HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (18)
ILIPOISHIA TOLEO
LILILOPITA
Yalipofika majira ya saa
kumi na mbili jioni Yasmin akaja.Alikuwa ametuletea chakula cha jioni. Ulikuwa
ni wali ule ule tuliokula mchana. Tukakiweka chakula hicho kusubiri usiku.
Yasmin akataka
nimsindikize arudi. Nikawambia wenzangu “Namsindikiza Yasmin”
“Usije ukachelewa
kurudi. Kumbuka usiku umekaribia” Shazume akaniambia.
“Sitachelewa” nikamjibu.
Tukaondoka na Yasmin.
Tukiwa njiani Yasmin alinitazama machoni mwangu kisha akaniambia.”Nimefurahi
sana leo kuwa peke yetu mimi na wewe”
“Kwanini?” nikamuuliza.
“Tangu juzi hatujapata
nafasi ya kuwa pamoja peke yetu. Mara nyingi unakuwa na wenzako. Jana jioni
nilitaka kukwambia nisindikize lakini marehemu Masudi akawahi yeye. Sikuweza
kumkatalia. Najua roho ilikuuma na mimi pia iliniuma” Yasmin akaniambia.
“Unajua jana
niliwafuatilia nikawakuta mnafukuzana ndani. Kuna wakati marehemu alikushika
kiuno mkaanguka chini pamoja”
Nilipomwambia hivyo
Yasmin alinywea.
“Kumbe ulikuja
kutuchungulia?” akaniuliza.
“Nilikuja, nilipouona
mchezo wenu nikaamua kurudi”
SASA ENDELEA
“Si mchezo wetu. Masudi
ndio alikuwa analazimisha. Alikuwa akinitaka kimapenzi nikamkatalia” Yasmin
aliniambia.
“Basi tusimseme sana kwa
sababu ameshakufa lakini nilishituka”
“Naomba unisamehe kwa
hilo kama limekuudhi”
Nikanyamaza kimya.
“Umeshanisamehe?” Yasmin
akaniuliza huku akinitazama machoni mwangu. Alinitazama kwa macho ya huruma
sana.
“Kwani wasiwasi wako ni
wa nini?”
“Nataka unisamehe!”
Yasmin akasisitiza.
“Nimekusamehe”
“Sasa tusizungumze tena
habari hiyo. Tuzungumze yanayotuhusu mimi na wewe. Kama tutafanikiwa kuondoka
katika kisiwa hiki utanioa?”
“Wewe ndio uniambie mimi
kama utakubali kuolewa na mimi”
“Mimi niko tayari hata
sasa hivi”
“Unadhani wazazi wako
watakubali?”
“Watakubali”
“Ujue kuwa wewe ni binti
wa rais na mimi ni mtoto wa kimasikini”
“Kusema hivyo si sahihi.
Sasa hapa tulipo mimi na wewe tuna tofauti gani?”
“Kwa hapa tuko sawa ila
ukirudi kwenu wewe utakuwa mwana wa rais”
“Huo ni ufinyu wa mawazo
ya binadamu. Binaadamu wote ni sawa. Mfano halisi ni wa hapa tulipo. Umesema
tupo sawa, basi tutakuwa sawa popote. Hata kama wewe ni mtoto wa kimasikini
lakini nimekupenda, utakataa?”
“Labda wewe unikatae
mimi”
“Una majibu
yasiyoniridhisha. Kwanini huniambii kuwa unanipenda na utanioa. Mimi nataka
utamke hivyo”
“Nimekupenda na
nitakuoa”
Yasmin nilipomwambia
vile alitabasamu. Nilihisi alikuwa akijaribu kuufariji moyo wake uliokosa
mapenzi kwa muda mrefu.
“Yasmin unaweza kusema
maneno hayo hapa kwa vile hatuna matumaini ya kupona. Lakini kama tutafanikiwa
kuondoka hapa unaweza kubadilika na kuniona mimi kama takataka”
“Nakuhakikishia kaka
yangu mpenzi sitabadilika. Mimi si kinyonga”
“Tuombe tuokoke katika
balaa hili lililotukabili”
“Ishaalah tutaokoka.
Tena wewe ndio utaniokoa mimi”
“Sio wewe uniokoe mimi?”
“Mimi nataka wewe
uniokoe mimi”
“Basi ishaala itakuwa
hivyo unavyotaka”
“Nikuimbie nyimbo?”
“Niimbie”
Yasmin aliacha kutembea
akasimama mbele yangu akiwa amenigeukia mimi. Kitendo hicho kilisababisha na
mimi nisimame. Akapeleke mikono yake kwenye mabega yangu.
“Mimi ni nani wako?”
akaniulza. huku akinitazama machoni mwangu.
“Wewe ni mpenzi wangu”
nilijua kuwa alikuwa anataka jibu hilo.
Nilipomjibu hivyo
alitabasamu na kuishusha mikono yake mabegani mwangu na kugeuka.
“Sasa ngoja nikuimbie”
akaniambia huku tunaenda.
Akaimba wimbo mzuri kwa
lugha ya Kikomoro. Wakati akiimba alikuwa akitingisha tingisha kichwa chake
kufuatia mawimbi ya sauti yake. Wakati akiimba alikuwa akitia mziki kwa mdomo.
Alionekana kuwa hodari sana wa kuimba na kutia mziki. Wimbo huo ulikuwa
unavutia ingawa sikujua tafsiri yake.
Alipomaliza kuimba
alinitafsiria kwa Kiswahili. Akaniambia “Ndege wawili dume na jike wamepotea
juu ya bahari. Hawajui watokako wala waendako. Wanalia swi! swi! swi!”
“Wamesafiri mchana kutwa
bila kupata mahali pa kutua. Sasa jua limekucwa na giza linaingia. Hawataweza
kusafiri usiku. Wanalia swi! swi! swi!”
Japo niliufurahia wimbo
huo tafsiri yake ilinisikitisha.Nikahisi kama ndege wawili hao walikuwa ni mimi
na yeye.
“Kumbe Yasmin unajua
sana kuimba!” nikamwambia.
“Hapana, najaribu tu”
“Si kujaribu, unajua”
“Kweli eh?”
“Umeniburudisha sana”
“Ukinioa nitakuwa
nakuimbia kila siku”
Tulikuwa tumeshafika
kwenye lile jumba analokaa.
Nikasimama kwenye
mlango.
“Mimi sitaingia ndani”
nikamwambia.
“Kwanini?” Yasmin
akaniuliza.
“Si nimekusindikiza tu”
“Ukinisindikiza ndio
huingii ndani, mbona siku nyingine unaingia?”
“Yasije yakanikuta
yaliyomkuta Masudi”
“Mimi naamini wewe huko
kama Masudi lakini kama umeamua uwahi kurudi, unaweza kurudi na nakutakia usiku
mwema. Tutaonana kesho.
“Asante. Usiku mwema na
kwako”
Nikamuacha Yasmin
amesimama akinitazama. Mimi nikarudi kule nyumbani tulikotoka. Nilirudi kwa
mwendo wa haraka haraka ili kiza kisinikute njiani kwani jua lilikuwa
limekuchwa sana.
Nilijikuta nikiwa na
furaha na mwenye matumaini kutokana na maneno ya Yasmin. Upendo aliouonesha
kwangu ulitosha kunipa hamasa ingawa tulikuwa katika hali ngumu.
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE KESHO KISA HIKI CHA KUSISIMUA
No comments:
Post a Comment