HADITHI
NILIJUA NIMEUA
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
Alitoa pochi mfukoni
akaifungua na kutoa noti mbili za elfu kumi kumi akanipa.
“Sasa nipe namba yako, naweza
kukuhitaji tena” Mtu huyo akaniambia.
Nikampa namba yangu ya simu
akaiandika kwenye simu yake kasha akaniuliza.
“Unaitwa nani?”
“Andika Majomba Teksi”
Baada ya kuandika jina hilo aliniambia.
“Vizuri, nitakutafuta”
“Sawa” nikamjibu. Nilijipakia
kwenye teksi yangu nikaiwasha na kuondoka.
Wakati naendesha nilijikuta
nikumuwaza huyo mwanamke mjamzito aliyetakiwa kufanyiwa operesheni. Sikuwa na
hakika kwamba alikuwa katika hali gani muda ule kwani kwa vyovyote vile yule
daktari alikuwa amechelewa sana kufika pale
hospitali kutokana na gari lake
kuharibika.
SASA ENDELEA
Sikuendelea kumuwazia sana mwanamke huyo ambaye
hata hivyo sikuwa nikimfahamu, nikajiambia sasa kumeshakucha. Nisingeweza tena
kurudi kulala kwani muda ule ulikuwa ndio wa kuanza kazi.
Sikujali kupoteza usingizi
wangu kwani nilikuwa nimeingiza zaidi ya shilingi elfu thelathini haraka
haraka.
Nilichokuwa ninakiwazia ni
kwenda kutia mafuta teksi yangu, nirudi nyumbani kuoga kasha nitoke tena.
Mpaka inafika saa mbili na
nusu nilikuwa kwenye mkahawa mmoja nikipata kifungua kinywa. Nilikuwa
nimeshaoga, kuvaa nguo nyingine na kuondoka nyumbani.
Baada ya kumaliza kufungua
kinywa nilikwenda kwenye kituo changu jirani na hospitali ya Ngamiani. Nilipata
safari mbili za haraka haraka, nikaingiza elfu kumi na mbili.
Wakati naegesha tena gari
simu yangu ikaita. Nilipoipokea niligundua aliyekuwa akinipigia alikuwa ni yule
daktari wa hospitali ya Bombo.
“Nimemaliza operesheni, sasa
ninataka uje ulivute gari langu twende kwa Habib Garage pale Gofu”
“Sawa. Ninakuja”
Nilitazama saa yangu. Ilikuwa
saa sita na robo. Nikaiondoa teksi yangu kuelekea hospitali ya Bombo.
Nilimkuta yule daktari
ameliegemea gari lake
ambalo tuliliegesha nyuma
ya mti.
Nilisimamisha teksi mbele ya
gari hilo
nikashuka. Nilikwenda kufungua boneti la nyuma ya teksi nikatoa ile kamba. Ncha
moja nikaifunga nyuma ya teksi na ncha nyingine nikaifunga mbele ya gari la
yule daktari.
“Tayari” nikamwambia.
Daktari huyo akaingia kwenye
gari lake. Na mimi nikaingia kwenye teksi yangu. Nilipowasha teksi tukaanza
safari ya kuelekea Gofu.
Tulipofika huko nililiingiza
gari hilo ndani
ya gereji ya Habib. Daktari huyo akanilipa pesa yangu niliyotaka, nikaondoka.
Tangu siku ile nikaanza kujuana na daktari
Augostino Kweka. Alikuwa daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya Bombo.
Mara kwa mara gari lake
lilipokuwa na matatizo
alikuwa akiniita mimi nimpeleke safari zake.
Tulijuana na hatimaye tukawa
marafiki wakubwa.
Kuna siku Mariam
alinibainishia jina lake
halisi. Aliniambia
anaitwa Halima. Si unajua wanawake wa
kitanga wanavyopenda kuficha majina yao.
Mpaka mzoeane sana
ndio atakutajia jina lake.
Wakati huo tulikuwa tumezoeana vya kutosha kiasi
kwamba aliweza kunikodi nimpeleke safari zake kIsha akaweka deni na huja
kunilipa siku nyingine.
Nilimuamini kwa sababu
alikuwa muaminifu na hakuwa akisahau deni. Siku anayoahidi kunilipa hunilipa
bila matatizo.
Ule ukaribu wetu ukafanya
tuwe marafiki. Kulikuwa na siku ambayo nilikuwa nimempakia kumpeleka sehemu.
Nikamueleza undani wangu kuwa nilimpenda.
“Umenipendaje?” akaniuliza.
Lilikuwa swali la kitoto lakini baadaye
niligundua lilikuwa na maana.
“Nataka uwe mke wangu”
“Kwani wewe huna mke, au
unataka niwe mke mwenza?”
“Sio mke mwenza, mimi sina
mke. Sijaoa bado’
“Sawa. Nipe muda nikufikirie”
“Usichukulie mzaha Halima,
nakwambia ukweli”
“Na mimi nakwambia ukweli”
“Sasa unataka nikupe muda
unifikirie nini, kwani ninaomba kazi?”
Halima akacheka.
“Si unaomba uchumba. Nataka
nikufikirie unanifaa au hunifai”
“Lini utanipa jibu?”
“Siku yoyote tu”
“Basi usinicheleweshe sana, nisije nikabadili
uamuzi wangu”
“Usijali”
Kutoka siku ile mara kwa mara
nikawa nampigia simu kumsalimia. Na yeye pia alikuwa akinipigia kuniuliza hali
hasa kama nimepitisha siku mbili au tatu bila
kumpigia.
Kuna siku nilikuwa naumwa
kichwa. Akanipigia simu na kuniambia alitaka kunitembelea nyumbani.
Nikamuelekeza ninapoishi. Baada ya muda kidogo akanipigia tena akaniambia yuko
nje ya nyumba yangu.
Nikatoka na kumkuta amesimama
pembeni mwa nyumba yangu. Nikamkaribisha ndani.
“Nilikuwa nimepotea, kama nisingeiona ile teksi yako pale barazani,
nisingeitambua hii nyumba” akaniambia wakati tumo chumbani.
“Lakini hapapotezi, labda
wewe hufiki sana
huku Msambweni”
“Labda. Unajisikiaje kuumwa?”
“Sijambo kidogo, nikuletee
soda?”
“Acha tu. Unaumwa na nini?”
“Kichwa. Kichwa kinauma sana. Siwezi hata
kuendesha gari. Sijui waswahili wameniroga?”
ITAENDELEA KESHO, usikose uhundo huu wa kusisimua kesho ni hapa hapa, www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment