TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA MAKAO MAKUU YA JESHI LA POLISI
Tunapoelekea
kipindi hiki cha sikukuu za Krismas na mwaka mpya, wananchi wenye imani
ya Kikristo na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu
pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe
ambapo uzoefu unaonyesha baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo
kufanya vitendo vya uhalifu hasa wa kujipatia vipato na mali.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la
Polisi nchini, katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana na
vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna vitendo
vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza kipindi hiki cha sikukuu na pale
ambapo vitajitokeza vitadhibitiwa kwa haraka. Ulinzi umeimarishwa kwenye
maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo
mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu. Hata hivyo,
watu wote watakaoenda maeneo ya beach wanatakiwa kuwa makini ili
kuepuka kuzama kwenye maji.
Aidha, tunawakumbusha wananchi
kuwa makini katika suala zima la usalama wa maisha na mali zao, hususani
kuchukua hatua stahiki na za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona
viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao na sehemu mbalimbali za
biashara, na watokapo kwenye makazi yao wasiache nyumba wazi ama bila
mtu na pale inapobidi watoe taarifa kwa majirani zao. Wazazi
wanakumbushwa kuwa makini na watoto kwa kutokuwaacha watembee peke yao,
ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu
yao ikiwemo kupotea. Aidha, wazazi waepuke kuwapeleka watoto kwenye
kumbi za disko toto ambazo siyo salama.
Vilevile, wamiliki wa kumbi za
starehe wazingatie usalama katika kumbi zao, hawarusiwi kujaza watu
kupita kiasi kwenye kumbi hizo, hususani kumbi za disko toto. Aidha,
wamiliki wa kumbi za starehe na maeneo mengine yenye mikusanyiko mikubwa
ya watu wanakumbushwa kufunga vifaa maalum vya kufuatilia mienendo ya
watu wanoingia na kutoka katika maeneo hayo (CCTV kamera).
Pia, Jeshi la Polisi
linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, kuwa
makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva
wa magari na pikipiki, kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi
wawapo kazini.
Mwisho, tunawaomba wananchi
waendelee kutoa taarifa za mipango yoyote ya uhalifu watakayoiona
ikiendelea mahali popote kwa kuwafichua wahalifu hao ili hatua za kuzuia
uhalifu huo ziweze kuchukuliwa mapema. Taarifa zinaweza kutolewa
kupitia namba ya simu 0754 78 55 57 au Simu za Makamanda wa Polisi wa
mikoa au katika kituo chochote cha Polisi.
No comments:
Post a Comment