Kumekucha blog
Muheza, POLISI Wilayani Muheza Mkoani Tanga,
imewakamata wahamiaji haramu sita kwa tuhuma za kuingia nchini bila kibali
wakiwa wamefichwa katika nyumba ya mtu anaesadikiwa kuwa ni wakala wa
kusafisrisha wahamiaji haramu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,
kamanda wa polisi Mkoani hapa, Freisser Kashai, alisema polisi ilipata taarifa
kutoka kwa wakazi kijiji cha Kicheba kuwepo kwa watu wanaokatisha mitaa ambao hawafahamu.
Alisema alituma askari wa upelelezi kuchunguza kuwepo
kwa watu hao na kubaini kama ni wahamiaji haramu na baada ya kujiridhisha kwao
waliweza kuvamia usiku wa saa 8 na kuwakamta watu wote na mwenyeji wao
kufanikiwa kutoroka.
“Jambo la kufurahisha ni kuona jamii inashirikiana na
polisi kwa kila jambo ambalo wanahisi kwao linaweza kuwaletea matatizo ----hili linaleta
faraja na tunawaomba wananchi kushirikiana na polisi kwa kila jambo” alisema
Kashai
Kamanda aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni,Gesemu
Abato(30), Hash Negash(20), Tsegaye Aliso(21), Jamal Godso(25), Alemayo
Ataro(22) na Erigudo Elitiro(25) wote walikamatwa wakiwa wamelala na kushindwa
kutoroka.
Alisema watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada
ya uchunguzi kukamilika na kwa sasa wanaendelea kumtafuta wakala wao ili kuweza
kumfikisha katika vyombo vya sheria na kuwa fundisho kwa wengine.
Katika tukio jengine, kamanda Kashai alilitaja kuwa ni
mkazi wa Kinondoni, Enerst Joseph, amefariki baada ya gari lake alilokuwa
akiendesha kuacha njia na kutumbukia katika mto na watu wawili waliokuwa ndani
kupata majereha.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 7 mchana eneo la
Kitumbi kata ya Mkata Wilayani Handeni barabara kuu ielekeayo Chalinze Mkoani
Pwani na kuwajeruhi watu wawili ambao hadi muda huo hawajatambuliwa majina yao.
“Uchunguzi wa kipolisi umeonyesha kuwa dereva wa gari
hilo alikuwa amelewa chakari na pombe zake kumfanya kwenda mwendo kasi bila
kujitambua----alipofika mlima wa Kitumbi na kuteremsha alishindwa kuimudu kona
ya daraja na kutumbukia” alisema Kashai
“Taarifa za dereva huyo ni kuwa hata katika kituo cha
ukaguzi kilichopo kilometa moja tu kutoka eneo la ajali aliposimamishwa hakusimama---pombe
zake bila kikomo zimemiondoa duniani” alisema Kashai
Akitoa wito kwa jamii inayoishi katika mipaka ya nchi
jirani na misitu inayotumiwa na wasafirishaji wa magendo na wapitishaji
wahamiaji haramu, Kashai alisema mtu yoyote ambaye atabainika kushirikiana na
watu hao atafikishwa katika vyombo vya sheria.
Mwisho
No comments:
Post a Comment