HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (22)
ilipoishia toleo lililopita
“Sidhani kama hapa ni karibu
na kwenu Comoro. Mimi nadhani kama tutapata msaada wa kuokolewa tutapelekwa
kwanza Zanzibar”
nikasema.
“Si vibaya Zanzibar pia ni nyumbani lakini baba akipata
habari atatuma ndege siku hiyo hiyo ituchukue pamoja na nyinyi”
“Itakuwa raha sana tukienda Comoro na
kupokewa na rais” nikasema.
Shazume alikuwa kimya
akitusikiliza. Bila shaka alikuwa anaona tunajidanganya kujifariji. Kwa mawazo
yake sisi tulikuwa ni wa kufa tu.
“Si unajua mzazi
aliyekwishamkatia tamaa mwanawe halafu anaambiwa amepatikana, atafurahije?”
Yasmin akaniuiza.
“Atafurahi sana”
Iliwezekana tulikuwa tulikuwa
tunajidanganya kweli kama alivyowaza Shazume
lakini tulifarijika. Saa zikapita.
Tulipomaliza kula Yasmin
alileta storitofauti tofauti kutuondoa katika mawazo mabaya. Tukawa
tunazungumza.
Aliondoka jioni sana. Tukamsindikizakwa
pamoja hadi nusu ya njia, tukarudi. Tukakaa kwenye kile kisehemu chetu kusubiri
usiku. Hatukujua nini kitatokea kati yetu usiku huo.
SASA ENDELEA
Usiku ule tulikesha macho kwa
sababu ya hofu. Tulikuwa tumejilaza chini kila mmoja upande wake lakini
hakukuwa na aliyelala usingizi. Mara kwa mara nilimuona Shazume akijigeuza kila
upande.
Ilikuwa kati kati ya usiku
Shazume aliposhika mguu wangu. Sikujua kama alikuwa anataka kuniamsha au
alitaka kujua nilikuwa macho lakini aliponishika nilishituka nikarusha mguu
wangu.
“Nini?” nikamuuliza nikiizuia
sauti yangu isisikike sana.
“Nimebanwa na haja ndogo”
akaniambia.
“Sasa?” nikamuuliza.
“Tunaweza kutoka
nikajisaidie”
“Haya tutoke” nikamwambia.
Shazume akainuka na mimi
nikainuka. Akatangulia kutoka kwenye mlango. Kulikuwa giza
sana.
Hatukuweza kuona kwa mbali.
“Twende nje au uani?” Shazume
akaniuliza.
“Naona tutoke uani”
nikamjibu.
Shazume akaelekea upande wa
uani. Mimi nilikuwa nikimfuata nyuma. Alifungua mlango akachungulia uani. Mwezi
ulikuwa unaangaza, ua ulikuwa mweupe. Baada ya kuchungulia kwa tahadhari
Shazume alivuka kizingiti cha mlango akatoka uani na mimi nikatoka.
Yeye alikwenda upande wake na
miminilikwenda upande wangu tukachutama na kujisaidia. Mimi sikuwa na haja
ndogo lakini baada ya mwenzangu kuniambiana mimi nikaisikia.
Tulipomaliza haja zetu
tulirudi ndani tukajilaza tena. Safari hii tulipojilaza tu usingizi ulitupitia
tukalala.
Wakati nipo usingizini
niliota Harishi anatufukuza baada ya kutufuma tukiwa na Yasmin kwenye lile
jumba lake. Tukaingia katika chumba kimoja kujificha chini ya mvungu wa
kitanda. Muda si muda Harishi akafungua mlango na kuingia mle chumbani
kututafuta.
Akaona mguu wa Shazume
umetokeza chini ya mvungu. Akaushika na kuuvuta. Shazume akawa anapiga kelele
kuniita.
Kelele hizo ndizo
zilizoniamsha. Nikaamka na kuangaza macho. Nikasikia Shazume akiendelea kupiga
kelele kuniita lakini sauti yake ilitokea kwa juu, sio pale chini tulipolala.
Nikashituka sana
kwa kujua kuwa haikuwa ndoto.
Nikatazama juu. Kwanza niliona kanzu nyeupe halafu nikaona upanga
uking’aa. Nilipoona hivyo nilijisogeza zaidi ndani ya makorokoro na kuendelea
kuchungulia.
Nilimuona Shazume ameinuliwa
juu juu na Harishi. Nikajiambia kumbe ile ndoto ilikuwa ni kweli. Shazume alitolewa
mle chumbani. Sikuweza kujua Harishi aliwasili muda gani na kumkamata Shazume.
Bila shaka kilichokuwa
kimeninusuru mimi, ni kuwa nililala nyuma ya mlango. Harishi alipoingia
alimuona Shazume na kumkamata yeye.
Ile ndoto niliyoota ilikuwa
ya kweli. Harishi alikuwa ametuingilia!
Jitihada zetu za kujaribu
kumkwepa zilikuwa za bure kwani Harishi alikuwa akitugundua kila tulipokwenda
kujificha na sababu ni kuwa alikuwa akifuata harufu zetu kama
vile m’bwa.
Harishi alipomtoa Shazume
ukumbini, nilimsikia Shazume akipiga ukulele mmoja tu “Nakufa!”. Halafu
sikusikia kitu tena.
Moyo ulikuwa ukinienda mbio
na nilikuwa nikihema kwa nguvu kama niliyekuwa
nafukuzwa. Tukio hilo lilikuwa la ghafla sana kiasi kwamba nililazimika
kujiuliza, kama bado nilikuwa kwenye ile ndoto au kilichokuwa
kinatokea kilikuwa kweli.
Hofu yangu sasa ilikuwa
kwangu. Nilijiua Harishi akimaliza kumuua Shazume ataniingilia na mimi kwani
alipoingia humo chumbani alituona tukiwa wawili.
Wazo hilo likanifanya nizidi kujisogeza kwenye
makorokoro ili Harishi akiingia tena asinione. Lakini muda ulipita. Sikumuona
tena Harishi.
Nikaendelea kukaa hapo hapo
hadi nikaona kunakucha. Nikahisi kwa muda ule Harishi atakuwa ameshaondoka.
Nikajiburuza kujitoa kwenye yale makorokoro nilikojiingiza.
Nilinyata hadi kwenye mlango
nikaufungua na kuchungulia ukumbini. Nilichungulia upande wa mbele na upande wa
uani. Niliiona maiti ya Shazume imelala chini kando ya mlango wa chumba
tulichokuwemo. Harishi mwenyewe hakuwepo.
Nikatoka nje na kuangalia
kila upande. Sikuona kitu. Kando ya ile nyumba palikuwa na mti. Nikapata wazo
kuwa nipande juu ya ule mti kujificha. Nikaenda kwenye mti huo nikaupanda na
kukaa kwenye tawi mahali ambapo nisingeweza kuonekana.
Wakati nipo juu ya ule mti
nilimuona Yasmin kwa mbali akija. Nikajiambia tuliobaki katika kisiwa kile
tulikuwa watu wawili tu, mimi na Yasmin.
Sikupenda kujisifu kuwa
nilikuwa nina bahati kwa sababu nimenusurika. Nilijua kuwa wakati wangu ulikuwa
haujafika. Pengine niliandikiwa niwe wa mwisho kufa.
Historia ya kisiwa hicho
tangu tulipofika kila siku alikufa mtu. Leo nimeishuhudia maiti ya Shazume,
huenda kesho Yasmin ataishuhudia maiti yangu.
Yasmin alipofika pale
nilimuacha aingie mle ndani. Mara moja nikamuona ametoka akiwa
amechanganyikiwa. Bila shaka alikuwa ameshitushwa na maiti ya Shazume.
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE KESHO NINI KITAJIRI
No comments:
Post a Comment