Rais Magufuli kazuia viongozi kwenda sherehe za Mwenge… na posho zirudishwe
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 12
Oktoba, 2016 Ikulu Dar es Salaam na katibu mkuu kiongozi balozi John
Kijazi imeeleza kuwa Rais Magufuli ameagiza viongozi wote wa serikali
walioalikwa kuhudhuria sherehe za kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru
kitaifa 14 Oktoba Bariadi Simiyu kutohudhuria sherehe hizo na wale ambao
walishalipwa fedha ya posho na safari wazirejeshe.
President ametoa maagizo hayo ikiwa ni
utekelezaji wa azma ya serikali ya awamu ya tano ya kubana matumizi
yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali nyingi katika shughuli za
maendeleo ya nchi.
Viongozi
waliotajwa kutakiwa kufuta safari zao za kwenda Bariadi ni pamoja na
wakuu wote wa mikoa, wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi wote wa mamlaka
za serikali za mitaa, mameya na wenyeviti wote wa Halmashauri za majiji,
manispaa, miji na wilaya pamoja na watumishi ambao huambatana nao
wakiwemo madereva na wasaidizi wao ambao kwa idadi hufikia takribani
1,500.
Kwa kuwa
sherehe za kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru huambatana na maadhimisho
ya siku ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere aliyefariki miaka 17 iliyopita, agizo hilo limewataka viongozi
wote wa mikoa na wilaya kubaki katika maeneo yao ya kazi na kujiwekea
utaratibu wa jinsi ya kuienzi siku hiyo.
Aidha,
Rais Magufuli ameagiza wilaya zote ambazo zimefanya vizuri katika
shughuli za maendeleo wakati Mwenge ulipokuwa katika maeneo yao,
zitambuliwe kwa kutangazwa rasmi katika siku ya kilele cha mbio za
Mwenge na kwamba zawadi zilizoandaliwa zitapelekwa kwa wahusika kwa
utaratibu utakaoelekezwa na mamlaka inayohusika kutoa zawadi hizo.
Hata hivyo
Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa kutokana na umuhimu wa mwenge wa Uhuru
kwa Taifa, Viongozi wote wa serikali ya mkoa wa simiyu na wilaya zake
pamoja na wananchi wote wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi na kushiriki
katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru siku hiyo ya tarehe 14 Oktoba,
2016.
Mgeni
Rasmi katika sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru atakuwa Rais wa Zanzibar
na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
millardayo
No comments:
Post a Comment