HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (19)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Nilipofika katika ile nyumba
niliwakuta wenzangu tayari wameshaanza kupata wasiwasi.
“Ilibaki kidogo tu tukufuate
kwa maana tuliona unachelewa” Haji akaniambia.
“Mlijua na mimi nimeshakwenda
na maji?” nikawatania.
“Si ajabu. Haa tunahesabiana
siku na saa tu”
“Tusikate tama kiasi hicho.
sisi ni wanaume. Mmeshakula?”
“Tulikuwa tunakusubiri wewe”
Shazume akaniambia.
“Mimi nimeshakuja. Toeni
chakula tule”
Chakula kikatolewa. Tukakaa
chini na kuanza kula.
Tulipomaliza kula tulikaa
uani tukawasha moto na kuuzunguka. Kiza kilikuwa kimeshaingia na kulikuwa na
baridi.
Tuliota moto hadi majira ya
saa mbili usiku. Tukaingia vyumbani kulala. Usiku ule haukuwa wa mawazo sana. Nilipitiwa na
usingizi mara moja.
Nilipoamka asubuhi
nilishituka nilipoona mlango wa nje ulikuwa umeng’olewa mzima mzima. Palibaki
uwazi mtupu. Mlango wa chumba alicholala Haji pia ulikuwa umeng’olewa. Mlango
wa chumba cha Shazume ulikuwa mefungwa.
Nikaenda katika ule mlango wa
chumba cha Haji na kuchungulia. Nilimkuta Haji akiwa amelala chini amekufa.
Kichwa chake kilikuwa kimetobolewa kwenye utosi. Damu iliyoganda ilionekana
kwenye nywele zake.
Hapo nilijua kuwa tulikuwa
tumeingiliwa. Bila shaka Harishi alikuwa amekuja usiku akang’oa milango na
kumuua Haji.
SASA ENDELEA
Lilikuwa tukio ambalo
sikulitegemea. Katika kundi letu Haji ndiye aliyekuwa mdogo kuliko sote. Kifo
chake kilinisikitisha na kunikatisha tamaa kabisa.
Nilijiambia kama Harishi
ameweza kutufuata huku na kumuua Haji na sisi hatutabaki. Tilichokuwa
tunasubiri ni siku na saa zetu ziwadie.
Baada ya kushangaa kwenye
mlango kwa sekunde kadhaa nilikwenda kumgongea Shazume. Shazume akaamka na
kufungua mlango.
“Una habari gani?”
nikamuuliza nikiwa nimetaharuki.
“Sina habari yoyote” Shazume
akanijibu huku akionesha kupata hofu.
“Haji ameuawa!” nikamwambia.
Shazume akagutuka.
“Haa! Haji naye ameuawa? Si
tulilala naye humu ndani jana usiku?”
“Tazama ule mlango wa nje”
Nilimuonesha Haji ule mlango
uliong’olewa kisha nikamwambia. “Harishi ameung’oa usiku”
Shazume aliutazama huku
akitikisa kichwa.
“Ameng’oa na mlango wa chumba
cha Haji” nikaendelea kumwambia.
Shazume akasogea kwenye
mlango wa kilichokuwa chumba cha Haji. Alipoiona maiti ya Haji alishituka sana.
“Mimi naona hatutapona”
“Kupona tusitegemee ndugu
yangu. Harishi ameshajua tupo hapa, usishangae kesho tukiamka mmoja wetu akawa
hayupo!”
“Hapa nyumbani hapafai tena
kukaa. Tutafute sehemu nyingine ya kujificha”
“Tutajificha wapi Shazume?”
“Popote tu, nyumba ziko
nyingi”
“Sawa. Tumngoje Yasmin aje
tumueleze kuwa mwenzetu ameuawa”
“Pia tumueleze kuwa
tunaondoka hapa. Harishi akija tena asitukute”
“Sawa, tutamueleza”
Tukaenda kunawa uso na
kusukutua maji bila kupiga mswaki. Tulikuwa tumeshachanganyikiwa. Tulipomaliza
tulikaa kumsubiri Yasmin.
Yasmin alikuja majira ya saa
tatu hivi. Hakuwa amechukua kitu.
Akatusalimia na kutuuliza
kwanini tumeng’oa milango.
“Hebu chungulia kwenye hicho
chumba” nikamwambia.
Yasmin akachungulia na
kugutuka.
“Haji amepatwa na nini?”
“Haji ameuawa usiku na
Harishi” nikamwambia.
“Mama yangu!” Yasmin alimaka
huku akijishika kichwa. “Kumbe Harishi alipotoka usiku alikuja huku?”
“Sisi tumeona asubuhi Harishi
ameuawa na milango imeng’olewa”
“Sasa tumepanga tuondoke
hapa” Shazume akamwambia Yasmin.
“Muondoke muende wapi?”
“Twende mahali pengine.
Tukiendelea kukaa hapa Harishi atakuja tena usiku”
“Sasa mmepanga muende wapi?’
“Mimi naona kama
tunajisumbua, kama ni kufa tutakufa tu”
nikasema.
“Hata kama tutakufa lakini
hapa tuondoke” Shazume akasisitiza.
“Ni sawa. Sasa tufikirie hapo
pa kwenda. Tutakwenda wapi?”
“Nyumba ziko nyingi”
“Yasmin unatushauri nini?”
Machozi yalikuwa yanamtoka
Yasmin. Bila shaka yalimtoka kutokana na ukweli kwamba sote tutakufa.
Hakunijibu.
“Yasmin usilie. Tunaomba
ushauri wako” nikamwambia.
Yasmin alijifuta machozi
kisha akatuambia. “Niwapeleke katika nyumba nyingine”
“Huko utakakotupeleka Harish
hatafika?” nikamuuliza.
Yasmin akaguna kisha akajibu.
Hatafika”
Nilijua alitujibu hivyo
kututia moyo tu lakini mawazo ya Shazume yalikuwa tofauti.
“Ni mahali gani?” Shazume
akamuuliza haraka.
“Kwanza
twendeni mkanywe uji”
“Turudi kule tena?” Shazume
akamaka.
“Mnakunywa uji tu halafu
tunaondoka”
Shazume akanitazama.
“Mimi sitakwenda”
“Si tunakwenda kunywa uji tu”
nikamwambia.
“Kwanza Harishi hatakuja muda
huu” Yasmin akasema.
“Mimi sitaki uji”
“Utashinda hivyo hivyo na njaa?”
Yasmin akamuuliza.
“Sioni njaa na ile hamu ya
kula pia sina”
“Kama tumeandikiwa kuuawa
tutauawa tu Shazume hata kama hutakula, ni
bora ule tu” nikamwambia Shazume.
ITAENDELEA KESHO. TUMA MAONI
YAKO KUHUSU HADITHI HII KWA NAMBA
0655 340572
No comments:
Post a Comment