Sunday, October 2, 2016

HADITHI, YAMENIKUTA SALMA MIE SEHEMU YA 12 INALETWA KWENU NA FREYS COACH, TANGA HADI SINGIDA

YAMENIKUTA SALMA MIE 12 inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya usafirishaji abiria ya Freys Coach, Tanga, Moshi, Arusha, Babati hadi Singida kila siku saa 12 kamili na 12 na 30. Mawasiliano yao 0622 292990
 
ILIPOISHIA
 
Nilipoingia ndani nilimkuta mume wangu amekaa sebuleni peke yake. Zacharia hakuwepo.
 
“Habari ya hapa?’ nikamsalimia.
 
“Nzuri, mbona umechelewa sana?”
 
“Nilikwenda huko kwa mama yangu. Kuna mtabibu pale mtaani kwetu amenipa dawa nije nikufanyie”
 
“Dawa gani?”
 
“Dawa ya majani. Ameniambia nikufikichie kwenye macho kwa siku tatu”
 
“Haya tujaribu”
 
“Ameniambia nikufanyie asubuhi na jioni. Asubuhi imeshapita tusubiri jioni tuanze”
 
“Unanifikichia vipi?”
 
Nikamueleza vile nilivyoagizwa na yule mganga.
 
SASA ENDELEA
 
“Haya utanifikichia tujaribu”
 
“Amenihakikishia kuwa itakusaidia”
 
“Lakini haiwashi machoni?”
 
“Hakuniambia lakini nafikiri haiwashi kama inawasha angeniambia”
 
Baada ya hapo niliingia jikoni na kuanza kupika. Ile dawa niliitunza mahali pazuri ambapo ingeweza kukaa bila kukauka.
 
Ilipofika jioni nilichomoa majani matatu ya dawa hiyo nikaenda sebuleni ambako mume wangu alikuwa amekaa nikamwambia alale chini kichalichali ili nimfikichie machoni.
 
Mume wangu aliondoka kwenye kochi alipokuwa ameketi akasogea mbele kidogo na kukaa chini kisha akajilaza kichalichali.
 
Nilichutama  na majani yangu nikayashika na kuyafikicha kabla ya kumkamulia machoni mwake.
 
Maji maji yaliyotoka kwenye  majani hayo yalipomuingia machoni alifumba macho.
 
“Usifumbe macho, yafumbue” nikamwambia. “Yafumbue dawa ikuingie vizuri”
 
Akayafumbua kiuoga.
 
“Fumbua bwana!”
 
“Nimeshayafubua”
 
“Bado, fumbua zaidi”
 
Macho yake yalikwishakuwa maoga. Alishindwa kuyamfumbua sawa sawa.
 
Nikamkamulia majani majani hayo hivyo hivyo. Maji maji machache yalimuingia machoni, mengine yalichirizika kingoni mwa macho na kumwagika chini.
 
Nilirudia kumkamulia mara tatu.
 
“Umeshamaliza?” akaniuliza.
 
“Nadhani imetosha”
 
Alikuwa anataka kuinuka nikamzuia.
 
“Ngoja kwanza dawa ikuingie vizuri, una haraka ya nini?”
 
Akatulia.
 
Baada ya dakika tatu hivi nikamwambia ainuke. Akainuka na kukaa kwenye kochi.
 
“Yanawasha?” nikamuuliza.
 
“Yanawasha kwa mbali”
 
Nilichukua kitambaa nikamfuta futa yale maji maji yaliyokuwa yamemchirizikia pembeni mwa macho kisha nikaondoka.
 
Asubuhi nilimfanyia tena,  nikarudia tena jioni.
 
“Vipi, hujaanza kuona ona” nikamuuliza.
 
“Bado. Naona kiza tu”
 
“Mganga mwenyewe ameniambia nikufanyie kwa siku tatu”
 
“Labda mpaka kesho kutwa”
 
Niliendelea kumfanyia Ibrahim dawa hiyo kwa siku tatu lakini macho ya Ibrahim hayakuona chochote. Siku ya nne yake nikarudi tena kwa yule mganga.
 
Nilipomueleza nilimuona akikunja uso.
 
“Bado hajaweza kuona?” akaniuliza.
 
“Hajaona bado”
 
Mganga akafikiri kisha akaniambia.
 
“Njoo kesho nitakupa dawa nyingine”
 
Nikaondoka. Kwa vile hata zile dawa alizopewa  hospitalini hazikuweza kumsaidia, kesho yake nilirudi tena kwa yule mganga. Kwa kweli aliniweka sana. Alipomaliza kuhudumia wateja wake akaniita na kuniambia niende tena kesho kwani hakupata nafasi ya kwenda kunichumia dawa nyingine.
 
Nikaondoka. Siku iliyofuata Ibrahim alipelekwa hospitali na mdogo wake na mimi nikatoka kwenda kwa mganga.
 
Nilipofika alinipa dawa ya ungaunga mweusi, akanimbia nichote kidogo niroweke kwenye maji ya vugu vugu kwa dakika moja kisha nimpe mume wangu anawe uso.
 
“Niroweke kwenye maji ya kiasi gani?” nikamuuliza kwa matumaini.
 
“Kama nusu lita hivi”
 
“Anawe uso yote?”
 
“Ndiyo anawe yote. Unamtilia asubuhi na jioni kidogo kidogo”
 
“Kwa siku ngapi?”
 
“Kwa siku tatu”
 
Baada ya mazungumzo hayo nikaondoka. Nilikuta mume wangu alikuwa amesharudi kutoka hospitali. Alikuwa amepewa dawa nyingine za kutumia kwa siku tatu.
 
“Na mimi nimekwenda kwa mtaalamu mwingine” nikamwambia.
 
“Amekwambiaje?”
 
“Baada ya kumueleza matatizo yako amenipa hii dawa”
 
“Ni dawa ya aina gani?”
 
“Ni ya unga unga. Ameniambia nitie kwenye maji ya vugu vugu kisha uoshe uso asubuhi na  jioni”
 
“Kwa sababu tuna shida tutafanya” Mume wangu aliponiambia hivyo niliona huzuni sana.
 
Tulifanya ile dawa kwa siku tatu bila mafanikio. Zile dawa za hospitali nazo hazikuleta matumaini yoyote.
 
Kwa vile niliona lile tatizo lilitokea kwa yule mganga nikarudi tena bila kuchoka. Mganga akanibadilishia dawa nyingine. Nazo pia hazikufaa.
 
Kwa upande wa hospitalini tulimaliza hospitali kadhaa za macho. Mume wangu aliambiwa hawezi kuona tena!
 
Sasa maisha yetu yalianza kuwa magumu. Mume wangu alikuwa hawezi tena kufanya kazi. Tulikuwa tunakula mtaji. Kusema kweli pesa nyingi zilimalizika kwa uchunguzi na matibabu yake.
 
Mwisho wake akanimabia anafikiria kuuza ile gari yake ili apate pesa za kuendelea kujitibu. Kulikuwa na watu ambao walikuwa wakimpa moyo kwamba asikate tamaa.
 
Akauza lile gari. Pesa hizo nazo zikaisha kwa chakula na kuwalipa madaktari. Siku za mwanzo mwanzo marafiki zake waliokuwa wanakuja nyumbani kumjulia hali walikuwa wakimpa pesa kumsaidia. Lakini mwisho marafiki hao walichoka. Nikawa sioni mtu.
 
Tulifikia mahali umeme ulikatwa nyumbani kwa sababu tulikuwa na deni kubwa. Tukawa tunatumia taa za mafuta
 
Kwa vile niliona lile tatizo lilianzia kwa yule mganga wa kienyeji nikarudi tena kule kule kumueleza hali halisi.
 
“Mpaka dakika hii ni kwamba mume wangu bado haoni” nikamwambia.
 
“Bado haoni hadi sasa?” Mganga akajidai kuniuliza kwa mshangao.
 
“Bado”
 
“Nilipoona hutokei nilijua mume wako amepona”
 
“Tulikuwa tunashughulikia matibabu ya hospitali. Kwa kweli tumetumia pesa nyingi sana bila mafanikio. Mume wangu kwa sasa haweza kufanya kazi, pesa hatuna. Juzi juzi ameuza gari lake na pesa tulizopata pia zimekwisha. Imefikia hadi nyumbani tumekatiwa umeme!”
 
ITAENDELEA nini kitajiri baada ya Ibrahimu kuambiwa hataona tena

No comments:

Post a Comment