Yanga na Azam Fc ngoma draw.
Ligi kuu ya soka Tanzania Bara imeendelea hii leo kwa michezo minne iliyopigwa kwenye mikoa tofauti kuanzia jijini Dar es salaam , Mkoani Morogoro na jijini Mbeya .
Kwenye uwanja wa taifa jijini Dar-es-salaam Mabingwa watetezi wa ligi hiyo Azam Fc na washindi wa pili kwa msimu uliopita Dar-es-salaam Young Africans walitoka sare ya 2-2 katika mchezo uliokuwa mkali na wenye kasi ya juu .
Azam walianza kufunga kupitia kwa mshambuliaji wa zamani wa Yanga Didier Kavumbagu akifanyia kazi makosa ya mlinzi wa Yanga Mbuyi Twite na kipa wake Deo Munishi Dida waliogongana wakienda kuokoa mpira mmoja .
Bao hilo lilidumu kwa takribani sekunde tisini baada ya Yanga kuanzisha shambulizi mara tu baada ya mchezo kuanza shambulizi lililozaa bao lililofungwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo Hamis Tambwe .
Yanga walipata bao la pili mapema kwenye kipindi cha pili mfungaji akiwa Simon Msuva aliyefunga kwa kichwa kufuatia krosi ya Haruna Niyonzima .
Mshambuliaji John Rafael Bocco ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Abubakar Salum Sureboy aliisawazishia Azam kwa mpira wake wa kwanza tu tangu aingie akimalizia kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Himid Mao Mkami .
Katika michezo mingine Mtibwa Sugar na Stand United walitoka sare ya 1-1 katika mchezo uliolazimika kucheza ndani ya siku mbili tofauti baada ya mvua kubwa kunyesha huko Manungu Tunriani Mkoani Morogoro na hivyo kufanya mchezo huo kuahirishwa na kumaliziwa hii leo , nao Polisi Moro waliwafunga Mgambo Jkt kwa matokeo ya 2-0 bila huku Mbeya City wakishinda mchezo wao dhidi ya Ndanda Fc toka Mtwara kwa matokeo ya 1-0 .
Matokeo haya yanamaanisha kuwa hakuna mabadiliko yoyote kwenye msimamo wa ligi hiyo kwa upande wa timu zinazoshika nafasi ya juu baada ya Mtibwa , Yanga na Azam Fc zote kupata sare katika michezo yake .
No comments:
Post a Comment