SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA
12
“Nimeshakupanda punda
wangu. Sasa twende” Bibi huyo alimwambia tena msichana huyo huku akimpiga
kofi kwenye makalio yake.
Msichana huyo akaanza
kutembea kwa kutumia magoti na mikono akiwa amembeba yule bibi
mgongoni.
Kwa jinsi msichana huyo
alivyokuwa mwembamba, ukilinganisha na uzito wa yule bibi, alikuwa akienda
kwa taabu akiwa amekunja uso kuonesha kuwa alikuwa anaumia. Pale alipoonesha
kusitasita, yule bibi alimpiga kofi la makalioni na kumuamrisha.
“Twende! Twende!”
Wakati kitendo hicho
kinafanyika, mke wangu alikuwa akicheka kuonesha kuwa kilikuwa kitendo
kilichomfurahisha. Wakati mwingine yule bibi alikuwa akimsukuma yule binti
makalioni mwake ili aende kwa haraka haraka.
Msichana huyo alipochoka
kabisa alijibwaga chini puu! Yule bibi akanyanyuka na kumwambia mke wangu
amuinue na amlaze kitandani. Chausiku akamuinua na kumlaza kitandani msichana
huyo aliyeonekana kuwa taabani sana.
Kama haitoshi, Bi kikongwe na Chausiku wakamchezea ngoma
kando ya kitanda pamoja na kumng’ong’a huku wakiwa wamemtolea macho. Baada ya
kumfanyia hivyo walimrushia vitu visivyoonekana kisha mke wangu akageuka na
kunishika mkono. Kufumba na kufumbua tukajikuta tuko nje ya dirisha. Baada ya
sekunde chache tukamuona yule bibi naye ameibuka nje ya dirisha.
Msafara ukaongoza njia ya
kurudi. Wakati tunarudi yule bibi alikuwa anabadilika badilika. Mara alikuwa
anageuka mbwa, mara alikuwa anageuka paka. Tulitembea mpaka tukafika kwenye
ule uwanja wetu tunapokutana. Safari ya kurudi pia ilikuwa fupi kama ile ya kwenda.
Tulikuta kundi la wenzetu
waliokwenda mahali kwingine wakitusubiri. Hapo wachawi hao wakaanza
kuhadithiana uchawi wao huku wakionekana kuridhika na vitendo walivyotenda.
Mimi tu ndio nilikuwa
nimefadhaika. Nilikuwa nikimfikiria yule binti wa kiarabu alivyokuwa anateswa
na yule bibi hadi kuanguka chini.
Kitendo kile
kilinitambulisha kwamba uchawi unahitaji moyo wa ukatili na yule bibi alikuwa
katili.
Vitendo vile vya kichawi
sasa vilianza kunichukiza lakini kwa vile nilikuwa nimeshajiingiza katika
kundi hilo
sikuwa na budi kuendelea nalo. Mke wangu alishanitishia kuwa nisipokubali
kuwa mchawi atakwenda kuniripoti polisi kuwa nimemuua mke wangu wa kwanza.
Hivyo niliona ni bora niendelee na udhalimu huo kuliko kukamatwa na polisi na
kwenda kushitakiwa kwa kosa la mauaji.
Baada ya wachawi hao
kuhadithiana hiki na kile, walianza kuvaa nguo zao. Mimi sikuwa na nguo. Yule
bibi akanigeukia.
“Tunakupa mazoezi ili upate
ujasiri. Leo tumekupeleka Songe, kesho utaenda mahali kwengine” Bibi huyo akaniambia.
“Sawa bibi”
“Yule msichana hatoolewa
ng’o na atabaki kuwa mbovu kila siku” Bibi akaendelea kusema huku akiendelea
kuvaa kaniki yake.
“Sisi tunakwenda” Mke wangu
akamuaga bibi.
“Haya nendeni, kesho uje
naye”
“Nitakuja naye” mke wangu
akamwaambia
Wakati nimeongozana na mke
wangu tukienda mahali alipoweka nguo zake, tulimsikia yule bibi akituambia
huko nyuma.
“Mwaambie aache uoga”
Mke wangu akaguna
“Mh!.... bibi huyu nae
hamalizi kusema!” kisha akamjibu “Ataacha uoga tu, ndio mwanzo bibi”
Tukaenda kwenye kichaka
ambako mke wangu aliweka nguo zake. Ulikuwa ni upande wa kaniki. Akajifunga
nao kisha tukaondoka kurudi nyumbani.
Tulipofika barazani mwa
nyumba yetu nilichukua ile shuka yangu nikaivaa kisha tukaingia ndani.
Kwa vile tulikuwa tumechoka
tulipojilaza tu usingizi ukatuchukua.Tulipozinduka kulikuwa kumekucha. Siku
ile nilipanga nisiende shamba.
Wakati tunakunywa chai na
mke wangu nikamuuliza ni kwanini waliamua kunifuata usiku wakati nilimwambia
nilikuwa najisikia kuumwa?.
“Ni bibi mwenyewe. Mimi
nilimwambia kama ulivyoniambia wewe.
Akaniambia mume wako ameanza uvivu. Ndio akaamua kukufuata” Mke wangu akanijibu.
alipoona nilikuwa nimenyamaza huku nikimtazama akaendelea kuniambia.
“Siku nyingine ukiwa na
dharura yako uende ukamwambie mwenyewe”
“Je ikitokea ukiumwa wewe
itakuwaje? Atakufuata?” nikamuuliza.
“Mimi nikiumwa ninamueleza
na hawaja nifuata hata siku moja”
“Tuseme na akiumwa yeye
inakuwaje?”
“Yule bibi haumwi, anakula
mizizi ya kwao kila siku. Usimuone vile mzee, ni mzima kweli. Hata kama
akisafiri usiku anapaa kwenye ungo anakuja uchawini ”
“Ala! Kumbe anapaa?”
“Anapaa kwa ungo”
“Wewe pia unapaa?”
“Amenifundisha yeye”
“Huo ungo wako, ukowapi?”
“Uko chumba cha pili,
nimeuweka”
“Mkipaa mnaenda wapi?”
“Kama tunataka kwenda
kufanya uchawi Dar es Salaam
au Tanga tunapaa. Yule bibi wakati mwingine anataka kwenda kukutana na wachawi
wenzake wa Sumbawanga na Mwanza, pia anapaa”
“Lakini mimi hajanifundisha
uchawi huo”
“Wewe bado kwanza, lakini
atakufundisha tu. Ngoja umalize angalau mwaka mmoja”
Tulipomaliza kunywa chai,
mimi nilitoka kwenda kuzunguukazunguuka. Nilirudi nyumbani saa sita mchana.
Mke wangu akaniuliza.
“Una njaa, nipike ugali?”
“Pika”
Akaenda jikoni. Na mimi
nikajipunzisha kitandani. Hapohapo usingizi ukanichukua. Mke wangu alikuja
kuniamsha majira ya saa nane na kuniambia.
“Chakula kimeiva”
Tulipomaliza kula
akaniambia anakwenda kumtembelea bibi. Mimi nikabaki pale nyumbani.
Chausiku alipoondoka
hakurudi tena hadi saa moja usiku. Akapika chakula cha usiku. Milo yetu ya kijijini haina masharti. Mchana mnaweza
kula ugali na matembere na usiku mnakula tena ugali huo huo.
Baada ya kula hatukukaa sana, tukaenda kulala. Kama kawaida yake mke wangu aliniamsha usiku wa
manane.Tukatoka.
Tulipofika kiwanjani
tuliwakuta baadhi ya wenzetu walikuwa wameshafika. Bibi akatupangia kazi.
Vile vitendo vyetu vya kichawi tulivichukulia kama
kazi.
Siku ile bibi alinipanga
mimi na wanawake wawili twende nyumbani kwa mwalimu mkuu wa ile shule
anakouzia mbaazi zake tukamchawie. Kisa, alimwambia yule bibi atamfukuza
asipeleke mbaazi zake shuleni hapo kwa
vile wanafunzi na walimu wanaokula mbaazi hizo wanaharisha. Kauli hiyo
ilimuudhi yule bibi.
Mke wangu na wenzake
wengine walitumwa sehemu zingine zingine.
Nyumbani kwa mwalimu mkuu
hakukuwa mbali sana
na pale kwenye kiwanja chetu.Tukaenda.
Kama kawaida tulipofika, wachawi wenzangu wakapiga pindu
kwenye mlango wa nyumba ya mwalimu mkuu huyo.Wakaniambia na mimi nipige
pindu, nikapiga pindu. Kisha tukazunguka duara na kuanza kucheza ngoma ya
kichawi barazani mwa ile nyumba. Zile pindu tulizopiga zilikuwa na malengo ya
kufanikisha ile kazi ya kichawi iliyotupeleka hapo. Na ile ngoma ilikuwa ni
ya kuwalaza usingizi watu wote waliokuwemo mle ndani.
Tulipomaliza kucheza ngoma
hiyo ikafuatia kazi ya kujipenyeza kiuchawi ndani ya ile nyumba. Laiti
ningejua ni kitu gani kitatutokea humo ndani, nisingekubali kuingia humo
ndani.
Je ni nini kitakachotokea?
Usikose hapo kesho hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment