Sunday, December 21, 2014

KISIWA CHA HARISHI

KISIWA CHA HARISHI (15)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Wenzangu wote walikuwa na wake zao isipokuwa mimi lakini Masudi alisema alioa kisha aliachana na mke wake. Nilichokuwa nakijua mimi ni kuwa Masudi alikuwa na mke wake.
 
Sikujua ni kwanini Yasmin alituuliza vile.
 
“Kwa hiyo wewe na Masudi ndio hamna wake?” Yasmin akaniuliza.
 
“Ninachojua mimi Masudi anaye mke” nilimwambia Yasmin.
 
Kauli ile ilimkera Masudi.
 
“Nina mke mimi?” Masudi akaniuliza kwa ukali kidogo.
 
“Unaye!” nikamwambia kwa mkazo.
 
“Mke si nilishamuacha?. Au wewe ulikuwa hujui?”
 
“Mimi najua watania tu lakini mke bado unaye”
 
“Basi na yaishe. Mimi niliuliza tu kutaka kujua. Kama unaye mke au huna hakuna tatizo” Yasmin akaingilia kati.
 
“Huyu bwana mdogo anapenda sana kuniingilia!” Masudi akaunguruma.
 
Nikaamua kunyamaza.
 
“Nimesema yaishe jamani. Ngoja tulete karata tucheze”
 
SASA ENDELEA
 
Yasmin alitumia hekima kuyageuza yale mazungumzo akaenda kuleta karata, tukawa tunacheza.
 
“Hivi hizi karata ulikuwa unacheza na nani?” nikamuuliza Yasmin wakati tunacheza.
 
“Ninacheza na huyo aliyezileta”
 
“Harishi?”
 
“Ndiye huyo huyo. Anapoona nimepooza ananiambia kalete karata”
 
“Anajua kucheza karata?” akaulizwa na Masudi.
 
“Anajua. Hawa majini ni kama watu tu. Tofauti yetu ni ndogo sana. Wanafanya mambo mengi wanayofanya binaadamu”
 
Mazungumzo ya Harishi yalitufanya tukose amani. Yalitukumbusha wenzetu waliouawa. Mwenzetu mmoja lakini si Masudi akatuambia.
 
“Tuondoke twende kule tulikohamia”
 
“Chukueni hizo karata mwende nazo. Mtakwenda kucheza huko huko” Yasmin akatuambia.
 
Ilibidi tuondoke twende katika ile nyumba lakini Yasmin tulimuacha.
 
Tulipofika tuliendelea kucheza karata. Baadaye sote tulipitiwa na usingizi tukalala.
 
Tuliamshana jioni tukaamua tutoke twende tukatembee tembee. Tulizunguka sana katika kile kisiwa. Tulienda pia kuliangalia jahazi letu. Tuliporudi jua lilikuwalimeshakuchwa.
 
Tulimkuta Yasmin akitusubiri. Alikuwa ametuletea chakula cha jioni.
 
“Mnatoka wapi?” akatuuliza.
 
“Tulikwenda kutembea tembea kidogo” Masudi akamjibu na kuongeza “Kukaa tu kunachosha”
 
“Umetuletea chakula?” nikamuuliza Yasmin.
 
“Nimewaletea kabisa. Ikifika usiku sitaweza kuja huku. Harishi anaweza kuja wakati wowowte” Yasmin alituambia na kutuwekea chakula hicho juu ya meza.
 
“Ngoja nikusindikize” Masudi akawahi kumwambia Yasmin. Nilijua alitaka kunipiku mimi kwani alijua mimi ndiye ningemsindikiza.
 
Yasmin akakubali kuondoka na Masudi. Kwa upande wangi kitendo kile cha Masudi nilikiona kama ulimbukeni uliopitiliza na kutaka kujipendekeza kwa Yasmin.
 
Walipoondoka sisi tulikaa barazani mwa ile nyumba hadi giza likaingia.
 
“Mbona masudi harudi?” Tukawa tunaulizana.
 
Kusema kweli kitendo chake cha kuchelewa kurudi kilinikera. Nikaamua nimfuate peke yangu nijua alikuwa anafanya nini muda wote huo.
 
Nikaenda huku nikiwa na hasira. Nilipofika sikuingia ndani. Niliamua kufanya upelelezi kwa kuchungulia kwenye madirisha.
 
Wakati nachungulia niliana kusikia sautiya Yasmin ikiwa katika dhihaka, mwenyewe sikumuon. Nilibadilisha dirisha na ndipo nilipowaona wote wawili. Masudi alikuwa akikimbizana na Yasmin mle ndani kam waliokuwa wakicheza. Wakati mwingine Masudi alimkamata Yasmin na kuanguka naye chini akiwa amemshika kiuno.
 
“Kumbe wana mchezo huu, ndio maana amesahau kurudi” nikajisemea kimoyo moyo.
 
Licha ya moyo wangu kuuma nilijiambia chaguo la Yasmin ni mimi, Masudi alikuwa akijipendekeza tu.
 
Macho yangu yaliwashuhudia wakiwa wamelala chini. Masudi alikuwa kama akibembeleza kitu kwa Yasmin. Yasmin alikuwa ametulia akimsikiliza.
 
Sikuweza kufikiria chochote zaidi ya kuhisi kuwa Masudi alikuwa akimtongoza Yasmin na alikuwa akinifitini mimi.
 
Sikutaka tena kuuona upumbvu wake. Nikaamua kuondoka kwani usiku ulikuwa unazidi kushamiri.
 
Yasmin haweza kumkubali Masudi, Yasmin amenipenda mimi, nilijiambia kujifariji wakati naondoka.
 
Nilirudi kwa wenzangu huku nikiuzuia moyo wangu usitaharuki kutokana na kitendo kile nilichokiona kwa Masudi kumkumbatia Yasmin.
 
“Umemkuta?” Wenzangu wakaniuliza.
 
“Sikufika” nkawadanganya. “Nimeamua kurudi njiani, naona usiku mwingi huu”
 
“Au twendeni sote?” Mmoja akaniuliza.
 
“Tumsubirini tu hapa hapa”
 
Sikutaka kuwambia ukweli kuwa nilimkuta akifanya vitendo vya kipuuzi. Nilihisi wangeweza kuja kumwambia mwenyewe halafu kwa akili za Masudi tunaweza kugombana bure.
 
Tukakaa kumsubiri hadi saa tatu. Tulipoona hatokeai tuliamua kula chakula na kumbakishia chake.
 
Nilikuwa nimebaki na wenzangu wawili Shazume na Haji. Kwa upande wangu nilishakijua kilichokuwa kinamchelewesha Masudi lakini wenzangu walikuwa na wasiwasi kwamba huenda Masudi amepata matatizo.
 
Walikuwa wakisisitiza kuwa twende tukamuangalie.
 
“Kutoka usiku huu si vizuri” nikawambia. “Acheni tungoje kesho asubuhi tutakwenda kumuangalia”
 
ITAENDELEA KESHO NA USIKOSE NINI KITATOKEA

No comments:

Post a Comment