HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (23)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Kile kitendo cha kutoniona
mimi inawezekana kilimpa hisia kuwa na mimi nilikuwa nimeuawa kama
Shazume. Tatizo ni kuwa mwili wangu hakuuona. Bila shaka alitoka nje kuutafuta
mwili wangu.
Alisimama mbele ya ile nyumba
akaangalia kila upande kisha akarudi tena mle ndani. Mimi nikashuka kwenye ule
mti.
Yasmin alipotoka tena
akanikuta nimesimama mbele ya mlango. Akashituka na kuniuliza. “Ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nimepanda juu ya
huu mti” nikamjibu.
Akaja kunikumbatia kifuani
kwangu. Kumbe alikuwa analia. Nilipoona analia na mimi nikaanza kulia. Kama
Yasmin alikuwa anaona uchungu jinsi tulivyokuwa tunauliwa na Harishi, mimi
niliona uchungu nilipowaza nitakavyouliwa na Harishi hapo kesho.
“Buriani Yasmin, ndio
tunaagana. Kesho hatutakuwa pamoja tena. Shazume ametutangulia leo” nikamwambia
Yasmin.
Yasmin akajifuta machozi yake
na kunitazama.
“Wewe hutaniacha, kama ni kufa tutakufa sote. Mwili wangu utalala juu ya
mwili wako” Yasmin akaniambia kwa sauti nzito lakini ya kijasiri.
Akaongeza. “Ili
uamini kuwa wewe utakufa na mimi turudi kule kule kwenye lile jumba,hatuna
sababu yoyote ya kujificha. Akija Harishi nitamwambia atuue sote, Anitangulize
mimi kisha wewe”
SASA ENDELEA
“Twende!” nikamwambia Yasmin
bila kusita.
Yasmin akanishika mkono
tukatembea kuelekea katikalile jumba. Hatukuzungumza kitu tena mpaka tulipofika
katika jumba hilo
Yasmin aliniuliza.
“Utakunywa uji?”
“Sitakunywa” nikamjibu kwa
mkato
“Kwanini?”
“Roho yangu imefadhaika sana”
“Hata roho yangu imefadhaika
lakini kama wanipenda tunywe kidogo”
Ilikumridhisha Yasmin
nilimkubalia. Yasmin aliniacha ukumbini akaenda jikoni. Baaada ya muda kidogo
alikuja na vikombe viwili vilivyojaa uji wa ngano uliotiwa asali.
Alinipa kikombe kimoja kisha
aliketi nami.
“Yasmin kweli tumeshindwa
kuondoka kwenye kisiwa hiki cha mauti” nikamuuliza Yasmin
“Tutaondokaje wakati
tumezungukwa na bahari na hatuna chombo!”
“Nashangaa kwamba hakuna
wavuvi wanaokuja katika kisiwa hiki!”
“Hiki kisiwa kiko mbali na
pia kinajulikana. Hakuna wavuvi wanaoweza kufika hapa”
“Chombo chetu
kilipotuharibikia tulipokiona kisiwa hiki tulidhani tumeokoka kumbe tumekuja
kuangamia”
“Hata kama msingekiona hiki
kisiwa pia mngeangamia. Mngekula nini? Mngekufa kwa njaa”
“Mimi naona bora kufa kwa
njaa kwa sababu njaa itakuwa imekulevya, hutajijua. Kuliko kusubiri….”
sikumalizia sentensi yangu.
Niliona nilikuwa najikumbusha
kifo kibaya cha kutobolewa utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na
ubongo1.
Siku zote tulizokaa hapa
kisiwani niliweza kujikaza na kuondoa hofu licha ya wenzangu kuendelea kuuawa
lakini kwa siku ile ambayo nilibakimimi na Yasmin peke yetu, sikuweza kuzuia hofu
yangu.
Mawazo ya kifo cha kutobolewa
utosi kwa ncha ya upanga na kufyonzwa damu na ubongo yalikuwa yametawala akili
yangu.
“Harishi ni kiumbe na sisi ni
viumbe. Huwezi kujua Mungu amepanga nini” Yasmin akaniambia.
“Namuamini Mungu na simkatii
tamaa”
“Hapo umezungumza kitu cha
maana sana.
Haifai kukata tama. Nimeshakwambia kama ni kufa leo tutakufa sote. Na mimi ndio
nitakufa kwanza”
“Unataka tuendelee kukaa humu
hadi usiku”
“Ndiyo. Unafikiri utakwenda
wapi?”
“Sioni pa kwenda”
“Basi tukae tu humu”
“Harishi akija atukute
pamoja?”
“Ndiyo”
“Aniue mbele yako!”
“Hapana. Ataniua mimi kwanza”
“Mimi sipendi nikusababishie
kifo, niache nife mwenyewe”
“Na mimi sitapenda
nikusababishie kifo”
“Wewe hutanisababishia kifo,
ni Harishi”
“Sikiliza kaka yangu. Sisi
tukae hapa hadi usiku.Litakalotokea lolote na litokee lakini kama
ni kufa nitatangulia mimi”
Nilimuangalia tu Yasmin,
sikumjibu kitu tena. Nikaendelea kunywa uji huku nikiwaza kama
ni kweli alikuwa amejitolea nafsi yake kwa ajili yangu.
Maneno yake yalionesha
alichokuwa akisema kilikuwa na udhati.
Hata hivyo niliwaza kuwa
msimamo wa Yasmin haukuwa na msaada wowote kwangu zaidi ya kuonesha upendo.
Ulikuwa msimamo wa kukata tamaa na haukuwana maana.
Atangulie yeye kufa halafu
nifuatie mimi? Maana yake ni kuwa sote tutafikwa na mauti. Jambo hilo kwangu lilikuwa
tishio ingawa yeye aliona lilikuwa la kijasiri.
Jambo la maana lilikuwa
kupata wazo la kutunusuru sote na sio tufe sote.
Tulibaki kimya tukinywa uji.
Uji huo niliunywa kwa kujilazimisha ili kumridhisha Yasmin. Kama
ningekuwa peke yangu ningebaki na njaa hadi mauti yatakaponikuta.
Nilipomaliza kikombe changu
cha uji Yasmin aliniuliza.
“Nikutilie tena?”
“Umetosha’ nikamjibu.
Yeye pia alikuwa amemaliza
uji wake akaniambia.
“Basi nenda ukaoge, umeshatia
nguvu kidogo”
Pamoja na kukabiliwa na
tishio hilo la kifo kusema kweli nilihitajika sana kuusafisha mwili
wangu. Nilikuwa nimechafuka sana
na nilikuwa sijaoga kwa siku tatu.
Niliona aibu kumwambia Yasmin
kuwa sitaoga. Nikainuka.
Yasmin akanipeleka bafuni
kisha akaondoka. Nilioga haraka haraka. Nilipomaliza niliondoka bafuni na
kumbishia Yasmin mlango.
Yasmin alinifungulia mlango
na kuniambia.
“Karibu”
Niliingia mle chumbani
alimokuwa. Hamkuwa na kiti. Akaniambia.
Kaa kitandani”
Nikakaa.
“Unajisikia vizuri kidogo?”
akaniuliza.
Nilijaribu kutabasamu bila
kufanikiwa. Niliishia kubenua midomo tu, uso haukukunjuka.
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE