KISIWA CHA HARISHI (20)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Shazume akatikisa kichwa bila
kusema lolote.
“Kakangu najua umepatwa na
fadhaa lakini tumbo lako likipata riziki ndio akili itakuja” Yasmin akamwambia
Shazume.
“Tulikuwa watu saba sasa
tumebaki wawili tu bado nile? Sitakula!”
“Wewe ni mwanaume Shazume
usiogope kula. Unatakiwa upambane mpaka dakika ya mwisho. Mnaweza kuokoka ndugu
zangu. Msikate tama kiasi hicho. Twende ukanywe uji japo kidogo!” Yasmin
alimwambia.
Shazume akakubali kwenda.
Tukaondoka sote kwenda kwa Yasmin. Ile maiti ya Haji tuliiacha pale pale. Tangu
wenzetu walivyoanza kuuawa hatukuzika maiti yoyote. Zote tuliziacha ziliwe na
kunguru.
Kwa hisia zetu tulikuwa kama watu tuliokuwa vitani. Akifa mtu hakuna kuzika.
Kuzika kuna utaratibu wake ambao kutokana na hali tuliyokuwa nayo tusingeuweza.
Tulipofika kwa Yasmin
alituandalia uji tukanywa. Mimi nilikunywa vikombe viwili, Shazume alikunywa
kikombe kimoja.
Wakati tumepumzika Shazume
akawa anahimiza tuondoke.
“Tumeshakunywa uji sasa
tunaweza kwenda”
“Tusubiri kidogo nifikirie pa
kuwapeleka” Yasmin akamwambia.
SAS ENDELEA
Baada ya kusubiri kwa muda
kidogo Yasmin akatuambia. “Haya twendeni tukatafute nyumba nyingine”
Tukatoka na Yasmin. Niliona
wazi kuwa Yasmin alikuwa na wasiwasi. Alikuwa akitupeleka katika nyumba
nyingine lakini hakuwa mtu aliyeonesha matumaini.
Tulizunguka sana kutafuta nyumba nyingine ambayo ingeweza
kutufaa kumkwepa Harishi. Tulikuta nyumba moja iliyokuwa ufukweni mwa bahari
iliyokuwa na hali nzuri kidogo.
“Mnaionaje nyumba hii?”
Yasmin akatuuliza huku akituonesha nyumba hiyo.
“Hii inafaa” nikamwambia
kisha nikamtazama Shazume ili nipate mawazo yake.
“Unaionaje Shazume?”
“Hapa pamejificha kidogo,
panafaa” akaniambia ingawa sauti yake haikuwa na nguvu.
Tukaingia katika ile nyumba.
Humo ndani ilikuwa kama stoo iliyosahauliwa.
Vitu vilikuwa vimerundikwa ovyo. Ubuibui na vumbi vilikuwa vimetanda pande
zote.
Binaadamu mwenye akili zake
timamu asingeweza kukaa ndani ya nyumba ile labda waduu kama
vile nyoka na matandu. Lakini sisi hatukuwa timamu. Tulikuwa tumetingwa.
Tungeweza kukaa.
Kama tungehitaji kufanya usafi ili nyumba hiyo iweze
kukalika tungelazimika kutoa nje vitu vyote vilivyokuwa ndani na kuanza
kufagia, kupiga deki na kusafisha kuta. Ingekuwa kazi kubwa. Ingetuchukua hata
kwa siku mbili.
Tuliingia katika chumba
kimoja tukatenga vitu na kupata upenyu mdogo ambao tuliusafisha na kuamua kukaa
hapo.
Kusema kweli siku ile sisi
sote hatukuwa na furaha. Tulikaa chini pamoja na Yasmin. Tukawa kimya. Kila mtu
akiwaza lake.
Mimi nilkuwa nikiomba usiku
usifike kwani karibu wenzetu wote waliuawa usiku.
Sikujua Yasmin na Shazume
walikuwa wakiwaza nini. Lakini kila nilivyomuangalia Shazume niliona mawazo
yake yalikuwa mbali sana.
Nilikisia kwamba alikuwa akikumbuka kwao Pemba,
akiwakumbuka wazazi wake na ndugu zake. Pengine hakuwa na matumaini ya kuwaona
tena.
Bila shaka Yasmin alikuwa akiwaza kama
tutauawa atakosa wenzake wa kuzungumza nao na ataendelea kuwa mkiwa.
Mimi licha ya kuwa na hofu
nlishajitolea kufa kupona. Sikupenda kujipa tama moja kwa moja kuwa nitapona na
sikutaka kujikatia tama.
Ghafla Shazume akaanza kuimba
kwa sauti ya huzuni. Ulikuwa wimbo maarufu uliokuwa unaimbwa na vikundi vya
ngoma za kiasili.
“We Yauledi we niletee mashua
twende Unguja!. We Yauledi niletee mashua twende Unguja!”
Na mimi nikamuitikia. “Ukipamba
mke nawe ujipambe ndio suna. Usipojipamba watu hukwambia umtumwa! We Yauledi
niletee mashua twende Unguja!”
Shazume aliendelea kuimba
ubeti wake kwa kughani huku na mimi nikimuitikia.
Sauti ya wimbo huo ilikuwa ya
huzuni lakini ilituchangamsha. Yasmin alikuwa akitutazama. Wakati ninamuitikia
Shazume, Yasmin alikuwa akinifuatisha ninavyoimba.
Pengine tulikuwa tunajifariji
kwa siku yetu ya mwisho kwani tangu tufike katika kisiwa kile, kila siku
mwenzetu mmoja aliuawa na Harishi. Hakukuwa na siku yoyote ambayo hakukutokea
kifo.
Kwa hiyo hatukujua usiku wa
siku ile atakufa nani kati yangu na Shazume.
Shazume aliendelea kuimba kwa
huzuni. Mimi nilikuwa nimenyamaza. Yasmin akawa anamuitikia.
Shazume alipoona mimi
nimenyamaza na yeye akaacha kuimba tukawa kimya. Baada ya muda kidogo nilipata
wazo.
“Tuombeni dua” nikawambia
wenzangu.
“Tulikuwa tumejisahau kidogo”
Shazume akasema
Nikasoma dua ndefu. Shazume
na Yasmin wakawa wanaitikia “Amin”
Nilipomaliza nilimwambia
Shazume aombe na yeye. Shazume akaomba dua ndefu, sisi tukamuitikia “Amin”
Alipomaliza nikamwambia
Yasmin. “Omba na wewe”
ITAENDELEA KESHO, NA NINI KITAJIRI, USIKOSE UHONDO HUU KESHO
No comments:
Post a Comment