Wednesday, December 24, 2014

KISIWA HARISHI SEHEMU YA (17)

HADITHI
 
KISIWA CHA HARISHI (17)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
“Tutakufa kama wenzetu. Sidhani kama tutapona kwa maana tulikuwa watu saba, sasa tumebaki watatu” nikamwambia Yasmin.
 
“Msikate tama ndugu zangu. Kama ni kufa tutakufa sote. Hamuwezi kufa mkaniacha mimi”
 
Nilimuona Haji akijifuta machozi.
 
“Usilie ndugu yangu. Ushinde moyo. Safari yenu bado ni ndefu” akaambiwa na Yasmin.
 
Shazume akageuza uso na kunitazama.
 
“Nina tama ndogo sana kama tutapona” akaniambia.
 
Sikumjibu kitu. Yasmin akanyanyuka.
 
Nitawatayarishia japokuwa uji mchangamke” akatuambia.
 
“Sawa” nikamjibu.
 
“Naenda kuwapikia halafu nitawaletea”
 
“Kama tutakusumbua ninaweza kuja kuuchukua”
 
“Harishi hatakuja tena leo. Mnaweza hata kuja nyote”
 
Nikawatazama wenzangu.
 
“Eti mnasemaje?”
 
SASA ENDELEA
 
“Akituletea huku itakuwa bora” Haji akasema.
 
“Tutakuwa tunamsumbua. Tungekwenda tu kwa vile ametuhakikishia kuwa leo hakuna tatizo” nikawambia wenzangu.
 
“Haya twendeni ila tusikae sana” Shazume akasema.
 
Tukaondoka pamoja na Yasmin kuelekea katika lile jumba la Harishi.
 
“Tangu mmekuja nyinyi nimejisikia kuchangamka sana” Yasmin alituambia tukiwa njiani.
 
“Kikwazo chetu kikubwa ni huyu Harishi. Kama si yeye tungekuwa na furaha sana” nikasema.
 
“Roho zetu sasa zina wasiwasi. Kila siku mmoja wetu anakufa. Tulikuwa watu saba, sasa tumebaki watatu” Haji akalalamika.
 
“Ni kweli Haji lakini kama nyinyi mtakuwa makini mnaweza kusalimika” Yasmin akatuambia.
 
“Yasmin unatuambia ukweli? Tutasalimikaje? Hata kama hatutauawa na Harishi tutakaa katika kisiwa hiki hadi lini?” nikamuuliza Yasmin.
 
“Kwani mimi nitakaa hadi lini?” Yasmin akatuulisa. Sauti yake ilikuwa imebadilika.
 
“Wewe mwenyewe umeshajitolea” nikamjibu.
 
“Kwa sababu sijipendi?”
 
“Hapana, si hivyo”
 
“Basi mimi na nyinyi ni sawa tu. Kama mimi nimejitolea na nyinyi mjitolee kama mimi. Muwe tayari kwa lolote”
 
“Sisi tumeshajitolea Yasmin. Hatuna la kufanya” nikamwambia Yasmin aliyekuwa amekasirika kidogo.
 
“Tunaona juhudi zako Yasmin” nikaendelea kumwambia. “Kama si wewe kutupokea kwa nia moja tungekuwa tumeshakufa kwa kuhangaika na njaa.
 
Tulipofiak kwenye lile jumba tulipumzika ukumbini. Yasmin alituletea karata kisha tukaenda kupika uji. Uji ulipokuwa tayari Yasmin alituletea tukanywa. Huji huo ulikuwa umechanganywa na asali.
 
Tuliposhiba Yasmin aliondoka tena kwenda kupika chakula cha mchana. Sisi tuliendelea kucheza karata, tulipochoka tukalala hapo hapo. Yasmin ndiye aliyekuja kutuamsha.
 
“Wenzangu kumbe mmelala?” akatuuliza.
 
“Ah! tumepitiwa na usingizi bila kujijua” nikamwambia na kumuuliza “Umeshapika?”
 
“Nimeshapika, kwani mna njaa niwapakulie?”
 
“Bado kwanza. Tusubiri kidogo”
 
“Naona mko wachovu sana. Twendeni bahari mchangamke kidogo”
 
Kwa vile hatukuwa na la kufanya tukakubaliana na wazo La Yasmin la kwenda baharini. Kisiwa hicho kilikuwa na fukwe nzuri zenye mchanga mweupe.
 
Tukiwa kwenye fukwe za kisiwa hicho tulibuni michezombalimbali ya kujichangamsha ikiwemo kukimbizana. Mwisho tuliamua kujitosa kwenye maji na kuogelea tukiwana nguo zetu.
 
Yasmin alikuwa hodari wa kuogelea. Alituambia alipokuwa Comoro kila siku za jumapili alikuwa akienda kuogelea na ndugu zake.
 
Tulipochoka kuogelea tulikaa kwenye fukwe hadi tukakauka maji. Tukaondoka kurudi katika jumba la Harishi
 
Yasmin alikwenda kuoga maji baridi. Alipomaliza na sisi tulikwenda kuoga. Hatukuwa na nguo za kubadili.
Yasmin alitupa mashuka tukajifunga. Zile nguo zetu tulizifua na kwenda kuzianika nje kwenye jua.
 
Tulipomaliza kuanika nguo ndipo Yasmin alipotuandalia chakula, tukala. Wakati tunakula alituambia kuwa tunaweza kuendelea kushinda hapo kwake hadi jioni lakini Haji akapinga ushauri wake na kutaka tuondoke tukimaliza chakula.
 
Baada ya chakula tulikubaliana kuwa turudi katika ile nyumba tuliyohamia. Tukamuaga Yasmin na kuondoka.
 
“Sasa wenzangu mna ushauri gani, hali ya hapa ndiyo kama hii tunayoiona?” nikawauliza wenzangu mara tu baada ya kufika kwenye ile nyumba
 
“Kwani wewe una ushauri gani?” Haji akaniuliza.
 
“Nia yetu sote ni kuondoka katika kisiwa hiki. Sasa nataka tujadili njia itakayotuwezesha kuondoka. Ni vizuri kila mmoja akatoa wazo lake alilonalo” nikasema.
 
“Ni kweli ulivyosema lakini tunajikuta tumekwama, tusingekuwa hapa hadi leo” Shazume akatuambia.
 
“Kwa hiyo hatujui tutaendelea kukaa hapa na Yasmin hadi lini?” nikauliza.
 
“Ukweli ndio huo” Haji akanikubalia.
 
Nikatikisa kichwa changu kusikitika, baada ya hapo sote tukawa kimya.
 
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE UHONDO HUU NINI KITAFUATA

No comments:

Post a Comment