KISIWA CHA HARISHI (21)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Yasmin naye akaomba dua.
Kwa muda wa nusu saa hivi
mahali hapo pakawa kama madarasa kutokana na
kurindima visomo vyetu vya dua.
“Pia tungekuwa tunaswali”
Shazume akatukumbusha.
Sikuzote binaadamu humkumbuka
sana mola wake
pale anapofikwa na matatizo. Siku zote hizo tulikuwa hatukumbuki kuswali ila ni
kwa siku ile ambayo tuliona tutamalizika.
“Pia ilitakiwa leo tufunge”
na mimi nikawakumbusha.
“Ni kweli” Shazume
akanikubalia na kuongeza “Lakini tumeshakunywa uji”
“Kama
tutanusurika leo tutafunga kesho. Umesikia Yasmin?”
“Nimesikia” Yasmin akanijibu.
“Sasa sisi hatuko tohara,
tutaswali vipi?’ nikawauliza wenzangu.
“Twendeni tukaoge baharini
tujitoharishe” Shazume akasema.
“Hizi nguo zetu pia hazina
tohara”
“Tuoge na nguo zetu ziweze
kutoharika, zikikauka tutaswali”
Tukakubaliana.
SASA ENDELEA
Tukaamua sasa twende baharini
tukaoge. Tukaenda sote watatu, mimi, Shazume na Yasmin. Yasmin alipotuona sisi
tunajitosa kwenye maji na yeye akajitosa. Tukawa tunaoga na kuogelea pamoja.
Tuliendelea kukaa kwenye maji
kwa muda kidogo ili kujisahaulisha matatizo yaliyokuwa yanatukabili.
Asubuhi ile maji yalikuwa
matamu kwa mtu ambaye alikusudia aogelee kwa starehe ila kwa sisi ilikuwa
starehe ya kujilazimisha. Mawazo mabaya yalituepuka kwa muda yakitusubiri
tumalize kuogelea.
Tulitamani tusitoke ndani ya
maji lakini nilipomuona Yasmin aliyekuwa akiogelea karibu yangu anarudi
ufukweni na mimi nikaamua kurudi.
Tukakaa ufukweni na kumsubiri
Shazume. Naye alipotuona tumerudi ufukweni akatufuata.
Tukakaa kuota jua. Nguo zetu
zilikuwa zimetota. Kitendo cha kuogelea na nguo zetu hakikuwa cha maana sana kwani mzizimo
ungeweza kutuletea madhara ya kiafya lakini hatukuwa na la kufanya.
Yasmin ambaye alikuwa na nguo
za kubadili alizokuwa akiletewa na Harishi alikuwa akifuata mkumbo tu,
haikumpasaaloweshe nguo zake ila alipotuona sisi tunaoga na yeye akajitosa.
Tulikaa kwa muda kwenye
ufukwe tukiangalia bahri na ndege waliokuwa wakiruka ruka. Ili
miiliyetu isisinyae tuliamua kufanya mazoezi ya kukimbizana.
Tulikimbizana mpaka
tulipochoka tukarudi kwenye ile nyumba. Tukapanga kwamba itakapofika sa saba
tuanze kuswali swala ya adhuhuri. Yasmin alituaga akatuambia kuwa anakwenda
kupika chakula cha mchana.
Kwa mustakabali wetu tatizo
la chakula halikuwepo. Chakula kilikuwepo kwa Yasmin. Tatizo lilikuwa ni la
kuuliwa na Harishi. Kama si tatizo hilo
mahali pale pangekuwa ni pazuri pa kuishi. Sikuvutika na kisiwa hicho pekee
bali pia nilivutika na Yasmin. Nilifarijika sana kuona jinsi alivyokuwa akitupa moyo na
matumaini japokuwa hali ilikuwa tete.
Baada ya Yasmin kuondoka
tuliendelea kukaa, hatimaye tukapitiwa na usingizi.
Tulipokuja kuamka yalikuwa
majira ya saa nane. Tukaenda kutawadha kwenye maji ya bahari na kuswali swala
ya adhuhuri.
Yasmin alikuja saa tisa akiwa
amechukua kapu la chakula. Alikuwa amebadili nguo zake na kuvaa mavazi mengine.
“Mmepauka kwa chumvi.
Mnasikitisha sana
kaka zangu” akatuambia.
“Ndiyo hivyo, tutafanyaje
sasa” nikamwambia huku nikimpokea lile kapu.
“Mmeshaswali?” akatuuliza.
“Tumeswali na wewe umeswali?”
Na mimi nikamuuliza.
“Mimi naswali kila siku
kuomba nusura na kuwaombea na nyinyi. Sijui kama nyinyi mmekumbuka kuniombea”
“Tumekuombea” nikamdanganya.
Tulikuwa tumemsahau.
“Mngesema mmesahau kuniombea
ningejua hamnipendi”
“Tunakupenda sana. Umetuletea chakula
gani?”
“Wali”
“Roho zetu zimekinai,
hatutamani hata kula” Shazume akasema.
“Shazume unaanza maneno
yako!” Yasmin akamwambia Shazume.
“Unafikiri nakudanganya, mimi
sina hamu ya kula kabisa”
“Mbona juzi na jana ulikuwa
unakula?”
“Nilikuwa na matumaini”
“Si vizuri hivyo. kuleni
japokuwa kidogo mpate nguvu. Mkiacha kula mtakuwa mnajitesa wenyewe. Mimi pia
sikula. Nimekuja huku nile na nyinyi”
Yasmin alitoa kile chakula
akakiweka chini. Akatoa tasa la maji tukaosha mikono kisha tukaanza kula.
Mimi pia sikuwa na hamu ya
kula lakini nilikula kumridhisha Yasmin.
Tuliendelea kula kidogo
kidogo hadi Shazume alipomuuliza Yasmin.
“Yasmin ukibaki peke yako
itakuwaje?”
“Hatuombei hivyo, tuombee
tubaki sote. Ukiomba dua uweke matumaini, isiwe unakata tama”
“Ni kweli Yasmin huwezi
kuomba kitu bila kukiwekea matumaini. Kama
huna matumaini na kitu hicho kwanini unakiomba?” nikasema.
Shazume akaguna.
“Pamoja na kuomba kwetu bado
naona wakati wetu umekaribia sana”
Shazume akasema kwa hali ile ile ya kukata tama.
“Shazume usiseme hivyo,
mnaweza kunusurika. Harishi ni kiumbe kama
nyinyi”
“Lakini mwenzetu amepewa
uwezo”
yasmin naye akaguna. Pakawa
kimya. Yasmin ndiye aliyeutanzua ukimya huo alipotuambia. “ Jamani tukinusurika
nitawachukua Comoro. Nitamwambia baba yangu nyinyi ni ndugu zangu wa damu.
Mtaenziwa kama watoto wa rais”
ITAENDELEA KESHO USIKOSE NI KITATOKEA
No comments:
Post a Comment