Wednesday, December 24, 2014

POLISI TANGA YACHARUKA

Kumekucha blog

Tanga,JESHI la Polisi Tanga limesema litawachukulia hatua kali za kisheria madereva wa magari na bodaboda pamoja na wakorofi ambao watajaribu kutibua sherehe ya Sikukuu ya Krismass na mwaka mpya kwa kuwaweka rumande hadi sherejhe kuisha.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, kamanda wa piolisi Mkoani hapa, Freisser Kashai, alisema polisi wamejipanga kuhakikisha wananchi wanasherehekea sikukuu kwa amani na utulivu kuanzia kesho.

Alisema polisi itaongeza doria katika maeneo  mbalimbali kwa kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani na kutoa tahadhari kwa madereva kuzingatia sheria zake na kuacha matumizi ya pombe wakati wakiendesha vyombo hivyo.

“Polisi itakuwa wakali sana zaidi ya vipindi vyote na natoa salamu kwa madereva wa vyombo vya moto hasa bodaboda----yoyote ambaye atavunja sheria tutamsweka ndani” alisema Kashai

“Kipimo cha kuwabaini wanaotumia vilevi vitatumika na tutakuwa tukiwasimamisha na kuwachunguza----zoezi hili litakuwa siku zote za sherehe za Krismass na mwaka mpya” alisema Kashai

Kamanda aliwataka wazazi na walezi kuchukua tahadhari kwa watoto wao wakati wa matembezi na kuhakikisha wanaweka usalama majumbani mwao ili kuepusha kutoa nafasi kwa wadokozi wa madirishani.

Alisema vipindi vya sherehe za sikukuu na mwaka mpya wezi hutumia mwanya wa familia kutoka na hivyo nyumba zao kuziwacha bila ulinzi jambo ambalo hutibua furaha za sikukuu.

Akizungumzia hali ya usalama katika mipaka ya Mkoa huo, kamanda alisema wameweza kudhibiti upitishaji wa mali za magendo na uvushaji wa wahamiaji haramu.

Alisema upitishaji wa wahamiaji haramu wameukomesha baada ya kumkamata kinara na mratibu wa kuwasafirisha   na hivyo kuwatahadharisha wananchi wanaokaa kandokando ya mpaka kuacha kushirikiana na makundi ya kihalifu.

“Msako wa kuwatafuta watu wanaojihusisha na biashara za magendo na biashara haramu ya wahamiaji haramu itaendelea na polisi haitochoka-----tuko katika uchunguzi watu wanaoishi katika mipaka kama wanashirikiana na wahalifu” alisema Kashai

Alisema kwa sasa polisi na maofisa upelelezi wanafanya uchunguzi kwa watu wanaoishi pembezoni mwa mpaka wa Kenya kubainika kama wanashirikiana na makundi ya wafanyabiashara za magendo na wapitishaji wa wahamiaji haramu.

                                            Mwisho

No comments:

Post a Comment