NILIJUA
NIMEUA
ILIPOISHIA
Kwa vile
nilikuwa kwenye mwendo wa kasi nililipita gari hilo na kwenda kusimama mbele.
Hapo hapo mawazo yangu yakabadilika. Niliwaza kwamba huenda gari hilo liliegeshwa
kwa hila lionekane limeharibika kumbe ni majambazi wanaosubiri magari yasimame
waanze kupora watu.
Nilikuwa
nimechelewa kufikiria hilo. Nilikuwa nimeshasimamisha teksi na jamaa
aliyenisimamisha alikuwa ameshafika kwenye dirisha la teksi yangu!
Chini ya
siti yangu ya dereva, siku zote huweka parange (sime ya kimasai) kwa ajili ya
kujihami endapo kutatokea tatizo la kuvamiwa na mtu au watu wenye nia mbaya.
Kwa vile
sikuwa na uhakika kuwa mtu huyo aliyenisimamisha alikuwa na nia mbaya au nzuri,
tayari nilishapeleke mkono wangu wa kulia kuushika mpini wa parange iliyokuawa
chini ya siti niliyokalia.
Nilikuwa
nimejiweka tayari, kama atakuwa na nia mbaya niweze kukabiliana naye.
SASA ENDELEA
“Samahani
bwana” Mtu huyo akaniambia. Ingawa sauti yake ilikuwa tulivu nay a kibinaadamu,
ilikuwa imeficha taharuki.
“Unasemaje?”
nikamuuliza nikiwa nimemkazia macho kusoma mawazo yake.
“Mimi ni
daktari wa hospitali ya Bombo. Nimepigiwa simu kuitwa hospitali,
kuna mama mjamzito anahitaji kufanyiwa operesheni ya dharura sasa hivi. Kwa
bahati mbaya gari langu limeharibika njiani. Naomba unipeke Bombo haraka”
akaniambia.
“Kusema
kweli nilimuelewa. Nikamuuliza.
“Na hilo
gari lako je?”
“Ningeomba
kama itawezekana unisaidie kulivuta niliondoe mahali hapa”
“Hiyo
itakuwa ni kazi nyingine” nikamwambia.
“Naomba
msaad wako kaka, sina jinsi na siwezi kuliacha hapa”
“Unataka
nilivute hadi wapi?”
“Hadi Bombo.
Nitaliegesha sehemu. Kutakapokucha nitajua la kufanya”
“Utanilipa
kiasi gain?”
“Sema wewe”
“Kulivuta
hilo gari lako pamoja na kukufikisha wewe Bombo utanilipa elfu ishirini”
“Sawa.
Nitakulipa”
Alipokubali
kima changu nilifungua mwa gari nikashuka.
“Una kamba?”
nikamuuliza.
“Kamba sina’
Nilikuwa na
kamba ya akiba kwenye boneti la teksi yangu. Nilikwenda nyuma ya gari,
nikafungua boneti na kutoa kamba. Nikaiweka chini.
Kisha
niliisogeza teksi mbele ya gari la mtu huyo lililokuwa pembeni. Nikashuka tena
na kufunga ncha moja ya kamba nyuma ya gari langu na ncha nyingine nikaifunga
mbele ya lile gari. Nilipomaliza nilimwambia mtu huyo ajipakie kwenye gari
lake.
Wakati
anajipakia na mimi nilikwenda kwenye mlango wa teksi nikaufungua na kujipakia.
Nilitia gea na kuiondo teksi taratibu. Kamba ilinyooka na kukaza kabla ya
kuanza kulivuta gari la nyuma.
Niliingia
barabarani nikawa naendesha taratibu. Kwa vile niliendesha kwa mwendo mdogo
tulifika Bombo saa kumi na mbili asubuhi.
Nilishuka
kwenye teksi nikaifungua ile kamba na kuiweka kwenye boneti.
“Nakushukuru
sana” Mtu huyo akaniambia baada ya kushuka kwenye gari lake.
Alitoa pochi
mfukoni akaifungua na kutoa noti mbili za elfu kumi kumi akanipa.
“Sasa nipe
namba yako, naweza kukuhitaji tena” Mtu huyo akaniambia.
Nikampa
namba yangu ya simu akaiandika kwenye simu yake kasha akaniuliza.
“Unaitwa
nani?”
“Andika
Majomba Teksi”
Baada ya
kuandika jina hilo aliniambia.
“Vizuri,
nitakutafuta”
“Sawa”
nikamjibu. Nilijipakia kwenye teksi yangu nikaiwasha na kuondoka.
Wakati
naendesha nilijikuta nikumuwaza huyo mwanamke mjamzito aliyetakiwa kufanyiwa
operesheni. Sikuwa na hakika kwamba alikuwa katika hali gani muda ule kwani kwa
vyovyote vile yule daktari alikuwa amechelewa sana kufika pale hospitali
kutokana na gari lake kuharibika.
ITAENDELEA
Usikose uhundo wa kisa hiki cha kusisimua hapa hapa www.tangakumekucha.blogspot.com
|
Friday, April 17, 2015
NILIJUA NIMEUA SEHEMU (4)
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment