengine ili mradi tu kila pande inashindwa kuelewa nini haswa kipo mbele yetu,” alisema Mwenyekiti na kuongeza:
“Tuache kwanza wananchi wapate elimu ya kutosha ili wajue nini kinajadiliwa na hata kitapopitishwa wajue kuna faida gani wanapata.”
Akizungumza na Majaji hao, Mtikila alidai kuwa lengo la kufungua kesi hiyo ni pamoja na kunyoosha mkondo wa sheria kwa sababu wapo wanaovunja sheria na kupuuza kazi za Mahakama.
Jopo hilo lilimshauri Mtikila kwamba kama ana nia ya kuendelea na maombi mengine yaliyopo kwenye kesi hiyo aiondoe mahakamani  na kwenda kuandaa upya maombi yake yasiyokuwa na kipengele cha Muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Mtikila alikubaliana na ushauri wa jopo hilo liliondoa kesi iliyosajiliwa kwa namba 14, ya mwaka huu.
Mtikila alisema baada ya kuliondoa shauri hilo mahakamani anatarajia kuandaa maombi mapya dhidi ya Waziri Mkuu, Pinda na wenzake ili waende waieleze mahakama kwa nini waliandaa muswada huo.
MTANZANIA
Watoto 140 wenye umri kati ya miaka 10 na 21 wamekamatwa wilayani Hai mkoani Kilimanjaro wakilelewa katika misikiti mitatu tofauti.
Taarifa zilizopatikana wilayani hapa zinasema watoto hao wamekuwa wakifundishwa mafunzo ya dini ya kiislam kinyume cha sheria.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, watoto hao waligundulika baada ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai kupata taarifa na kuwafuatilia kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kati ya Machi 25 na 27 mwaka huu.
Taarifa hizo zimeyataja maeneo waliyokutwa watoto hao kuwa ni Misikiti ya Masjid Bilal, Masjid Othiman na Msikiti wa Kwa Kiriwe.
Taarifa hizo zimesema katika Msikiti wa Masjid Bilal uliopo Mtaa wa Kibaoni wilayani hapa, walikutwa watoto wa kiume 70 wanaotoka katika mikoa mbalimbali nchini.
Watoto wengine 50 wa kiume walikutwa katika Msikiti wa Masjid Othiman uliopo Mtaa wa Uzunguni ambao nao inasemekana wamekusanywa kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa hizo zinasema watoto wengine 27 walikutwa katika Msikiti wa Kwa Kiriwe ambako pia walikuwa wakifundishwa mafunzo ya dini ya kiislam na walimu Watanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Anthoy Mtaka, alikiri kuwapo watoto hao wilayani kwake.
“Tukio hilo lipo na wanaohusika ni watu wanaotumia mwamvuli wa dini fulani kufanya mambo yasiyofaa katika jamii.
“Kwa hiyo naziomba mamlaka husika likiwamo Baraza Kuu la Waisalam Tanzania (BAKWATA) kutambua miskiti na shughuli zinazoendelea katika nyumba hizo za ibada.
Hili lazima walifanyie kazi kwa sababu hao vijana inasemekana wanafundishwa mazoezi makali ya kareti na judo katika nyumba hizo za ibada,” Mtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alisema atazungumzia tukio hilo leo.
Kupatikana kwa watoto hao ni mwendelezo wa matukio ya watoto wanaolelewa kinyume cha sheria mkoani Kilimanjaro baada ya matukio mawili ya aina hiyo kuripotiwa hivi karibuni.
La kwanza lilihusisha watoto 18 na la pili lilihusisha watoto 11 waliokutwa katika maeneo ya Lyamungo wilayani Hai.
MTANZANIA
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amemwandikia barua Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima akimtaka afike mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa mahojiano.
Inaelezwa kuwa Makonda alimtumia Askofu Gwajima barua hiyo Machi 30 mwaka huu, akiwa amelazwa katika Hospitali ya TMJ.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa kiroho amegoma akisema hawezikwenda ofisini kwa mkuu huyo wa wilaya kwa mahojiano. Mmoja wa wasaidizi wa Askofu Gwajima alisema jana kuwa hatua ya Makonda kumtumia barua haikumpendeza kiongozi huyo wa kanisa.
Makonda alikuja katika Hospitali ya TMJ na kudai amekuja kumwona Askofu Gwajima huku akiwa amebeba barua yake. Baada ya kumwuliza hali ya maendeleo ya afya yake alitoa barua na kumkabidhi jambo ambalo halikuwa jema.
“Baada ya muda Askofu Gwajima alituita wasaidizi wake na kutueleza kuwa amepewa barua ya wito kwa DC, sasa tukajiuliza askofu anaumwa. Je, inakuaje aende tena katika mahojiano na mkuu wa wilaya? “Na kama ni hivyo nini kazi ya polisi maana wamemuhoji tangu siku ya kwanza baada ya kumkamata.
Mtu anahojiwa na polisi sasa inakuaje tena aitwe na DC ahojiwe na kamati ya ulinzi? Amesema hatokwenda,” alisema msaidizi huyo wa Gwajima ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda alitoa ufafanuzi wa barua yake hiyo, ambapo alijibu kwa kifupi kuwa ni kweli amemwandikia barua ya wito kiongozi huyo. Alipoulizwa ni hatua zipi Askofu Gwajima atachukuliwa kwa kutaa kutii wito huo, Makonda alisema. “Kuhusu hatua subirini mtaziona wenyewe” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Gwajima kuripoti polisi Wakati hohuo, Askofu Gwajima leo anatarajiwa kuripoti katika Kituo Kuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuendelea kuhojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Gwajima aliachiwa kwa dhamana juzi baada ya kutoka katika Hospitali ya TMJ ambako alikuwa amelazwa kwa matibabu baada ya kuanguka ghafla wakati akihojiwa na polisi.
Mwanasheria wa Gwajima, John Mallya alisema baada ya kuruhusiwa juzi, leo anatakiwa kuripoti tena katika kituo hicho kuendelea na mahojiano. “Polisi walituambia twende kesho (leo) kwa mahojiano kwa sababu yalikuwa hayajakamilika… lakini tunaamini polisi wanaweza kumruhusu kurudi nyumbani kupumzika au kuendelea na mahojiano mengine, Mallya.
Alisema mpaka sasa anaendelea vizuri na matibabu na afya yake inaendelea kuimarika siku hadi siku tofauti na alivyokuwa awali. Gwajima alifikishwa polisi kwa madai ya kumtukana na kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Wakati anahojiwa alianguka na kuzimia hali iliyosababisha akimbizwe katika hospitali ya polisi Kurasini kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na baadaye Hospitali ya TMJ kwa matibabu zaidi.
Juzi Askofu Gwajima alikwenda polisi akiwa amepandishwa kwenye baiskeli maalumu ya wagonjwa.
HABARILEO
Siku chache baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kutaka uangaliwe uwezekano wa kushusha nauli za vyombo vya usafiri nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema inatekeleza agizo hilo na kwamba nauli za daladala na mabasi ya mikoani zitashuka wakati wowote kuanzia sasa.
Imeongeza kuwa, licha ya bei ya mafuta kupanda kidogo jana, hakutaathiri kushuka kwa nauli, kwani ukokotoaji utafanyika kwa wastani wa bei ya mafuta ilivyoshuka kwani haitapanda kwa kiasi kikubwa kwa mara moja.
Hayo yalisemwa jana na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, David Mziray aliyesema wanatekeleza agizo la Waziri Sitta aliyetaka nauli zishuke kufikia kesho, lakini wamechelewa kutokana na muda wa kuwasilisha maoni kwa wadau waliopewa siku 14 kufikia ukomo leo.
Tunawahakikishia wananchi kuwa baada ya kumaliza siku za kupokea maoni ya wadau hususan wamiliki wa mabasi ya daladala waliopewa siku 14, mchakato huu utakwenda haraka na mapema iwezekanavyo tutatangaza nauli hizo mpya,” alisema.
Mziray alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kutoshusha nauli, bali wanafuata taratibu na kanuni hivyo kuwataka wananchi kuwa na subira kwa siku chache zijazo.
Wiki hii, Waziri Sitta aliwataka Sumatra kuharakisha mchakato huo wa kushusha nauli ufanyike haraka iwezekanavyo na ifikapo kesho wawe wametangaza nauli hizo mpya, kwani kwa muda mrefu bei za mafuta zimeshuka kutoka zaidi ya sh 2,200 hadi chini ya Sh 1,800.
Wadau wa usafiri walipendekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za daladala zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa kilometa 10.
Walitaka kwa mabasi ya kawaida kwa Moshi na Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh 22,700), Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh 42,000), Mbeya (Sh 23,365) badala ya Sh 30,700), Bukoba (Sh 40,756 badala ya Sh 55,000) na Dodoma (Sh 12,678 badala ya Sh 16,700). Kwa usafiri wa daladala wamesema wanataka iwe
HABARILEO
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imependekeza kwa Serikali iongeze adhabu ya faini kutoka Sh milioni tatu na kifungo kisichopungua miezi sita na kuwa faini ya Sh milioni tano na kifungo kisichopungua miezi sita kwa wale wote watakaotuma katika mtandao taarifa za uongo.
Aidha, kamati hiyo imependekeza katika adhabu kwa watu wanaonyanyasa wenzao kupitia mtandaoni, adhabu yao iongezwe kutoka kifungo cha mwaka mmoja na kuwa kifungo cha miaka mitano.
Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Uhalifu wa Mtando wa mwaka 2015, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba alisema adhabu zilizowekwa katika sheria hiyo hazitoshelezi kulingana na athari za makosa hayo.
“Kamati imeona umuhimu wa kuongeza adhabu hizi katika maeneo haya, kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaodhalilisha utu wa watu wengine katika mitandao ya kompyuta jambo lililoathiri watu wengi, familia, jamii na nchi kwa ujumla,” alisema Serukamba.
Alisema kamati hiyo, pia inashauri uwekwe utaratibu wa Serikali kuchukua hatua za ufuatiliaji kabla ya mtu aliyenyanyaswa kuripoti. “Hii ihusishe mfumo wa kuweza kumtambua mtu aliyesambaza picha ama taarifa hizo.
” Awali akiwasilisha maelezo ya muswada huo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, alisema kutokana na kukua kwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kumesababisha kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo kuibuka kwa makosa ya mtandao.
Alitaja makosa ya mtandao yaliyokithiri kwa sasa kuwa ni makosa dhidi ya faragha, usalama na upatikanaji wa taarifa za kompyuta na mifumo ya kompyutam makosa yanayohusu maudhui, makosa dhidi ya mifumo ya kompyuta na makosa ya kawaida yanayofanywa kwa kutumia mitandao.
Alisema waathirika na waathirika wa makosa hayo ni pamoja na Serikali, sekta binafsi, watu binafsi na jamii kwa ujumla na takwimu kutoka jeshi la polisi zinaonesha kuwa makosa ya uhalifu wa mtandao yaliyoripotiwa na kuchunguzwa kati ya mwaka 2012 hadi Agosti mwaka jana ni 400.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment